Hekalu na Msingi Wako wa Kiroho
Wakati mabadiliko ya aina yoyote yanapotokea katika maisha yako, mahali salama zaidi pa kuwa kiroho ni kuishi ndani ya maagano yako ya hekaluni!
Kaka na dada zangu wapendwa, ninafurahi kuwa nanyi asubuhi hii ili kushiriki hisia za moyo wangu.
Kama mnavyojua, tunafanya marekebisho makubwa kwenye Hekalu la kihistoria la Salt Lake. Mradi huu mgumu unahusisha uimarishaji mkubwa wa msingi wake wa asili, ambao umedumu kwa zaidi ya karne. Lakini hekalu hili lazima lisimame kwa muda mrefu zaidi. Mwishoni mwa mwezi Mei, nilikagua maendeleo ya mradi huu mkubwa. Nilifikiri mngeshukuru kuona kile ambacho mimi na mke wangu Wendy tulikiona. Nadhani mtaona kwa nini wimbo “Msingi Imara”1 umekuja kuwa na maana mpya kwetu.
Video kutoka eneo la marekebisho la Hekalu la Salt Lake: “Tunatazama msingi wa asili wa Hekalu la Salt Lake. Nimesimama juu ya eneo ambapo chini yake kulikuwa na Chumba cha Bustani. Ninapotazama ustadi wa jengo hili lote, ninashangazwa kwa kile waanzilishi walichoweza kufanikisha. Ninastaajabu kabisa ninapozingatia kwamba walijenga hekalu hili la kuvutia kwa vifaa na utaalamu uliokuwepo kipindi hicho cha zaidi ya karne iliyopita.
“Miongo hii mingi baadaye, hata hivyo, kama tutakagua msingi kwa umakini, tunaweza kuona madhara ya mmomonyoko, mapungufu katika kazi ya awali ya mawe na mapungufu ya uimara katika kazi ya ujenzi.
“Sasa ninaposhuhudia kile wahandisi wa sasa, wasanifu majengo na wataalamu wa ujenzi wanachoweza kufanya ili kuimarisha msingi huo wa asili, hakika ninastaajabu. Kazi yao inashangaza!
“Msingi wa jengo lolote, hasa kubwa kama hili, lazima uwe imara na wenye uthabiti vya kutosha kustahimili matetemeko, mmomonyoko, pepo kali na mipangilio isiyozuilika ambayo inaathiri majengo yote. Kazi ngumu ya uimarishaji inayoendelea sasa italiimarisha hekalu hili takatifu kwa msingi ambao unaweza na utaweza kustahimili mitihani ya nyakati zote.”
Tunafanya kila juhudi inayowezekana ili kulipa hekalu hili la heshima, ambalo limezidi kuwa dhaifu, msingi ambao utastahimili nguvu za asili mpaka kwenye milenia. Katika hali sawa na hiyo, ni muda sasa kwamba kila mmoja achukue hatua za ziada—huenda hatua ambazo hatujawahi kuzichukua hapo kabla—ili kuimarisha misingi yetu binafsi ya kiroho. Nyakati za kipekee huhitaji hatua za kipekee.
Akina kaka na dada zangu wapendwa, hizi ni siku za mwisho. Kama mimi na wewe tunapaswa kustahimili hatari na mashinikizo yajayo, ni muhimu kwamba kila mmoja awe na msingi imara wa kiroho uliojengwa juu ya mwamba wa Mkombozi wetu, Yesu Kristo.2
Kwa hivyo ninawauliza kila mmoja wenu, Msingi wako ni imara kiasi gani? Na ni uimarisho gani unahitajika kwenye ushuhuda na uelewa wako wa injili?
Hekalu ni kitovu cha kuimarisha imani yetu na uimara wa kiroho kwa sababu Mwokozi na mafundisho Yake ndiyo kiini hasa cha hekalu. Kila kitu kinachofundishwa ndani ya hekalu, kupitia maelekezo na kupitia Roho, huongeza uelewa wetu wa Yesu Kristo. Ibada Zake muhimu hutuunganisha Kwake kupitia maagano matakatifu ya ukuhani. Kisha, tunapotunza maagano yetu, Yeye hutubariki kwa nguvu Yake ya uponyaji na uimarisho.3 Na lo, ni kiasi gani tutahitaji nguvu Yake katika siku zijazo.
Tumeahidiwa kwamba “kama tumejitayarisha hatutaogopa.”4 Hakikisho hili lina matokeo makubwa leo. Bwana ametangaza kwamba mbali na changamoto kubwa za leo, wale wanaojenga misingi yao juu ya Yesu Kristo, na wamejifunza jinsi ya kuvuta nguvu Yake, hawahitaji kujisalimisha kwenye hofu za kipindi hiki.
