Mkutano Mkuu
Kupendelewa na Bwana katika Siku Zangu Zote
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2021


Kupendelewa na Bwana katika Siku Zangu Zote

Je, tunachukulia kwa namna gani taabu zetu? je! Tunahisi shukrani kwa sababu tumefokazi zaidi kwenye baraka zetu kuliko kwenye matatizo?

Janga la UVIKO-19 imekuwa moja ya majaribio na changamoto ambazo watoto wa Mungu wamekutana nazo katika historia ya ulimwengu. Mwanzoni mwa mwaka huu, mimi na familia yangu pendwa tuliishi katika siku za giza. Janga hilo na sababu zingine zilileta kifo na maumivu kwa familia yetu kupitia kufariki kwa wapendwa wetu. Licha ya matibabu, kufunga, na sala, wakati wa majuma matano kaka yangu Charly, dada yangu Susy, na shemeji yangu Jimmy walivuka kwenda upande mwingine wa pazia.

Wakati mwingine nimekuwa nikishangaa kwa nini Mwokozi alilia wakati alimuona Mariamu akihuzunishwa na kifo cha Lazaro, kaka yake, Japo Alijua kwamba alikuwa na uwezo wa kumrudishia uhai Lazaro na kwamba hivi karibuni Angetumia nguvu hii kumrudishia uhai rafiki Yake kutoka mautini.1 Nimeshangazwa na upendo na huruma ya Mwokozi kwa Mariamu; Alielewa maumivu yasiyoelezeka ambayo Mariamu alihisi kwenye kifo cha kaka yake, Lazaro.

Tunahisi maumivu hayo hayo tunapopata kutengana kwa muda na wapendwa wetu. Mwokozi ana huruma kamili kwetu. Yeye hatulaumu kwa uoni wetu mdogo wala kwa kuwa na uwezo wenye kikomo kuona picha kamili ya safari yetu ya milele. Badala yake, ana huruma juu ya huzuni na mateso yetu.

Baba wa Mbinguni na Mwanawe, Yesu Kristo, wanataka tuwe na furaha.2 Rais Russell M. Nelson alifundisha: “Furaha tunayohisi haichangiwi na hali ya maisha yetu na kila kitu kinachohusu fokasi ya maisha yetu. Wakati fokasi ya maisha yetu iko kwenye Mpango wa Mungu wa wokovu, … tunaweza kuhisi furaha bila kujali nini kinatokea—au kutotokea—katika maisha yetu.”3

Nilipokuwa mmisionari, nakumbuka wakati mmisionari mmoja mzuri ambaye nilikuja kupendezwa naye alipopokea habari mbaya. Mama yake na mdogo wake walikuwa wamefariki katika ajali mbaya. Rais wa misheni alimpa mzee huyu uchaguzi wa kurudi nyumbani kwa ajili ya mazishi. Hatahivyo, baada ya kuzungumza na baba yake kwa simu, mmisionari huyu aliamua kukaa na kumaliza misheni yake.

Picha
Kumtembelea mmisionari hospitalini

Muda mfupi baadaye, tulipokuwa tukitumikia katika eneo moja, mimi na mwenzangu tulipigiwa simu ya dharura; baadhi ya wezi walikuwa wameiba baiskeli ya mmisionari huyo huyo na walikuwa wamemjeruhi kwa kisu. Yeye na mwenzake walilazimika kutembea kwenda hospitali ya karibu, ambapo mimi na mwenzangu tulikutana nao. Nikiwa njiani kwenda hospitalini, nilikuwa nikiomboleza kwa ajili ya mmisionari huyu. Nilifikiri kwamba roho yake ingekuwa ya chini na kwamba hakika, baada ya uzoefu huu wa kiwewe, sasa angetaka kurudi nyumbani.

Walakini, tulipofika hospitalini, nilimwona mmisionari huyu amelala kitandani kwake, akingojea kupelekwa chumba cha upasuaji—na alikuwa akitabasamu. Niliwaza, “Angewezaje kutabasamu wakati kama huu?” Wakati alikuwa akipona hospitalini, kwa shauku alitoa vijitabu na nakala za Kitabu cha Mormoni kwa madaktari, manesi, na wagonjwa wengine. Hata katika majaribu haya, hakutaka kwenda nyumbani. Badala yake, alitumika hadi siku ya mwisho ya misheni yake kwa imani, nguvu, uwezo, na shauku.

