Kukabiliana na Vimbunga Vyetu vya Kiroho kwa Kuamini katika Kristo
Tunakabiliana na vimbunga vyetu vya kiroho vyema zaidi kwa kuamini katika Kristo na kushika amri Zake.
Kwa miaka sita iliyopita, kipenzi changu, Ann, pamoja nami tumeishi Texas karibu na ufukwe wa Gulf, ambapo baadhi ya vimbunga vikubwa vimeipiga Marekani, vikiacha uharibifu mkubwa na hata upotevu wa maisha. Kwa huzuni sana, miezi ya karibuni haijawa mipya kwa matukio haya ya kukatisha tamaa. Upendo wetu na maombi viwafikie wale wote ambao wameathirika kwa namna yoyote ile. Mnamo 2017, sisi binafsi tulikumbwa na Kimbunga Harvey, ambacho kiliweka rekodi ya mvua iliyofikia mpaka inchi 60 (150 sm).
Kanuni za asili huongoza ufanyikaji wa vimbunga. Joto la bahari lazima liwe angalau nyuzi 80 za Farenhaiti (nyuzi 27 sentigredi), likisambaa kufikia futi 165 (50 m) chini ya uso wa bahari. Pale upepo unapokutana na maji vuguvugu ya bahari, husababisha maji kuchemka na kuinuka mpaka kwenye angahewa, ambapo huyeyushwa. Kisha mawingu hufanyika, na upepo huleta hali ya mzunguko juu ya uso wa bahari.
Vimbunga ni vikubwa kwa kipimo, hufikia futi 50,000 (15,240 m) au zaidi kwenye angahewa na husambaa angalau maili 125 (200 km). Cha kushangaza, pale vimbunga vinapokutana na ardhi, huanza kudhoofika kwa sababu haviko kwenye maji ya moto tena ambayo uhitajika kuongeza nguvu yake.1
Unaweza usikumbane na kimbunga cha kuangamiza maishani mwako. Hata hivyo, kila mmoja wetu amedhoofika na atadhoofika wakati vimbunga vya kiroho hutishia amani yetu na kujaribu imani yetu. Katika ulimwengu wa leo, vinaonekana kuongezeka kwa kiwango na uzito. Kwa shukrani, Bwana ametupatia njia ya uhakika ambapo kwa shangwe tutavishinda. Kwa kuishi injili ya Yesu Kristo, tunahakikishiwa kwamba “mawingu ya kiza yakija na kutisha amani yetu, tumaini angavu li mbele yetu.”2
Rais Russell M. Nelson alielezea:
“Watakatifu wanaweza kuwa na furaha katika hali yoyote. Tunaweza kuwa na furaha hata kama tuna siku mbaya, wiki mbaya, au hata mwaka mbaya!
“… Furaha tunayoihisi inahusika kwa kiasi kidogo na hali ya maisha yetu na inahusika na kila kitu kinachohusu fokasi ya maisha yetu.
“Wakati fokasi ya maisha yetu i katika … Yesu Kristo na injili Yake, tunaweza kuhisi shangwe bila kujali nini kinatokea—au hakitokei—katika maisha yetu.”3
Kama vile kanuni za asili zinavyoongoza vimbunga vya bahari, kanuni takatifu huongoza jinsi ya kuhisi shangwe nyakati za vimbungwa vyetu vya kiroho. Shangwe au huzuni tunayohisi tunapokabiliana na vimbunga vya maisha vimefungwa katika sheria ambazo Mungu ameziweka. Rais Nelson ameshiriki, “Zinaitwa amri, lakini ni za kweli kama vile tu kanuni za lifti, kanuni ya uvutano, [na] kanuni inayoongoza mapigo ya moyo.”
Rais Nelson anaendelea “Ni kanuni nyepesi sana: Kama unataka kuwa na furaha, shika amri.”4
Mashaka ni adui wa imani na shangwe. Kama vile maji ya vuguvugu ni chanzo cha vimbunga, mashaka ni chanzo cha vimbunga vya kiroho. Kama vile kuamini ni chaguo, vivyo hivyo na mashaka. Tunapochagua kuwa na mashaka, tunachagua kutendewa, kwa nguvu ya adui, kisha kutuacha dhaifu na wanyonge.5
Shetani hutafuta kutuongoza kwenye hali ya mashaka. Anatafuta kuifanya mioyo yetu kuwa migumu ili kwamba tusiamini.6 Hali ya mashaka inaweza kuonekana yenye kuvutia kwa sababu huonekana kama ya amani, maji ya vuguvugu hayatuhitaji kuishi “kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.”7 Katika maji hayo Shetani hutujaribu ili tulegeze uangalifu wetu wa kiroho. Kukosa huko umakini kunaweza kupelekea kukosekana kwa uimara kiroho, ambapo tunakuwa “si baridi wala moto.”8 Kama hatujaimarishwa kwa Kristo, mashaka na vishawishi vyake vitatuongoza kwenye kutojali ambapo hatutapata miujiza, furaha ya kudumu, au “raha nafsini [mwetu].”9
Kama vile vimbunga hudhoofika vifikapo ardhini, mashaka huondolewa na imani pale tunapojenga msingi wetu kwa Kristo. Kisha tunaweza kuona vimbunga vya kiroho katika mtazamo wake halisi, na uwezo wetu wa kuvishinda huongezeka. Kisha, “ibilisi atakapotuma mbele pepo zake kali, ndio, mishale yake kimbungani, … hautakuwa na uwezo … [kutuvuta] chini kwenye shimo la taabu na msiba usioisha, kwa sababu ya mwamba ambako kwake [tumejengwa], ambao ni msingi imara.”10
Rais Nelson amefundisha:
Imani katika Yesu Kristo ni msingi wa imani yote na ni mfereji wa nguvu za kimungu.
