Mkutano Mkuu
“Je, Wanipenda Mimi Zaidi Ya Hawa?”
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2021


13:6

“Je, Wanipenda Mimi Zaidi Ya Hawa?”

Mambo gani unayoweza kufanya ndani ya maisha yako mwenyewe kuonesha kwamba unampenda Bwana kwanza?

Mnamo November 2019, rafiki yangu na mimi tulitembelea Nchi Takatifu. Tukiwa kule, tuliangalia upya na kujifunza maandiko kuhusu maisha ya Yesu Kristo. Asubuhi moja tulisimama juu ya ufukwe kaskazini magharibi ya Bahari ya Galilaya kwenye sehemu ambayo ingeweza kuwa sehemu ambayo Yesu alikutana na wanafunzi wake kufuatia Kufufuka Kwake.

Baada ya Kufufuka kwa Yesu, tunasoma katika Yohana sura ya 21, Petro na wanafunzi wengine walivua usiku mzima bila mafanikio.1 Wakati wa asubuhi, walimwona mtu amesimama ufukweni ambaye aliwaambia watupe nyavu zao upande mwingine wa mashua. Kwa kustaajabishwa, nyavu zilijaa kimiujiza.2

Mara moja waligundua kwamba yule mtu alikuwa Bwana, na walimkimbilia kumwamkia.

Wakati walipokuwa wanavuta nyavu ufukweni, ikiwa imejaa samaki, Yesu alisema, “Njooni na tule.”3 Yohana anaripoti kwamba “wakati walipokwisha kula, Yesu alimwambia Simoni Petro, Simoni, mwana wa Yohana, je, unanipenda mimi zaidi ya hawa?”4

Wakati nilikuwa nimesimama kwenye ufukwe ule ule, nilielewa kwamba swali la Mwokozi lilikuwa moja ya maswali muhimu sana ambayo anaweza kuniuliza siku moja. Niliweza takriban kusikia sauti Yake akiuliza, “Russell, unanipenda mimi zaidi ya hawa?”

Je unajiuliza juu ya kile Yesu alichokuwa anamaanisha alipomwuliza Petro, “Je, Wanipenda Mimi zaidi ya hawa?”

Kuhusisha swali hili kwetu sisi wenyewe katika siku hizi, Bwana anaweza kuwa anatuuliza kuhusu jinsi tulivyo na shughuli nyingi na kuhusu ushawishi mwingi chanya na hasi ukishindana kwa ajili ya usikivu wetu na muda wetu. Anaweza kuwa anauliza kwa kila mmoja wetu kama tunampenda Yeye zaidi kuliko mambo ya ulimwengu huu. Hili linaweza kuwa swali kuhusu nini kwa kweli tunathamini maishani, nani tunamfuata, na jinsi tunavyoangalia mahusiano yetu na wanafamilia na majirani. Au huenda anauliza ni kipi kwa kweli kinatuletea furaha na shangwe.

Je, mambo ya ulimwengu huu yanatuletea furaha, shangwe, na amani ambayo Mwokozi alitoa kwa wanafunzi Wake na anayotupatia sisi? Yeye pekee anaweza kutuletea furaha ya kweli, shangwe, na amani kupitia kumpenda Yeye na kufuata mafundisho Yake.

Ungejibuje swali “Je, unanipenda mimi zaidi ya hawa?”

Wakati tutapogundua maana kamili ya swali hili, tunaweza kuwa wanafamilia wazuri zaidi, majirani, raia, waumini wa Kanisa, na wana na mabinti wa Mungu.

Katika umri wangu, nimehudhuria mazishi mengi. Nina hakika wengi wenu mmeona kile nilichokiona. Wakati tunakumbuka maisha ya marehemu mwanafamilia au rafiki, ni mara chache kwa msemaji kuzungumza kuhusu ukubwa wa nyumba yake, wingi wa magari, au salio la akaunti za benki. Kwa kawaida hawazungumzii kuhusu kilichowekwa kwenye mitandao ya kijamii. Karibu katika mengi ya mazishi ambayo nimehudhuria, hulenga kwenye mahusiano ya mpendwa wao, huduma kwa wengine, masomo ya maisha na uzoefu, na upendo wa mpendwa wao kwa Yesu Kristo.

Msinielewe vibaya. Sisemi kwamba kuwa na nyumba mzuri au gari zuri ni makosa au kwamba kutumia vyombo vya habari ni vibaya. Kile ninachokisema ni kwamba mwishoni, mambo hayo yana umuhimu mdogo sana kulinganisha na kumpenda Mwokozi.

Wakati tunampenda na kumfuata Yeye, tuna imani Naye. Tunatubu. Tunafuata mfano Wake na tunabatizwa na kumpokea Roho Mtakatifu. Tunavumilia mpaka mwisho na kubaki kwenye njia ya agano. Tunawasamehe wanafamilia na majirani kwa kuacha kinyongo tunachoweza kuwa nacho. Tunajitahidi kwa dhati kutii amri za Mungu. Tunajitahidi kuwa watiifu. Tunafanya na kutii maagano. Tunawaheshimu baba na mama zetu. Tunaweka pembeni ushawishi hasi wa kidunia. Tunajiandaa wenyewe kwa ajili ya Ujio Wake wa Pili.

