Mkutano Mkuu
Ustahili Si Kukosa Dosari
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2021


Ustahili Si Kukosa Dosari

Wakati unapohisi kuwa umeshindwa mara nyingi kuendelea kujaribu, kumbuka Upatanisho wa Kristo na neema utoayo ni halisi.

Wakati mmoja niliwatumia binti yangu na mkwe wangu ujumbe mfupi nikitumia kibadili sauti-kuwa maneno kwenye simu yangu. Nilisema, “Habari yenu ninyi wawili. Kweli ninawapenda.” Wao walipokea, “Nawachukia ninyi wawili. Ninapaswa kuwapenda.” Je, si ya kushangaza jinsi ilivyo rahisi ujumbe chanya na wenye dhamira nzuri unavyoweza kueleweka vibaya? Hiki ndicho wakati mwingine hutokea kwa ujumbe wa Mungu wa toba na ustahili.

Wengine kimakosa wanapokea ujumbe kwamba toba na badiliko havina haja. Ujumbe wa Mungu ni kwamba ni vya muhimu.1 Lakini Mungu si anatupenda licha ya mapungufu yetu? Bila shaka! Yeye anatupenda kikamilifu. Ninawapenda wajukuu zangu, licha ya mapungufu na vyote, lakini hiyo haimaanishi sitaki wao wawe bora na kuwa yale yote wanayoweza kuwa. Mungu anatupenda jinsi tulivyo, lakini Yeye pia anatupenda sana kiasi cha kutotaka sisi tubaki hivi tulivyo.2 Kukua katika Bwana ndiyo kile maisha ya dunia yanachomaanisha.3 Badiliko ndiyo kile Upatanisho wa Yesu humaanisha. Si tu Kristo anaweza kufufuka, kutakasa, kupoza moyo na kutuponya, bali kupitia yote, Yeye anaweza kutubadilisha kuwa zaidi kama Yeye.4

Baadhi kimakosa hupokea ujumbe kwamba toba ni tukio la mara moja. Ujumbe wa Mungu ni kwamba, kama ambavyo Rais Russell M. Nelson amefundisha “Toba … ni mchakato.”5 Toba yaweza kuchukua muda na juhudi za kujirudia,6 hivyo kuacha dhambi7 na kutokuwa na “tamaa ya kutenda maovu tena, lakini kutenda mema daima”8 ni utafutaji wa maisha yote.9

Maisha ni kama safari ya barabarani ya masafa marefu. Hatuwezi kufika mwisho wa safari kwa tenki moja la mafuta. Inatubidi tujaze tenki tena na tena. Kupokea sakramenti ni kama kwenda kituo cha mafuta. Tunapotubu na kufanya upya maagano yetu, tunathibitisha utayari wetu wa kushika amri, na Mungu na Kristo wanatubariki kwa Roho Mtakatifu.10 Kwa ufupi, tunaahidi kusonga mbele kwenye safari yetu, na Mungu na Kristo wanaahidi kujaza tena tenki.

Baadhi kimakosa wanapokea ujumbe kwamba hawastahili kushiriki kikamilifu katika injili kwa sababu hawako huru kikamilifu kutokana na mazoea mabaya. Ujumbe wa Mungu ni kwamba ustahili si kukosa dosari.11 Ustahili ni kuwa mwaminifu na mwenye kujaribu. Ni lazima tuwe waaminifu kwa Mungu, viongozi wa ukuhani, na wengine ambao wanatupenda,12 na lazima tujitahidi kushika amri za Mungu na kamwe tusife moyo kwa sababu tu tumeteleza.13 Mzee Bruce C. Hafen alisema kwamba kukuza sifa kama za Kristo “huhitaji subira na uthabiti zaidi kuliko inavyohitaji kukosa dosari.”14 Bwana amesema vipawa vya Roho “hutolewa kwa manufaa ya wale ambao hunipenda Mimi na hushika amri zangu zote, na yule atafutaye kufanya haya.”15

Mvulana mmoja nitamwita Damon aliandika: “Wakati nakua nilisumbuliwa na pornografia. Daima nilihisi aibu sana kiasi kwamba sikuweza kufanya mambo sawa sawa.” Kila wakati Damon alipoteleza, uchungu wa majuto ulikuwa mwingi sana, alijihukumu mwenyewe kuwa hakustahili aina yoyote ya neema, msamaha, au nafasi za ziada kutoka kwa Mungu. Alisema: “Niliamua kwamba nilihitaji tu kuhisi vibaya muda wote. Niliona Mungu labda alinichukia kwa sababu sikuwa nikiweka bidii sana na kushinda jambo hili mara moja. Ningeendelea kwa wiki na wakati mwingine hata mwezi, lakini kisha ningeshindwa na kufikiria, ‘Kamwe sitakuwa mzuri vya kutosha, kwa hiyo kuna haja gani ya kujaribu?’”

Wakati kama huo wa fikra mbaya, Damon alimwambia kiongozi wake wa ukuhani, “Labda napaswa tu kuacha kuja kanisani. Nimechoka kuwa mnafiki.”

