Amani ya Kristo Huondoa Uadui
Pale upendo wa Kristo unapojaza maisha yetu, tutatatua kutokukubaliana kwa upole, uvumilivu na wema.
Wapendwa akina kaka na akina dada, wakati wa upimaji moyo, kazi kwenye moyo huongezwa. Mioyo inayoweza kustahimili utembeaji inaweza kusuasua wakati wa kukimbia kupanda kilima. Kwa njia hii, upimaji wa moyo unaweza kuonyesha ugonjwa uliojificha ambao vinginevyo usingeonekana. Tatizo lolote linalogundulika linaweza kutibiwa kabla ya kusababisha matatizo makubwa katika maisha ya kila siku.
Janga la ulimwengu la UVIKO-19 kwa hakika limekuwa ni kipimo cha moyo cha ulimwengu! Kipimo kimeonyesha matokeo mchanganyiko. Chanjo salama na za kufaa zimetengenezwa.1 Wataalamu wa madawa, walimu, watoa huduma na wengineo wamejitoa kishujaa—na wanaendelea kufanya hivyo. Watu wengi wameoyesha ukarimu na wema—na wanaendelea kufanya hivyo. Na bado, hasara zilizojificha zimeweza kugundulika. Watu walio katika mazingira hatarishi wameteseka—na wanaendelea kuteseka. Wale wanaofanya kazi kuzungumzia kukosekana huku kwa uwiano wanapaswa kutiwa moyo na kushukuriwa.
Janga hili pia ni kipimo cha kiroho kwa Kanisa la Mwokozi na waumini wake. Matokeo hali kadhalika ni mchanganyiko. Maisha yetu yamebarikiwa kwa kuhudumu katika “njia ya ya juu na takatifu zaidi,”2 mtaala wa Njoo, Unifuate na kujifunza injili kunakolenga nyumbani, kunakosaidiwa na Kanisa. Wengi wametoa msaada wa dhati na faraja wakati wa nyakati hizi ngumu na wanaendelea kufanya hivyo.3
Lakini bado, katika baadhi ya mifano, kipimo cha kiroho kinaonyesha tabia za mabishano na mgawanyiko. Hii inapendekeza kwamba tunayo kazi ya kufanya ya kubadilisha mioyo yetu na kuungana kama wafuasi wa kweli wa Mwokozi. Hii sio changamoto mpya, lakini ni ngumu sana.4
Mwokozi alipowatembelea Wanefi, Alifundisha “Na hakutakuwa na ugomvi miongoni mwenu. … Yule ambaye ana roho ya ubishi siye wangu, lakini ni wa ibilisi, ambaye ni baba wa ubishi, na huchochea mioyo ya watu kubishana na hasira mmoja kwa mwingine.”5 Tunapobishana sisi kwa sisi kwa hasira, Shetani huchekelea na Mungu huuzunika.6
Shetani huchekelea na Mungu huuzunika kwa angalau sababu mbili. Moja, mabishano hudhohofisha ushuhuda wetu wa pamoja wa Yesu Kristo kwa ulimwengu na wokovu unaokuja kupitia “fadhila, … rehema, na neema.”7 Mwokozi alisema: “Amri mpya nawapa, Mpendane. … Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.”8 Kinyume chake pia ni ukweli—kila mmoja anajua kwamba sisi sio wafuasi Wake wakati hatuonyeshi upendo miongoni mwetu. Kazi Yake ya siku za mwisho hukwama wakati mabishano au uadui9 ukiwepo miongoni mwa wafuasi wake.10 Pili, mabishano hayaleti afya kiroho kwetu sisi kama watu binafsi. Tunanyang’anywa amani, shangwe, na pumziko na uwezo wetu wa kuhisi Roho unazuiliwa.
Yesu Kristo alielezea kwamba mafundisho Yake “sio kuchochea mioyo ya wanadamu kwa hasira, mmoja dhidi ya mwingine; lakini mafundisho [Yake] [ni] kwamba vitu kama hivi viondolewe mbali.”11 Kama mimi ni mwepesi wa kukasirika au kujibu tofauti za mawazo kwa kuwa na hasira au mwenye kuhukumu, basi “nimeshindwa” kipimo cha kiroho. Kushindwa huku hakumaanishi kwamba sina tumaini tena. Bali, kunaonesha kwamba nahitaji kubadilika. Na hilo ni vyema kujua.
