Jina la Kanisa Si Jambo la Mjadala
Wakati bila shuruti tunapofuata ushauri wa Bwana kama ulivyofunuliwa kupitia nabii Wake aliye hai, hususan ikiwa unapita fikra zetu za juu, ukihitaji unyenyekevu na dhabihu, Bwana anatubariki kwa nguvu za ziada za kiroho.
Katika mkutano na wanahabari mnamo Agotsi 16, 2018, Rais Russell M. Nelson alisema: “Bwana alileta msukumo akilini mwangu juu ya umuhimu wa jina ambalo Yeye amelifunua kwa ajili ya Kanisa Lake, hata Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.1 Tuna Kazi mbele yetu ya kujileta kwenye uwiano na mapenzi Yake.2
Siku mbili badaye, mnamo Agosti 18, nilikuwa pamoja na Rais Nelson huko Montreal, Kanada. Baada ya mkutano wetu katika Palais de Congré yenye kuvutia, Rais Nelson alijibu maswali ya waandishi wa habari. Alikiri kwamba “itakuwa changamoto [kujenga upya jina la Kanisa, na] kuondoa utamanduni wa zaidi ya miaka mia moja.” Lakini aliongeza, “Jina la Kanisa si jambo la mjadala.”3
Wiki saba baadaye, Raisi Nelson alizungumza katika mkutano mkuu: “Bwana alileta msukumo akilini mwangu juu ya umuhimu wa jina Yeye alilotamka kwa ajili ya Kanisa Lake, hata Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. … Alikuwa ni Mwokozi Mwenyewe aliyesema,‘Kwani hivyo ndivyo kanisa langu litakavyoitwa.’” Kisha Rais Nelson akarudia tena, “Jina la Kanisa si jambo la mjadala.”4
Swali Zuri
Swali zuri likaibuka: “Kwa nini sasa?” wakati kwa miongo mingi tumelikubali jina la utani “Mormoni”? “Kwaya ya Mormoni Tabenako,” video fupi za “Mimi ni Mmormoni,” wimbo wa Msingi “Mimi ni Mvulana Mmormoni”?
Mafundisho ya Kristo hayabadiliki na ni ya milele. Bali hatua mahususi na muhimu za kazi ya Mwokozi zinafunuliwa katika wakati ufaao. Asubuhi ya leo Rais Nelson alisema, “Urejesho ni mchakato, si tukio.”5 Na Bwana alisema, “Mambo yote lazima yatakuja kutimia katika wakati wake.”6 Sasa ni wakati wetu na tunajenga upya jina lililofunuliwa la Kanisa.
Utambulisho na hatma ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho huhitaji kwamba tuitwe kwa jina Lake. Hivi karibuni nilikuwa Kirtland, Ohio, pale ambapo Nabii Joseph Smith, akiwa na waumini wachache tu wa Kanisa, alitoa unabii, “Kanisa hili litaijaza Amerika Kaskazini na Kusini—litaujaza ulimwengu.”7 Bwana alielezea kazi ya kipindi hiki cha maongozi ya Mungu kama “kazi ya maajabu na ya kushangaza.”8 Alizungumza juu ya “agano [ambalo] litatimizwa katika siku za mwisho,” likiruhusu “dunia yote ibarikiwe.”9
Maneno ya mkuatano huu yanatafsiriwa mubashara katika lugha 55. Hatimaye, maneno haya yatasikika na kusomwa katika lugha 98 katika zaidi ya nchi na mataifa 220.
Wakati Mwokozi atakaporejea kwa ukuu na utukufu, waumini waaminifu wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho watakuwa miongoni mwa mataifa yote, watu wote, makabila yote, na tamaduni zote za dunia.
Ushawishi Unaoongezeka wa Kanisa
Ushawishi wa Kanisa la Yesu Kristo lilirejeshwa hautakuwa tu kwa wale ambao ni waumini wa Kanisa. Kwa sababu ya madhihirisho ya kimbingu katika siku yetu, kwa sababu ya maandiko matakatifu yaliyorejeshwa duniani na kipawa chenye nguvu cha Roho Mtakatifu, tutakuwa nuru iangazayo juu ya mlima wakati vivuli vya kiza cha kutoamini katika Yesu Kristo vikiufunika ulimwengu. Ingawa wengi wanaweza kuruhusu ulimwengu utie giza imani yao katika Mkombozi, sisi “hatutaondoshwa kutoka mahali [petu].”10 Wakristo ambao hawapo miongoni mwa uumini wetu watakubali kazi yetu na ushahidi wetu wa uhakika wa Kristo. Hata wale Wakristo ambao wametutazama kwa wasiwasi watatukumbatia kama marafiki. Katika siku hizi zijazo, tutaitwa kwa jina la Yesu Kristo.