Kiongozi wake alijibu, “Wewe si mnafiki kwa sababu una mazoea mabaya unayojaribu kuacha. Unakuwa mnafiki kama unayaficha, kudanganya au unajaribu kujishawishi kwamba Kanisa lina shida kwa kuweka viwango vya juu sana. Kuwa mwaminifu kuhusu matendo yako na kuchukua hatua za kusonga mbele si kuwa mnafiki. Ni kuwa mfuasi.”16 Kiongozi huyu alimnukuu Mzee Richard G. Scott, ambaye alifundisha, “Bwana huona udhaifu kwa njia tofauti na vile Yeye anavyoona uasi. … Wakati Bwana anapoongea juu ya udhaifu, daima ni kwa rehema.”17

Mtazamo huo ulimpa Damon tumaini. Alitambua Mungu hakuwa huko juu akisema, “Damon ameteleza tena.” Badala yake, Yeye alikuwa pengine akisema, “Tazama umbali aliotembea Damon.” Mvulana huyu mwishowe aliacha kuinamisha kichwa kwa aibu au kutazama pembeni kwa visingizio na kujipa moyo. Alitazama juu kwa ajili ya msaada wa Mungu na aliupata.18

Damon alisema, “Wakati pekee nilipokuwa nimemgeukia Mungu hapo awali ilikuwa ni kuomba msamaha, lakini sasa naomba pia kwa ajili ya neema—‘nguvu Yake ya kuwezesha’ [Kamusi ya Biblia, “Neema”]. Kamwe sikuwahi kufanya hivyo hapo awali. Siku hizi natumia muda kidogo kujichukia kwa kile ambacho nimefanya na muda mwingi kumpenda Yesu kwa kile ambacho Yeye amenitendea.”

Ukitazama muda mrefu kiasi gani Damon alikuwa amesumbuka, haingekuwa yenye msaada na uhalisia kwa wazazi na viongozi wanaomsaidia kusema “usirudie tena” upesi sana au bila kujali kuweka viwango fulani vya uzuiaji ili aweze kuwa mwenye “kustahili.” Badala yake, walianza kwa malengo madogo, yanayofikika. Waliondoa matarajio yote ya kushindwa au kufanikiwa na kufokasi juu ya ukuaji mdogo mdogo, ambao ulimruhusu Damon kujenga juu ya mwendelezo wa mafanikio badala ya kushindwa.19 Yeye, kama watu wa Limhi waliokuwa utumwani, alijifunza “kustawi hatua kwa hatua.”20

Mzee D. Todd Christofferson alishauri: “Ili kupambana na kitu kikubwa sana, itatubidi tukifanyie kazi kidogo kidogo, kila siku. … Kuanza kutumia mazoea mapya na mazuri katika hulka yetu au kushinda mazoea mabaya au uraibu mara [nyingi] humaanisha juhudi za leo zikifuatiwa na zingine kesho na kisha zingine, na pengine kwa siku nyingi, hata miezi na miaka. … Lakini tunaweza kwa sababu tunaweza kumsihi Mungu … kwa ajili ya msaada tunaohitaji kila siku.”21

Sasa, akina kaka na akina dada, janga la UVIKO-19 halijawa rahisi kwa mtu yeyote, lakini kujitenga kunakoambatana na viuizi vya karantini kumefanya maisha kuwa magumu hasa kwa wale wanaosumbuka kwa mazoea mabaya. Kumbuka badiliko linawezakana, toba ni mchakato, na ustahili si kukosa dosari. Cha muhimu zaidi, kumbuka kwamba Mungu na Kristo wako tayari kutusaidia hapa na sasa.22

Baadhi kimakosa wanapokea ujumbe kwamba Mungu anangojea kutusaidia mpaka baada ya kuwa tumetubu. Ujumbe wa Mungu ni kwamba Yeye daima atatusaidia wakati tunapotubu. Neema Yake inapatikana kwetu “bila kujali pale tulipo katika njia ya utiifu.”23 Mzee Dieter F. Uchtdorf amesema: “Mungu hahitaji watu ambao hawana dosari. Anatafuta wale ambao watatoa ‘mioyo na akili zao zilizo tayari’ [Doctrine and Covenants 64:34], naye atawafanya wakamilifu katika Kristo’ [Moroni 10:32–33].”24

Wengi sana wameumizwa kwa mahusiano ya kifamilia yaliyovunjika na kuzorota kiasi kwamba ni vigumu kwao kuamini katika faraja na uvumilivu wa Mungu. Wanasumbuka kumwona Mungu kama Yeye alivyo—Baba mwenye upendo ambaye huja kwetu wakati wa mahitaji yetu25 na anajua jinsi ya “kutoa vitu vizuri kwa wale wanaomuomba.”26 Neema Yake si tu tuzo kwa wale wenye kustahili. Ni “msaada wa kiungu” ambao Yeye hutoa ambao hutusaidia kuwa wastahili. Si tu zawadi kwa watu wema. Ni “endaumenti ya nguvu” ambayo Yeye hutoa ambayo hutusaidia kuwa wema.27 Sisi hatutembei tu kuwaelekea Mungu na Kristo. Tunatembea pamoja Nao.28

Kote katika Kanisa, vijana wanakariri Dhima ya Wasichana na ya Akidi ya Ukuhani wa Haruni. Kutoka New Zealand hadi Hispania hadi Ethiopia hadi Japani, wasichana wanasema, “Ninathamini zawadi ya toba.” Kutoka Chile hadi Guatemala hadi Moroni, Utah, wavulana wanasema, “Pale ninapojitahidi kutumikia, kufanyia kazi imani, kutubu, na kuwa bora kila siku, nitastahili kupokea baraka za hekaluni na furaha ya kudumu ya injili.”

Ninaahidi baraka hizo na furaha hiyo ni halisi na viko ndani ya ufiko wa wale wanaotii amri zote na “yule atafutaye kufanya hivyo.”29 Wakati unapohisi kuwa umeshindwa mara nyingi kuendelea kujaribu, kumbuka Upatanisho wa Kristo na neema utoayo ni halisi.30 Mikono “[Yake] ya rehema imenyoshwa kukuelekea wewe.”31 Wewe unapendwa—leo, katika miaka 20, na milele. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.

Chapisha