Mkutano Mkuu
Kuwa Mfuasi wa Kristo
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2021


9:49

Kuwa Mfuasi wa Kristo

Kuwa mfuasi wa Kristo ni kujitahidi kufanya matendo, tabia na maisha yetu yaendane na yale ya Mwokozi.

Katika kujifunza kwangu binafsi maandiko, nimevutiwa na uongofu wa Sauli wa Tarso, ambaye baadaye alikuja kujulikana kama Paulo, kama ilivyoelezwa katika Biblia.

Paulo alikuwa mtu mwenye ari katika kulitesa Kanisa na Wakristo. Lakini kwa sababu ya nguvu ya mbinguni na Upatanisho wa Yesu Kristo, alibadilishwa kabisa na akawa mmoja wa watumishi wakuu wa Mungu. Mfano wake wa maisha ulikuwa ni Mwokozi Yesu Kristo.

Katika moja ya mafundisho ya Paulo kwa Wakorintho, aliwaalika wawe wafuasi wake kwani yeye mwenyewe alikuwa mfuasi wa Kristo (ona 1 Wakorintho 11:1). Huu ni mwaliko wa dhati na thabiti toka wakati wa Paulo mpaka leo: kuwa mfuasi wa Kristo.

Nilianza kutafakari juu ya kile inachomaanisha kuwa mfuasi wa Kristo. Na muhimu zaidi, nilianza kujiuliza, ni kwa njia ipi ninapaswa kuiga mfano Wake?

Kuwa mfuasi wa Kristo ni kujitahidi kufanya matendo, tabia na maisha yetu yaendane na yale ya Mwokozi. Ni kutafuta utu wema. Ni kuwa mwanafunzi wa kweli wa Yesu Kristo.

Nimejifunza baadhi ya vipengele vya maisha ya Mwokozi na nimehifadhi, kama sehemu ya ujumbe wangu leo, sifa nne kati ya sifa Zake ambazo ninajaribu kuiga na ambazo ninazishiriki nanyi.

Sifa ya kwanza ya Mwokozi ni unyenyekevu. Yesu Kristo alikuwa mnyenyekevu sana tangu kwenye maisha kabla ya kuzaliwa duniani. Kwenye Baraza Mbinguni, Yeye alitambua na kuruhusu mapenzi ya Mungu yashinde katika mpango wa wokovu kwa ajili ya mwanadamu. Alisema, “Baba, mapenzi yako na yatimizwe, na utukufu uwe wako milele na milele” (Musa 4:2).

Tunajua kwamba Yesu Kristo alifundisha unyenyekevu na alijinyenyekeza Mwenyewe ili kumpa utukufu Baba Yake.

Acha tuishi katika unyenyekevu kwa sababu unaleta amani (ona Mafundisho na Maagano 19:23). Unyenyekevu hutangulia utukufu na unaleta upendeleo wa Mungu juu yetu: “Vivyo hivyo ninyi muwe chini ya kila mmoja na jifungeni unyenyekevu: kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema” (1 Petro 5:5). Unyenyekevu huleta majibu ya upole. Ni chanzo cha sifa njema.

Mzee Dale G. Renlund alifundisha:

“Watu ambao hutembea kwa unyenyekevu na Mungu wanakumbuka kile Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo wamewafanyia.”

“Tunatenda kwa heshima kwa Mungu kwa kutembea kwa unyenyekevu pamoja naye” (“Tenda kwa Haki, Penda Neema na Tembea kwa Unyenyekevu na Mungu,” Liahona, Nov. 2020).

Sifa ya pili ya Mwokozi ni ujasiri. Ninapomfikiria Yesu Kristo katika umri wa miaka 12, ameketi ndani ya hekalu la Mungu kati ya walimu wa sheria na akiwafundisha mambo matakatifu, ninatambua kuwa Yeye tayari, mapema katika maisha Yake, alikuwa na chembechembe ya ujasiri, ujasiri maalumu. Wakati wengi wangetarajia kuona mvulana akifundishwa na walimu wa sheria, Yeye alikuwa akiwafundisha wao wakati “wakimsikiliza na kumuuliza maswali” (Tafsiri ya Joseph Smith , Luka 2:46 [katika Luka 2:46, tanbihi c]).

Tulihudumu katika misheni ya Mbuji-Mayi Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo kuanzia 2016 mpaka 2019. Njia ya kusafiri tukiwa misheni kutoka kanda moja mpaka nyingine ilikuwa kwa barabara. Tukio lilikuwa limetukia katika eneo ambapo wanyang’anyi waliojiami kwa silaha kali waliingia barabarani na kuvuruga mwendo wa wasafiri.

Wamisionari watano waliokuwa wakisafiri kutoka kanda yetu kwenda nyingine kama sehemu ya uhamisho walikuwa wahanga wa vurugu hizi. Tukiwa wahanga wa tukio hili sisi wenyewe hapo kabla, tulianza kuhofia maisha na usalama wetu sote, hata kusita kusafiri katika njia hizi kuwatembelea wamisionari na kufanya mikutano ya kanda. Hatukufahamu matukio hayo yangedumu kwa muda gani. Niliandika ripoti, ambayo niliituma kwa Urais wa Eneo na nilielezea hisia zangu za hofu kuhusu kuendelea kusafiri wakati ambapo barabara ilikuwa ndiyo njia pekee ya kuwafikia wamisionari wetu.

