Mkutano Mkuu
Huruma ya Kudumu ya Mwokozi
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2021


13:12

Huruma ya Kudumu ya Mwokozi

Onyesho la huruma kwa wengine ndicho kiini cha injili ya Yesu Kristo.

Moja ya kanuni muhimu sana zilizofundishwa na Mwokozi wakati wa huduma Yake duniani ilikuwa ni kuwatendea wengine kwa huruma. Acha tuitazame kanuni hii na matumizi yake katika hali halisi kwa kurejelea masimulizi ya matembezi ya Yesu katika nyumba ya Simoni Mfarisayo.

Injili ya Luka inaeleza kwamba mwanamke mmoja, aliyefikiriwa kuwa mtenda dhambi, aliingia katika nyumba ya Simoni wakati Yesu akiwa humo. Katika hali ya unyenyekevu, mwanamke yule alimsogelea Yesu, akaosha miguu Yake kwa machozi yake, akayapangusa machozi kwa nywele zake na kisha akaibusu na kuipaka miguu kwa manukato maalumu.1 Mwenyeji mwenye majivuno, aliyejihesabu mwenyewe kama mwenye maadili ya juu zaidi ya yule mwanamke, alifikiria mwenyewe kwa kiburi na jeuri, “Mtu huyu, kama angekuwa nabii, angelijua huyu ni nani na ni mwanamke wa aina gani ambaye anamgusa: kwani ni mtenda dhambi.”2

Mtazamo wa Mfarisayo wa mimi mtakatifu kuliko wewe ulimwongoza katika kuwahukumu isivyo haki wote Yesu na yule mwanamke. Lakini katika Kujua kwake Yote, Mwokozi alijua mawazo ya Simoni na, kwa hekima kubwa, akatoa changamoto kwa dharau ya Simoni, pamoja na kumkemea kwa kukosa kwake heshima katika kumpokea mgeni maalumu kama Mwokozi ndani ya nyumba yake. Kwa kweli, karipio la Yesu la moja kwa moja kwa Mfarisayo yule lilitumika kama ushahidi kwamba Yesu hakika alikuwa na kipawa cha unabii na kwamba mwanamke huyu aliye na moyo wa unyenyekevu na uliopondeka, alikuwa ametubu na kusamehewa dhambi zake.3

Na kama matukio mengine mengi wakati wa huduma ya Yesu duniani, hadithi hii inathibitisha kwamba Mwokozi alikuwa akitenda kwa huruma kwa wote ambao wangekuja Kwake—pasipo kutofautisha—na mahususi zaidi kwa wale ambao walihitaji msaada Wake zaidi. Majuto na unyenyekevu wa upendo vilivyoonyeshwa kwa Yesu na yule mwanamke vilikuwa ni ushahidi wa toba yake ya dhati na tamanio la kupokea ondoleo la dhambi zake. Hata hivyo, hali ya ukuu wa kujikweza wa Simoni, ukizidishwa na ugumu wa moyo wake,4 vilimzuia yeye kuonyesha huruma kwa ile nafsi ya mwenye kutubu, na kumwelezea hata Mwokozi wa ulimwengu bila kujali na kwa dharau. Mtazamo wake ulionyesha kwamba njia yake ya maisha haikuwa lolote zaidi ya nidhamu kali na utii usio wa dhati wa sheria na dhihirisho la nje la imani yake kupitia kujikweza na utakatifu wa uongo.5

Utumishi wa huruma na wa binafsi wa Yesu katika hadithi hii unaonyesha mfano mkamilifu wa jinsi ya kuchangamana na majirani zetu. Maandiko yana mifano isiyo na idadi ya jinsi Mwokozi, akiongozwa na huruma ya kina na ya kudumu, alichangamana na watu wa siku Yake na kuwasaidia wale waliokuwa wakiteseka na “wamechoka, na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji.”6 Yeye alinyoosha mkono Wake wa rehema kwa wale waliohitaji msaada kutokana na mizigo yao, yote ya kimwili na kiroho.7