Ibada na maagano ya hekaluni ni vya kale. Bwana alimwamuru Adamu na Hawa kusali, kufanya maagano na kutoa sadaka.5 Ndio, “Wakati wowote ambao Bwana amekuwa na watu duniani ambao watatii neno Lake, wameamriwa kujenga mahekalu.”6 Mafundisho yetu ya msingi yamejazwa na marejeleo ya mafundisho ya hekalu, mavazi, lugha na mengine mengi.7 Kila kitu tunachoamini na kila ahadi ambayo Bwana ameifanya kwa watoto Wake wa agano huja pamoja hekaluni. Katika kila zama, hekalu limesisitiza ukweli wa thamani kwamba wale wanaofanya maagano na Mungu na kuyatunza wao ni watoto wa agano.
Hivyo, katika nyumba ya Bwana, tunaweza kufanya maagano kama ambayo Ibrahimu, Isaka na Yakobo walifanya na Mungu. Na tunaweza kupokea baraka kama walizopokea wao!
Mahekalu yamekuwa sehemu ya kipindi hiki cha maongozi ya Mungu toka enzi za kale.8 Eliya alitoa funguo za mamlaka ya kuunganisha kwa Joseph Smith ndani ya Hekalu la Kirtland. Utimilifu wa ukuhani ulirejeshwa ndani ya Hekalu la Nauvoo.9
Mpaka kuuawa kwake, Joseph Smith aliendelea kupokea ufunuo ambao uliendeleza urejesho wa ibada za endaumenti na kuunganisha.10 Alitambua, hata hivyo, kwamba marekebisho ya ziada yalihitajika. Baada ya kutoa endaumenti kwa Brigham Young mnamo Mei 1842, Joseph alimwambia Brigham, “Hili halijapangiliwa vyema, lakini tumefanya kadiri tuwezavyo katika hali tuliyonayo na ninaomba ulichukue swala hili na upangilie na kuweka mfumo wa ibada hizi zote.”
Kufuatia kifo cha Nabii, Rais Young alisimamia ukamilikaji wa Hekalu la Nauvoo12 na baadaye kujenga mahekalu katika Milki ya Utah. Katika uwekaji wakfu wa ghorofa za chini za Hekalu la St. George, Brigham Young kwa nguvu alitangaza uharaka wa kazi za hekaluni kwa ajili ya wafu aliposema, “Ninapofikiria suala hili, ninataka sauti kubwa na imara iwafahamishe watu mambo haya.”13
Toka wakati huo na kuendelea, ibada za hekaluni mara kwa mara ziliboreshwa. Rais Harold B. Lee alielezea kwa nini mpangilio, sera na hata utolewaji wa ibada za hekaluni huendelea kubadilika ndani ya Kanisa la urejesho la Mwokozi. Rais Lee alisema: “Kanuni za injili ya Yesu Kristo ni takatifu. Hakuna anayebadili kanuni na [mafundisho] ya Kanisa isipokuwa Bwana kwa ufunuo. Lakini njia hubadilika kama mwongozo uliofunuliwa utakuja kwa wale wanaosimamia kwa wakati huo.”14
Fikiria jinsi kuhudumia sakramenti kulivyobadilika kwa miaka sasa. Katika siku za mwanzo, maji ya sakramenti yalikuwa yakitolewa kwa watu katika chombo kimoja kikubwa. Kila mmoja alikunywa kutoka kwenye chombo hicho. Na sasa tunatumia kila mtu kikombe chake. Utaratibu umebadilika, lakini maagano yamebakia yale yale.
Tafakari kweli hizi tatu:
-
Urejesho ni mchakato, sio tukio na utaendelea mpaka Bwana atakapokuja.
-
Lengo la msingi la kukusanya Israeli15 ni kuleta baraka za hekalu kwa watoto waaminifu wa Mungu.
-
Tunapotafuta jinsi ya kufanikisha lengo hilo vizuri zaidi, Bwana hufunua uelewa zaidi. Urejesho endelevu unahitaji ufunuo endelevu.
Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili mara kwa mara wamemuuliza Bwana kama kuna njia nzuri zaidi za kufikisha baraka za hekaluni kwa watoto Wake waaminifu. Tunatafuta mwongozo mara kwa mara wa jinsi ya kuhakikisha usahihi na uendelevu wa maelekezo, maagano na ibada za hekaluni licha ya tofauti za lugha na tamaduni.
Chini ya mwongozo wa Bwana na katika majibu ya maombi yetu, marekebisho ya kiutaratibu yamefanywa hivi karibuni. Yeye ndiye anayewataka ninyi muelewe kwa usahihi mkubwa zaidi kwa nini mnafanya maagano. Yeye ndiye anayewataka ninyi mpokee kikamilifu ibada Zake takatifu. Yeye anataka ninyi mfahamu fursa zenu, ahadi na majukumu. Yeye anataka ninyi mpate utambuzi na uamsho wa kiroho ambao kamwe hamjawahi kuupata. Hili analihitaji kwa wote wanaoenda hekaluni, bila kujali wapi wanaishi.
