Mkutano Mkuu
Kwa Nguvu za Mungu katika Utukufu Mkuu
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2021


13:16

Kwa Nguvu za Mungu katika Utukufu Mkuu

(1 Nefi 14:14)

Kuheshimu maagano kunatukinga kwa wema pamoja na nguvu za Mungu katika utukufu mkuu.

Ninaomba kwamba Roho Mtakatifu atatutia nuru na kutuadilisha sisi sote tunapozingatia kwa pamoja kazi kuu ya wokovu na kuinuliwa katika kipindi cha ujalivu wa nyakati.

Matembezi ya Kwanza ya Moroni kwa Joseph Smith

Takribani miaka mitatu baada ya Ono la Kwanza, mnamo usiku wa Septemba 21, 1823, kijana Joseph Smith alikuwa akisali ili kupokea ondoleo la dhambi zake na kujua hali yake na msimamo wake mbele ya Mungu.1 Kiumbe akamtokea kando ya kitanda chake, akamwita Joseph kwa jina, na kutamka “alikuwa ni mjumbe aliyetumwa kutoka katika uwepo wa Mungu … na kwamba jina lake lilikuwa Moroni.” Alieleza “kwamba Mungu ana kazi kwa ajili ya [Joseph] kufanya”2 na kisha kumuelekeza kuhusu ujio wa Kitabu cha Mormoni. Muhimu sana, Kitabu cha Mormoni kilikuwa mojawapo ya mada za kwanza zilizozungumzwa katika ujumbe wa Moroni.

Kitabu cha Mormoni ni ushuhuda mwingine wa Yesu Kristo na chombo kikuu cha uongofu katika siku za mwisho. Kusudi letu la kushiriki injili ni kuwaalika wote kuja kwa Yesu Kristo,3 kupokea baraka za injili iliyorejeshwa, na kuvumilia hadi mwisho kupitia imani katika Mwokozi.4 Kuwasaidia watu kupata badiliko kuu la moyo5 na kujifunga wenyewe kwa Bwana kupitia maagano na ibada takatifu ni malengo ya msingi ya kuhubiri injili.

Utangulizi wa Moroni wa Kitabu cha Mormoni kwa Joseph Smith ulianzisha kazi ya wokovu na kuinuliwa kwa watu kwenye upande huu wa pazia katika kipindi cha ujalivu wa nyakati.

Akiendelea na maelekezo yake kwa Joseph, Moroni kisha alinukuu kutoka kitabu cha Malaki katika Agano la Kale, kwa tofauti ndogo katika lugha iliyotumika kwenye toleo la King James:

“Tazama, nitaufunua kwenu Ukuhani, kwa mkono wa Eliya, nabii, kabla ya kuja kwa siku ile kuu na ya kutisha ya Bwana.

“… Naye atapandikiza katika mioyo ya watoto ahadi zilizofanywa kwa baba, na mioyo ya watoto itawageukia baba zao. Kama haingekuwa hivyo, dunia yote ingeliharibiwa kabisa wakati wa kuja kwake.”6

Kusudi letu la kujenga mahekalu ni kufanya maeneo matakatifu yapatikane ambapo maagano na ibada takatifu zinazohitajika za wokovu na kuinuliwa kwa familia ya mwanadamu ziweze kutekelezwa, kwa wote walio hai na wafu. Maelekezo ya Moroni kwa Joseph Smith kuhusu kazi muhimu ya Eliya na mamlaka ya ukuhani yalipanua kazi ya wokovu na kuinuliwa kwenye upande huu wa pazia na kuanzisha katika kipindi chetu kazi kwa ajili ya wafu kwenye upande mwingine wa pazia.

Katika muhtasari, mafundisho ya Moroni katika Septemba ya mwaka 1823 kuhusu Kitabu cha Mormoni na ujumbe wa Eliya yalithibitisha msingi wa kimafundisho kwa ajili ya kazi ya wokovu na kuinuliwa kwenye pande zote za pazia.

