Mwalike Kristo Aandike Hadithi Yako
Hebu hadithi yako iwe ya imani, ikifuata Mfano wako, Mwokozi Yesu Kristo.
Ninaanza kwa kuuliza maswali kadhaa, yenye kusudio la kutafakari kibinafsi.
-
Je, ni aina gani ya hadithi ya kibinafsi unayoiandika kwa ajili ya maisha yako?
-
Je, njia unayoielezea katika hadithi yako imenyooka?
-
Je, hadithi yako inaishia pale ilipoanzia, nyumbani kwako mbinguni?
-
Je, kuna mfano katika hadithi yako—na je, ni Mwokozi Yesu Kristo?
Nashuhudia kwamba Mwokozi ndiye “mwanzilishi na mkamilishaji wa imani yetu.”1 Je, Utamwalika awe mwanzilishi na mkamilishaji wa hadithi yako?
Anajua mwanzo kutokea mwishoni. Alikuwa Muumba wa mbingu na nchi. Anataka turudi nyumbani Kwake na kwa Baba yetu wa mbinguni. Anawekeza kila kitu ndani yetu na anataka tufanikiwe.
Je, unadhani ni nini kinatuzuia kugeuza hadithi zetu kwake?
Labda mfano huu utasaidia kujitathmini kwako.
Wakili bora wa kesi anajua kwamba wakati wa kuhoji, unapaswa mara chache kumuuliza shahidi swali ambalo hujui jibu lake. Kuuliza swali kama hilo ni kukaribisha shahidi kukuambia wewe—hakimu na baraza la mahakama—kitu ambacho hujui bado. Unaweza kupata jibu ambalo linakushangaza na ni kinyume na simulizi uliyoitayarisha kwa ajili ya kesi yako.
Ingawa kumuuliza shahidi swali ambalo hujui jibu lake sio busara kwa wakili wa kesi, kinyume chake ni kweli kwetu. Tunaweza kuuliza maswali kuhusu Baba yetu wa Mbinguni mwenye upendo, katika jina la Mwokozi wetu mwenye huruma, na shahidi anayejibu maswali yetu ni Roho Mtakatifu, ambaye hushuhudia kweli daima.2 Kwa sababu Roho Mtakatifu hufanya kazi katika muungano mkamilifu na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo, tunajua kwamba udhihirisho wa Roho Mtakatifu ni wa kuaminika. Kwa nini basi, wakati mwingine tunakataa kuomba aina hii ya msaada wa mbinguni, ukweli udhihirishwe kwetu na Roho Mtakatifu? Kwa nini tunasita kuuliza swali ambalo hatujui jibu lake wakati shahidi sio tu ni rafiki lakini atasema ukweli daima?
Labda ni kwa sababu hatuna imani ya kukubali jibu tutakalopokea. Labda ni kwa sababu mwanaume au mwanamke wa asili ndani yetu anapinga kugeuza mambo kikamilifu kwa Bwana na kumwamini Yeye kikamilifu. Labda ndio sababu tunachagua kushikamana na simulizi ambayo tumejiandikia wenyewe, toleo bora la hadithi yetu lisilohaririwa na Mwandishi Mkuu. Hatutaki kuuliza swali na kupata jibu ambalo haliendani vizuri na hadithi tunayojiandikia sisi wenyewe.
Kwa kweli, ni wachache wetu ambao labda tungeandika katika hadithi zetu kuhusu majaribu ambayo hutufanya kuwa bora. Lakini je, hatupendi mwisho mtukufu wa hadithi tunayosoma wakati mhusika mkuu anashinda mapambano? Majaribu ni mambo ya njama ambayo hufanya hadithi zetu pendwa kuwa za kuvutia, zisizopitwa na wakati, zenye kukuza imani na zenye kustahili kusimuliwa. Mapambano mazuri yaliyoandikwa kwenye hadithi zetu ndio yanayotusogeza karibu na Mwokozi na kutusafisha, kutufanya tuwe zaidi kama Yeye.