Katika majibu yake, Mzee Kevin Hamilton, ambaye alikuwa rais wetu wa Eneo la Afrika Kusini mashariki, aliniandikia: “Ushauri wangu ni kwamba ufanye kadiri ya uwezo wako. Kuwa mwenye busara na mwenye kuomba. Kwa kujua msijiweke ninyi au wamisionari wenu kwenye hatari, lakini wakati huo huo songeni mbele kwa imani. ‘Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi’ (2 Timotheo 1:7).”

Ushawishi huu ulituimarisha kwa kiasi kikubwa na kuturuhusu kuendelea kusafiri na kutumikia kwa ujasiri mpaka mwisho wa misheni yetu kwa sababu tulisikia maelekezo kutoka kwa Baba yetu wa Mbinguni kupitia andiko lile.

Katika maandiko ya siku za leo, tunasoma maneno yenye uvuvio ya Nabii Joseph Smith yakizungumzia maneno ya Bwana ya kututia moyo: “Ndugu, je, si lazima sisi tuendelee katika kazi hii iliyo kuu? Twende mbele na siyo nyuma. Tuweni wajasiri, ndugu; na mbele, mbele kwenye ushindi!” (Mafundisho na Maagano 128:22).

Acha tuwe na ujasiri wa kutenda kile kilicho sahihi hata kama hakina umaarufu—ujasiri wa kutetea imani yetu na kutenda kwa imani. Acha tuwe na ujasiri wa kutubu kila siku, ujasiri wa kukubali mapenzi ya Mungu na kutii amri Zake. Acha tuwe na ujasiri wa kuishi kwa uadilifu na kutenda kile kinachotarajiwa kwetu katika majukumu na nafasi mbalimbali.

Sifa ya tatu ya Mwokozi ni msamaha. Wakati wa huduma Yake duniani, Mwokozi alimlinda mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi dhidi ya kupigwa mawe. Alimpa agizo “enenda zako; wala usitende dhambi tena.” (Yohana 8:11). Hili lilimuongoza kwenye toba na hatimaye msamaha, kwani kama maandiko yanavyorekodi, “mwanamke alimtukuza Mungu toka saa ile na kuamini katika jina lake” (Tafsiri ya Joseph Smith, Yohana 8:11 [katika Yohana 8:11, tanbihi c).

Wakati wa ibada ya Krismasi mnamo Desemba 2018, Rais wetu mpendwa Russell M. Nelson alizungumza kuhusu zawadi nne tulizopokea kutoka kwa Mwokozi. Alisema kwamba zawadi moja ambayo Mwokozi anatoa ni uwezo wa kusamehe:

“Kupitia Upatanisho Wake usio na mwisho, unaweza kuwasamehe wale wanaokuudhi na ambao kamwe hawawezi kukubali kuwajibika kwa ajili ya ukatili wao kwako.

“Ni rahisi mara zote kumsamehe mtu ambaye kwa dhati na kwa unyenyekevu anatafuta msamaha wako. Lakini Mwokozi atakupa uwezo wa kumsamehe yeyote ambaye amekutendea vibaya katika njia yoyote” (“Zawadi Nne Ambazo Yesu Kristo Anatoa Kwako” [First Presidency Christmas devotional, Dec. 2, 2018], broadcasts.ChurchofJesusChrist.org).

Acha kwa dhati tusameheane ili kupokea msamaha wa Baba. Msamaha hutuweka huru na kutufanya wenye kustahili kupokea sakramenti kila Jumapili. Msamaha unahitajika kwa ajili yetu ili tuwe wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo.

Sifa ya nne ya Mwokozi ni dhabihu. Ni sehemu ya injili ya Yesu Kristo. Mwokozi alitoa dhabihu ya juu ya maisha Yake kwa ajili yetu ili kwamba tuweze kukombolewa. Akihisi maumivu ya dhabihu, Alimwomba Baba Yake kumuondolea kikombe, lakini aliendelea mpaka mwisho wa dhabihu ya milele. Huu ni Upatanisho wa Yesu Kristo.

Rais M. Russell Ballard alifundisha hili: “Dhabihu [ni] kielelezo cha upendo msafi. Kiwango cha upendo wetu kwa Bwana, kwa injili na kwa wanadamu wenzetu kinaweza kupimwa kwa kile tulicho tayari kutoa dhabihu kwa ajili yao” (“The Blessings of Sacrifice,” Ensign, Mei 1992).

Tunaweza kutoa dhabihu muda wetu ili kuhudumu, kuwatumikia wengine, kutenda mema, kufanya kazi ya historia ya familia na kukuza miito yetu ya Kanisa.

Tunaweza kutoa fedha zetu kwa kulipa zaka, matoleo ya mfungo na matoleo mengine ili kujenga ufalme wa Mungu duniani. Tunahitaji dhabihu ili kutunza maagano tuliyofanya na Mwokozi.

Ombi langu ni kwamba kwa kumfuata Yesu Kristo na kupokea baraka za Upatanisho Wake, tuwe wanyenyekevu zaidi na zaidi, tuwe wenye ujasiri zaidi na zaidi, tusamehe zaidi na zaidi na tutoe dhabihu zaidi na zaidi kwa ajili ya ufalme Wake.

Ninashuhudia kwamba Baba yetu wa Mbinguni yu hai na kwamba Yeye anatujua sisi binafsi, kwamba Yesu ndiye Kristo, kwamba Rais Russell M. Nelson ni nabii wa Mungu leo. Ninashuhudia kwamba Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni ufalme wa Mungu duniani na Kitabu cha Mormoni ni cha kweli. Katika jina la Yesu Kristo, Mkombozi wetu, amina.