Mambo ya Nafsi Yangu
Je, ni vitu gani unavyotafakari? Je, ni mambo gani ni ya muhimu kwako? Je, ni mambo gani ya nafsi yako?
Akina kaka na dada zangu, ninaposimama katika Ukumbi wetu wa Mikutano kwa mara nyingine, ninakumbuka maneno ya Mtume Petro: “Bwana, ni vizuri kwetu kuwa hapa.”1
Mawazo yangu leo yamejikita katika maneno ya nabii Nefi, ambaye aliweka rekodi ya watu wake kufuatia kifo cha Baba Lehi. Nefi aliandika, “Na juu ya haya ninaandika mambo ya roho yangu.”
Nilikuwa nimezoea kuupita mstari huu, nikifikiria neno mambo halikuwa la kuvutia sana au la kiroho, sio kubwa la kutosha kuendana na “roho yangu.” Walakini nimejifunza kwamba neno mambo limetumika katika maandiko mara 2,354.3 Kwa mfano, katika kitabu cha Musa: “Mimi Ndimi Mwanzo na Mwisho, Mungu Mwenyezi; kwa Mzaliwa Wangu wa Pekee niliumba hivi vitu.”4 Na maneno ya Nefi: “Tazama, nafsi yangu hufurahia mambo ya Bwana; na moyo wangu huyatafakari mara kwa mara mambo ambayo nimeyaona na kuyasikia.”5
Maneno ya Nefi yanaibua maswali “Je, ni mambo gani unayoyatafakari?” “Je, ni mambo gani ni ya muhimu kwako?” “Je, ni mambo gani ya nafsi yako?”
Mambo ya roho zetu mara nyingi hufafanuliwa na kuwa ya kina kwa kuuliza maswali.
Wakati wa janga la ulimwengu nimekutana na vijana kutoka kote ulimwenguni katika ibada nyingi, kubwa na ndogo, kupitia matangazo na mitandao ya kijamii, na tukajadili maswali yao.
Joseph Smith wa miaka kumi na nne alikuwa na swali ndani ya nafsi yake, na akamuuliza Bwana. Rais Russell M. Nelson amesisitiza: “Peleka maswali yako kwa Bwana na kwa vyanzo vingine vya kuaminika. Jifunze kwa hamu ya kuamini badala ya kuwa na tumaini kwamba unaweza kupata kasoro katika maisha ya nabii au kasoro kwenye maandiko. Acha kuongeza mashaka yako kwa kuyarudia na … wenye mashaka. Ruhusu Bwana akuongoze kwenye safari yako ya ugunduzi wa kiroho.”6
Vijana mara nyingi wananiuliza ninaamini nini na ni kwa nini ninaamini.
Nakumbuka nilimtembelea msichana mmoja nyumbani kwake. Nilimwuliza ikiwa ni mara ya kwanza kwa Mtume kuwa nyumbani kwake. Kwa haraka alitabasamu na alijibu, “Ndio.” Swali lake kwangu lilikuwa zuri: “Je, ni mambo gani muhimu zaidi ninayopaswa kuyajua?”
Nilijibu kwa kusema mambo ya nafsini mwangu, mambo ambayo yananiandaa kusikia msukumo, ambao huinua uoni wangu zaidi ya njia za ulimwengu, ambayo hutoa kusudi kwa kazi yangu katika injili na kwenye maisha yangu.
Je, ninaweza kushiriki nanyi baadhi ya mambo ya nafsi yangu? Mambo haya yanatumika kwa wote wanaotafuta kuwa wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo. Mambo kumi yatapendeza, yaweza kukumbukwa. Lakini leo nawapa mambo saba kwa matumaini kwamba mtakamilisha nane, tisa, na kumi kutoka kwenye uzoefu wako mwenyewe.
Kwanza, mpende Mungu Baba na Yesu Kristo, Mwokozi wetu.
Yesu aliamuru amri kuu ya kwanza: “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote.”7
Rais Nelson alitangaza kujitolea kwake kwa Mungu, Baba yetu wa Milele, na kwa Mwanawe, Yesu Kristo, alipoitwa kuongoza Kanisa la Bwana, akisema, “Ninawajua, nawapenda, na ninaahidi kuwatumikia Wao—na wewe—kwa kila pumzi iliyobaki ya maisha yangu.”8
Hivyo kwanza, mpende Baba na Mwana.
