Ninyi si Wageni Tena
Katika Kanisa hili hamna wageni na waliotengwa. Kuna tu ndugu na dada.
Wengi wetu wakati mmoja au mwingine tumekuwa katika hali ambayo ilikuwa mpya kwetu, ambapo tulihisi ugeni na kutokuwa salama. Hali hii ilitendekea familia yetu takriban miaka mitano iliyopita baada ya Rais Thomas S Monson kunipa wito kuhudumu kama Kiongozi Mwenye Mamlaka wa Kanisa. Wito huu ulilazimisha kuhama kwa familia yetu kutoka kwa sehemu nzuri tuliyokuwa tumefurahia kwa zaidi ya miongo miwili. Mke wangu nami bado tunakumbuka majibu ya papo ya watoto wetu wakati walijua kuhusu mabadiliko. Mwana wetu wa umri wa miaka 16 alisema, “Si tatizo kamwe. Mnaweza kwenda; nitabaki!”
Kisha basi aliamua kwa haraka kuambatana nasi na kwa uaminifu kukubali fursa hii mpya katika maisha yake. Kuishi katika mazingira mapya zaidi ya miaka michache iliyopita kumekuwa tukio la kujifunza na ya kufurahisha kwa familia yetu, hasa kutokana na mapokezi ya upendo na wema wa Watakatifu wa Siku za Mwisho. Tulivyoishi katika nchi mbalimbali, tumekuja kufahamu kwamba umoja wa watu wa Mungu duniani kote ni jambo halisi na linaloonekana.
Wito wangu umenisababisha nisafiri nchi nyingi na umenipa fursa nzuri ya kusimamia mikutano mingi. Ninapotazama mikusanyiko mbalimbali, mara nyingi mimi hutazama washiriki wakiwakilisha nchi nyingi, lugha, na tamaduni. Kipengele kimoja kizuri cha injili ya wakati wetu ni kuwa haijazuiwa kwa eneo la kijiografia au kundi la mataifa. Ni ya kimataifa na kwa kila mtu. Inatayarisha ujio wa Mwana wa Mungu kwa kukusanya “watoto wake kutoka pembe nne za ulimwengu.”1
Ingawa ushiriki wa Kanisa unaongezeka katika utofauti wake, urithi wetu mtakatifu unashinda tofauti zetu. Kama washiriki wa Kanisa, tunakaribishwa ndani ya nyumba ya Israeli. Tunakuwa ndugu na dada, warithi sawa kwa ukoo, sawa wa kiroho. Mungu alimuahidi Ibrahimu kwamba “kwani kadiri wengi watakavyoipokea Injili hii wataitwa kwa jina [lake], nao watahesabiwa kuwa uzao [wake], na watainuliwa na kumbariki [yeye] kama baba yao.”2
Ahadi imetolewa kwa kila mmoja atakaye kuwa mshiriki wa Kanisa: “Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bila ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu.”3
Neno mgeni linatoka kwa neno la kilatini extraneus, linalomaanisha “nje” ama ‘kutoka nje”. Kwa kawaida, linamtambulisha mtu ambaye ni “mgeni” kwa sababu mbalimbali, iwe ni kwa sababu ya asili, utamaduni, maoni, au dini. Kama wanafunzi wa Yesu Kristo ambao wanajitahidi kuwa katika ulimwengu lakini wasio wa ulimwengu, wakati mwingine sisi huhisi kama watu wa nje. Sisi, zaidi ya wengi, tunajua kwamba milango fulani inaweza kufungwa kwa wale ambao wanachukuliwa kuwa tofauti.