Katika “Kristo Aliye Hai: Ushuhuda wa Mitume,” tunasoma: “[Yesu] atarudi siku moja duniani. … Atatawala kama Mfalme wa Wafalme na kutawala kama Bwana wa Mabwana, na kila goti litakunjwa na kila ulimi utasema katika kuabudu mbele Yake. Kila mmoja wetu atasimama kuhukumiwa na Yeye kulingana na kazi zetu na matamanio ya mioyo yetu.”5

Kama mmoja wa Mitume aliyeweka sahihi hati ya “Kristo Aliye Hai” Naweza kusema kwamba kujua kwamba Yesu “ni nuru, maisha, na tumaini la ulimwengu”6 inanipa mimi hamu kubwa mno kumpenda Yeye zaidi kila siku.

Ninashuhudia kwamba Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo wanaishi. Ninashuhudia kwamba wanatupenda. Maandiko yanafundisha kwamba “Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanaye wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”7 Maandiko pia yanafundisha kwamba Yesu aliupenda ulimwengu akautoa uhai wake mwenyewe, ili kwamba wale wote watakaoamini waweze kuwa wana wa Mungu”8

Baba wa Mbinguni hivyo alitupenda sisi kwamba Aliandaa mpango Wake wa ukombozi pamoja na Mwokozi kama mtu mkuu. Na Yesu alitupenda sisi kwamba katika Baraza kuu Mbinguni, wakati Baba wa Mbinguni alipouliza, “Nimtume Nani?” Yesu, ambaye alikuwa mzaliwa wa watoto wa kiroho wa Baba, alijibu, “Mimi hapa, nitume mimi.”9 Alisema kwa Baba, “Baba, mapenzi yako yafanyike, na utukufu uwe wako milele.”10 Yesu alijitolea kuwa Mwokozi na Mkombozi wetu ili tuweze kuwa kama wao na kurudi kwenye uwepo wao.

Maandiko haya mawili pia yanafundisha kwamba kurudi kwenye uwepo Wao tunahitaji kuamini. Tunahitaji kuamini katika Yesu na mpango wa Mungu wa furaha. Kuamini ni kupenda na kumfuata Mwokozi wetu na kutii amri, hata kati ya majaribu na migongano.

Ulimwengu wa leo umevurugika. Kuna maudhi, kutoafikiana, mateso, na kuvutwa mawazo.

Rais Dallin H. Oaks, akizungumza mnamo mwaka 2017, aliandika yafuatayo: “Hizi ni nyakati za changamoto, zilizojazwa na wasiwasi mkubwa: vita na uvumi wa vita, uwezekano wa magonjwa ya mlipuko ya kuambukiza, ukame, mafuriko, na ongezeko la joto ulimwenguni,”11

Hatuwezi kupoteza upendo wetu kwa ajili ya na tegemeo katika Yesu, hata kama tunakumbana na changamoto zinazoonekana kutushinda kabisa. Baba wa Mbinguni na Yesu kamwe hawatatusahau. Wanatupenda.

Oktoba iliyopita, Rais Russell M. Nelson alitufundisha umuhimu wa kumweka Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo katika maisha yetu. Rais Nelson alitufundisha kwamba maana moja ya neno Israeli ni “acha Mungu ashinde.”12

Alituuliza kila mmoja wetu maswali haya: “Je, wewe uko radhi kuacha Mungu ashinde katika maisha yako? Je, wewe uko radhi kuacha Mungu awe na ushawishi muhimu zaidi katika maisha yako? Je, utaruhusu neno Lake, amri Zake, na maagano Yake, yashawishi kile unachofanya kila siku? Je, utaruhusu sauti Yake ichukue kipaumbele cha juu zaidi ya sauti zingine zote? Je, wewe uko radhi kuruhusu chochote Yeye anachohitaji wewe ufanye kiwe cha kwanza juu ya lengo lingine lolote? Je, wewe uko radhi kuruhusu mapenzi yako yamezwe katika Yake?”13

Siku zote hatuna budi kukumbuka kwamba furaha yetu ya kweli inategemea juu ya mahusiano yetu na Mungu, pamoja na Yesu Kristo, na sisi wenyewe.

Njia moja ya kuonesha upendo wetu ni kwa kuunganisha familia, marafiki, na majirani katika kufanya baadhi ya mambo madogo kuhudumiana vizuri zaidi sisi kwa sisi. Kufanya mambo ambayo yanafanya ulimwengu huu mahala bora zaidi.

Mambo gani unayoweza kufanya ndani ya maisha yako mwenyewe kuonesha kwamba unampenda Bwana kwanza?

Tunapofokasi kwenye kuwapenda majirani zetu kama Yeye anavyowapenda, tunaanza kwa kweli kuwapenda wale wanaotuzunguka.14

Ninauliza tena, ungejibuje swali la Mwokozi “Je, unanipenda mimi zaidi ya hawa?”

Unapofikiria swali hili kama nilivyofanya, ninaomba kwamba uweze kujibu kama Petro alivyofanya kitambo kilichopita,”Ndiyo Bwana; unajua kwamba ninakupenda”15 na kisha kuuonesha kwa kumpenda na kumtumikia Mungu na wale wote wanaokuzunguka.

Ninashuhudia kwamba tumebarikiwa kuwa na injili ya Yesu Kristo kutuongoza katika njia tunayoishi na kutendeana sisi kwa sisi. Katika Yeye, tunagundua kwamba kila binti na mwana wa Mungu ni wa thamani Kwake.

Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo ni Mwokozi wetu Mpendwa. Yeye ndiye Mwana Pekee wa Mungu. Na ninatoa ushuhuda kwa unyenyekevu huu katika jina la Yesu Kristo, amina.