Urejesho wa Kila Siku
Tunahitaji mwendelezo wa kila siku wa upokeaji wa mwangaza wa kimbingu. Tunahitaji “nyakati za kuburudishwa.” Nyakati za urejesho binafsi
Tunakusanyika asubuhi hii ya kupendeza ya Sabato kuzungumza kuhusu Kristo, kufurahia katika injili Yake na kusaidia na kuungana mkono wakati tukitembea katika “njia” ya Mwokozi wetu.1
Kama waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, tunakusanyika kwa dhumuni hili kila siku ya Sabato kwa mwaka mzima. Kama wewe si muumini wa Kanisa, tunakualika kwa dhati na kukushukuru kwa kuungana nasi katika kumwabudu Mwokozi na kujifunza kuhusu Yeye. Kama ilivyo kwako, tunajitahidi—japo si kiukamilifu—kuwa marafiki, majirani na wanadamu bora,2 na tunatafuta kufanya hivi kwa kumfuata Mfano wetu, Yesu Kristo.
Tunatumaini unaweza kuhisi ushuhuda wetu wa dhati. Yesu Kristo yu hai! Yeye ni Mwana wa Mungu aliye hai, na Huongoza manabii duniani hivi leo. Tunawaalika wote kuja, kusikia neno la Mungu, na kushiriki fadhila Zake! Ninatoa ushuhuda wangu binafsi kwamba Mungu yu miongoni mwetu na kwamba Yeye hakika atasonga karibu kwa wote ambao watasonga karibu Yake.3
Tunachukulia kuwa ni heshima kutembea nawe katika njia ya ufuasi iliyonyooka na nyembamba ya Bwana.
Ufundi wa Kutembea Katika Njia Iliyonyooka
Kuna nadharia inayojirudia rudia kwamba watu ambao wanapotea wanatembea katika miduara. Si muda mrefu, wanasayansi katika Chuo cha Max Planck cha Utafiti wa Tabia za Viumbe walijaribu nadharia hiyo. Waliwapeleka washiriki kwenye msitu mnene na kuwapa maelekezo rahisi “Tembeeni katika njia nyoofu.” Hakukuwa na alama za kuonekana. Waliokuwa wakijaribiwa walitakiwa kutegemea tu katika ufahamu wao wa uelekeo.
Unafikiri walifanyaje?
Wanasayansi walihitimisha, “Watu kweli [wanatembea] katika miduara wakati wanapokuwa hawana viashirio vya uelekeo katika matembezi yao.”4 Walipoulizwa baada ya hapo, baadhi ya washiriki kwa ujasiri walisema kwamba hawakuacha njia hata kidogo. Bila kujali ujasiri wao katika hilo, data za GPS zilionyesha kwamba walikuwa wametembea katika mzunguko wa kama kipenyo cha mita 20.
Kwa nini tunakuwa na wakati mgumu kutembea katika njia nyoofu? Baadhi ya wachunguzi wanatoa nadharia kwamba kutoka huko kudogo kwenye njia kusikodhaniwa, huleta utofauti. Wengine wameonyesha kwenye ukweli kwamba sote tuna mguu mmoja ambao ni mrefu kuliko mwingine. “Zaidi,” hata hivyo, tunapata shida kutembea katika njia nyoofu kwenda mbele “[kwa sababu] ya ongezeko la wasiwasi wa wapi ni panyoofu kwenda mbele.”5
Bila kujali sababu, ni kawaida ya binadamu: bila kuwa na alama elekezi za kuonekana, tunapotea toka uelekeo sahihi.
Kupotea Njia
Je, si ya kushangaza jinsi vitu vidogo, vionekanavyo visivyo vya muhimu vinaweza kuleta tofauti kubwa katika maisha yetu?
Ninajua hili kutoka uzoefu binafsi kama rubani. Kila mara nilipoanza kukaribia uwanja wa ndege, nilijua kwamba kazi yangu kubwa iliyobaki ingejumuisha kufanya marekebisho kidogo ya uelekeo kila mara ili kwa usalama kuielekeza ndege katika njia ya kutua tunayoitegemea.
Unaweza kuwa na uzoefu sawa na huo wakati ukiendesha gari. Upepo, utofauti wa barabara, uwiano wa matairi usio mkamilifu, kukosa umakini—bila kusahau matendo ya madereva wengine—vyote vinaweza kukutoa katika njia yako uliyotarajiwa. Shindwa kuwa makini kwenye vitu hivi na unaweza kuishia kuwa na siku mbaya.6
Hii inatumika kwetu sote kimwili.
