Mkutano Mkuu
Kuzungumzia Afya ya Akili
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2021


9:27

Kuzungumzia Afya ya Akili

Niruhusuni nishiriki ugunduzi kadhaa niliofanya wakati familia yangu ilipopitia majaribu.

Japokuwa familia yetu imefurahia baraka tele wakati tukitembea kwa furaha kwenye njia ya agano, tumekabiliwa pia na majaribu makubwa ya maisha. Nataka kushiriki uzoefu binafsi sana kuhusu ugonjwa wa akili. Uzoefu huu hujumuisha mfadhaiko mkubwa, wasiwasi mkubwa, kukasirika ghafla, kupoteza umakini—na wakati mwingine mchanganganyiko wa hayo yote. Ninashiriki uzoefu huu wa huruma kwa idhini ya wale wanaohusika.

Wakati wa huduma yangu, nimekutana na mamia ya watu pamoja na familia zenye uzoefu sawa na huu. Nyakati zingine ninajiuliza ikiwa “maradhi ya ukiwa” yanayoifunika nchi, kama yalivyotajwa katika maandiko, yanaweza kujumuisha ugonjwa wa akili.1 Ni wa ulimwengu wote, ukifikia kila bara na utamaduni, na ukiwaathiri wote—mdogo, mkubwa, tajiri na masikini. Waumini wa Kanisa hawajaachwa kando.

Wakati huo huo mafundisho yetu yanatufundisha kujitahidi kuwa kama Yesu Kristo na kukamilishwa ndani Yake. Watoto wetu huimba, “Ninajaribu Kuwa Kama Yesu.”2 Tunatamani kuwa wakamilifu kama Baba yetu wa Mbinguni na Yesu Kristo walivyo wakamilifu.3 Kwa sababu ugonjwa wa akili unaweza kuingilia mtazamo wetu wa ukamilifu, mara nyingi unabaki kuwa jambo lisilozungumziwa. Kama matokeo, kuna ujinga mwingi, maumivu mengi ya kimya kimya, na kukata tamaa kwingi. Wengi, wakihisi kuzidiwa kwa sababu hawakidhi viwango vinavyotambulika, kimakosa huamini kwamba hawana nafasi ndani ya Kanisa.

Ili kukabiliana na uongo huo, ni muhimu kukumbuka kwamba “Mwokozi anampenda kila mmoja wa watoto Wake. Anafahamu kikamilifu maumivu na mateso ambayo wengi huyapitia wakati wanapoishi wakiwa na changamoto nyingi za afya ya akili. Yeye aliteseka ‘maumivu na masumbuko na majaribio ya kila aina; … [akijichukulia] maumivu na magonjwa ya watu wake’ (Alma 7:11; msisitizo umeongezwa; ona pia Waebrania 4:15–16; 2 Nefi 9:21). Kwa sababu anaelewa maumivu yote, Yeye anafahamu jinsi ya ‘kuwaponya waliovunjika moyo.’ (Luka 4:18; ona pia Isaya 49:13–16).”4 Changamoto mara nyingi huashiria hitaji la nyenzo za ziada na msaada na si dosari ya kitabia.

Niruhusuni nishiriki ugunduzi kadhaa niliofanya wakati familia yangu ilipopitia majaribu.

Kwanza, watu wengi wataomboleza pamoja nasi; hawatatuhukumu. Kutokana na hisia kali za kushindwa, wasiwasi na mfadhaiko, kijana wetu alirejea nyumbani kutoka kwenye misheni yake baada ya wiki nne tu. Kama wazazi wake, tulipata wakati mgumu kushughulikia ukataji tamaa na huzuni kwa sababu tulikuwa tumeomba sana kwa ajili ya mafanikio yake. Kama vile wazazi wote, tunataka watoto wetu wafanikiwe na wawe na furaha. Misheni ilikuwa tukio muhimu kwa kijana wetu. Tulijiuliza pia kile ambacho wengine wangefikiria.

Bila kujua kilichokuwa mbele yetu, kurejea kwa kijana wetu lilikuwa jambo la kuumiza sana kwake. Kumbuka kwamba alimpenda Bwana na alitaka kutumikia, na bado asingeweza kutokana na sababu alizopambana kuzielewa. Punde alijikuta kwenye hatua ya kukosa tumaini kabisa, akipambana na hatia kubwa. Hakuhisi tena kukubalika bali kufa ganzi kiroho. Alizidiwa na hisia za kujirudia za kifo.

