Njoo, Unifuate
Desemba 16–22: “Mje kwa Kristo, na Mkamilishwe Ndani Yake.” Moroni 10


“Desemba 16–22: ‘Mje kwa Kristo, na Mkamilishwe Ndani Yake.’ Moroni 10,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: Kitabu cha Mormoni 2024 (2023)

“Desemba 16–22. Moroni 10,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2024 (2023)

Yesu akiwatokea Wanefi

Kwamba Muweze Kufahamu, na Gary L. Kapp

Desemba 16–22: “Mje kwa Kristo, na Mkamilishwe Ndani Yake”

Moroni 10

Kitabu cha Mormoni kinaanza na ahadi ya Nefi kutuonesha kwamba “huruma nyororo za Bwana ziko juu ya wale ambao amewachagua, kwa sababu ya imani yao” (1 Nefi 1:20). Kitabu kinatamatisha kwa ujumbe sawa na huo kutoka kwa Moroni: “Tukumbuke jinsi vile Bwana amekuwa na huruma” (Moroni 10:2–3). Ni mifano ipi ya huruma ya Bwana umeiona katika Kitabu cha Mormoni? Ungeweza kufikiria njia ya huruma ambayo kupitia hiyo Mungu aliiongoza familia ya Lehi nyikani na kuwavusha katika yale maji makuu, huruma nyororo aliyomuonesha Enoshi wakati nafsi yake ilipopata njaa ya msamaha au huruma aliyomuonesha Alma, adui mkali wa Kanisa ambaye aligeuka na kuwa mmoja wa watetezi shupavu wa Kanisa. Au mawazo yako yanaweza kugeukia huruma ambayo Mwokozi aliyefufuka aliionesha kwa watu wakati alipowaponya wagonjwa wao na kuwabariki watoto wao wadogo. Pengine cha muhimu zaidi, yote haya yanaweza kukukumbusha wewe “jinsi Bwana alivyo mwenye huruma” kwako, kwani Kitabu cha Mormoni kiliandikwa kumwalika kila mmoja wetu apokee huruma ya Mungu—mwaliko unaodhihirishwa kwa urahisi katika ujumbe wa buriani wa Moroni, “Mje kwa Kristo na mkamilishwe ndani yake” (Moroni 10:32).

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani

Moroni 10:3–7

ikoni ya seminari
Ninaweza kujua ukweli wa mambo yote kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.

Ahadi iliyoko katika Moroni 10:3–7 imebadilisha maisha ya mamilioni ya watu kote ulimwenguni. Je, ni kwa jinsi gani imebadili maisha yako? Unaposoma Moroni 10:3–7, fikiria kusoma kwa uangalifu zaidi kuliko vile ambavyo umefanya hapo awali. Unaweza kuchunguza kila kirai, ukijiuliza maswali kama haya: Hiki kina maana gani? Ni kwa jinsi gani ninaweza kufanya hili vyema zaidi? Ni uzoefu upi nimeupata kutokana na hili?

Unapotafakari uchunguzi wako binafsi wa ukweli wa kiroho, ingeweza kuwa yenye msaada kujifunza jinsi wengine walivyopata ukweli kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Mzee Mathias Held alieleza uzoefu wake kama muumini mpya wa Kanisa (ona “Kutafuta Maarifa Kupitia Roho,” Liahona, Mei 2019, 31–33). Mzee David F. Evans alieleza uzoefu wake kama mtu aliyelelewa katika Kanisa na bado alikuwa na maswali (ona “Ukweli wa Mambo Yote,” Liahona, Nov. 2017, 69–70). Fikiria kusoma mojawapo au zaidi ya jumbe hizi na uandike kitu chochote unachojifunza kutokana na uchunguzi wako kwa ajili ya ukweli ambao umekusaidia kwenye ukweli wako mwenyewe.

Ungeweza pia kuchunguza kitu ambacho Mungu amekifundisha kuhusu ukweli kwa kusoma baadhi ya vifungu katika Mwongozo wa Maandiko, “Ukweli” (Maktaba ya Injili). Ni maandiko yapi yanaonekana kuwa yenye kuleta utambuzi maalumu kwako? Pengine ungeweza kuchagua andiko moja la kushiriki na mtu mwingine ambaye pia anatafuta ukweli kupitia Roho.

Ona pia Henry B. Eyring, “Imani ya Kuuliza na Kutenda,” Liahona, Nov. 2021, 74–76; “Mwache Roho Alinde,” Nyimbo za Dini, na. 75; Mada za Injili, “Seek Truth and Avoid Deception,” Maktaba ya Injili.

Andika Misukumo. Kuwa mwongofu kwenye injili ya Yesu Kristo humaanisha vyote kujua na kuishi injili. Una uwezekano mkubwa zaidi wa kutenda juu ya kile ulichojifunza kama unakiandika. Kama unafundisha, waalike watu unao wafundisha waandike misukumo yao ya kiroho.

Moroni 10:8–25

Mungu amenipa karama za kiroho.

Kuna njia nyingi ambazo mtu anaweza “[kukataa] … karama za Mungu” (Moroni 10:8). Baadhi ya watu hawakubali kuwa karama hizi zipo. Wengine wanazikataa karama zao kwa kuzipuuza au kushindwa kuzikuza. Unaposoma Moroni 10:8–25, tafuta kweli ambazo zitakusaidia ugundue karama zako za kiroho na uzitumie kuwabariki watoto wa Mungu. Maswali kama haya yanaweza kusaidia: Karama za kiroho ni zipi? Zinatolewa kwa akina nani? Kwa nini zinatolewa? Ni kwa jinsi gani tunazipokea? Je, unaweza kufikiria mifano ya watu wakitumia karama zilizoorodheshwa katika Moroni 10:9–16?

