Mkutano Mkuu
Asilimia Moja Bora Zaidi
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2021


10:1

Asilimia Moja Bora Zaidi

Kila juhudi ya kubadilika tuifanyayo—bila kujali ni ndogo kiasi gani kwetu—inaweza kuleta badiliko kubwa katika maisha yetu.

Kwa zaidi ya karne moja, timu za kitaifa za mbio za baisikeli za Uingereza zilikuwa kicheko cha ulimwengu wa baiskeli. Wakiwa wamemezwa kwenye ukawaida, waendesha baisikeli wa Uingereza walikuwa na kiganja kimoja tu cha medani za dhahabu kwa miaka 100 ya mashindano ya Olimpiki na walidhoofishwa zaidi katika tukio la kuendesha baiskeli la marquee, mashindano yenye ushindani mkali ya wiki 3 ya Tour de France—ambapo hakuna mwendesha baisikeli wa Uingereza aliyeshinda kwa miaka 110. Ilikuwa ya kusikitisha sana kwa waendesha baisikeli wa Uingereza kwamba baadhi ya watengenezaji wa baisikeli walikataa kuuza baiskeli kwa Waingereza, wakihofia kuwa ingeweza kuchafua sifa ya kampuni. Na licha ya kutumia rasilimali nyingi katika teknolojia na kila aina mpya ya mafunzo, hakuna kilichofanya kazi.

Waendesha baiskeli wa Uingereza

Hakuna chochote, mpaka 2003, wakati mabadiliko madogo, ambayo hayakutambuliwa kwa ukubwa yalitokea ambayo yangebadilisha kabisa mfumo wa uendeshaji baisikeli wa Uingereza. Mbinu hiyo pia ingeainisha kanuni ya milele—yenye ahadi—kuhusu dhumuni letu la kutatanisha la maisha haya ya duniani la kuwa bora zaidi. Hivyo ni nini kilitokea katika uendeshaji wa baisikeli huko Uingereza ambacho kina uhusiano mkubwa na dhumuni letu binafsi la kuwa wana na mabinti bora wa Mungu?

Mnamo 2003, Bwana Dave Brailsford aliajiriwa. Tofauti na makocha waliopita ambao walijaribu mabadiliko makubwa, kwa mara moja, Bwana Brailsford badala yake alijikita kwenye mkakati ambao aliutaja kama “ujumuishaji wa faida kidogo kidogo.” Hii ilijumuisha kutekeleza maboresho madogo madogo katika kila kitu. Hiyo ilimaanisha kufuatilia takwimu mara kwa mara na kujikita kwenye mafunzo yanayolenga kwenye udhaifu maalum.

Hili linaendana na wazo la nabii Samweli Mlamani aliloliita “kutembea kwa uangalifu.”1 Mtazamo huu mpana na jumuishi unaepuka mtego wa kuwa na mtazamo usiobadilika kwenye tatizo la kawaida au dhambi. Brailsford alisema, “Kanuni yote ilikuja kutokana na wazo kwamba ikiwa utanyumbulisha kila kitu unachoweza kufikiria ambacho kinahusiana na uendeshaji baisikeli, na kisha kukiboresha kwa asilimia moja, utapata ongezeko kubwa wakati utakapounganisha vyote.”2

Mbinu yake inaendana vyema na ile ya Bwana, ambaye alitufundisha umuhimu wa asilimia 1—hata kwa gharama ya asilimia 99. Ndiyo, alikuwa akifundisha injili ya umuhimu wa kuwatafuta watu walio na uhitaji. Lakini vipi ikiwa tutatumia kanuni hiyo hiyo kwenye kanuni nzuri ya pili ya injili, toba? Badala ya kufadhaishwa na ghasia na kuambaa ambaa kati ya dhambi na toba, vipi ikiwa mbinu yetu ingekuwa kuileta fokasi yetu mahala pamoja—hata pale tunapoikuza? Badala ya kujaribu kufanya kila kitu sawia, vipi kama tukishughulikia kitu kimoja?