Asanteni kwa juhudi zenu za kiungwana kusongesha mbele jina la Kanisa. Katika mkutano miaka mitatu iliyopita, Rais Nelson alituahidi “kwamba umakini wetu wa kutumia jina sahihi la Kanisa la Mwokozi… [utatuletea] ongezeko la imani na ufikiaji wa nguvu kubwa ya kiroho.”11
Ahadi hii imetimia kwa wafuasi waliojitoa kwa dhati kote ulimwenguni.12
Kaka Lauri Ahola kutoka mashariki ya Marekani anakiri kwamba wakati mwingine anapata ugumu kushiriki jina kamili la Kanisa. Lakini kwa sababu ya ushauri wa nabii, anaendelea kulitumia. Wakati mmoja, alikuwa amemtembelea rafiki kwenye kanisa la imani nyingine. Haya ni maneno yake:
Mtu mmoja aliuliza, “Wewe ni Mmormoni?”
“‘Mimi ni muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, ndiyo,’ nilisema. Alianza kuniuliza maswali kadhaa, kila moja likianza na: ‘Je, Kanisa la Mormoni linaamini … ?’ Na kila wakati, nilianza jibu langu kwa kifungu hiki: ‘Katika Kanisa lililorejeshwa la [Yesu] Kristo, tunaamini…’
“… Wakati alipogundua kwamba sikuwa nikikubali jina la ‘Mormoni,’ aliniuliza kwa kuweka wazi, ‘Je, wewe si Mmormoni?’
“Hivyo nilimuuliza ikiwa alijua Mormoni alikuwa nani—hakujua. Nilimwambia kwamba Mormoni alikuwa nabii, … [na mimi] ninafurahia kuhusiana [naye].
“‘Lakini,’ niliendelea, ‘Mormoni hakufa kwa ajili ya dhambi zangu. Mormoni … hakuteseka huko Gethsemane au kufa msalabani [kwa ajili yangu]. … Yesu Kristo ni Mungu wangu na Mwokozi wangu. … Na ni kwa jina Lake kwamba mimi ninataka kujulikana. …’
“… Baada ya ukimya wa sekunde chache, [yule mtu akasema kwa mshangao],‘Kwa hivyo, Wewe ni Mkristo!’”13
Mnakumbuka maneno ya Rais Nelson? “Ninawaahidi kuwa kama tutafanya bidii kurejesha jina sahihi la Kanisa la Bwana, Yeye ambaye hili Kanisa ni Lake atatoa nguvu Zake na baraka juu ya vichwa vya Watakatifu wa Siku za Mwisho, nguvu na baraka ambazo hatujapata kuziona.”14
Bwana Daima Hufungua Njia
Bwana daima anatimiza ahadi Zake. Yeye hufungua njia kwa ajili yetu tunapofanya kazi Yake.
Kwa miaka mingi tulitumainia kununua amwani za tovuti za intaneti za ChurchofJesusChrist.org na ChurchofJesusChrist.com. Hakuna yoyote iliyokuwa inauzwa. Karibu na wakati wa tangazo la Rais Nelson, zote zilipatikana ghafla. Ilikuwa ni muujiza.15
Bwana amekuza juhudi zetu za kurekebisha majina ambayo kwa muda yalihusiana na Kanisa.
Tukisonga mbele kwa imani, jina la Kwaya ya Mormon Tabernacle lilibadilishwa kuwa Kwaya ya Tabenako hapa Temple Square. Tovuti ya LDS.org, ambayo hupata kutembelewa kwa zaidi ya mara milioni 21 kila mwezi, iligeuzwa kuwa ChurchofJesusChrist.org.16 Jina la LDS Business College lilibadilishwa kuwa Ensign College. Tovuti Mormon.org ilibadilishwa kuwa ChurchofJesusChrist.org. Zaidi ya bidhaa elfu moja ambazo zilikuwa na jina “Mormon” au “LDS” likiambatishwa nazo zimebadilishwa. Watakatifu Waaminifu wa Siku za Mwisho wamebadilisha tovuti zao, podcast, na akaunti za Twitter.
Tulipitisha alama mpya iliyojikita katika Yesu Kristo.