Kote katika nyakati watu wa Mungu wameamrishwa wawahudumie watu wote ambao ni wageni ama ambao huenda wakatazamiwa kuwa tofauti. Katika nyakati za kale, mgeni alinufaika na wajibu ule ule wa ukarimu kama mjane ama yatima. Kama wao, mgeni alikuwa katika hali ya hatari sana, na maisha yake yalitegemea ulinzi aliopokea kutoka kwa wenyeji. Watu wa Israeli walipokea maelekezo ya mahususi juu ya mada hii: “Mgeni akaaye pamoja nawe atakuwa kama mzaliwa kwenu, mpende kama nafsi yako; kwa maana ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri.”4
Wakati wa huduma Yake hapa duniani, Yesu alikuwa mfano wa yule ambaye alikwenda mbali zaidi ya wajibu rahisi wa ukarimu na kuvumiliana. Wale ambao walikuwa wametengwa na jamii, wale ambao walikuwa wamekataliwa na kuchukuliwa kuwa wachafu na waliojiona kuwa wenye haki, walipewa huruma yake na heshima. Walipokea sehemu sawa ya mafundisho yake na huduma.
Kwa mfano, Mwokozi alienda kinyume na tamaduni zilizokuwa zimewekwa za nyakati Zake kumzungumzia mwanamke wa Samaria, akimuomba maji. Aliketi chini kula na wanasiasa na waokotaji ushuru. Hakusita kumwendea mwenye ukoma, kumshika na kumponya. Akiwa amefurahishwa na imani ya akida wa Kirumi, aliambia umati, “nawaambieni, sijaona imani kubwa namna hii, kwa yeyote katika Israeli.”5
Yesu ametuuliza tutii sheria ya upendo kamilifu, ambayo ni karama ya ulimwenguni kote na isiyo na masharti. Alisema:
“Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?
“Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la zaidi? Hata watu wa mataifa, Je, Nao hawafanyi kama hayo?
“Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.”6
Katika kanisa hili, hakuna wageni na waliotengwa. Kuna tu ndugu na dada. Maarifa ambayo tunayo ya Baba wa Milele yanatusaidia kuwa waangalifu zaidi kwa udugu na udada ambao unafaa kuwepo miongoni mwa wanaume na wanawake wote duniani.
Kifungu kutoka riwaya Les misérables kinaeleza jinsi wamiliki wa ukuhani wanaweza kutendea wale watu wanaotazamiwa kuwa wageni. Jean Valjean alikuwa amewachiliwa tu kama mfungwa. Akiwa amechoshwa na safari ndefu na kuwa anakufa njaa na kiu, aliwasili katika mji mdogo akitafuta mahali pa kupata chakula na malazi usiku huo. Wakati habari ya kuwasili kwake ilienea, mmoja baada ya mwingine, kila mkazi alifunga milango yao kwake. Si hoteli, si nyumba ya wageni, si hata gerezani angekaribishwa ndani. Alikataliwa, akafukuzwa, akatengwa. Hatimaye, akiwa hana nguvu, alizimia mlangoni mwa mbele wa askofu wa mji.
Kasisi huyo mwema alikuwa anafahamu vyema historia ya Valjean, lakini alimkaribisha mhuni nyumbani kwake na maneno haya ya upendo:
“Hii si nyumba yangu, ni nyumba ya Yesu Kristo. Mlango huu hauulizi aliyeingia kama ana jina, lakini kama ana huzuni. Unateseka, una njaa na kiu; umekaribishwa. ... nina haja gani kujua jina lako? Hata hivyo, kabla uniambie [jina lako] ulikuwa na moja ambaye nilimjua”
“[Valjean] akafungua macho yake kwa mshangao.
“Hakika? Ulijua nilikuwa ninaitwa nani?”
“Ndio, akamjibu Askofu, “unaitwa ndugu yangu.’”7
Katika Kanisa hili, kata yetu na jamii zetu si mali yetu. Ni mali ya Yesu Kristo. Yeyote aingiaye makanisani mwetu anapaswa kujihisi nyumbani. Wajibu wa kukaribisha kila mtu una umuhimu wa kuongezeka. Dunia ambamo tunaishi inapitia kipindi cha mageuzi makubwa. Kwa sababu ya ongezeko la upatikanaji wa vyombo vya usafiri, kasi ya mawasiliano, na utandawazi wa uchumi, dunia inakuwa kijiji kimoja kikubwa ambapo watu na mataifa yanakutana, yanaungana, na kutangamana kwa njia ambayo kamwe haijawa.