Mafundisho ya Nabii Joseph Smith

Masomo ambayo Joseph Smith alijifunza kutoka kwa Moroni yalishawishi kila kipengele cha huduma yake. Kwa mfano, katika mkutano wa Ibada uliofanyika katika Hekalu la Kirtland mnamo Aprili 6, 1837, Nabii alisema, “Baada ya yote yale ambayo yamesemwa, kazi kuu sana na muhimu sana ni kuhubiri injili.”7

Karibu takriban miaka saba baadaye, mnamo Aprili 7, 1844, Joseph Smith alitoa hotuba inayojulikana leo kama mahubiri ya hadhara ya King Follett. Alitamka katika hotuba hiyo “Jukumu kuu katika ulimwengu huu ambalo Mungu ameliweka mbele yetu ni kuwatafuta wafu wetu.”8

Lakini inawezekanaje kuhubiri injili na kuwatafuta wafu wetu iwe kazi pekee kuu na jukumu ambalo Mungu ameweka juu yetu? Ninaamini Nabii Joseph Smith alikuwa akisisitiza katika kauli zote ukweli wa msingi kwamba maagano, tunayofanya kupitia ibada chini ya mamlaka ya ukuhani, yanaweza kutuunganisha kwa Bwana Yesu Kristo na ni kiini muhimu cha kazi ya wokovu na kuinuliwa kwenye pande zote za pazia.

Kazi ya ummisionari na hekalu na historia ya familia ni vipengele vinavyoshabihiana na kuhusiana vya kazi moja kuu ambayo inafokasi juu ya maagano na ibada takatifu ambazo zinatuwezesha kupokea nguvu za Uchamungu katika maisha yetu na, hatimaye, kurudi katika uwepo wa Baba wa Mbinguni. Hivyo, kauli mbili za Nabii ambazo mwanzo zinaweza kuonekana zina mkanganyiko, hakika, zinaangazia kitovu cha kazi hii kuu ya siku za mwisho.

Fungamana na Mwokozi kupitia Maagano na Ibada

Mwokozi alisema:

“Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu.

“Kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”9

Tunachukua nira ya Mwokozi juu yetu tunapojifunza kuhusu, kupokea kwa ustahiki, na kuheshimu maagano na Ibada takatifu. Tunafungamana kwa uthabiti pamoja na Mwokozi wakati tunapokumbuka kwa uaminifu na kufanya kadiri ya uwezo wetu kuishi kulingana na masharti tuliyokubali. Na muunganiko huo Kwake ni chanzo cha nguvu za kiroho katika majira yote ya maisha yetu.

Watu wa Agano wa Bwana

Ninawaalikeni mfikirie baraka zilizoahidiwa kwa wafuasi wanaotunza maagano wa Yesu Kristo. Kwa mfano, Nefi “aliliona kanisa la Mwanakondo [katika siku za mwisho], na idadi yake ilikuwa chache, … watakatifu wa Mungu, pia nao walikuwa kote usoni mwa dunia; na utawala wao … ulikuwa mdogo.”10

Yeye pia “aliona nguvu za mwana kondoo wa Mungu, kwamba ziliwashukia watakatifu wa kanisa la mwanakondoo, na kwa watu wa agano wa Bwana, … walikuwa wamejikinga kwa utakatifu na kwa nguvu za Mungu katika utukufu mkuu.”11

Kirai “wamejikinga kwa utakatifu na kwa nguvu za Mungu katika utukufu mkuu” si tu wazo zuri au mfano wa lugha nzuri ya kimaandiko. Badala yake, baraka hizi zipo wazi tayari katika maisha ya wafuasi wasio na idadi wa siku za mwisho wa Bwana.

Kazi zangu kama mshiriki wa wale Kumi na Wawili zimenilipeleka kote duniani. Na nimebarikiwa kukutana na kujifunza masomo ya kukumbukwa kutoka kwa wengi wenu. Ninashuhudia kwamba watu wa agano wa Bwana leo hakika wamejikinga kwa utakatifu na kwa nguvu za Mungu katika utukufu mkuu. Nimeshuhudia imani, ujasiri, mtazamo, uthabiti na furaha ambavyo husambaa mbali zaidi ya uwezo wa binadamu—na kwamba Mungu pekee ndiye awezaye kuvitoa.