Mwanzoni mwa Kitabu cha Mormoni, Nefi anasema, “Baada ya kuona mateso mengi katika siku zangu, hata hivyo, nikiwa nimependelewa sana na Bwana katika siku zangu zote.”4

Ninafikiria kuhusu majaribu mengi ambayo Nefi aliyapata, mengi ambayo yamejumuishwa katika maandishi yake. Majaribu yake yanatusaidia kuelewa kwamba sisi sote tuna siku zetu za giza. Moja ya majaribu haya yalitokea wakati Nefi aliamriwa kurudi Yerusalemu kupata mabamba ya shaba ambayo Labani alikuwa nayo. Baadhi ya kaka za Nefi walikuwa watu wa imani ndogo, na hata walimpiga Nefi kwa fimbo. Nefi alipata jaribu lingine wakati alipovunja upinde wake na hakuweza kupata chakula kwa ajili ya familia yake. Baadaye, wakati Nefi alipoamriwa kujenga meli, ndugu zake walimdhihaki na kukataa kumsaidia. Licha ya majaribu haya na mengine mengi wakati wa maisha yake, Nefi daima alitambua wema wa Mungu.

Picha
Nefi akiwa amefungwa melini

Wakati familia yake ilipokuwa ikivuka bahari njiani kuelekea nchi ya ahadi, baadhi ya familia ya Nefi “walianza kujifurahisha,” kuongea kwa ukali, na kusahau kuwa ni nguvu ya Bwana iliyokuwa imewahifadhi. Wakati Nefi alipowarudi, walichukizwa na kumfunga kwa kamba kwamba asiweze kusogea. Kitabu cha Mormoni kinasema kwamba ndugu zake “walimtendea kwa ukali mwingi”; mikono yake na vifundoni “vilikuwa vimevimba sana, na uchungu ulikuwa mkubwa.”5 Nefi alihuzunishwa na ugumu wa mioyo ya kaka zake na wakati mwingine alihisi kushindwa na huzuni.6 “Walakini, nilimtazama Mungu wangu, na nilimsifu siku yote nzima; na sikumlalamikia Bwana kwa sababu ya masumbuko yangu.”7

Kaka na dada zangu wapendwa, tunachukulia kwa namna gani taabu zetu? Je! tunalalamika mbele za Bwana kwa sababu ya hizo? Au, kama Nefi na rafiki yangu wa zamani mmisionari, je! tunahisi shukrani kwa neno, mawazo, na tendo kwa sababu tunafokasi zaidi kwenye baraka zetu kuliko taabu zetu?

Mwokozi wetu, Yesu Kristo alitupatia mfano wakati wa huduma yake hapa duniani. Wakati wa shida na jaribu, kuna mambo machache ambayo hutuletea amani kubwa na kuridhika tofauti na kutumikia wenzetu. Kitabu cha Mathayo kinasimulia kile kilichotokea wakati Mwokozi alipogundua kuwa Yohana Mbatizaji binamu yake alikuwa amekatwa kichwa na Mfalme Herode ili kumpendeza Herodias binti yake:

“Wanafunzi wake wakaja, wakachukua mwili, wakauzika, wakaenda wakamwambia Yesu.

“Yesu aliposikia hayo, akatoka hapo kwa mashua, akaenda mahali pa faragha peke yake: na makutano waliposikia, walimfuta kwa miguu toka mijini mwao.

“Yesu akatoka, akaona mkutano mkubwa, akawahurumia, akawaponya wagonjwa wao.

“Kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimjia, wakisema, Hapa ni mahali pa jangwani, na wakati umepita; waache watu waende, waingie vijijini, na kujinunulia chakula.

“Lakini Yesu akawaambia, Hawana haja ya kuondoka; wapeni ninyi chakula.”8

Yesu Kristo alituonyesha kwamba wakati wa jaribu na shida, tunaweza kutambua shida za wengine. Kwa kusukumwa na huruma, tunaweza kufikia na kuwainua. Na tunapofanya hivyo, tunainuliwa pia na huduma yetu kama ya Kristo. Rais Gordon B. Hinckley alisema: “Dawa bora ninayojua ya wasiwasi ni kazi. Dawa bora ya kukata tamaa ni huduma. Tiba bora ya uchovu ni changamoto ya kumsaidia mtu ambaye amechoka zaidi.”9

Katika hili, Kanisa la Yesu Kristo, nimekuwa na fursa nyingi za kuwahudumia na kuwamtumikia wenzangu. Ni katika nyakati hizo ninahisi kwamba Baba wa Mbinguni hupunguza mizigo yangu. Rais Russell M. Nelson ndiye nabii wa Mungu duniani; yeye ni mfano mzuri wa jinsi tunapaswa kuhudumia wengine wakati wa majaribu magumu. Ninaunganisha ushuhuda wangu pamoja na wa wale wa Watakatifu wengine wengi, kwamba Mungu ni Baba yetu wa Mbinguni mwenye upendo. Nimehisi upendo Wake usio na kipimo wakati wa siku zangu za giza. Mwokozi wetu, Yesu Kristo anaelewa maumivu yetu na shida zetu. Anataka kutupunguzia mzigo na kutufariji. Lazima tufuate mfano Wake kwa kuwahudumia wale walio na mizigo mikubwa kuliko yetu. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Chapisha