Mabadiliko ya sasa ya utaratibu wa hekaluni, na mengineyo yatakayofuatia, ni ushahidi endelevu kwamba Bwana analiongoza Kanisa Lake. Yeye hutoa fursa kwa kila mmoja wetu kuegemeza misingi yetu ya kiroho vyema zaidi kwa kuyaweka maisha yetu Kwake na katika ibada na maagano ya hekalu Lake. Unapoleta kibali chako cha hekaluni, moyo uliopondeka na akili ya kutafuta kwenye nyumba ya Bwana ya kujifunza, Yeye atakufunza.
Kama umbali, changamoto za kiafya au vikwazo vingine vitazuia uhudhuriaji wako hekaluni kwa muda, ninakualika kutenga muda maalumu wa kufanyia mazoezi akilini mwako maagano uliyoyafanya.
Kama bado hupendi kuhudhuria hekaluni, nenda mara kwa mara—siyo mara chache. Mruhusu Bwana, kupitia Roho Wake, akufundishe na kukupa msukumo ukiwa huko. Ninakuahidi kwamba baada ya muda, hekalu litakuwa mahala pa usalama, faraja na ufunuo.
Kama ingekuwa inawezekana kwangu kuzungumza na kijana mmoja mmoja, ningewaomba mtafute mwenza ambaye unaweza kuunganishwa naye hekaluni. Mnaweza kujiuliza hili litaleta tofauti gani kwenye maisha yenu. Ninawaahidi hili litaleta tofauti yote! Mnapofunga ndoa hekaluni na kurejea mara kwa mara, mtaimarishwa na kuongozwa katika maamuzi yenu.
Kama ningeweza kuzungumza na kila mume na mke ambao bado hawajaunganishwa hekaluni, ningewasihi wachukue hatua stahiki ili kupokea ibada hiyo ya juu, yenye kubadili maisha.16 Je, hili litaleta tofauti yoyote? Ni kama tu mnataka kuendelea milele na kuwa pamoja milele. Kutamani tu kuwa pamoja milele hakutafanya hilo liwezekane. Hakuna sherehe nyingine yoyote au mkataba wowote utakaofanya hilo liwezekane.17
Kama ningeweza kuzungumza na kila mwanamume au mwanamke ambaye anatamani ndoa lakini bado hawajapata wenza wao wa milele, ningewashauri msisubiri mpaka ndoa ili kupokea endaumenti katika nyumba ya Bwana. Anza kujifunza sasa na kupata uzoefu wa kile inachomaanisha kukingwa kwa nguvu ya ukuhani.
Na kwenu ninyi ambao mmefanya maagano ya hekaluni, ninawasihi mtafute—kwa sala na kila mara—kuelewa maagano na ibada za hekaluni.18 Milango ya kiroho itafunguka. Utajifunza jinsi ya kugawa pazia kati ya mbingu na dunia, jinsi ya kuomba malaika wa Mungu wakuhudumie na namna nzuri ya kupokea mwongozo kutoka mbinguni. Juhudi zako zenye bidii za kufanya hayo zitaimarisha na kutia nguvu msingi wako wa kiroho.
Akina kaka na dada zangu wapendwa, wakati marekebisho katika Hekalu la Salt Lake yatakapokamilika, hakutakuwa na sehemu salama wakati wa tetemeko katika bonde la Salt Lake zaidi ya ndani ya hekalu hilo.
Vivyo hivyo, wakati mabadiliko ya aina yoyote yanapotokea katika maisha yako, mahali salama zaidi pa kuwa kiroho ni kuishi ndani ya maagano yako ya hekaluni!
Tafadhali mniamini ninaposema kwamba wakati msingi wako wa kiroho unapojengwa kwa uimara juu ya Yesu Kristo, huna haja ya kuogopa. Unapokuwa mkweli kwenye maagano yako uliyoyafanya hekaluni, utaimarishwa kwa nguvu yake. Kisha, wakati matetemeko ya kiroho yajapo, utaweza kusimama imara kwa sababu msingi wako wa kiroho ni imara na usioyumba.
Ninawapenda, wapendwa akina kaka na akina dada. Kweli hizi ninazijua: Mungu, Baba yetu wa Mbinguni, anataka ninyi mchague kurejea Kwake nyumbani. Mpango Wake wa kuendelea milele siyo mgumu, na unaheshimu haki yako ya kujiamulia. Uko huru kuchagua ni nani unataka uwe—na utakuwa hivyo ukiwa na nani—katika ulimwengu ujao!
Mungu yu hai! Yesu ndiye Kristo! Hili ni Kanisa Lake, lililorejeshwa kukusaidia kutimiza hatma yako ya kiungu. Ninashuhudia hivyo, katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.