Akiwa katika hali hii ya kutoweza kufanya maamuzi sahihi, kijana wetu aliamini kwamba suluhisho pekee lililobakia lilikuwa ni kuondoa uhai wake. Ilichukua Roho Mtakatifu na jeshi la malaika pande zote mbili za pazia kumwokoa.

Wakati akipigania maisha yake na wakati wa kipindi hiki kigumu sana, familia yetu, viongozi wa kata, waumini na marafiki walifanya juhudi ya ziada ili kutusaidia na kutuhudumia.

Sikuwahi kamwe kuhisi mmiminiko wa upendo kama huo. Sikuwahi kamwe kuhisi kwa nguvu kubwa na katika njia binafsi zaidi kile inachomaanisha kuwafariji wale wanaohitaji kufarijiwa. Familia yetu daima itakuwa yenye shukrani kwa mmiminiko huo.

Siwezi kuelezea miujiza isiyo na idadi ambayo iliambatana na matukio haya. Kwa shukrani, kijana wetu alinusurika, lakini imechukua muda mrefu na uangalizi mkubwa wa madawa, matibabu na kiroho kwa yeye kupona na kukubali kwamba anapendwa, anathaminiwa na anahitajika.

Ninatambua kwamba si matukio yote ya aina hiyo huisha kama letu. Ninahuzunika pamoja na wale ambao wamepoteza wapendwa wao mapema sana na kwa sasa wamebaki na hisia za majonzi na maswali yasiyo na majibu.

Ugunduzi wangu wa pili ni kwamba inaweza kuwa ngumu kwa wazazi kutambua masumbuko ya watoto wao, lakini lazima tujielimishe. Ni jinsi gani tunaweza kufahamu tofauti kati ya magumu yanayoambatana na ukuaji wa kawaida na dalili za ugonjwa? Kama wazazi, tuna jukumu takatifu la kuwasaidia watoto wetu kupita katika changamoto za maisha; hata hivyo, wachache kati yetu ni wataalamu wa afya ya akili. Sisi, hata hivyo, tunahitaji kuwajali watoto wetu kwa kuwasaidia wajifunze kuridhika kwa juhudi zao za dhati wakati wanapojitahidi kukidhi matarajio sahihi. Kila mmoja wetu anafahamu kutokana na mapungufu yetu binafsi kwamba ukuaji wa kiroho ni mchakato endelevu.

Sasa tunaelewa kwamba “hakuna suluhisho rahisi la jumla kwa tiba ya akili. Tutapitia uzoefu wa msongo wa mawazo na msukosuko kwa sababu tunaishi katika ulimwengu ulioanguka tukiwa na mwili ulioanguka. Kwa nyongeza, mambo mengi yanayochangia yanaweza kuongoza kwenye utambuzi wa ugonjwa wa akili. Licha ya kuwa kwetu vizuri kiakili na kihisia, kufokasi kwenye ukuaji kunaleta afya zaidi kuliko kufikiria kuhusu mapungufu yetu.”5

Kwangu mimi na mke wangu, kitu kimoja ambacho daima kimetusaidia kilikuwa ni kuwa karibu na Bwana kadiri ilivyowezekana. Katika utambuzi, sasa tunaona ni jinsi gani Bwana kwa uvumilivu alitufunza kupitia nyakati za wasiwasi mkubwa. Nuru yake ilituongoza hatua kwa hatua kupita nyakati za giza. Bwana alitusaidia kuona kwamba thamani ya nafsi ya mtu ni muhimu zaidi katika mpango wa milele kuliko jukumu lolote au mafanikio ya kidunia.

Tena, kujielimisha kuhusu ugonjwa wa akili kunatuandaa kujisaidia sisi na wengine ambao yaweza kuwa wanateseka. Mijadala ya wazi na ya uaminifu kwa kila mmoja itasaidia mada hii muhimu kupata umakini inayostahili kupata. Hata hivyo, taarifa hutangulia msukumo na ufunuo. Changamoto hizi zisizoonekana mara nyingi zinaweza kumuathiri yeyote, na tunapokabiliana nazo, zinaonekana hazitatuliki.

