“Desemba 23–29: ‘Atakuja Duniani Kuwakomboa Watu Wake.’ Krismasi,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: Kitabu cha Mormoni 2024 (2023)
“Desemba 23–29. Krismasi,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2024 (2023)
Desemba 23–29: “Atakuja Duniani Kuwakomboa Watu Wake”
Krismasi
Kuanzia Nefi mpaka Moroni, kila nabii katika Kitabu cha Mormoni alijitolea kwa kusudi takatifu lililofanyiwa muhtasari katika ukurasa wa jina wa kitabu hiki: “Kuwathibitishia [watu wote] kwamba Yesu ndiye Kristo.” Nabii mmoja alimuona Yeye kama roho kabla ya maisha ya sasa, na mwingine aliona huduma Yake ya duniani katika ono. Mmoja alisimama juu ya ukuta kutangaza ishara za kuzaliwa Kwake na kifo Chake, na mwingine akapiga magoti mbele ya mwili Wake uliofufuka, akigusa vidonda kwenye mikono, miguu na ubavuni Mwake. Wote walijua ukweli huu muhimu: “Hakuna njia nyingine wala namna ambayo kwayo binadamu anaweza kuokolewa, isipokuwa kupitia damu ya upatanisho ya Yesu Kristo, ambaye … atakuja kuukomboa ulimwengu” (Helamani 5:9).
Kwa hivyo wakati wa msimu huu wa Krismasi, wakati waaminio kote ulimwenguni wanasherehekea wema na upendo wa Mungu kwa kumtuma Mwana Wake, tafakari jinsi ambavyo Kitabu cha Mormoni kimeimarisha imani yako katika Kristo. Unapofikiria kuhusu kuzaliwa Kwake, tafakari ni kwa nini alikuja na jinsi kuja Kwake kulivyoyabadili maisha yako. Kisha unaweza kupata uzoefu wa furaha ya kweli ya Krismasi—zawadi ambayo Yesu Kristo anakupatia.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani
Yesu Kristo alizaliwa kuwa Mwokozi wangu.
Ni desturi kusoma hadithi ya kuzaliwa kwa Mwokozi katika Agano Jipya wakati wa Krismasi, lakini pia unaweza kupata unabii wenye kusisimua wa tukio hili takatifu katika Kitabu cha Mormoni. Kwa mfano, unabii wa kuzaliwa kwa Mwokozi na huduma Yake hupatikana katika 1 Nefi 11:13–36; Mosia 3:5–10; Helamani 14:1–13. Ni misukumo ipi kuhusu Yesu Kristo inakujia unaposoma vifungu hivi na kutafakari alama za ishara za kuzaliwa Kwake? Ni kwa jinsi gani shuhuda za manabii hawa zimeimarisha ushuhuda wako juu ya Kristo na huduma Yake?
Hapa kuna baadhi ya mapendekezo mengine ya kukusaidia ufokasi kwa Yesu Kristo wakati wa Krismasi:
-
Je, unajua kwamba unaweza kuangalia jumbe kutoka kwenye ibada za Krismasi zilizopita za Urais wa Kwanza katika Maktaba ya Injili? Zitafute katika mkusanyiko wa “Christmas Videos.” Fikiria kushiriki jumbe hizi na muziki ili usambaze furaha ya Krismasi.
-
Wewe na familia yako mngeweza pia kufurahia kusikiliza chaguzi kutoka “Christmas Music” mkusanyiko katika maktaba ya Injili.
-
Fikiria kupanga shughuli ambazo wewe na familia yako mnaweza kufanya katika siku zinazoelekea kufikia Krismasi ili kumhisi Roho wa Kristo, kama vile kumhudumia mtu au kuimba nyimbo za Krismasi kwa pamoja. Ona LighttheWorld.org kwa ajili ya mawazo.
Ona pia Mathayo 1:18–25; 2; Luka 2; 3 Nefi 1:4–22; “Away in a Manger,” Nyimbo za Dini, na. 206.
Yesu Kristo ni Mkombozi wa ulimwengu.
Sababu kubwa ya kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu Kristo ni kwa sababu ya dhabihu Yake ya kulipia dhambi. Kwa sababu ya dhabihu hiyo, Yeye anaweza kutuokoa sote kutoka katika dhambi na mauti, kutufariji katika mateso, na kutusaidia “tukamilishwe ndani Yake”.(Moroni 10:32). Umejifunza nini kutoka kwenye Kitabu cha Mormoni mwaka huu kuhusu uwezo wa Mwokozi wa kukukomboa? Je, kuna matukio au mafundisho yoyote yanayojitokeza kwako? Fikiria kile ambacho vifungu vifuatavyo vinakifundisha kuhusu huduma ya Mwokozi ya ukombozi: 2 Nefi 2:6; Alma 7:7–13; 11:40; na Helamani 5:9; 14:16–17. Je, unahisi kutiwa msukumo kufanya kipi ili kumwonesha Yeye shukrani zako?
Kitabu cha Mormoni hushuhudia juu ya Yesu Kristo.
“Ushuhuda Mwingine wa Yesu Kristo” ni zaidi ya kichwa kidogo cha habari cha Kitabu cha Mormoni; ni kauli ya lengo lake takatifu. Tafakari kile unachojifunza kutokana na maandiko yafuatayo kuhusu misheni ya Kitabu cha Mormoni ya kushuhudia juu ya Kristo: 1 Nefi 6:4; 19:18; na 2 Nefi 25:23, 26; 33:4, 10.