“Katikati ya alama ni uwakilishi wa sanamu ya marumaru ya Thorvaldsen Christus. Inamuelezea Bwana aliyefufuka, aliye hai akinyoosha mikono kuwakumbatia wote ambao watamwendea Yeye.
“Kiishara, Yesu Kristo amesimama chini ya tao [kutukumbusha] sisi juu ya Mwokozi aliyefufuka akitoka kaburini.”17
Alama na usanifu mpya wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho vimebadilishwa katika lugha zaidi ya 50. Majina mapya ya maeneo husika yamepatikana ulimwenguni kote.
Shukrani kwa Usaidizi wa Watu Wengine
Tunawashukuru watu wengi wazuri na wema ambao wameheshimu shauku yetu ya kuitwa kwa jina letu sahihi. Nilisoma makala hivi karibuni ambayo ilimnukuu kadinali wa Katoliki akirejelea “Watakatifu wa Siku za Mwisho.”18 Nilipokutana na kiongozi wa kanisa la Kikristo mwezi mmoja uliopita mashariki ya Marekani, alirejelea Kanisa katika rejeleo lake la kwanza kwa jina letu lote, na kuendelea zaidi ya mara moja kusema “Kanisa la Yesu Kristo.”
Tuligundua kwamba kuongeza maneno sita kwenye jina letu haitakuwa rahisi kwa vyombo vya habari, lakini kama Rais Nelson alivyosema mapema, “vyombo vya habari vinavyowajibika vitakuwa na huruma katika kujibu ombi letu.”19 Asanteni kwa kutupatia sisi heshima sawa na ile inayotolewa kwa tamaduni, wanariadha, wanasaisa, au taasisi za kijamii kwa kutumia jina letu lililopendekezwa.
Kutakuwa na wachache ambao, wakitumaini kuchepua au kufifisha dhamira yetu, wataendelea kutuita sisi “Wamormoni” au “Kanisa la Mormoni.” Kwa heshima, tunaviomba tena vyombo vya habari visivyopendelea upande wowote kuhesimu shauku yetu ya kuitwa kwa jina letu la takriban miaka 200.
Ujasiri wa Watakatifu wa Siku za Mwisho
Kuna maefu na maefu ya Watakatifu wa Siku za Mwisho ambao kwa ujasiri wametangaza jina la Kanisa. Tunapofanya sehemu yetu, wengine watafuata. Naipenda hadithi hii kutoka Tahiti.
Iriura Jean wa miaka kumi aliamua kufuata ushauri wa Rais Nelson.
“Katika darasa lake la shule walizungumzia wikiendi zao … na Iriura alizungumza kuhusu … kanisa.
“Mwalimu wake, Vaite Pifao, alisema, ‘Oh, kwa hiyo wewe ni Mmormoni?’
“Iriura alisema kwa ushupavu, ‘Hapana … Mimi ni muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho!’
“Mwalimu wake akajibu ‘Ndiyo, … wewe ni Mmormoni.’
“Iriura akasisitiza, ‘Hapana mwalimu, Mimi ni muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho!’
“Dada Pifao alishangazwa na ukakamavu wa Iriura na kujiuliza kwa nini alisisitiza sana kwenye kutumia jina refu la kanisa lake. [Aliamua kujifunza zaidi kuhusu Kanisa.]
“[Baadaye, wakati Dada] Pifao alipobatizwa [alitoa shukrani] kwamba Iriura alishikilia ushauri wa Rais Nelson.”
“Jina la Kanisa si jambo la mjadala.” Acha tusonge mbele kwa imani. Wakati bila shuruti tunapofuata ushauri wa Bwana, kama ulivyofunuliwa kupitia nabii Wake aliye hai hususan ikiwa unapita fikra zetu za juu, ukihitaji unyenyekevu na dhabihu, Bwana anatubariki kwa nguvu za ziada za kiroho na kutuma malaika Zake ili watusaidie na kusimama nasi.21 Tunapokea uthibitisho wa Bwana na ukubali Wake.
Mimi ni shahidi wa nguvu za mbinguni ambazo zipo juu ya nabii wetu mpendwa Rais Russell M. Nelson. Shauku yake ya dhati ni kumpendeza Bwana na kuwabariki watoto wa Baba yetu wa Mbinguni. Kutoka kwenye uzoefu mtakatifu, binafsi, ninashuhudia upendo wa Bwana kwake. Yeye ni nabii wa Mungu.
Ninashuhudia kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu. Katika jina la Yesu Kristo, amina.