Mtazamo wa huruma wa Yesu umejikita kwenye hisani,8 ikimaanisha, katika upendo Wake ulio safi na mkamilifu, ambao ndio kitovu cha dhabihu Yake ya upatanisho. Huruma ni tabia ya msingi ya wale wanaojitahidi kwa ajili ya utakaso na sifa hii takatifu hufungamana na sifa nyingine za Kikristo kama vile kuomboleza na wale wanaoomboleza na kuhisi kile anachohisi mwingine, rehema na ukarimu.9 Onyesho la huruma kwa ajili ya wengine ni, kwa ukweli, kitovu cha injili ya Yesu Kristo na alama iliyowekwa ya ukaribu wetu wa kiroho na kihisia kwa Mwokozi. Zaidi ya hayo, inaonyesha kiwango cha ushawishi Mwokozi alichonacho kwenye njia yetu ya maisha na kuonyesha ukubwa wa roho zetu.

Ni muhimu kutambua kwamba matendo ya huruma ya Yesu hayakuwa ya muda tu au maonyesho ya kulazimishwa yakiwa kama orodha ya kazi za kukamilishwa bali ni madhihirisho ya kila siku ya uhalisia wa upendo Wake msafi kwa Mungu na kwa watoto Wake na hamu yake ya kudumu ya kuwasaidia watoto hao.

Yesu aliweza kutambua mahitaji ya watu hata wakiwa mbali. Hivyo, haishangazi, kwa mfano, mara baada ya kumponya mtumwa wa akida mmoja,10 Yesu alisafiri kutoka Kapernaumu hadi mji ulioitwa Naini. Huko ndipo ambapo Yesu alitenda moja ya miujiza mikuu katika huduma yake ya hapa duniani wakati alipomwamuru kijana aliyekufa, mwana pekee wa mama mjane, aamke na kuishi. Yesu sio tu alitambua mateso makali ya yule mwanamke maskini bali hali ngumu za maisha yake na akashikwa na huruma ya dhati kwa ajili yake.11

Kama yule mwanamke mwenye dhambi na yule mjane wa Naini, watu wengi katika maeneo tunayoishi wanatafuta faraja, kusikilizwa, kujumuishwa, na msaada wowote tunaoweza kuwapatia. Sisi sote tunaweza kuwa vyombo mikononi mwa Bwana na kuwatendea kwa huruma wale wenye mahitaji, kama vile Yesu alivyofanya.

Ninamjua msichana mdogo aliyezaliwa akiwa na tatizo kubwa la midomo iliyoachana na paa la kinywa lililo wazi. Ilibidi afanyiwe upasuaji wa kwanza katika mtiririko wa upasuaji mwingi katika siku yake ya pili ya maisha. Wakiongozwa na huruma ya dhati kwa wale wanaopitia changamoto kama hiyo, msichana huyu na wazazi wake wanatafuta kutoa msaada, uelewa na msaada wa kihisia kwa wengine wanaokabiliwa na ugumu huu. Waliniandikia hivi karibuni na kushiriki: “Kwa kupitia changamoto ya binti yetu, tulipata fursa ya kukutana na watu wazuri sana waliohitaji faraja, msaada na kutiwa moyo. Wakati fulani uliopita, binti yetu, ambaye ana umri wa miaka 11 sasa, aliongea na wazazi wa mtoto mwenye changamoto kama hiyo. Wakati wa maongezi haya, binti yetu kwa muda mchache alivua barakoa aliyokuwa ameivaa kutokana na janga la ulimwengu ili wale wazazi waweze kuona kwamba kuna matumaini, ingawa yule mtoto wao bado alikuwa na safari ndefu katika miaka michache ijayo ili kurekebisha tatizo lile. Tunahisi kuwa wenye furaha kwa fursa ya kuhisi maumivu ya wengine kwa wale wanaoteseka, kama Mwokozi afanyavyo kwetu sisi. Tunahisi kupunguza maumivu yetu kila wakati tunapompunguzia mtu mwingine maumivu yake.”