Kwa mfano, vipi ikiwa kwa mtazamo wako mpya, unagundua umepuuzia kusoma Kitabu cha Mormoni kila siku? Naam, badala ya kujaribu kwa bidii kumaliza kurasa zote 531 kwa usiku mmoja, vipi kama tutajikita kusoma asilimia moja tu ya hiyo—hiyo ni kurasa tano tu kwa siku—au kiasi kingine unachohisi kitaendana na lengo lako? Je, ujumuishaji wa nyongeza ndogo ndogo lakini za mara kwa mara katika maisha yetu hatimaye ingeweza kuwa njia ya ushindi hata kwenye changamoto za mapungufu yetu? Je, njia hii ya kidogo kidogo kushughulikia mawaa yetu kweli inafanya kazi?

Mwandishi mahiri James Clear anasema mbinu hii inaweka hesabu katika pembe mraba kwa manufaa yetu. Anasisitiza kuwa “tabia ni ‘riba iongezekayo ya ukuaji binafsi’. Ikiwa unaweza kupata angalau asilimia moja tu ya kuwa bora kwenye kitu fulani kila siku, mwisho wa mwaka … utakuwa bora zaidi mara 37.”3

Maboresho madogo madogo ya Brailsford yalianza na mambo ya kawaida, kama vile vifaa vya baiskeli, vitambaa, na mifumo ya mafunzo. Lakini timu yake haikuishia hapo. Waliendelea kutafuta maboresho ya asilimia moja katika maeneo yaliyopuuzwa na yasiyotarajiwa kama lishe na hata changamoto za utunzaji baiskeli. Baada ya muda, haya maelfu ya maboresho madogo madogo yalijumuishwa na kuwa matokeo mazuri, ambayo yalikuja haraka kuliko ambavyo mtu yeyote angeweza kufikiria. Kwa kweli, walikuwa kwenye kanuni ya milele ya “mstari juu ya mstari, amri juu ya amri, hapa kidogo na pale kidogo.”4

Je, maboresho madogo madogo yanaweza kuleta “badiliko kuu”5 unalolitamani? Yakitekelezwa vizuri, nina uhakika asilimia 99 yataleta badiliko! Lakini tahadhari moja juu ya mbinu hii ni kwamba ili faida ndogo ndogo zijikusanye, lazima kuwe na juhudi endelevu, za siku hadi siku. Na ingawa hatuwezi kuwa wakamilifu, lazima tuazimie kuonyesha jitihada zetu kwa uvumilivu. Fanya hivyo, na thawabu tamu za ongezeko la uadilifu zitaleta furaha na amani unayotafuta. Kama Rais Nelson alivyofundisha: “Hakuna kinacholeta uhuru zaidi, cha kiungwana zaidi, au cha muhimu zaidi kwa ukuaji wetu binafsi kuliko ilivyo fokasi yetu ya kila siku, kwenye toba. Toba siyo tukio; ni mchakato. Ni ufunguo kwa furaha na amani ya akili. Inapoambatana na imani, toba hufungua ufikiaji wetu kwenye nguvu za Upatanisho za Yesu Kristo.”6

Mbegu ya haradali
Mti wa muharadali

Kwa kuwa toba hufuatia imani, maandiko yako wazi. Yote yanayohitajika kwanza ni “chembe ya imani.”7 Na ikiwa tunaweza kuilea hii “mbegu ya haradali”8 kimawazo, sisi pia tunaweza kutarajia maboresho yasiyotarajiwa na ya kipekee katika maisha yetu. Lakini kumbuka, kama vile ambavyo hatuwezi kujaribu kutoka kuwa kama Atila wa kabila la Hun kuwa Mama Teresa kwa usiku mmoja, vivyo hivyo tunapaswa kurekebisha mifumo yetu ya maboresho kidogo kidogo. Hata kama mabadiliko yanayohitajika katika maisha yako ni ya jumla, anza kwa kiwango kidogo. Hiyo ni kweli hasa ikiwa unahisi kuzidiwa au kukata tamaa.

Mchakato huu mara zote hautimii kwa mtindo wa aina moja. Hata kati ya wale waliodhamiria zaidi bado kunaweza kuwa na vikwazo. Nikiwa nimepitia maudhi ya hili katika maisha yangu mwenyewe, najua kwamba wakati mwingine inaweza kuonekana kama asilimia 1 mbele na asilimia 2 nyuma. Walakini ikiwa tutabaki bila hofu katika azimio letu la kupata faida ya asilimia 1, Yeye ambaye “amebeba huzuni zetu”9 hakika atatubeba.

