Njoo, Unifuate 2024
Oktoba 21–27: “Hakujakuwa na Watu Ambao Wangekuwa na Furaha Zaidi.” 3 Nefi 27–4 Nefi


“Oktoba 21–27: “Hakujakuwa na Watu Ambao Wangekuwa na Furaha Zaidi.’ 3 Nefi 27–4 Nefi,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: Kitabu cha Mormoni 2024 (2023)

“Oktoba 21–27. 3 Nefi 27–4 Nefi,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2024 (2023)

Picha
Yesu aliyefufuka akiwafundisha watu

Oktoba 21–27: “Hakujakuwa na Watu Ambao Wangekuwa na Furaha Zaidi”

3 Nefi 274 Nefi

Mafundisho ya Yesu Kristo ni zaidi ya falsafa nzuri ya kutafakari. Yanakusudiwa kutupatia msukumo tuwe kama Yeye alivyo. Kitabu cha 4 Nefi kinaonesha tu jinsi ambavyo injili ya Mwokozi inaweza kumbadili kabisa mtu. Kufuatia huduma fupi ya Yesu, karne za mabishano kati ya Wanefi na Walamani zilikoma. Mataifa mawili yaliyojulikana kwa uasi na kiburi yalikuja kuwa “kitu kimoja, watoto wa Kristo” (4 Nefi 1:17), na “vitu vyao vyote vilitumiwa kwa usawa miongoni mwao” (4 Nefi 1:3). Mapenzi ya Mungu … yaliishi katika mioyo ya watu,” na “hakujakuwa na watu ambao wangekuwa na furaha zaidi miongoni mwa watu wote ambao waliumbwa na mkono wa Mungu” (4 Nefi 1:15–16). Hivi ndivyo mafundisho ya Mwokozi yalivyowabadili Wanefi na Walamani. Ni kwa jinsi gani yanakubadili wewe?

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani

3 Nefi 27:1–12

Kanisa la Yesu Kristo linaitwa kwa jina Lake.

Wanafunzi wa Mwokozi walipoanza kuanzisha Kanisa Lake kote nchini, kuliibuka swali ambalo, kwa baadhi ya watu, linaweza kuonekana kama hoja ndogo—ni lipi liwe jina la Kanisa? (ona 3 Nefi 27:1–3). Unajifunza nini kuhusu umuhimu wa jina hili kutokana na jibu la Mwokozi katika 3 Nefi 27:4–12?

Mwokozi alifunua jina la Kanisa Lake leo hii katika Mafundisho na Maagano 115:4. Tafakari kila neno katika jina hilo. Ni kwa jinsi gani maneno haya yanatusaidia tujue sisi ni akina nani, nini tunaamini, na jinsi tunavyopaswa kutenda?

Ona pia Russell M. Nelson, “Jina Sahihi la Kanisa,” Liahona, Nov. 2018, 87–89; “Jesus Christ Declares the Name of His Church and His Doctrine” (video), Maktaba ya Injili.

3 Nefi 27:10–22

Kanisa la Yesu Kristo limejengwa juu ya injili Yake.

Baada ya kueleza kwamba Kanisa Lake lazima “lijengwe juu ya injili [Yake]” (3 Nefi 27:10), Mwokozi alieleza injili Yake ni nini. Ni kwa jinsi gani unaweza kufanya muhtasari wa kile Yeye alichokisema katika 3 Nefi 27:13? Kulingana na maelezo haya, inamaanisha nini kwa Kanisa—na wewe pia—kujengwa juu ya injili Yake?

Andika kile unachojifunza. Tazama kile Mwokozi alichowafundisha wanafunzi wake katika 3 Nefi 27: 23–26. Kwa nini ni muhimu kuweka kumbukumbu ya uzoefu wa kiroho? Unahisi kutiwa msukumo kuandika kitu gani pale ulipojifunza huduma ya Mwokozi katika 3 Nefi?

3 Nefi 28:1–11

“Ni kitu gani ambacho mnahitaji?”

Je, ni kipi ungesema kama Mwokozi angekuuliza, kama alivyowauliza wanafunzi Wake, “Ni kitu gani ambacho mnahitaji kutoka kwangu?” (3 Nefi 28:1). Fikiria kuhusu hili unaposoma 3 Nefi 1–11. Unajifunza nini kuhusu matamanio ya mioyo ya wanafunzi kutokana na majibu yao kwa swali Lake? Ni kwa jinsi gani matamanio yako yanabadilika kadiri unavyoishi injili ya Yesu Kristo?

Nyimbo mara nyingi huonesha matamanio ya moyoni—“Nipe Uongofu” ni mfano mzuri (Nyimbo za Dini, na. 64). Fikiria kupata wimbo ambao unaakisi matamanio yako.

3 Nefi 29–30

Kitabu cha Mormoni ni ishara kwamba kazi ya siku za mwisho ya Mungu inatimizwa.

Fikiria kuhusu ishara ambazo zinakuruhusu wewe ujue kitu fulani kitatokea. Kwa mfano, ni kwa jinsi gani wewe unajua kwamba mvua inakuja au majira yanabadilika? Kulingana na 3 Nefi 29:1–3, ni kwa jinsi gani unajua kazi ya Mungu ya kuwakusanya watu Wake “imeanza kutimizwa”? (ona pia 3 Nefi 21:1–7). Ungeweza pia kugundua katika 3 Nefi 29:4–9, mambo ambayo watu wangekana katika siku yetu. Je! Kitabu cha Mormoni kimeimarisha vipi imani yako katika vitu hivi?