Mabadiliko haya makubwa duniani kote yanatekeleza miundo ya Mwenyezi Mungu. Mkusanyiko wa wateule wake kutoka pembe nne za dunia haitendeki tu kwa kutuma wamisionari kwa nchi za mbali lakini pia pamoja na kuwasili kwa watu kutoka maeneo mengine katika miji yetu wenyewe na vitongoji. Wengi, bila kujua, wanaongozwa na Bwana hadi mahali ambapo wanaweza kusikia Injili na kuja katika zizi Lake.
Kuna uwezekano mkubwa sana kwamba mtu mwingine atakayeongoka kwa injili katika kata yako hatakuwa mtu ambaye ametoka kwa marafiki wako wa kawaida ama watu unaowajua. Huenda ukagundua hili kwa muonekano wake, lugha, namna ya mavazi, au rangi ya ngozi. Mtu huyu huenda alikuwa mzima katika dini nyingine, na historia tofauti au maisha tofauti.
Ushirika ni wajibu muhimu wa ukuhani. Jamii ya ukuhani wa Haruni na Melkizediki zinafaa zifanye kazi pamoja na kina dada chini ya uongozi wa askofu ili kuhakikisha kuwa kila mtu amekaribishwa kwa upendo na wema. Walimu wa nyumbani na walimu watembelezi watakuwa makini ili kuhakikisha kwamba hakuna aliyesahaulika ama kupuuzwa.
Sote tunapaswa tushirikiane ili kujenga umoja wa kiroho miongoni mwa kata na matawi yetu. Mfano wa umoja mkamilifu ulikuwepo miongoni mwa watu wa Mungu baada ya kuenda kwa Kristo kule Amerika. Kumbukumbu inaeleza kuwa “hakukuwa na Walamani, wala aina yoyote ya vikundi; lakini walikuwa kitu kimoja, watoto wa Kristo, na warithi wa ufalme wa Mungu.”8
Umoja haupatikani kwa kupuuza ama kutenga washiriki wanaoonekana kuwa tofauti ama wanyonge na kujihusisha tu na watu ambao ni kama sisi. Kinyume chake, umoja hupatikana kwa kuwakaribisha na kuwahudumia wale ambao ni wapya ama ambao wana mahitaji maalum. Washiriki hawa ni baraka kwa Kanisa na wanatupa fursa ya kuhudumia majirani zetu na hivyo basi kusafisha mioyo yetu.
Hivyo basi, ndugu zangu, ni jukumu lenu kumfikia yeyote ambaye anajitokeza mlangoni mwa majengo yenu ya Kanisa. Wakaribishe kwa shukrani na bila hila. Watu ambao huwajui wanapotembea ndani ya mojawapo ya mikutano yenu, wasalimie kwa upendo na wakaribishe waketi nawe. Tafadhali kuwa wa kwanza kuwasaidia wahisi wamekaribishwa na wanapendwa badala ya kungoja wao wakukujie.
Baada ya kukutana nao kwa mara ya kwanza, fikiria jinsi unavyoweza kuendelea kuwatumikia. Nilisikia hapo awali juu ya kata moja ambapo, baada ya ubatizo wa akina dada wawili viziwi, akina dada wema wawili wa Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama waliamua kujifunza lugha ya ishara ili wangeweza kuwasiliana vyema zaidi na hawa waongofu wapya. Ni mfano mzuri sana kiasi gani, wa upendo wa akina ndugu na dada zetu wapendwa katika injili.
Ninashuhudia kwamba hakuna aliye mgeni kwake Baba yetu wa Mbinguni. Hakuna ambaye roho yake si ya thamani Kwake. Pamoja na Petro, ninashuhudia kwamba “Mungu hana upendeleo: bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na Yeye.”9
Ninaomba kuwa wakati Bwana atakapokusanya kondoo Wake katika siku ya mwisho, aweze kusema kwa kila mmoja wetu, “nalikuwa mgeni, mkanikaribisha.”
Kisha tutamwambia Yeye, “Ni lini tulipokuona u mgeni, na tukakukaribisha?”
Na Yeye atatujibu “Amin, nawaambia kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.”10
Katika jina la Yesu Kristo, amina.