Vivyo hivyo na kiroho.
Mabadiliko mengi katika maisha yetu ya kiroho—yote chanya na hasi—hutokea taratibu, hatua kwa hatua. Kama washiriki katika utafiti wa Max Planck, tunaweza tusitambue wakati gani tunateleza toka kwenye njia nyoofu. Tunaweza hata kuwa na ujasiri mkubwa kwamba tunatembea katika njia nyoofu. Lakini ukweli ni kwamba bila kuwa na alama elekezi kutuongoza, bila kudhamiria tunatoka katika njia sahihi na kuishia katika sehemu ambazo tusingedhani tungeishia.
Hili ni kweli kwa watu wote. Pia ni kweli kwa jamii na mataifa. Maandiko yamejaa mifano.
Kitabu cha Waamuzi kinasema kwamba baada ya Yoshua kufariki, “kikainuka kizazi … ambacho hakikumjua Bwana, wala hawakuijua hiyo kazi ambayo alikuwa ameitenda kwa ajili ya Israeli.”7
Bila kujali usaidizi wa kushangaza wa kimbingu, kutembelewa, kuokolewa na ushindi wa kimiujiza kulikoshuhudiwa na watoto wa Israeli wakati wa maisha ya Musa na Yoshua, ndani ya kizazi kimoja watu walikuwa wameiacha Njia na kuanza kutembea kulingana na nia zao wenyewe. Na, bila shaka, haikuchukua muda mrefu walilipa bei ya tabia hiyo.
Wakati mwingine kuanguka huku hutokea baada ya vizazi vingi. Wakati mwingine hutokea baada ya miaka au miezi kadhaa.8 Lakini sote ni wahanga. Bila kujali ni imara kiasi gani uzoefu wetu wa kiroho ulikuwa hapo awali, kama wanadamu tunapotea. Hivyo ndivo ilivyo tangu siku za Adamu hadi sasa.
Habari Njema
Lakini si vyote vimepotea. Tofauti na jaribio la kutafuta uelekeo, tuna alama elekezi za kutegemewa ambazo tunaweza kuzitumia kutathmini uelekeo wetu.
Alama hizo ni zipi?
Hakika zinajumuisha sala ya kila siku na kutafakari maandiko na kutumia nyenzo zilizovuviwa kama Njoo, Unifuate. Kila siku, tunaweza kukikaribia kiti cha Mungu kwa unyenyekevu na uaminifu. Tunaweza kutafakari matendo yetu na kurejelea nyakati za siku yetu—tukilinganisha mapenzi na nia zetu na zile za Kwake. Kama tumepotea, tunamsihi Mungu kuturejesha, na tunadhamiria kufanya vizuri zaidi.
Muda huu wa kujichunguza ni fursa kwa ajili ya marekebisho. Ni bustani ya tathmini ambapo tunaweza kutembea na Bwana na kuelekezwa, kuinuliwa, na kutakaswa kupitia maneno yaliyoandikwa na kuvuviwa na Roho ya Baba yetu wa Mbinguni. Ni wakati mtakatifu ambapo tunakumbuka maagano yetu ya kumfuata Kristo mwenye ukarimu, wakati tukitathmini ukuaji wetu na kujioanisha na alama elekezi za kiroho ambazo Mungu amezitoa kwa ajili ya watoto Wake.
Fikiria hilo kama urejesho kila siku wako binafsi. Kwenye safari yetu kama wafuasi tukielekea njia ya utukufu, tunajua ni jinsi gani ilivyo rahisi kuanguka. Lakini kama ilivyo kwa makosa madogo yanaweza kutotoa katika Njia ya Mwokozi, vivyo hivyo matendo madogo na rahisi ya kujirekebisha hakika huturudisha kwenye njia. Wakati kiza kinaponyemelea maisha yetu, kama ilivyo kawaida, urejesho wetu wa kila siku hufungua mioyo yetu kwa ajili ya nuru ya kimbingu, ambayo huangaza nafsi zetu, ikifukuza kiza, hofu na mashaka.