Baada ya Mwokozi kutembelea Amerika, watu waliungana; “hakukuwa na ubishi katika nchi yote.”12 Je, unadhani watu waliungana kwa sababu wote walikuwa sawa, au kwa sababu hawakuwa na tofauti ya maoni? Sidhani. Badala yake, mabishano na uadui vilitoweka kwa sababu waliweka ufuasi wao wa Mwokozi juu ya vyote. Tofauti zao zilionekana kuwa ndogo kuliko upendo wao wa pamoja wa Mwokozi, na waliungana kama “warithi wa ufalme wa Mungu.”13 Hatma yake ni kwamba “hakujakuwa na watu ambao wangekuwa na furaha zaidi … ambao waliumbwa na mkono wa Mungu.”14
Umoja unahitaji juhudi.15 Unaongezeka pale tunapokuza upendo wa Mungu katika mioyo yetu16 na kufokasi katika hatma yetu ya milele.17 Tunaunganishwa kwa utambulisho wetu wa msingi wa pamoja kama watoto wa Mungu18 na dhamira yetu kwenye kweli za injili ya urejesho. Kama malipo, upendo wetu kwa Mungu na ufuasi wetu kwa Yesu Kristo huleta kujali wengine kwa dhati. Tunathamini tabia tofauti tofauti za wengine, mitazamo na vipawa.19 Kama hatuwezi kuweka ufuasi wetu kwa Yesu Kristo juu ya matamanio binafsi na maoni, tunapaswa kutathmini vipaumbele vyetu upya na tubadilike.
Tunaweza kulazimisha kusema, “Ni kweli tunaweza kuwa na umoja—kama tu utakubaliana nami!” Jibu zuri ni kwa kuuliza, “Je, naweza kufanya nini kuimarisha umoja? Je, nijibu vipi ili kumsaidia mtu huyu kusogea karibu na Kristo? Naweza kufanya nini ili kupunguza mabishano na kujenga jamii ya Kanisa yenye huruma na inayojali?”
Pale upendo wa Kristo unapojaza maisha yetu,20 tutatatua kutokukubaliana kwa upole, uvumilivu na wema.21 Hatutahofia sana kuhusu hisia zetu bali zaidi kuhusu majirani zetu. Tunatafuta “kuweka mambo sawa na kuunganisha.”22 Hatujihusishi katika “mabishano yasiyo na manufaa,” hatuwahukumu wale tusiokubaliana nao, au kujaribu kuwafanya wakosee.23 Badala yake, tunachukulia kwamba wale ambao hatukubaliani nao wanafanya kadiri wawezavyo kwa uzoefu wa maisha walio nao.
Mke wangu amejihusisha na sheria kwa zaidi ya miaka 20. Kama wakili, mara kwa mara alifanya kazi na wengine ambao kwa dhahiri walitetea mawazo pinzani. Lakini alijifunza kutokukubaliana bila kuwa mkali au mkatili. Angeweza kusema kwa ushauri pinzani, “Naona hatutakubaliana katika swala hili. Ninakupenda. Naheshimu maoni yako. Natumaini utanionyesha heshima kama niliyokuonyesha.” Mara kwa mara, hili liliruhusu heshima ya pamoja na hata urafiki licha ya kuwepo tofauti.
Hata maadui wa zamani wanaweza kuwa pamoja katika ufuasi wao kwa Mwokozi.24 Mnamo 2006, nilihudhuria uwekaji wakfu wa Hekalu la Helsinki Finland kwa heshima ya baba yangu na mababu zangu ambao walikuwa waongofu wa mwanzo wa Kanisa huko Finland. Wafin, akiwemo baba yangu, walikuwa na ndoto ya hekalu huko Finland kwa miongo kadhaa. Kwa wakati huo, Wilaya ya Hekalu ilikuwa ikihusisha Finland, Estonia, Latvia, Lithuania, Belarus na Urusi.
Wakati wa kuweka wakfu, nilijifunza kitu cha kushangaza. Siku ya kwanza ya ufanyaji kazi wa hekalu iliwekwa kwa ajili ya waumini wa Urusi kufanya ibada za hekaluni. Ni vigumu kuelezea jinsi hii ilivyokuwa ya kushangaza. Urusi na Finland walikuwa wamepigana vita vingi kwa karne nyingi. Baba yangu hakuiamini na hakuipenda sio tu Urusi bali Warusi wote. Alionyesha hisia hizo toka moyoni, na hisia zake zilikuwa zile za uadui wa Wafin kwa Warusi. Alikuwa amekariri mashairi ya utenzi ya vita vya nyakati za karne ya 19 kati ya Wafin na Warusi. Uzoefu wake wakati wa Vita ya II ya Dunia, wakati ambapo Finland na Urusi zilikuwa tena pande pinzani, haukusaidia lolote kubadili mitazamo yake.
