Mkutano Mkuu
Imani ya Kuuliza na Kisha Kutenda
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2021


Imani ya Kuuliza na Kisha Kutenda

Imani katika Yesu Kristo ni msingi wa kupokea ufunuo wa ukweli.

Kaka na dada zangu wapendwa, Nashukuru kwa fursa hii ya kuzungumza nanyi katika kikao cha Jumamosi Jioni cha mkutano mkuu. Katika utangulizi wake kwenye mkutano asubuhi ya leo, Rais Russell M. Nelson alisema kwamba “ufunuo halisi kwa ajili ya maswali katika moyo wako utafanya mkutano huu kuwa wenye thawabu na usiosahaulika. Kama bado hujatafuta kuhudumiwa na Roho Mtakatifu ili akusaidie kusikia kile Bwana angetaka ukisikie katika siku hizi mbili, nakualika kufanya hivyo sasa.”1 Nimetafuta baraka hiyo ninapokuwa najitayarisha kupokea ufunuo kwa ajili ya mkutano huu pamoja nanyi. Sala yangu ya dhati ni kwamba muweze kupokea ufunuo kutoka kwa Mungu.

Njia ya kupokea ufunuo kutoka kwa Mungu haijabadilika kutoka siku za Adamu na Hawa. Imekuwa vivyo hivyo kwa watumishi wote walioitwa na Bwana kutoka mwanzo mpaka siku ya leo. Ndivyo ilivyo kwenu na kwangu. Hili hufanyika daima kwa kuonyesha imani.2

Kijana Joseph Smith alikuwa na imani ya kutosha kumwuliza swali Mungu, akiamini kwamba Mungu angejibu hitaji lake la dhati. Jibu ambalo lilikuja lilibadili ulimwengu. Alitaka kujua kanisa gani la kujiunga ili kuweza kusafishwa dhambi. Jibu alilolipata lilimtia moyo kuendelea kuuliza maswali mazuri zaidi na kutenda juu ya mwendelezo wa ufunuo endelevu ambao ndio ulikuwa kwanza umeanza.3

Uzoefu wako unaweza kuwa sawa na huo katika mkutano huu. Una maswali ambayo unatafuta majibu. Unayo angalau imani ya kutosha ya kutegemea kwamba utapokea majibu kutoka kwa Bwana kupitia watumishi Wake.4 Hutakuwa na fursa ya kuuliza kwa sauti kwa ajili ya majibu kutoka kwa wanenaji, bali unaweza kumwuliza Baba yako mwenye upendo katika sala.

Ninajua kutokana na uzoefu kwamba majibu yatakuja sawa na mahitaji yako na maandalizi yako ya kiroho. Kama unahitaji jibu ambalo ni muhimu kwa ustawi wako wa milele au ule wa wengine, jibu huenda litakuja. Lakini hata hivyo, unaweza kupokea—kama ilivyokuwa kwa Joseph Smith—jibu la kuwa na subira.5

Kama imani yako katika Yesu Kristo imepelekea kwenye moyo kulainishwa kupitia matokeo ya Upatanisho Wake, utakuwa na uwezo zaidi wa kuhisi minong’ono ya Roho katika jibu kwa sala zako. Uzoefu wangu binafsi ni kwamba sauti ndogo tulivu—ambayo ni halisi—ni dhahiri na yenye kutambulika katika akili yangu wakati ninapohisi utulivu moyoni na utii kwa mapenzi ya Mungu. Hisia hiyo ya unyenyekevu inaweza kuelezwa vizuri zaidi kama “Sio mapenzi yangu, bali Yako yafanyike.”6

Mchakato huu wa ufunuo ndio sababu utawasikia wanenaji wanafundisha katika mkutano huu kile kinachoitwa mafundisho ya Kristo.7 Ufunuo unakuja kwetu kwa kiwango ambacho tumetafuta kuchukua mafundisho ya Kristo ndani ya mioyo yetu na kuitekeleza injili hiyo katika maisha yetu.