Vyombo Elekezi Vidogo, Meli Kubwa
Kama tutatafuta, hakika “Mungu [atatupatia] maarifa kwa njia ya Roho wake Mtakatifu, ndiyo, kwa kipawa chake kisichosemeka cha Roho Mtakatifu.”9 Kadiri kila mara tutakapoomba, Yeye atatufundisha Njia na kutusaidia kuifuata.
Hili, bila shaka, huhitaji juhudi endelevu kwa upande wetu. Hatuwezi kuridhika na uzoefu wa kiroho wa zamani. Tunahitaji mtiririko endelevu.
Hatuwezi kutegemea shuhuda za wengine milele. Lazima tutengeneze wa kwetu.
Tunahitaji mwendelezo wa kila siku wa upokeaji wa mwangaza wa kimbingu.
Tunahitaji “nyakati za kuburudishwa.”10 Nyakati za urejesho binafsi
“Maji yaendayo kasi” hayawezi “kubakia machafu.”11 Ili kuweka mawazo na matendo yetu safi, lazima tusonge mbele!
Hata hivyo, Urejesho si kitu ambacho kilitokea mara moja kwa kila mtu. Ni mchakato endelevu—siku moja kwa wakati, moyo mmoja kwa wakati.
Kadiri siku zetu zinavyosonga, ndivyo pia na maisha yetu. Mwandishi mmoja aliiweka hivi: “Siku moja ni kama maisha yote. Unaanza kwa kufanya kitu kimoja, lakini unaishia kufanya kitu kingine, unapanga kufanya shughuli moja, lakini kamwe huimalizi. … Na mwisho wa maisha yako, uhai wako wote unakuwa na hali ya shaghlabaghala hio hio, pia. Maisha yako yote yana umbo kama la siku moja.”12
Je, unataka kubadili jinsi maisha yako yalivyo?
Badilisha jinsi siku yako ilivyo.
Je, unataka kubadili siku yako?
Badilisha sasa.
Badilisha jinsi unavyofikiri, kuhisi, na kutenda kwa wakati huu.
Chombo elekezi kidogo kinaweza kuongoza meli kubwa.13
Matofali madogo yanaweza kuwa jengo kubwa.
Mbegu ndogo inaweza kuwa mti mkubwa wa mbao.
Dakika na saa zitumiwazo kwa ufasaha ni matofali ya ujenzi wa maisha yaliyo mazuri. Zinaweza kuhamasisha uzuri, kutuinua kutoka kwenye tope la kutokamilika, na kutuongoza juu kwenye njia okozi ya msamaha na utakaswaji.
Mungu wa Mwanzo Mpya
Pamoja nawe, ninainua moyo wangu kwa shukrani kwa ajili ya zawadi kuu ya fursa mpya, maisha mapya, tumaini jipya.
Tunainua sauti zetu katika kusifu juu ya wingi na Mungu mwenye kusamehe. Kwa hakika Yeye ni Mungu wa mwanzo mpya. Hatma yake ya mwisho ya kazi Zake zote ni kutusaidia sisi, watoto Wake, kufanikiwa kwenye hamu yetu katika maisha haya na uzima wa milele.14
Tunaweza kuwa viumbe vipya katika Kristo, kwani Mungu ameahidi, “Ndiyo, na kila mara watu wangu watatubu, nitawasamehe makosa yao dhidi yangu”15 na sizikumbuki tena.”16
Kaka na dada zangu wapendwa, rafiki wapendwa, sote hupotea mara kwa mara.
Lakini tunaweza kurudi tena kwenye njia. Tunaweza kutembea kwenye njia yetu kupita kiza na majaribu ya maisha haya na kuipata njia yetu ya kurudi kwa Baba yetu mpendwa wa Mbinguni kama tutatafuta na kuzikubali alama elekezi za kiroho Yeye alizotoa, kuthamini ufunuo binafsi, na kujitahidi kwa ajili ya urejesho wa kila siku. Hivi ndivyo tunavyokuwa wafuasi wa kweli wa Mwokozi wetu mpendwa, Yesu Kristo.
Tufanyapo hivyo, Mungu atatabasamu juu yetu. “Bwana atakubarikia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako. Bwana atakuweka uwe taifa takatifu kwake.”17
Ni sala yangu kwamba tutatafuta urejesho wa kila siku na kuendelea kujitahidi kutembea kwenye Njia ya Yesu Kristo. Katika jina la Yesu Kristo, amina.