Nimeshuhudia wema na nguvu za Mungu katika utukufu mkuu, vilivyopokelewa kupitia uaminifu kwenye maagano na ibada, katika maisha ya muumini kijana wa Kanisa ambaye alipooza upande mmoja kutokana na ajali ya gari. Baada ya miezi migumu ya kupata nafuu na kujizoesha maisha mapya ya kizuizi cha kutembea, nilikutana na kuzungumza na mtu huyu shujaa. Wakati wa mazungumzo yetu niliuliza, “Je, Uzoefu huu umekusaidia kujifunza nini?” Jibu la upesi lilikuwa, “Mimi sina huzuni. Sijakasirika. Na kila kitu kitakuwa sawa.”

Nilishuhudia wema na nguvu za Mungu katika utukufu mkuu, vilivyopokelewa kupitia uaminifu kwenye maagano na ibada, katika maisha ya waumini wa Kanisa waliobatizwa na kuthibitishwa hivi karibuni. Waongofu hawa walikuwa na hamu ya kujifunza na kutumikia, wakiwa tayari lakini mara nyingi bila kuwa na uhakika kuhusu jinsi ya kuweka kando tabia za zamani na desturi zilizokita mizizi, na bado kuwa na furaha kuwa “wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu.”12

Nilishuhudia wema na nguvu za Mungu katika utukufu mkuu, vilivyopokelewa kupitia uaminifu kwenye maagano na ibada, katika maisha ya familia ambayo ilimtunza kwa makini mwenza na mzazi ambaye ana ugonjwa wa kufisha. Wafuasi hawa majasiri walielezea nyakati ambapo familia yao ilihisi kuwa wapweke—na nyakati ambazo walijua mkono wa Bwana ulikuwa ukiwainua na kuwaimarisha. Familia hii ilitoa shukrani za dhati kwa uzoefu mgumu wa maisha haya ambao huturuhusu kukua na kuwa zaidi kama Baba yetu wa Mbinguni na Mkombozi wetu, Yesu Kristo. Mungu aliisaidia na kuibariki familia hii kwa wenzi wa Roho Mtakatifu na kuifanya nyumba yao mahali patakatifu pa kimbilio kama hekalu.

Nilishuhudia wema na nguvu za Mungu katika utukufu mkuu, vilivyopokelewa kupitia uaminifu kwenye maagano na ibada, katika maisha ya muumini wa Kanisa ambaye alipata kuumia moyo kwa sababu ya talaka. Dhiki ya kiroho na kihisia ya dada huyu iliongezeka kwa sababu ya unyanyasaji uliohusiana na uvunjaji wa maagano wa mwenza wake na kuvunjika kwa ndoa yao. Alidai haki na uwajibikaji.

Mwanamke huyu mwaminifu alipokuwa akitaabika na haya yote yaliyomtokea yeye, alijifunza na kutafakari Upatanisho wa Mwokozi kwa kusudi na uzito zaidi kuliko hapo awali katika maisha yake. Pole pole, uelewa wa kina wa huduma ya ukombozi ya Mwokozi ulimiminika nafsini mwake—kuteseka Kwake kwa ajili ya dhambi zetu, na pia uchungu wetu, udhaifu wetu, kuvunjika kwetu moyo, na mafadhaiko yetu. Na alipata motisha kujiuliza swali la kupenya moyoni: Kwa vile gharama tayari imelipwa kwa ajili ya dhambi hizo, je, ungedai kwamba gharama ilipwe mara mbili? Aligundua kwamba hitaji hilo lingekuwa si haki wala rehema.

Mwanamke huyu alijifunza kwamba kujifunga mwenyewe kwa Mwokozi kupitia maagano na ibada kungeponya vidonda vilivyosababishwa na utekelezaji mwovu wa haki ya kujiamulia ya mtu mwingine na kulimwezesha kupata uwezo wa kusamehe na kupata amani, rehema, na upendo.

Ahadi na Ushuhuda

Ahadi na baraka za agano vinawezekana tu kwa sababu ya Mwokozi wetu,Yesu Kristo. Yeye anatualika tumtegemee Yeye13 tuje Kwake,14 tujifunze Kwake,15 na tujifunge Kwake16 kupitia maagano na ibada za injili Yake iliyorejeshwa. Ninashuhudia na kuahidi kwamba kuheshimu maagano kutatukinga kwa utakatifu na kwa nguvu za Mungu katika utukufu mkuu. Na ninashuhudia kwamba Bwana Yesu Kristo aliye hai ni Mwokozi wetu. Juu ya kweli hizi ninashuhudia kwa furaha katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.