Pili, “Mpende jirani yako.”9
Hilo sio wazo zuri tu; ni amri kuu ya pili. Jirani zako ni mwenzi wako na familia yako, waumini wa kata, wafanyakazi wenzako, unaokaa nao chumba kimoja, ambao sio wa imani yetu, wale wanaohitaji msaada, na, kusema ukweli, kila mtu. Kiini cha “Mpende jirani yako” kimeonyeshwa katika wimbo “Love One Another.”10
Rais Nelson anatukumbusha, “Tunapompenda Mungu kwa mioyo yetu yote, Yeye hubadilisha mioyo yetu kwa ustawi wa wengine.”11
Tatu, jipende mwenyewe.
Hapo ndipo wengi wanaposumbuka. Je, si ajabu kwamba kujipenda sisi wenyewe huonekana kutokuwa rahisi kuliko kuwapenda wengine? Walakini, Bwana amesema, “Mpende jirani yako kama nafsi yako.”12 Anathamini uungu ulio ndani yetu; nasi tuuthamini. Tunapolemewa na makosa, maumivu ya moyo, hisia za kutostahili, kukatishwa tamaa, hasira, au dhambi, nguvu ya Upatanisho wa Mwokozi ni, kwa mpango wa kiungu, moja ya mambo ambayo huinua roho.
Nne, shika amri.
Bwana ameweka wazi: “Kama mnanipenda, zishikeni amri zangu.”13 Jitahidi kila siku kuwa na kufanya vizuri kidogo na kusonga mbele kwa haki.
Tano, daima kuwa mstahiki kuhudhuria hekalu.
Ninaliita hili kupendekezwa kwa Bwana. Uwe na fursa ya hekalu mahali ulipo au la, kuwa mwenye kustahili kupata kibali hai cha hekalu kunakufanya ufokasi kwenye mambo yenye faida, njia ya agano.
Sita, furahi na uchangamke.
“Jipeni moyo, na wala msiogope,”14 Bwana amesema. Kwa nini? Na ni kwa jinsi gani, wakati changamoto zinatukabili kila wakati? Kwa sababu ya ahadi iliyotolewa na Yesu Kristo: “Mimi Bwana nipo pamoja nanyi, na nitasimama karibu yenu.”15
Rais Nelson anafafanua injili iliyorejeshwa kama “ujumbe wa furaha!”16 Na anafafanua, “Furaha tunayoihisi inahusika kwa kiasi kidogo na hali ya maisha yetu na kila kitu kinachohusu fokasi ya maisha yetu.”17
Saba, fuata nabii wa Mungu aliye hai.
Hii inaweza kuwa ya saba kwenye orodha yangu ya vitu, lakini ndilo la kwanza kwenye akili yangu kwa kuzingatia umuhimu wake leo.
Tunaye nabii wa Mungu duniani leo! Kamwe usipunguze maana ya hilo kwako. Kumbuka yule msichana niliyemtaja mwanzoni. Alitaka kujua ni mambo gani yana umuhimu zaidi. “Mfuate nabii aliye hai,” nilisema kipindi hicho na ninasisitiza tena leo.
Tunatofautishwa kama kanisa linaloongozwa na manabii, waonaji na wafunuzi walioitwa na Mungu kwa wakati huu. Ninakuahidi kwamba unaposikiliza na kufuata ushauri wao, kamwe hautapotoshwa. Kamwe!
Tunaishi katika wakati ambao “tunarushwa huku na huko,”18 wakati hali ya kiroho, adabu, uadilifu na heshima vinashambuliwa. Tunapaswa kufanya chaguzi. Tunayo sauti ya Bwana kupitia nabii Wake kutuliza woga wetu na kuinua macho yetu, kwani wakati Rais Nelson anapozungumza, anazungumza kwa ajili ya Bwana.
Tumebarikiwa na maandiko na mafundisho ambayo yanatukumbusha, “Mawazo yangu sio mawazo yenu, wala njia zenu sio njia zangu, asema Bwana.”19
Ndivyo ilivyokuwa kwa Naamani, kiongozi mkuu wa kijeshi huko Siria, lakini alikuwa na ukoma, ambaye aliambiwa kwamba nabii Elisha anaweza kumponya. Elisha alimtuma mjumbe wake amwambie Naamani ajioshe katika Mto Yordani mara saba naye angekuwa safi. Naamani alidhihaki. Hakika kulikuwa na mto mashuhuri kuliko Yordani, na kwa nini atume mtumishi wakati alimtarajia Elisha, nabii, amponye? Naamani aliondoka, lakini mwishowe alishawishiwa na watumishi: “Ikiwa nabii angekuamuru ufanye jambo kubwa, je! Usingelifanya?”20 Naamani mwishowe alijitumbukiza mara saba katika Mto Yordani na aliponywa.
