Upendo wa Mungu: Unafurahisha moyo kwa shangwe
Upendo wa Mungu haupatikani katika hali za maisha yetu bali katika uwepo Wake ndani ya maisha yetu.
Akina Kaka na akina dada, Je mnajua kikamilifu jinsi Mungu, Baba yetu wa Mbinguni, anavyowapenda? Je, mmeweza kuhisi upendo Wake kwa kina ndani ya nafsi zenu?
Unapojua na kuelewa jinsi kwa ukamilifu unavyopendwa kama mtoto wa Mungu, hilo hubadilisha kila kitu. Linabadilisha namna unavyohisi kuhusu wewe binafsi wakati unapofanya makosa. Linabadilisha jinsi unavyohisi wakati mambo magumu yanapotokea. Linabadilisha mtazamo wako wa amri za Mungu. Linabadilisha mtazamo wako juu ya wengine, na juu ya uwezo wako wa kuleta utofauti.
Mzee Jeffrey R. Holland alifundisha: “ amri kuu ya kwanza ya milele yote ni kumpenda Mungu kwa moyo wetu wote, uwezo, akili na nguvu—hiyo ndiyo amri kuu ya kwanza. Lakini ukweli mkuu wa kwanza wa milele yote ni kwamba Mungu anatupenda sisi kwa moyo Wake wote, nguvu, akili na uwezo.”1
Ni kwa namna gani kila mmoja wetu anaweza kujua kwa kina nafsini mwetu ukweli huo wa milele?
Nabii Nefi alioneshwa kwenye ono ushahidi wenye nguvu kubwa wa upendo wa Mungu. Alipoona mti wa uzima, Nefi aliomba kujua tafsiri yake. Katika kujibu, malaika alimwonesha Nefi mji, mama na mtoto mchanga. Nefi alipokuwa akitazama mji la Nazareti na mama mwenye haki Mariamu, akiwa amembeba mtoto Yesu mikononi mwake, malaika alitangaza, “Tazama Mwanakondoo wa Mungu, ndiyo, hata Mwana wa Baba wa milele!”2
Katika wasaa ule mtakatifu, Nefi alielewa kwamba katika kuzaliwa kwa Mwokozi, Mungu alikuwa akionesha upendo Wake wa kweli na mkamilifu. Upendo wa Mungu, Nefi alishuhudia, “umejieneza wenyewe kila mahala katika mioyo ya watoto wa watu.”3
Tunaweza kuuelezea upendo wa Mungu kama nuru inayosambaa kutoka kwenye mti wa uzima, ikijieneza kila mahala juu ya dunia yote mpaka ndani ya mioyo ya watoto wa watu. Nuru ya Mungu na upendo vinasambaa kwa viumbe vyake vyote.4
Wakati mwingine kimakosa tunadhani kwamba tunaweza tu kuhisi upendo wa Mungu baada ya kufuata fimbo ya chuma na kula tunda. Upendo wa Mungu, hata hivyo haupokelewi tu na wale wanaokuja kwenye mti bali ni nguvu hasa ambayo inatusababisha sisi tuutafute ule mti.
“Kwa sababu hii, ni wa kutamanisha mno zaidi ya vitu vyote,” Nefi alifundisha, na malaika alitamka, “Ndiyo, na inafurahisha moyo kwa shangwe.”5
Miaka ishirini iliyopita, mwana familia mpendwa aliacha Kanisa. Alikuwa na maswali mengi yasiyo na majibu. Mke wake, mwongofu, alibaki mkweli kwenye imani yake. Walifanya kazi kubwa kuitunza ndoa yao katika tofauti zilizojitokeza.
Mwaka uliopita aliandika maswali matatu kuhusu Kanisa ambayo yalikuwa magumu kwake kuridhia na aliyatuma kwa wanandoa wawili ambao wamekuwa rafiki zake kwa miaka kadhaa. Aliwaomba wayatafakari maswali hayo na waje kwenye chakula cha jioni kushiriki mawazo yao.
Kufuatia ziara hii na marafiki, alikwenda kwenye chumba chake na alianza kufanyia kazi mradi fulani. Mazungumzo ya jioni na upendo aliooneshwa na rafiki zake vilikuja mbele ya akili zake. Baadaye aliandika kwamba alilazimika kusimamisha kazi yake. Alisema: “Nuru angavu iliijaza nafsi yangu. … Nilikuwa na uzoefu na hisia hizi za kina zenye kuelimisha, lakini katika jambo hili ziliendelea kukua kwa nguvu kubwa kuliko hapo kabla na zilidumu kwa dakika kadhaa. Nilikaa kwa utulivu nikiwa na hisia hizi, ambazo nilikuja kuzielewa kama onesho la upendo wa Mungu kwa ajili yangu. … Nilihisi msukumo wa kiroho ambao uliniambia kwamba ningeweza kurudi Kanisani na kuonesha upendo huu wa Mungu katika kile ninachokifanya huko.”