Unakumbuka kutoka katika Kitabu cha Mormoni kwamba Nefi alitufundisha kwamba imani katika Yesu Kristo ni msingi wa kupokea ufunuo wa ukweli na msingi wa kuwa na ujasiri kwamba tunafuata mwelekeo wa Mwokozi. Nefi aliandika maneno yafuatayo karne nyingi kabla ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo duniani:

“Malaika wanazungumza kwa uwezo wa Roho Mtakatifu; kwa hivyo, wanazungumza maneno ya Kristo. Kwa hivyo, niliwaambia, shiriki maneno ya Kristo; kwani tazama, maneno ya Kristo yatawaelezea vitu vyote mnavyostahili kutenda.

“Kwa hivyo, na sasa baada ya kuzungumza maneno haya, kama hamwezi kuyafahamu, ni kwa sababu hamuombi, wala kubisha; kwa hivyo, hamjaletwa kwenye nuru, lakini lazima mwangamie gizani.

“Kwani tazama, tena nawaambia kwamba kama mtaingia kwa njia hiyo, na kupokea Roho Mtakatifu, atawaonyesha vitu vyote ambavyo mnastahili kutenda.

“Tazameni, haya ndio mafundisho ya Kristo, na hakutakuwa na mafundisho mengine yatakayotolewa hadi atakapojidhihirisha kwenu katika mwili. Na atakapojithirihisha kwenu katika mwili, mambo ambayo atayasema kwenu mtachunguza na kufanya vile vitu atakavyowaambia.”8

Bwana atasema mambo kupitia watumishi Wake kwenu na kwangu leo na siku zijazo. Atatuambia vitu gani tunapaswa kufanya.9 Mwokozi hatapaza sauti ya kukuamrisha wewe na mimi. Jinsi Yeye Alivyomfundisha Eliya:

“Na alisema, Nenda, na simama juu ya mlima mbele ya Bwana. Na, tazama, Bwana alipita, na upepo mkubwa na wenye nguvu ulipasua milima, na kuyavunja vunja mawe mbele ya Bwana; bali Bwana hakuwemo ndani ya upepo: na baada ya upepo tetemeko la nchi; bali Bwana hakuwemo ndani ya tetemeko la nchi:

“Na baada ya tetemeko la nchi moto; bali Bwana hakuwemo katika moto: na baada ya moto sauti ndogo tulivu.”10

Ili kuweza kusikia sauti hiyo kutakuja kutokana na imani yetu Kwake. Tukiwa na imani ya kutosha, tutauliza uelekeo kwa nia ya kwenda na kufanya chochote Anachotaka.11 Tutakuwa tumekuza imani kujua kwamba chochote Anachotaka kitabariki wengine, na kwamba tunaweza kutakaswa katika mchakato kwa sababu ya upendo Wake kwetu sisi.

Wakati imani yetu katika Yesu Kristo itatuongoza kumwomba Baba majibu, imani hiyo pia itaweza kuleta mguso laini wa kutosha wa Mwokozi ili tuweze kusikia maelekezo Yake na kuamua na kwa furaha kutii. Kisha tutaimba maneno ya wimbo wa Kanisa kwa shangwe, hata wakati kazi ni ngumu: “Kazi tamu, Mungu wangu, Mfalme wangu.”12

Tunavyokuwa na zaidi ya mafundisho ya Kristo katika maisha na mioyo yetu, tunahisi zaidi upendo mkuu na huruma kwa ajili ya wale ambao kamwe hawajapata baraka za imani katika Yesu Kristo au wanajitahidi kuidumisha. Ni vigumu kutii amri za Bwana bila imani na tumaini Kwake. Wakati baadhi wanapoteza imani yao kwa Mwokozi, wanaweza hata kushambulia ushauri Wake, wakiita jema kuwa ovu na ovu kuwa jema.13 Ili kuepuka kosa hili, ni muhimu sana kwamba ufunuo binafsi tunaopokea uwe sambamba na mafundisho ya Bwana na manabii Wake.

Akina kaka na dada, inahitaji imani ili kuwa mtiifu kwa amri za Bwana. Inahitaji imani katika Yesu Kristo ili kuwatumikia wengine kwa ajili Yake. Inahitaji imani ili kwenda kufundisha injili Yake na kuitoa kwa watu ambao hawawezi kuhisi sauti ya Roho au wanaweza hata kukanusha ukweli wa ujumbe. Bali tunapotumia imani yetu katika Kristo—na kumfuata nabii Wake anayeishi—imani huongezeka ulimwenguni kote. Kwa sababu ya teknolojia, labda wengi wa watoto wa Mungu watasikia na kutambua neno la Mungu wikiendi hii kuliko siku mbili zozote katika historia.

