Mkutano Mkuu
Wakumbuke Watakatifu Wako Wanaoteseka, Ee Mungu Wetu
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2021


Wakumbuke Watakatifu Wako Wanaoteseka, Ee Mungu Wetu

Kutunza maagano kunafungua nguvu ya dhabihu ya upatanisho wa Yesu Kristo ili kutoa nguvu na hata shangwe kwako wewe unayeteseka.

Mpango wa furaha wa Baba wa Mbinguni unajumuisha uzoefu wa maisha ya duniani ambapo watoto Wake wote watajaribiwa na kukabiliana na majaribu.1 Miaka mitano iliyopita niligundulika kuwa na saratani. Nimehisi na bado ninahisi maumivu ya mwili kutokana na upasuaji, matibabu ya mionzi pamoja na matokeo ya matumizi ya madawa. Nimepitia mapambano ya kihisia nyakati za mateso za kukosa usingizi usiku. Takwimu za kitabibu zinaonesha pengine nitaondoka katika maisha haya mapema kuliko nilivyotarajia, nikiacha nyuma, kwa kipindi kifupi, familia ambayo inamaanisha kila kitu kwangu.

Bila kujali popote unapoishi, mateso ya kimwili au kihisia kutokana na majaribu mbalimbali na udhaifu wa maisha haya yamekuwa, ni, au siku moja yatakuwa sehemu ya maisha yako.

Mateso ya kimwili yanaweza kutokana na kuongezeka umri, magonjwa yasiyoratajiwa na ajali zisizotarajiwa, njaa au kukosa makazi; au unyanyasaji, matendo ya vurugu na vita.

Mateso ya kihisia yanaweza kutokana na wasiwasi au msongo wa mawazo; usaliti wa mwenza, mzazi au kiongozi wa kuaminika; kupoteza kazi au pesa; hukumu isiyo haki kutoka kwa wengine; chaguzi za marafiki, watoto au wanafamilia wengine; unyanyasaji katika aina zake nyingi; ndoto ambazo hazijatimia za ndoa au watoto; ugonjwa wa kudhoofisha au kifo cha mapema cha mpendwa; au vyanzo vingine vingi.

Ni kwa jinsi gani unaweza kuvumilia mateso ya kipekee na wakati mwingine ya kudhoofisha ambayo huja kwa kila mmoja wetu?

Kwa shukrani, tumaini hupatikana katika injili ya Yesu Kristo na tumaini linaweza pia kuwa sehemu ya maisha yako. Leo ninashiriki kanuni nne za tumaini zilizotolewa kwenye maandiko, mafundisho ya kinabii, matembezi mengi ya uhudumiaji na jaribu langu mwenyewe endelevu la kiafya. Kanuni hizi si tu zinatumika kwa kiasi kikubwa bali pia ni binafsi sana.

Kwanza, mateso hayamaanishi kwamba Mungu hapendezwi na maisha yako. Miaka elfu mbili iliyopita, wanafunzi wa Yesu walimwona mtu kipofu hekaluni na kuuliza, “Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu?”

Wanafunzi wake walionekana kuamini kimakosa kama ilivyo kwa wengi leo, kwamba magumu na mateso yote katika maisha ni matokeo ya dhambi. Lakini Mwokozi alijibu, “Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake: bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake.”2

Kazi ya Mungu ni kuleta kutokufa kwetu na uzima wa milele.3 Lakini ni jinsi gani majaribu na mateso—hususan mateso yanayoletwa na matumizi ya dhambi ya mtu mwingine ya haki ya kujiamulia4—hatimaye husongesha kazi ya Mungu?