4 Nefi 1:1–18

Picha
ikoni ya seminari
Kufuata mafundisho ya Yesu Kristo huongoza kwenye umoja na furaha.

Je, ingeweza kuwaje kuishi katika miaka iliyofuatia ziara ya Mwokozi? Unapojifunza 4 Nefi 1:1–18, fikiria kuorodhesha baraka ambazo watu walizipokea. Ungeweza pia kuwekea alama au kuandika chaguzi ambazo walifanya ambazo ziliongoza kwenye maisha haya ya baraka. Yesu aliwafundisha nini ambacho kilileta msukumo kwenye chaguzi zao njema? Hapa kuna baadhi ya mifano, lakini unaweza kutafuta mingine: 3 Nefi 11:28–30; 12:8–9, 21–24, 40–44; 13:19–21, 28–33; 14:12; 18:22–25.

Tafakari kile unachoweza kufanya kuisaidia familia yako, kata au jumuia kuishi katika umoja mkubwa zaidi na furaha. Unaweza kufanya nini kusaidia kushinda migawanyiko na kuwa “wamoja” na watoto wengine wa Mungu? Ni mafundisho yapi ya Yesu Kristo yanakusaidia utimize lengo hili?

Kwa huzuni, jamii ya Sayuni iliyoelezwa katika 4 Nefi hatimaye iliangukia kwenye uovu. Unaposoma 4 Nefi 1:19–49, tafuta mitazamo na tabia ambazo ziliweka ukomo kwenye furaha na umoja wao. Ni kipi unaweza kufanya ili kusaidia kuondoa mitazamo au tabia hizi?

Ona pia Musa 7:18; D. Todd Christofferson, “Jamii Endelevu,” Liahona, Nov. 2020, 32–35; Reyna I. Aburto, “Kwa Moyo Mmoja,” Liahona, Mei 2018, 78–80; Mada za Injili, “Kuwa wa Kanisa la Yesu Kristo,” Maktaba ya Injili.

Kwa mawazo zaidi, ona toleo la mwezi huu la Liahona na magazeti ya Kwa ajili ya Nguvu kwa Vijana.

Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto

3 Nefi 27:3–8

Mimi ni wa Kanisa la Yesu Kristo.

  • Ili kutambulisha umuhimu wa jina la Kanisa la Yesu, zungumza na watoto wako kuhusu majina yao wenyewe. Kwa nini majina yetu ni muhimu? Kisha mngeweza kusoma 3 Nefi 27:3 pamoja, mkitafuta swali ambalo wanafunzi wa Yesu walikuwa nalo. Wasaidie watoto wako wapate majibu katika 3 Nefi 27:5–6. Kwa nini jina la Kanisa ni muhimu?

  • Ungeweza pia kuwasaidia watoto wako wafikirie makundi tofauti waliyomo, kama vile familia au darasa la Msingi. Waulize kile wanachokipenda kuhusu kuwa wa kila kundi. Kisha mngeweza kuimba “The Church of Jesus Christ” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 77), pamoja na kuzungumza kuhusu kwa nini wana shukrani kuwa wa Kanisa la Mwokozi.

3 Nefi 27:13–16

Kanisa la Yesu Kristo limejengwa juu ya injili Yake.

  • Mwokozi alifanya ufupisho wa injili Yake katika 3 Nefi 27. Ungeweza kuwaeleza watoto kwamba neno injili linamaanisha “habari njema.” Ni habari njema zipi wanazipata katika 3 Nefi 27:13–16? Tumia ukurasa wa shughuli ya wiki hii kufundisha kwamba Kanisa la Mwokozi limejengwa juu ya injili Yake.

3 Nefi 27:30–31

Baba wa Mbinguni hufurahia wakati watoto Wake wanaporudi Kwake.

  • Fikiria kucheza mchezo ambapo mtu mmoja anajificha na wengine wanajaribu kumtafuta. Hii inaweza kuongoza kwenye mazungumzo kuhusu shangwe tunayoihisi wakati mtu fulani aliyekuwa amepotea anapopatikana. Baada ya kusoma 3 Nefi 27:30–31, ungeweza kuzungumza kuhusu jinsi ya kusaidiana wao kwa wao kubaki karibu na Baba wa Mbinguni ili kwamba “kusiwe na … atakayepotea.”

4 Nefi

Kumfuata Kristo kunanipa shangwe.

  • Ili kuwasaidia watoto wako wajifunze kuhusu furaha ya watu walioelezwa katika 4 Nefi, ungeweza kuwaonesha picha za watu wenye furaha. Kisha, mnaposoma pamoja mistari 2–3 na 15–17 (au “Mlango wa 48: Amani katika Amerika; Hadithi za Kitabu cha Mormoni, 136–37), wangeweza kuonesha picha kwa vidole vyao wakati unapofika kwenye kitu fulani katika hadithi ambacho kinaleta furaha.

  • Ili kuwasaidia watoto wako wafanyie kazi kile kilichofundishwa katika 4 Nefi 1:15–16, ungeweza kuwafikisha kwenye hali ambapo watu wamekasirikiana wao kwa wao. Waalike waigize hali ingekuwaje kama tungekuwa na “upendo wa Mungu” katika mioyo yetu.

Kwa ajili ya mawazo zaidi, ona toleo la mwezi huu la gazeti la Rafiki.

Picha
Yesu akizungumza na wanafunzi watatu Wanefi

Kristo na Wanafunzi Watatu Wanefi, na Gary L. Kapp

Chapisha