Fikiria kuandika katika shajara jinsi gani kujifunza Kitabu cha Mormoni mwaka huu kumekuleta karibu zaidi na Kristo. Ushawishi ufuatao ungeweza kusaidia:
-
“Kitu fulani nilichojifunza au kuhisi kuhusu Mwokozi mwaka huu kilikuwa …”
-
“Kujifunza kuhusu Mwokozi katika Kitabu cha Mormoni kulibadilisha jinsi ambavyo mimi …”
-
“Mtu ninayempenda sana [au hadithi] katika Kitabu cha Mormoni ilinifundisha kwamba Mwokozi …”
Pengine kuna mtu ambaye angebarikiwa kujua jinsi unavyohisi kuhusu Kitabu cha Mormoni. Ni kwa jinsi gani ungeweza kuelezea uzoefu na ushuhuda wako? Ungeweza kuhisi kutiwa msukumo kutoa nakala kama zawadi ya Kristmas. Aplikesheni ya Kitabu cha Mormoni hufanya iwe rahisi kushiriki.
Askofu Gérald Caussé aliorodhesha kweli kadhaa kutoka katika Kitabu cha Mormoni kuhusu Yesu Kristo (ona “Shahidi Hai wa Kristo Aliye Hai,” Liahona, Mei 2020, 39–40. Ungeweza kuangalia orodha yake na kutafakari jinsi kila moja ya kweli hizi zilivyobadili—au zingeweza kubadili—maisha yako.
Ona pia Mada za Injili, “Kitabu cha Mormoni,” Maktaba ya Injili.
Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto
Yesu Kristo ni zawadi ya Baba wa Mbinguni kwangu.
-
Ili kuwasaidia watoto wako wafokasi juu ya zawadi ambayo Baba wa Mbinguni alitupatia kwa kumtuma Mwana Wake, unaweza kuifunga picha ya Yesu Kristo kama Zawadi ya Krismasi. Wewe na watoto wako mngeweza kuzungumza kuhusu zawadi pendwa za Krismasi ulizopokea au unazotumaini kupokea. Kisha wangeweza kuifungua picha ya Kristo na kujadili jinsi ambavyo Yeye amekua zawadi ya thamani kwetu sisi. Wimbo kama “He Sent His Son” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 34–35) ungeweza kuongezea kwenye mazungumzo haya. Wasaidie watoto wako wapate virai katika wimbo huu ambavyo vinaelezea baraka tulizonazo kwa sababu ya kuzaliwa kwa Yesu.
Yesu Kristo alizaliwa kuwa Mwokozi wangu.
-
Watoto wako wangeweza kufurahia kushiriki nawe kile ambacho wanakijua kuhusu kuzaliwa kwa Yesu. Kitabu cha Sanaa za Injili kina picha kadhaa ambazo zinaweza kusaidia kueleza hadithi hii (ona na. 28, 29, 30, 31). Ungeweza pia kutazama picha zinazoonesha maisha ya Mwokozi na dhabihu ya kulipia dhambi. Je, ni kwa nini Baba wa Mbinguni alimtuma Yesu Kristo?
-
Watoto wako pia wangeweza kufurahia kuchora picha zao wenyewe za kuzaliwa kwa Yesu na huduma Yake. Pengine wangeweza kuchora kile kilichoelezwa katika 1 Nefi 11:13–23; Mosia 2: 5– 10; Helamani 14:1–13; na 3 Nefi 3:4–22. Kisha wangeweza kushiriki nawe kile ambacho picha zao zinafundisha kuhusu Yesu Kristo.
-
Ili kusisitiza kwamba Biblia na Kitabu cha Mormoni vyote vinafundisha juu ya kuzaliwa kwa Yesu, ungeweza kuorodhesha matukio yaliyoelezwa katika Luka 2:4–14; Mathayo 2:1–2; na 3 Nefi 1:15, 19–21. Kisha watoto wako wangechunguza maandiko haya ili kubainisha ni matukio yapi yalitokea Bethlehemu, Amerika, au kote. Kwa nini tuna shukrani kuwa na Kitabu cha Mormoni kama shahidi wa pili wa kuzaliwa kwa Yesu?
Kitabu cha Mormoni kinashuhudia juu ya Yesu Kristo.
-
Wewe na watoto wako mnapohitimisha kujifunza kwenu Kitabu cha Mormoni mwaka huu, ingekuwa wakati mzuri wa kushiriki ninyi kwa ninyi hadithi zenu pendwa au vifungu kutoka katika kitabu hiki kitakatifu. Kuangalia baadhi ya picha katika Njoo, Unifuate au Hadithi za Kitabu cha Mormoni kungeweza kuwasaidia watoto wako wakumbuke kile ambacho wamejifunza mwaka huu. Wasaidie waone kitu ambacho hadithi hizi zinatufundisha kuhusu Yesu Kristo.
-
Ungeweza pia kuwapa watoto wako picha ya Yesu au waruhusu wachore picha zao wenyewe. Waalike wanyanyue juu picha zao kila mara wanaposikia jina la Kristo wakati unaposoma 2 Nefi 25:23, 26. Shuhudia kwamba Kitabu cha Mormoni kiliandikwa ili kutusaidia “tuamini katika Kristo” (2 Nefi 25:23).