Wapendwa marafiki zangu, tunapojitahidi kwa kukusudia kuhusisha mtazamo wa huruma katika njia ya maisha yetu, kama ilivyoonyeshwa kwa mfano na Mwokozi, tutakuwa makini sana kwenye mahitaji ya watu. Kwa kuongezeka kwa umakini huo, hisia za dhati za kujali na upendo zitapenya katika kila tendo letu. Bwana atatambua jitihada zetu, na hakika tutabarikiwa kwa fursa za kuwa vyombo mikononi Mwake katika kulainisha mioyo na kuleta ahueni kwa hao “mikono iliyolegea.”12

Onyo la Yesu kwa Simoni Mfarisayo pia liliweka wazi kwamba hatupaswi kufanya hukumu ya haraka na katili kwa majirani zetu, kwa sababu sote tunahitaji kusikilizwa na rehema kwa ajili ya madhaifu yetu kutoka kwa Baba yetu mpendwa wa Mbinguni. Je, hili silo haswa Mwokozi alilofundisha katika tukio jingine wakati aliposema, “Basi mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii?”13

Tunahitaji kuelewa kwamba siyo rahisi kuelewa hali zote zinazochangia kwenye mtazamo au matendo ya mtu mwingine. Mwonekano unaweza kudanganya na mara nyingi hauwakilishi kipimo halisi cha tabia ya mtu. Tofauti na mimi na wewe, Kristo anao uwezo wa kuona kwa uwazi kabisa pande zote za hali fulani.14 Hata kufahamu udhaifu wetu wote, Mwokozi hakimbilii kutushutumu bali anaendelea kufanya kazi pamoja nasi kwa huruma, akitusaidia kuondoa boriti kutoka kwenye jicho letu. Yesu daima huangalia kwenye moyo na siyo mwonekano.15 Yeye mwenyewe alitangaza, “Msihukumu hukumu ya macho tu.”16

Sasa, zingatia ushauri wa hekima wa Mwokozi kwa wale wanafunzi kumi na wawili wa Kinefi kuhusu swali hili:

“Na mjue kwamba nyinyi mtakuwa waamuzi wa watu hawa, kulingana na hukumu ambayo nitawapatia ambayo itakuwa ya haki. Kwa hivyo mnapaswa kuwa watu wa aina gani? Amini ninawaambia, hata kama nilivyo.”17

“Kwa hivyo, ningependa kwamba mngekuwa wakamilifu, hata kama vile nilivyo au Baba yenu ambaye yuko mbinguni ambaye ni mkamilifu.”18

Katika maudhui haya, Bwana hutoa hukumu kwa wale wanaojichukulia juu yao kuhukumu mapungufu ya wengine bila haki. Ili kufuzu hatua ya kufanya hukumu ya haki, tunapaswa kujitahidi kuwa kama Mwokozi na kuangalia mapungufu ya watu wengine kwa huruma, hata kupitia macho Yake. Ukizingatia bado tunayo safari ndefu ili kufikia ukamilifu, pengine ingekuwa bora kama tukikaa miguuni pa Yesu na kuomba rehema kwa ajili ya mapungufu yetu, kama alivyofanya yule mwanamke aliyetubu katika nyumba ya Mfarisayo, na tusitumie muda na nguvu nyingi sana kukazia macho mapungufu yanayoonekana ya wengine.

Wapendwa marafiki zangu, ninashuhudia kwamba tunapojitahidi kuhusisha mfano wa huruma ya Mwokozi ndani ya maisha yetu, uwezo wetu wa kusifu wema wa majirani zetu utaongezeka na hisia zetu za asili za kuhukumu mapungufu yao utapungua. Ushirika wetu na Mungu utakua, na kwa hakika maisha yetu yatakuwa matamu zaidi, hisia zetu zitakuwa nyororo zaidi, na tutapata chanzo kisichokauka cha furaha. Tutafahamika kama wapatanishi,19 ambao maneno yao ni ya upole kama umande wa asubuhi ya majira ya kuchipua.

Nianaomba kwamba tuwe wavumilivu na waelewa wa wengine na kwamba rehema ya Bwana, katika upole mkamilifu, itapozaza kukosa kwetu uvumulivu kwa mapungufu ya wengine. Huu ni mwaliko wa Mwokozi kwetu sisi. Ninashuhudia kwamba Anaishi. Yeye ni mfano mkamilifu wa ufuasi wenye rehema na subira. Ninatoa ushuhuda wangu juu ya kweli hizi katika jina takatifu la Mwokozi Yesu Kristo, amina.