Kwa ongezeko la imani kwamba hili ni Kanisa la Bwana na ufalme duniani, waumini zaidi wanalipa zaka na wanachanga kusaidia wale wenye mahitaji, hata wakati waumini hao wanakabiliana na majaribu yao wenyewe. Kwa imani kwamba wameitwa na Yesu Kristo, wamisionari ulimwenguni kote wamepata njia za kuinuka juu ya changamoto zilizoletwa na janga la ulimwengu, wakifanya hivyo kwa ujasiri na furaha. Na katika juhudi zao za ziada, imani yao imekuwa imara.

Upinzani na majaribu vimekuwa kwa muda mrefu kitalu kwa ajili ya ukuaji wa imani. Hiyo imekuwa kweli siku zote, hususani tangu mwanzo wa Urejesho na kuanzishwa kwa Kanisa la Bwana.14

Kile Rais George Q. Cannon alichosema muda mrefu uliopita ni cha kweli leo na kitakuwa hivyo mpaka Mwokozi atapokuja kibinafsi kuongoza Kanisa Lake na watu Wake: “Utii kwa injili unaleta [watu] kwenye ukaribu zaidi na mahusiano ya ndani na Bwana. Unaweka muungano wa karibu kati ya binadamu duniani na Muumbaji wetu Mkuu mbinguni. Unaweka kwenye akili ya binadamu hisia za ujasiri timilifu kwa Mwenyezi na utayari Wake wa kusikiliza na kujibu maombi ya wale wanaomwamini Yeye. Katika nyakati za majaribu na shida, ujasiri huu ni zaidi ya thamani. Tatizo laweza kuja juu ya mtu binafsi au juu ya watu, maafa yanaweza kutishia na kila tumaini la binadamu linaweza kuonekana kupinduliwa, bado, pale [watu] wanapokuwa wamenufaika na faida ambayo utii kwenye Injili unaleta, wana sehemu ya uhakika ya kusimama; miguu yao ipo juu ya mwamba ambao hauwezi kuondolewa.”15

Ni ushuhuda wangu kwamba mwamba ambao juu yake tunasimama ni ushahidi wetu kwamba Yesu ni Kristo, kwamba hili ni Kanisa Lake ambalo yeye binafsi Analiongoza, na kwamba Rais Russell M. Nelson ni nabii Wake anayeishi leo.

Rais Nelson anatafuta na kupokea maelekezo kutoka kwa Bwana. Yeye ni mfano kwangu wa kutafuta mwelekeo huo na kuwa na nia ya kuufuata. Nia hiyo hiyo ya kuwa mtiifu kwa maelekezo ya Bwana ipo ndani ya mioyo wa wale wote waliozungumza au watazungumza, kusali, au kuimba katika mkutano huu mkuu wa Kanisa Lake.

Ninaomba kwamba wale duniani kote wanaoangalia au kusikiliza mkutano huu watapata hisia ya upendo wa Bwana kwa ajili yao. Baba wa Mbinguni amejibu sala yangu kwamba niweze kuhisi angalau sehemu ndogo ya upendo wa Mwokozi kwa ajili yenu na upendo Wake kwa ajili ya Baba Yake wa Mbinguni, ambaye pia ni Baba yetu wa Mbinguni.

Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo yu hai. Yeye ni Mwokozi na Mkombozi wetu. Hili ni kanisa Lake. Yeye ndio mkuu wa Kanisa. Yeye, pamoja na Baba Yake wa Mbinguni, walimtokea Joseph Smith katika kijisitu cha miti huko New York. Injili ya Yesu Kristo na ukuhani Wake vilirejeshwa kupitia wajumbe wa mbinguni.16 Ni kwa nguvu za Roho Mtakatifu, Ninajua kwamba hiyo ni kweli.

Ninaomba kwamba muweze kuwa na ushahidi kama huo. Ninaomba kwamba mtamwomba Baba wa Mbinguni kwa ajili ya imani katika Yesu Kristo mnayohitaji ili kufanya na kutii maagano ambayo yatamruhusu Roho Mtakatifu kuwa mwenza wenu daima. Ninawaachia upendo wangu na ushahidi wangu kweli katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.

Chapisha