Simulizi ya Naamani inatukumbusha juu ya hatari za kuchukua na kuchagua sehemu za ushauri wa kinabii ambazo zinafaa mawazo yetu, matarajio au desturi za kileo. Nabii wetu daima hutuelekeza kwenye Mto wetu wa Yordani ili kuponywa.
Maneno muhimu zaidi ambayo tunaweza kusikia, kutafakari na kufuata ni yale yaliyofunuliwa kupitia nabii wetu aliye hai. Ninashuhudia kwamba nimekaa katika baraza la ushauri na Rais Nelson kujadili mambo mazito ya Kanisa na ya ulimwengu, na nimeona ufunuo ukitiririka kupitia yeye. Anamjua Bwana, anajua njia zake na anatamani kwamba watoto wote wa Mungu wamsikie, Bwana Yesu Kristo.
Kwa miaka mingi tumesikia kutoka kwa nabii mara mbili kwa mwaka katika mkutano mkuu. Lakini pamoja na maswala magumu ya siku zetu, Rais Nelson anazungumza mara nyingi zaidi kwenye vikao,21 mitandao ya kijamii,22 ibada,23 na hata kwenye mikutano na waandishi wa habari.24 Nimemuona akiandaa na kuwasilisha ujumbe mzito wa ufunuo ambao umehimiza shukrani zaidi, kukuza ushirikishwaji mkubwa wa kaka na dada zetu wote duniani, na ongezeko la amani, tumaini, furaha, afya, na uponyaji katika maisha yetu binafsi.
Rais Nelson ana kipawa cha mawasiliano, lakini muhimu zaidi, yeye ni nabii wa Mungu. Hilo ni la kushangaza unapolifikiria, lakini ni muhimu kutambua kwamba maelekezo yake ya wazi yatatulinda dhidi ya udanganyifu, ujanja na njia za kilimwengu zinazoshika kasi ulimwenguni leo.25
Mavazi ya kinabii yanahusu ufunuo. “Urejesho wa Utimilifu wa Injili ya Yesu Kristo: Tangazo la Miaka Mia Mbili kwa Ulimwengu,” lililotolewa kwenye mkutano mkuu wa Aprili 2020, unasisitiza kwamba Bwana anaongoza kazi hii. Katika tangazo hili, Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili wanasema: “Tunatangaza kwa furaha kwamba Urjesho ulioahidiwa unaendelea kupitia ufunuo unaoendelea. Dunia kamwe haitabaki kama ilivyo, kwani Mungu ‘atavijumlisha vitu vyote katika Kristo’ (Waefeso 1:10).”26
“Mambo yote katika Kristo”27 na “mambo ya nafsi yangu”28 ni kuhusu Kanisa hili, injili hii, na watu hawa.
Ninafunga kwa mwaliko kwa kila mmoja wenu kuzingatia “mambo saba ya nafsi yangu” ambayo nimeshiriki leo: mpende Mungu Baba na Yesu Kristo, Mwokozi wetu; mpende jirani yako; jipende mwenyewe; shika amri; daima uwe mwenye kustahili kibali cha hekalu; kuwa na furaha na mchangamfu; na mfuate nabii wa Mungu aliye hai. Ninakualika uweke nane, tisa, na kumi za kwako. Fikiria njia ambazo unaweza kushiriki “mambo” yako ya moyoni na wengine na uwahimize kuomba, kutafakari, na kutafuta mwongozo wa Bwana.
“Mambo ya nafsi yangu” ni ya thamani kwangu kama yalivyo ya kwako. Mambo haya huimarisha huduma yetu katika Kanisa na katika maeneo yote ya maisha. Yanatuweka kwa Yesu Kristo, yanatukumbusha maagano yetu na hutusaidia kujihisi salama mikononi mwa Bwana. Nashuhudia kwamba Yeye anatamani kwamba nafsi zetu “hazitapata njaa wala kiu, lakini zitajazwa”29 na upendo Wake tunapotafuta kuwa wafuasi Wake wa kweli, kuwa kitu kimoja pamoja Naye kama Yeye alivyo na Baba. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.