Bwana hahitaji imani kamilifu kwetu ili kufikia uwezo Wake mkamilifu. Lakini anatuomba tuamini.”11
Tangu mkutano mkuu wa Aprili, mimi pamoja na familia yangu tumekuwa tukitafuta kuimarisha imani yetu katika Yesu Kristo na Upatanisho Wake ili kutusaidia “kubadili changamoto [zetu] kuwa ukuaji wa kipekee na fursa.”12
Mjukuu wetu wa kike, Ruby, amebarikiwa na dhamira imara ya kutimiza majukumu. Alipozaliwa, umio lake lilikuwa halijaungana na tumbo. Hata kama mtoto mchanga, pamoja na msaada wa wazazi wake, alikabiliana na jaribu hili kwa dhamira ya kipekee. Ruby sasa ana miaka mitano. Ingawa bado ni mdogo sana, ni mfano wa dhati wa asiyekubali hali zake zikatishe furaha yake. Ni mwenye furaha muda wote.
Mei iliyopita, Ruby alikabiliana na kimbunga cha ziada katika maisha yake kwa imani. Ruby pia alizaliwa akiwa na mkono ambao haukukua kikamilifu ambao ulihitaji upasuaji wa kuurekebisha. Kabla ya upasuaji huu mgumu, tulikutana naye na kumpatia mchoro ambao kwa uzuri ulionyesha mkono wa mtoto ambao kwa upendo umeshikilia mkono wa Mwokozi. Tulipomuuliza kama alikuwa na woga, alijibu, “Hapana, nina furaha!”
Kisha tulimuuliza, “Ni kwa sababu gani?”
Ruby kwa ujasiri alisema, “Kwa sababu ninajua kwamba Yesu atashikilia mkono wangu.”
Uponyaji wa Ruby umekuwa wa kimiujiza, na anaendelea kuwa na furaha. Ni jinsi gani usafi wa imani ya mtoto hutofautiana na upumbavu wa mashaka ambayo mara kwa mara vinaweza kutujaribu pale tunapoendelea kuwa wakubwa!13 Lakini sote tunaweza kuwa watoto wadogo na kuchagua kuweka pembeni kutoamini kwetu. Ni uchaguzi rahisi.
Baba anayejali kwa bidii alimwomba Mwokozi, akisema, “Ukiweza neno lolote, … tusaidie.”14
Kisha Yesu akasema kwake:
“Ukiweza, yote yawezekana kwake aaminiye.”
“Mara baba … akapaza sauti akasema akilia, Bwana, Naamini, nisaidie kutokuamini kwangu.”15
Baba huyu mnyenyekevu kwa busara alichagua kuweka imani yake katika Kristo kuliko kwenye mashaka yake. Rais Nelson ameshiriki, “Ni kutoamini kwako ambako kutamfanya Mungu asikubariki na miujiza ya kuhamisha milima katika maisha yako.”16
Mungu ni wa rehema kiasi gani hata atuwekee kipimo katika kiwango cha kuamini na si katika kiwango cha kujua!
Alma anafundisha:
“Heri yule ambaye anaamini katika neno la Mungu.”17
“[Kwani] Mungu ni mwenye hekima kwa wote wanaoamini katika jina lake; kwa hivyo, anataka kwa mara ya kwanza, kwamba mwamini.”18
Ndio, katika hatua ya awali, Mungu anatamani kwamba tumwamini Yeye.
Tunakabiliana na vimbunga vyetu vya kiroho vyema zaidi kwa kuamini katika Kristo na kushika amri Zake. Imani yetu na utii hutuunganisha na nguvu zaidi ya tulizonazo ili kushinda “[chochote] kinachotokea—au kisichotokea—katika maisha yetu.”19 Ndio, Mungu “hutubariki [sisi] papo hapo” kwa kuamini na kutii.20 Ndio, baada ya muda hali yetu hubadilika kuwa ya furaha na “tumefanywa hai katika Kristo” pale tunapoonyesha imani yetu Kwake na kushika amri Zake.21
Akina kaka na dada basi na tuchague leo “kutokuwa na shaka, lakini muwe mkiamini.”22 “Njia sahihi ni kuamini katika Kristo.”23 “Tumechorwa … katika viganja vya mikono [Yake].”24 Yeye ni Mwokozi na Mkombozi wetu, ambaye husimama katika mlango wetu na kugonga.25 Katika Jina la Yesu Kristo, amina.