Moja ya vitu vya mwanzo tunavyohitaji kujifunza ni kwamba hakika hatuko peke yetu. Ninawaalika mjifunze mada ya afya ya akili katika kipengele cha Msaada wa Maisha cha programu ya Maktaba ya Injili. Kujifunza kutaongoza kwenye uelewa zaidi, ukubali zaidi, huruma zaidi, upendo zaidi. Kunaweza kupunguza majanga, wakati kukitusaidia kukuza na kusimamia matarajio yenye afya na mahusiano yenye afya.

Ugunduzi wangu wa mwisho: tunahitaji daima kujaliana. Lazima tupendane na tupunguze kuhukumu—hasa wakati matarajio yetu hayakufikiwa kwa haraka. Tunapaswa kuwasaidia watoto na vijana wetu wahisi upendo wa Yesu Kristo katika maisha yao, hata wakati wanapopambana kuhisi upendo juu yao wenyewe. Mzee Orson F. Whitney, aliyehudumu kama mshiriki wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, aliwashauri wazazi jinsi ya kuwasaidia watoto wanaoteseka: “Ombeni kwa ajili ya … watoto wenu, washikilieni kwa imani yenu.”6

Mara nyingi nimetafakari kile inachomaanisha kuwashikilia kwa imani. Ninaamini inajumuisha matendo rahisi ya upendo, upole, ukarimu na heshima. Inamaanisha kuwaruhusu wakue katika spidi yao wenyewe na kutoa ushuhuda ili kuwasaidia wahisi upendo wa Mwokozi wetu. Inatuhitaji tuwafikirie zaidi wao na kidogo kuhusu sisi au wengine. Hilo kwa kawaida humaanisha kuzungumza kidogo na kusikiliza sana, sana zaidi. Lazima tuwapende, tuwawezeshe na tuwasifu mara kwa mara katika juhudi zao za kufanikiwa na kuwa waaminifu kwa Mungu. Na mwisho, tunapaswa kufanya kila kitu ndani ya uwezo wetu kuwa karibu nao—kama vile tunavyokuwa karibu na Mungu.

Kwa wale wote ambao binafsi wameathiriwa na ugonjwa wa akili, shikilia kwa uimara maagano yako, hata ikiwa huwezi kuhisi upendo wa Mungu kwa wakati huu. Fanya chochote kilicho ndani ya uwezo wako na kisha “simama imara … kuuona wokovu wa Mungu, na kwa mkono wake kufunuliwa.”7

Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo ni Mwokozi wetu. Yeye anatujua. Yeye anatupenda, na atatungojea. Wakati wa majaribu ya familia yetu, nimekuja kujua ni jinsi gani Yeye alivyo karibu sana. Ahadi Zake ni za kweli:

Msiogope, nipo pamoja nanyi; ee, msivunjike moyo,

Kwani ndimi Mungu wenu na nitawasaidia.

Nitawapa nguvu, nitawasaidia, na nitawafanya msimame, …

Nitawashika, kwa mkono wangu mkuu, wenye haki.

Kwa kujua ni jinsi gani msingi wetu ulivyo imara, na daima tutangaze kwa furaha:

Nafsi iliyomtumaini Yesu kwa ajili ya pumziko

Kamwe, kwa maadui sitamuacha;

Nafsi hiyo, japo nguvu za jehanamu zijapotisha, …

Mtu wangu kamwe sitamuacha!8

Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Mafundisho na Maagano 45:31.

  2. “I’m Trying to Be Like Jesus,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 78–79.

  3. Ona 3 Nefi 12:48.

  4. Like a Broken Vessel,” Mental Health: General Principles, ChurchofJesusChrist.org.

  5. Sheldon Martin, “Jitahidi Kuwa—Mpangilio kwa ajili ya Ukuaji na Afya ya Akili na Hisia,” Liahona, Ago. 2021, 14.

  6. Orson F. Whitney, katika Conference Report, Apr. 1929, 110.

  7. Mafundisho na Maagano 123:17.

  8. “How Firm a Foundation,” Nyimbo za Kanisa,, na. 85.