Kwa Daudi kumsinda Goliathi, mvulana huyo alilazimika kupambana na jitu. Simulizi nzuri kwa Daudi ingekuwa kurejea kwenye kuchunga kondoo. Lakini badala yake, alitafakari juu ya uzoefu wake wa kuokoa kondoo kutoka kwa simba na dubu. Na kujenga juu ya matukio hayo ya kishujaa, alijipa imani na ujasiri na kumruhusu Mungu aandike hadithi yake, akitangaza, “Bwana aliyeniokoa kutoka kwa makucha ya simba, na katika makucha ya dubu, ataniokoa na mkono wa Mfilisti huyu.”3 Kwa hamu ya kumruhusu Mungu ashinde, na sikio kwa Roho Mtakatifu, na kwa nia ya kuruhusu Mwokozi awe mwanzilishi na mkamilishaji wa hadithi yake, mvulana Daudi alimshinda Goliathi na kuokoa watu wake.
Kanuni tukufu ya uhuru wa kujichagulia inaturuhusu tuandike hadithi zetu wenyewe—Daudi angeweza kurudi nyumbani, kwenye kuchunga kondoo. Lakini Yesu Kristo yuko tayari kututumia kama vyombo vitakatifu, penseli zilizonolewa mkononi Mwake, ili kuandika kitu cha thamani kubwa! Yeye yuko tayari kwa rehema kunitumia mimi, penseli mbaya, kama chombo mikononi Mwake, ikiwa nina imani ya kumruhusu Yeye, ikiwa nitamruhusu Aandike hadithi yangu.
Esta ni mfano mwingine mzuri wa kumruhusu Mungu ashinde. Badala ya kushikamana na simulizi ya tahadhari ya kujilinda mwenyewe, alitumia imani, akijielekeza moja kwa moja kwa Bwana. Hamani alikuwa akipanga kuangamizwa kwa Wayahudi wote huko Uajemi. Mordekai, jamaa ya Esta, alitambua njama hiyo na akamwandikia Esta, akimsihi azungumze na mfalme kwa niaba ya watu wake. Esta limwambia Mordekai kwamba mtu anayemwendea mfalme bila kuitwa alihukumiwa kifo. Lakini kwa tendo kubwa la imani, alimwomba Mordekai kuwakusanya Wayahudi na kufunga kwa ajili yake. “Nami na wajakazi wangu tutafunga vilevile,” alisema, “kisha nitaingia kwa mfalme, kinyume cha sheria; kama nikiangamia, na niangamie.”4
Esta alikuwa tayari kumruhusu Mwokozi aandike hadithi yake ingawa, kupitia lenzi ya maisha haya, mwisho unaweza kuonekana wa kuogofya. Kama baraka, mfalme alimpokea Esta, na Wayahudi katika Uajemi waliokolewa.
Kwa kweli, kiwango cha ujasiri wa Esta hakiulizwi sana kwetu. Lakini kumruhusu Mungu ashinde, kumfanya Yeye awe mwanzilishi na mkamilishaji wa hadithi zetu, inahitaji sisi kushika amri zake na maagano ambayo tumefanya. Ni katika kushika kwetu amri na agano ambapo kutafungua njia ya mawasiliano ya sisi kupokea ufunuo kupitia Roho Mtakatifu. Na ni kupitia udhihirisho wa Roho kwamba tutahisi mkono wa Mwalimu ukiandika hadithi zetu pamoja nasi.