Bwana aliwaambia watu Wake wa agano, Nimekusafisha … ; nimekuchagua katika tanuru ya mateso.”5 Bila kujali sababu ya mateso yako, Baba yako wa Mbinguni mwenye upendo anaweza kuyaongoza yasafishe nafsi yako.6 Nafsi zilizosafishwa zinaweza kubeba mizigo ya wengine kwa huruma ya dhati.7 Nafsi zilizosafishwa ambazo zimetoka “katika dhiki ile iliyo kuu” zimeandaliwa kuishi kwa shangwe katika uwepo wa Mungu milele na “Mungu atayafuta machozi yote katika macho yao.”8

Pili, Baba wa Mbinguni anaelewa kwa kina mateso yako. Tukiwa katikati ya majaribu, tunaweza kimakosa kudhani kwamba Mungu yuko mbali na hajali maumivu yetu. Hata Nabii Joseph Smith alielezea hisia hii kwenye wakati mgumu katika maisha yake. Alipofungwa katika Jela ya Liberty wakati maelfu ya Watakatifu wa Siku za Mwisho wakifukuzwa kutoka kwenye miji yao, Joseph alitafuta uelewa kupitia sala: “Ee Mungu, uko wapi? Na ni wapi lilipo hema lifichalo mahali pako pa kujificha?” Alihitimisha kwa ombi hili: “Wakumbuke watakatifu wako wanaoteseka, Ee Mungu wetu.”9

Jibu la Bwana lilimhakikishia Joseph na wale wote wanaoteseka:

“Mwanangu, amani iwe katika nafsi yako; taabu yako na mateso yako yatakuwa kwa muda mfupi;

“Na halafu, kama utastahimili vyema, Mungu atakuinua juu.”10

Watakatifu wengi wenye mateso wameshiriki nami jinsi walivyohisi upendo wa Mungu wakati wa majaribu yao. Ninafikiria dhahiri uzoefu wangu mwenyewe kwenye wakati fulani katika mapambano yangu ya saratani wakati ambapo madaktari walikuwa bado hawajagundua sababu ya maumivu makali. Niliketi pamoja na mke wangu, nikitarajia kutoa baraka kwa ajili ya chakula chetu cha mchana. Badala yake, yote niliyoweza kufanya ilikuwa kulia tu, “Baba wa Mbinguni, tafadhali nisaidie. Ninaumwa sana.” Kwa sekunde 20 mpaka 30 zilizofuatia, nilikuwa nimezungukwa na upendo Wake. Sikupewa sababu yoyote ya ugonjwa wangu, hakuna kiashirio cha hatma ya matokeo na hakuna nafuu ya maumivu. Nilihisi tu upendo Wake msafi na hilo lilikuwa, na, ni la kutosha.

Ninashuhudia kwamba Baba yetu wa Mbinguni, anayejua hata anguko la shomoro mmoja, anafahamu mateso yako.11

Tatu, Yesu Kristo anatoa nguvu Yake ya uwezesho ili kukusaidia uwe na nguvu ya kuvumilia mateso yako vyema. Nguvu hii ya uwezesho inafanywa iwezekane kupitia Upatanisho Wake.12 Nina hofu kwamba waumini wengi wa Kanisa wanadhani ikiwa ni wagumu kiasi, wanaweza kushinda mateso yoyote wao peke yao. Hii ni njia ngumu ya kuishi. Muda wako mfupi wa kuwa na nguvu kamwe hauwezi kulinganishwa na utoaji usio na mwisho wa nguvu ya Mwokozi ya kuimarisha nafsi yako.13

Kitabu cha Mormoni kinafundisha kwamba Yesu Kristo “angejichukulia” maumivu yetu, magonjwa na unyonge wetu ili Aweze kutusaidia.14 Ni jinsi gani unaweza kuvuta nguvu ambayo Yesu Kristo anatoa kukusaidia na kukuimarisha katika nyakati za mateso? Jambo muhimu ni kujiunganisha kwa Mwokozi kwa kutii maagano uliyofanya Naye. Tunafanya maagano haya wakati tunapopokea ibada za ukuhani.15