Moroni 10:30–33

Ninaweza kukamilishwa kupitia neema ya Yesu Kristo.

Ushauri wa Moroni “mje kwa Kristo” unajumuisha zaidi ya kujifunza juu ya Kristo na kumfikiria Yeye. Badala yake, huu ni mwaliko wa kuja kwa Kristo katika fasili kamili iwezekanavyo—kuwa jinsi Yeye alivyo. Unaposoma Moroni 10:30–33, weka akilini vifungu vya maneno vinavyokusaidia uelewe maana ya kuja kwa Kristo, jinsi inavyofanywa iwezekane, na matokeo ya kufanya hivyo.

Rudi nyuma kwenye kujifunza kwako Kitabu cha Mormoni mwaka huu, na utafakari kitu ambacho umehisi na kujifunza kuhusu Yesu Kristo. Kwa mfano, ni kwa jinsi gani Kitabu cha Mormoni kimekusaidia wewe uje Kwake? Je, ni kwa jinsi gani kimekusaidia utegemee kikamilifu neema Yake? Je, ni kwa jinsi gani kimekusaidia “kutokataa” nguvu ya Mwokozi? Fikiria kushiriki ushahidi wako mwenyewe juu ya Kitabu cha Mormoni na mtu ambaye anahitaji kuusikia, ikijumuisha wapendwa na marafiki ambao wanaweza kuwa hawajui ujumbe wake.

Ona pia “Moroni Invites All to Come unto Christ” (video), Maktaba ya Injili.

Kwa mawazo zaidi, ona toleo la mwezi huu la Liahona na magazeti ya Kwa ajili ya Nguvu kwa Vijana.

Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto

Moroni 10:3–4

Ninaweza kujua mimi binafsi kwamba Kitabu cha Mormoni ni cha kweli.

  • Ni kwa jinsi gani unaweza kuwasaidia watoto wako wakubali mwaliko wa Moroni wa kumuuliza Mungu ikiwa Kitabu cha Mormoni ni cha kweli? Fikiria kuwapa vipande vya karatasi vilivyo na maneno Soma, Kumbuka, Tafakari, na Omba yaliyoandikwa juu yake. Watoto wako wangeweza kupata maneno haya katika Moroni 10:3–4. Je, sisi tunapaswa tusome, tukumbuke, tutafakari na tuombe nini ili tupate au tuimarishe shuhuda zetu juu ya Kitabu cha Mormoni? Watoto wako wangeweza pia kutafuta mifanano kati ya mistari hii na wimbo “Search, Ponder, and Pray” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 109).

  • Watoto wako wangeweza kutumia picha iliyo mwishoni mwa muhtasari huu kuzungumza kuhusu Moroni akizika mabamba ya dhahabu (Mlango wa 54: Ahadi ya Kitabu cha Mormoni,” Hadithi za Kitabu cha Mormoni, 156). Watoto wadogo zaidi wanaweza kufurahia kujifanya kuwa Moroni akiandika kwenye mabamba na kuyazika. Shirikini kila mmoja na mwenzake shuhuda zenu juu ya Kitabu cha Mormoni.

Moroni 10:8–19

Baba wa Mbinguni hunipa karama za kiroho.

  • Ili kuwafundisha watoto wako kuhusu karama za kiroho, ungeweza kuandika namba 9 hadi 16 kwenye vipande tofauti vya karatasi na ufunge kila karatasi kama zawadi. Watoto wako wangeweza kufanya zamu kufungua zawadi, wakisoma mistari kutoka Moroni 10:9–16 ambayo inahusiana na namba na kutambua kila karama ya kiroho. Ungeweza kuzungumza kuhusu jinsi Baba wa Mbinguni anavyotutaka tutumie karama hizi ili kuwabariki watoto Wake. Ungeweza pia kuwasaidia watoto wako watambue karama ambazo Baba wa Mbinguni amewapatia.

Moroni 10:32–33

Yesu Kristo anataka nije Kwake.

  • Je, watoto wako wanajua kile inachomaanisha “kuja kwa Kristo”? Pengine ungeweza kusoma Moroni 10:32 na kuwaalika warudie kifungu hicho cha maneno pamoja nawe. Wangeweza kisha kufunga macho yao huku wewe ukiweka picha ya Yesu mahali fulani katika chumba. Kisha waruhusu wafumbue macho yao, watafute picha hiyo, na wakusanyike kuizunguka na wazungumzie jinsi ambavyo tunaweza kuja kwa Kristo. Pengine ingekuwa msaada kuandika swali Inamaanisha nini kuja kwa Kristo? Wasaidie wachunguze Moroni 10:32–33 ili kupata majibu yamkini ( ona pia Mafundisho na Maagano 1: 3– 4). Shirikianeni kuorodhesha kile ambacho Kristo anataka tufanye na kitu ambacho Yeye anaahidi kufanya kwa ajili yetu.

  • Pengine watoto wako wangefurahia kutengeneza na kupamba beji zenye umbo la moyo zinazosema “Nampenda Mungu kwa uwezo wangu wote, akili zangu zote, na nguvu zangu zote” (onaMoroni 10:32). Wanapofanya hivyo, zungumza nao kuhusu jinsi ambavyo sisi tunamwonesha Mungu kwamba tunampenda.

Kwa ajili ya mawazo zaidi, ona toleo la mwezi huu la gazeti la Rafiki.

Moroni akizika mabamba ya dhahabu

Kabla ya kuzika kumbukumbu, Moroni alitualika “tukumbuke jinsi gani Bwana amekuwa na huruma” (Moroni 10:3).