Mwaka mmoja kabla ya uwekwaji wakfu wa Hekalu la Helsinki Finland, kamati ya hekalu, ikujumuisha Wafin pekee, ilikaa kujadili mipango ya uwekaji wakfu. Wakati wa kikao, mjumbe mmoja alisema kwamba Waumini wa Urusi wangesafiri siku kadhaa ili kuhudhuria uwekaji wakfu na wanaweza kuhitaji kupokea baraka zao za hekaluni kabla ya kurudi nyumbani. Mwenyekiti wa kamati, Kaka Sven Eklund, alipendekeza kwamba Wafin wangeweza kusubiria kidogo, kwamba Warusi wawe waumini wa kwanza kufanya ibada za hekaluni katika Hekalu. Wanakamati wote walikubali wazo hilo. Waumini waaminifu wa Siku za Mwisho wa Finland walisubirisha baraka zao za hekaluni ili kuruhusu zile za Waumini wa Urusi kufanyika kwanza.
Rais wa Eneo aliyekuwepo wakati wa kikao hicho cha kamati, Mzee Dennis B. Neuenschwander, aliandika: “Sikuwahi kuwa mwenye kujivunia zaidi juu ya Wafin kama ilivyokuwa kwa wakati huo. Historia ngumu ya Finland pamoja na majirani zake wa mashariki … na furaha yao ya hatimaye kuwa na [hekalu] kujengwa kwenye ardhi yao wenyewe vyote viliwekwa pembeni. Kuwaruhusu Warusi kuingia hekaluni kwanza [ilikuwa] ni kauli ya upendo na dhabihu.”25
Nilipomsimulia baba yangu kuhusu wema huu, moyo wake ulilainika na alilia, tukio lisiloonekana mara kwa mara kwa jasiri huyo wa Kifin. Kutoka wakati huo hadi kifo chake, miaka mitatu baadaye, kamwe hakuonyesha tena hisia nyingine hasi kuhusu Urusi. Akiwa ametiwa moyo kwa mfano wa Wafin wenzake, baba yangu alichagua kuweka ufuasi wake kwa Yesu Kristo juu ya matamanio mengine. Wafin hawakudharaulika tena; Warusi hawakudharaulika tena; hakuna kundi lilioachana na mila zake, historia au uzoefu wa kukomesha uadui. Hawakuhitaji kufanya hivyo. Badala yake, walichagua kufanya ufuasi wao kwa Yesu Kristo kama zingatio lao la Msingi.26
Kama wao wanaweza kufanya hivyo, hata nasi twaweza. Tunaweza kuleta urithi wetu, mila na uzoefu kwenye Kanisa la Yesu Kristo. Samweli hakuonea aibu urithi wake kama Mlamani,27 wala Mormoni hakuonea aibu urithi wake kama Mnefi.28 Lakini kila mmoja aliweka ufuasi wake kwa Mwokozi kwanza.
Kama sisi sio wamoja, sisi sio Wake.29 Mwaliko wangu ni tuwe majasiri kwa kuweka upendo wetu kwa Mungu na ufuasi kwa Mwokozi juu ya matamanio mengine yote.30 Acha tuimarishe agano tulilonalo katika ufuasi wetu—agano la kuwa wamoja.
Acha tufuate mfano wa Watakatifu kote ulimwenguni ambao kwa mafanikio wamekuwa wafuasi wa Kristo. Tunaweza kumtegemea Yesu Kristo, ambaye ni “amani yetu, ambaye … amekibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga; naye akiisha kuuondoa ule uadui [kwa dhabihu ya upatanisho].”31 Ushahidi wetu wa Yesu Kristo kwa ulimwengu utaimarika na utabaki wenye afya kiroho.32 Ninashuhudia kwamba “tunapoachana na mabishano” na kuwa na “mtazamo sawa na Bwana katika upendo na kuunganika Naye katika imani,” amani Yake itakuwa yetu33 Katika Jina la Yesu Kristo, amina.