Watu wa Alma waliingia kwenye agano la ubatizo. Baadaye waliteseka katika utumwa na walizuiliwa kuabudu hadharani au hata kuomba kwa sauti. Lakini bado walitunza maagano yao vizuri kadiri walivyoweza kwa kuomba kimya kimya ndani ya mioyo yao. Kama matokeo, nguvu ya kiungu ilikuja. “Bwana aliwapatia nguvu kwamba wabebe mizigo yao kwa urahisi.”16

Katika siku yetu Mwokozi anaalika, “Nitegemeeni katika kila wazo; msitie shaka, msiogope.”17 Wakati tunapotunza agano letu la sakramenti la daima kumkumbuka, Yeye anaahidi kwamba Roho Wake atakuwa pamoja nasi. Roho hutupatia nguvu ya kuvumilia majaribu na kufanya kile tusichoweza kufanya peke yetu. Roho anaweza kutuponya, japokuwa kama Rais James E. Faust alivyofundisha, “Baadhi ya uponyaji huu unaweza kutokea katika ulimwengu mwingine.”18

Tumebarikiwa pia kwa maagano na ibada za hekaluni, ambapo kwazo “nguvu za uchamungu hudhihirika.”19 Nilimtembelea mwanamke ambaye alimpoteza binti kijana katika ajali mbaya, kisha baadaye mumewe kwa saratani. Nilimuuliza jinsi anavyoweza kuvumilia upotevu na mateso kama hayo. Alijibu kwamba nguvu ilikuja kutokana na mahakikisho ya kiroho ya familia ya milele, yaliyopokelewa wakati wa kuabudu mara kwa mara hekaluni. Kama ilivyoahidiwa, ibada za nyumba ya Bwana zilimkinga kwa nguvu za Mungu.20

Nne, chagua kupata shangwe kila siku. Wale wanaopata mateso mara kwa mara wanahisi kwamba mateso yanaendelea tena na tena na nafuu kamwe haitakuja. Ni SAWA kulia.21 Ndiyo, ukijikuta katika usiku wa kiza wa mateso, kwa kuchagua imani unaweza kuamka kwenye asubuhi angavu za shangwe.22

Kwa mfano, nilimtembelea mama kijana aliyekuwa akipatiwa matibabu ya saratani, akitabasamu kwa ujasiri katika kiti chake licha ya maumivu na kukosa nywele. Nilikutana na wanandoa wa umri wa kati kwa furaha wakihudumu kama viongozi wa vijana japo hawakuwa na uwezo wa kuzaa watoto. Niliketi pamoja na mwanamke mpendwa—ambaye ni bibi, mama na mke—ambaye angefariki ndani ya siku chache; na bado katikati ya machozi ya familia kulikuwepo vicheko na kumbukumbu zenye shangwe.

Watakatifu hawa wanaoteseka wanadhihirisha kile Rais RussellM. Nelson alichofundisha:

“Shangwe tunayoihisi inahusika kwa kiasi kidogo na hali ya maisha yetu na inahusika na kila kitu kinachohusu fokasi ya maisha yetu.

“Wakati fokasi ya maisha yetu ipo katika mpango wa Mungu wa wokovu … na Yesu Kristo na injili Yake, tunaweza kuhisi shangwe bila kujali nini kinatokea—au hakitokei—katika maisha yetu.”23

Ninashuhudia24 kwamba Baba yetu wa Mbinguni anawakumbuka Watakatifu Wake wanaoteseka, anawapenda na anawajua kwa kina. Mwokozi wetu anafahamu jinsi mnavyohisi. “Kwa hakika amechukua ghamu zetu, na kubeba huzuni zetu.”25 Ninajua—kama mpokeaji wa kila siku26—kutunza maagano hufungua nguvu ya dhabihu ya upatanisho wa Yesu Kristo ili kutoa nguvu na hata shangwe kwako wewe unayeteseka.

Kwa wote mnaoteseka, ninaomba, “Mungu akubali kwamba mizigo yenu iwe miepesi, kupitia shangwe inayotokana na Mwana wake.”27 Katika Jina la Yesu Kristo, amina.

Chapisha