Ni dhahiri kwamba, ikiwa tumejihusisha katika dhambi kubwa, Bwana ameweka wazi na kwa usahihi; tunahitaji kuacha, tupate msaada kutoka kwa askofu wetu, na tuachane na mazoea kama hayo mara moja. Lakini kama vile Mzee David A. Bednar alivyofundisha: “Maboresho madogo madogo, thabiti, ya kuwa bora kiroho ni hatua ambazo Bwana angependa tuchukue. Kujiandaa kutembea bila hatia mbele za Mungu ni moja ya malengo ya msingi ya maisha ya duniani na dhumuni la maisha yote; halitokei mara moja kutokana na shughuli mbalimbali za kiroho.”10

Waendesha baiskeli wa Uingereza

Je, njia hii rahisi ya toba na mabadiliko ya kweli inafanya kazi? Je, hili ni kweli katika uendeshaji baisikeli? Tafakari kile kilichotokea kwa waendesha baisikeli wa Uingereza katika miongo miwili iliyopita tangu kutekelezwa kwa falsafa hii. Waendesha baiskeli wa Uingereza sasa wameshinda mara sita taji la Tour de France. Wakati wa Michezo minne ya Olimpiki iliyopita, Uingereza imekuwa nchi yenye mafanikio zaidi katika taaluma zote za baiskeli. Na katika Olimpiki ya Tokyo iliyomalizika hivi karibuni, Uingereza ilishinda medali nyingi za dhahabu kwenye baiskeli kuliko nchi nyingine yoyote.

Washindi wa olimpiki

Picha za waendesha baiskeli wa Uingereza na (kutoka kulia kwenda kushoto) Friedemann Vogel, John Giles, na Greg Baker/Getty Images

Lakini ipitayo hata fedha au dhahabu ing’aayo, ni ahadi yetu ya thamani kuelekea umilele kwamba kwa kweli “tutashinda katika Kristo.”11 Na tunapodhamiria kufanya maboresho madogo madogo lakini endelevu, tunaahidiwa “taji ya utukufu isiyofifia.”12 Ili wewe pia uweze kufurahi kwenye mwangaza usiofifia, ninakualika uchunguze maisha yako na uone kile kinachokukwamisha au kukupunguzia kasi kwenye njia ya agano. Kisha angalia kiupana. Fanya marekebisho ya staha yenye kujenga katika maisha yako ambayo yanaweza kuleta furaha tamu ya kuwa bora kidogo kidogo.

Kumbuka, Daudi alitumia jiwe moja tu dogo kuliangusha jitu lililoonekana lisiloshindwa. Lakini alikuwa na mawe mengine manne tayari. Vivyo hivyo, tabia ya uovu ya Alma Mdogo na hatma ya milele ilibadilika kwa wazo moja rahisi, la dhati—kumbukumbu ya mafundisho ya baba yake kuhusu rehema okozi za Yesu Kristo. Na ndivyo ilivyo kwa Mwokozi wetu, ambaye, ingawa hakuwa na dhambi, “hakupokea utimilifu kwanza, … lakini aliendelea kutoka neema hadi neema, hata alipopokea utimilifu wote.”13

Yesu Kristo

Ni Yeye anayejua wakati shomoro anapoanguka ambaye vilevile Anazingatia dakika na vilevile wakati muhimu maishani mwetu na ambaye yuko tayari sasa hivi kukusaidia katika chochote ambacho asilimia yako 1 italeta kutoka kwenye mkutano huu. Kwa sababu kila juhudi ya kubadilika tuifanyayo—bila kujali ni ndogo kiasi gani kwetu—inaweza tu kuleta badiliko kubwa maishani mwetu.

Kwa dhumuni hili, Mzee Neal A. Maxwell alifundisha, “Kila madai ya tamanio la haki, kila tendo la huduma, na kila tendo la ibada, hata liwe dogo na kubwa kiasi gani, linaongeza kwenye kasi yetu ya kiroho.”14 Kweli, ni kwa vitu vidogo, rahisi, na, ndiyo, hata vya asilimia 1 tu kwamba mambo makubwa hufanyika.15 Ushindi kamili ni asilimia 100, “baada ya yote tunayoweza kufanya,”16 kupitia, uwezo, fadhila na rehema za Bwana wetu na Mwokozi, Yesu Kristo. Ninashuhudia hivyo katika jina la Yesu Kristo, amina.