Mnamo Aprili 2021, nabii wetu, Rais Russell M. Nelson, alituomba kutafakari kile tunachoweza kufanya ikiwa tuna imani zaidi kwa Yesu Kristo. Kwa imani zaidi katika Yesu Kristo, tunaweza kuuliza swali ambalo hatujui jibu lake—muulize Baba yetu wa Mbinguni, kwa jina la Yesu Kristo, atume jibu kupitia Roho Mtakatifu, anayeshuhudia ukweli. Kama tungekuwa na imani zaidi, tungeuliza swali na kisha kuwa tayari kukubali jibu tunalopokea, hata ikiwa haliendani na simulizi yetu nzuri. Na baraka iliyoahidiwa ambayo itatokana na kutenda kwa imani katika Yesu Kristo ni ongezeko la imani Kwake kama mwanzilishi na mkamilishaji wetu. Rais Nelson alitangaza kwamba sisi “tunapokea zaidi imani kwa kufanya kitu ambacho kinahitaji zaidi imani.”5
Kwa hivyo, wenzi wasio na mtoto wanaoteseka kwa utasa wanaweza kuuliza kwa imani ikiwa wanapaswa kuasili mtoto na kuwa tayari kukubali jibu, ingawa simulizi waliyojiandikia ni pamoja na kuzaa kimiujiza.
Wanandoa waandamizi wanaweza kuuliza ikiwa ni wakati wao kutumikia misheni na kuwa tayari kwenda, ingawa simulizi ambayo walijiandikia wenyewe ilijumuisha muda mwingi katika kazi. Au labda jibu litakuwa “bado,” na watajifunza katika sura zijazo za simulizi yao kwa nini walihitajika nyumbani kwa muda mrefu kidogo.
Kijana au msichana anaweza kuuliza kwa imani kama kujikita katika michezo au masomo au muziki ni ya thamani zaidi na kuwa tayari kufuata misukumo ya shahidi kamili, Roho Mtakatifu.
Kwa nini tunataka Mwokozi awe mwanzilishi na mkamilishaji wa hadithi zetu? Kwa sababu anajua uwezo wetu kikamilifu, Atatufikisha mahali ambapo hatujawahi kupafikiria. Anaweza kutufanya kuwa Daudi au Esta. Atakuza uwezo wetu na kutusafisha ili tufanane Naye zaidi. Vitu tutakavyofanikisha tunapotenda kwa imani zaidi vitaongeza imani yetu katika Yesu Kristo.
Akina kaka na dada, mwaka mmoja tu uliopita nabii wetu mpendwa aliuliza: “Je, uko tayari kumruhusu Mungu ashinde katika maisha yako? … Je, wewe uko radhi kuruhusu chochote Yeye anachohitaji wewe ufanye kiwe kipaumbele juu ya lengo lingine lolote?”6 Ninaongeza kwa unyenyekevu kwenye maswali hayo ya kinabii: “Je, utamruhusu Mungu awe mwanzilishi na mkamilishaji wa hadithi yako?”
Katika Ufunuo tunajifunza kwamba tutasimama mbele za Mungu na kuhukumiwa kutoka katika vitabu vya uzima, kulingana na kazi zetu.7
Tutahukumiwa kwa kitabu chetu cha uzima. Tunaweza kuchagua kujiandikia hadithi nzuri. Au tunaweza kumruhusu Mwandishi Mkuu na Mkamilishaji aandike hadithi yetu pamoja nasi, tukiruhusu jukumu Analohitaji sisi kufanya kuwa kipaumbele kuliko matamanio mengine.
Hebu Kristo awe mwanzilishi na mkamilishaji wa hadithi yako!
Acha Roho Mtakatifu awe shahidi wako!
Andika hadithi ambayo njia uliyoko sasa imenyooka, kwenye njia inayokuongoza kurudi kwenye makazi yako ya mbinguni kuishi katika uwepo wa Mungu.
Acha dhiki na shida ambavyo ni sehemu ya kila hadithi nzuri viwe ni sehemu ya kukuleta karibu, na kuwa zaidi kama Yesu Kristo.
Simulia hadithi ambayo unatambua kwamba mbingu zi wazi. Uliza maswali ambayo hujui jibu lake, ukijua kwamba Mungu yu radhi kukujulisha mapenzi Yake kwako kupitia Roho Mtakatifu.
Hebu hadithi yako iwe ya imani, ikifuata Mfano wako, Mwokozi Yesu Kristo. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.