Kisha alijiuliza kuhusu maswali yake. Hisia aliyoipata ilikuwa kwamba Mungu aliheshimu maswali yake na kwamba kutokuwa na majibu yaliyo wazi hakupaswi kumzuia kusonga mbele.6 Anapaswa kushiriki upendo wa Mungu kwa wote wakati akiendelea kutafakari. Wakati alipotendea kazi msukumo ule, alihisi undugu na Joseph Smith, ambaye alisema baada ya Ono lake la Kwanza, “Roho yangu ilijawa na upendo, na kwa siku nyingi niliweza kufurahi kwa furaha kuu.”7
Cha kushangaza, miezi michache baadaye, mwanafamilia huyu alipata wito uleule aliokuwa nao miaka 20 kabla. Mara ya kwanza alipokuwa na wito, alifanya wajibu wake kama muumini mtiifu wa Kanisa. Sasa swali kwake likawa siyo “Je, ni kwa jinsi gani ninaweza kutimiza wito huu?” Bali “Je, ni kwa jinsi gani ninaweza kuonesha upendo wa Mungu kupitia huduma yangu?” Kwa mtazamo huu mpya, alihisi furaha, maana na lengo katika vipengele vyote vya wito wake.
Akina dada na akina kaka, tunawezaje kupokea nguvu ya kubadilisha ya upendo wa Mungu? Nabii Mormoni anatutaka sisi “kuomba kwa Baba kwa nguvu zote za moyo, kwamba mjazwe na upendo huu, ambao ametoa kwa wote ambao ni wafuasi wa kweli wa Mwana wake, Yesu Kristo.”8 Mormoni hatualiki tu kuomba kwamba tuweze kujazwa na upendo Wake kwa wengine bali kuomba ili tuweze kujua juu ya upendo msafi wa Mungu kwa ajili yetu wenyewe.9
Tunapopokea upendo Wake, tunapata shangwe kuu katika kujitahidi kupenda na kutumikia kama Yeye alivyofanya, tukiwa “wafuasi wa kweli wa Mwana wake, Yesu Kristo.”10
Upendo wa Mungu haupatikani katika hali za maisha yetu, bali katika uwepo Wake ndani ya maisha yetu. Tunafahamu kuhusu upendo Wake wakati tunapopokea nguvu zaidi ya zetu wenyewe na wakati Roho Wake anapoleta amani, faraja na mwongozo. Nyakati zingine inaweza kuwa vigumu kuhisi upendo Wake. Tunaweza kuomba kuwa na macho yetu yakiwa yamefunguliwa ili kuuona mkono Wake katika maisha yetu na kuuona upendo Wake katika uzuri wa uumbaji Wake.
Tunapoyatafakari maisha ya Mwokozi na dhabihu yake isiyo na mwisho, tunaanza kuelewa upendo Wake kwa ajili yetu. Kwa unyenyekevu tunaimba maneno ya Eliza R. Snow: “Damu Yake ya thamani aliimwaga bila shuruti; maisha yake aliyatoa bila shuruti.”11 Unyenyekevu wa Yesu katika mateso kwa ajili yetu unamiminika juu ya nafsi zetu, ukifungua mioyo yetu kutafuta msamaha kwenye mikono Yake na kutujaza kwa hamu ya kuishi jinsi Alivyoishi.12
Rais Nelson aliandika, “Tunapojitoa zaidi kuweka maisha yetu kama yalivyokuwa Yake, upendo wetu unakuwa msafi zaidi na mtakatifu zaidi.”13
Mwana wetu alikumbuka: “Nilipokuwa na umri wa miaka 11, mimi na rafiki zangu tuliamua kujificha na kukwepa nusu ya kwanza ya darasa letu la Msingi. Hatimaye wakati tulipowasili, kwa mshangao wetu, mwalimu alitupokea kwa furaha. Kisha alitoa sala ya dhati ambapo alitoa shukrani ya dhati kwa Bwana kwamba tumeamua kuja darasani siku ile kwa mapenzi yetu wenyewe. Siwezi kukumbuka somo lilikuwa kuhusu nini au hata jina la mwalimu wetu, lakini sasa, kiasi cha miaka 30 baadaye, bado ninaguswa na upendo msafi alionionesha siku ile.”
Miaka mitano iliyopita, niliona mfano wa upendo mtakatifu wakati nikihudhuria darasa la Msingi huko Urusi. Nilimwona dada mwaminifu akipiga magoti mbele ya wavulana wawili na kushuhudia kwao kwamba hata kama wangekuwa ni wavulana pekee wanaoishi duniani, Yesu angeteseka na kufa kwa ajili yao.
Ninashuhudia kwamba Bwana wetu na Mwokozi hakika alikufa kwa ajili ya kila mmoja wetu. Lilikuwa ni onesho la upendo Wake usio na mwisho kwa ajili yetu na kwa ajili ya Baba Yake.
“Ninajua kwamba Mkombozi Wangu yu Hai.” Faraja iliyoje sentensi hii tamu inatoa! … Yu hai kutubariki [sisi] kwa upendo Wake.”14
Na tufungue mioyo yetu ili kupokea upendo msafi ambao Mungu anao kwa ajili yetu na kisha kuumimina upendo huo katika yote tunayofanya na yale tuliyo. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.