Mkutano Mkuu
Miujiza ya Injili ya Yesu Kristo
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2021


Miujiza ya Injili ya Yesu Kristo

Ninajua kwamba injili yake inaweza kutuletea tumaini, amani na shangwe, sio tu kwa sasa, lakini pia itawabariki na wengine wengi katika vizazi vijavyo.

Mabuhay! Nawaleteeni upendo na salamu za kusisimua kutoka kwa Watakatifu wema wa Ufilipino. Huu ni mwaka wa 60 tangu wamisionari wa kwanza walipofika katika visiwa vya Ufilipino. Leo, kuna misheni 23 na zaidi ya waumini 800,000 wa Kanisa katika vigingi 123. Sasa kuna mahekalu saba yanayofanya kazi, yanayojengwa au yaliyotangazwa. Kwa kweli huu ni muujiza. Tunashuhudia utimizwaji wa unabii katika 2 Nefi 10:21: “Kubwa ni ahadi za Bwana kwa wale walio kwenye visiwa vya bahari.”

Picha
Rais Hinckley akiwa Ufilipino

Muujiza huu pia ni utimizwaji wa unabii uliotolewa kwenye sala wakati huo na Mzee Gordon B. Hinckley huko Manila mnamo 1961. Katika sala ile, Mzee Hinckley alisema: “Tunatoa baraka Zako juu ya watu wa kisiwa hiki, kwamba watakuwa rafiki na wakarimu na wema na wenye fadhila kwa wale watakaokuja hapa, na kwamba wengi, ndio Bwana, tunaomba kwamba watakuwa [wengi,] wengi maelfu ambao watapokea ujumbe huu na kubarikiwa nao. Wabariki na akili sikivu na mioyo ya kuelewa pamoja na imani ya kupokea, pamoja na ujasiri wa kuishi kanuni za injili” (dedicatory prayer at American War Memorial Cemetery, Philippines, Apr. 28, 1961).

Picha
Familia ya Revillo

Mbali na wengi, wengi maelfu ya Watakatifu wa Siku za Mwisho waaminifu, muujiza wa injili umeleta mabadiliko chanya ndani ya nchi na watu wake. Mimi ni ushahidi hai wa hili. Nilikuwa na miaka sita wakati wazazi wangu walipojiunga na Kanisa huko kisiwa cha kusini cha Mindanao. Kwa wakati huo, kulikuwa na misheni moja tu nchi nzima na hakukuwa na kigingi. Milele nitakuwa na shukrani kwa ujasiri na jitihada za wazazi wangu za kumfuata Mwokozi. Ninawaheshimu wao pamoja na waanzilishi wote wa Kanisa huko Ufilipino. Waliandaa njia kwa ajili ya vizazi vijavyo kubarikiwa.

Mfalme Benjamini katika Kitabu cha Mormoni alisema: “Na zaidi, ningetamani mtafakari juu ya hali ya baraka na yenye furaha ya wale wanaotii amri za Mungu. Kwani tazama, wanabarikiwa katika vitu vyote, vya muda na vya kiroho” (Mosia 2:41).

Tunapoishi na kutii kanuni na ibada za injili, tunabarikiwa, kubadilishwa na kuongolewa ili kuwa zaidi kama Yesu Kristo. Hivyo ndivyo jinsi injili ilivyowabadili na kuwabariki Watakatifu wa Ufilipino, ikiwemo familia yangu. Kweli injili ndio njia ya maisha ya furaha na maisha tele.

Kanuni ya kwanza ya injili ni imani katika Bwana Yesu Kristo. Wafilipino wengi wana imani ya asili katika Mungu. Ni vyepesi kwetu sisi kumwamini Yesu Kristo na kujua kwamba tunaweza kupokea majibu ya maombi yetu.

Picha
Familia ya Obedoza

Familia ya Obedoza ni mfano mkubwa wa hili. Kaka Obedoza alikuwa rais wangu wa tawi nilipokuwa kijana. Hamu kubwa ya Kaka na Dada Obedoza ilikuwa ni kuunganishwa na familia yao katika hekalu la Manila. Waliishi katika jiji la General Santos, maili 1,000 (1600 km) kutoka Manila. Kwa familia ya watu tisa, kufanya safari kwenda hekaluni kulionekana kusikowezekana. Lakini kama mfanya biashara aliyekwenda na kuuza vyote alivyonavyo ili kununua lulu yenye thamani kubwa (ona Mathayo 13:45–46), wanandoa hawa waliamua kuuza nyumba yao ili kulipia gharama za safari. Dada Obedoza alikuwa na wasiwasi kwa sababu hawangekuwa na nyumba watakaporudi. Lakini Kaka Obedoza alimhakikishia mkewe kwamba Bwana atatoa.

Waliunganishwa kama familia kwa muda na milele yote katika hekalu mnamo 1985. Ndani ya hekalu walipata shangwe isiyolinganishwa na chochote—lulu yao ya thamani kuu. Na Maneno ya Kaka Obedoza yalikuwa kweli, Bwana alitoa. Waliporudi kutoka Manila, wasamaria wema waliwapa sehemu za kuishi, na hatimaye walipata nyumba yao wenyewe. Bwana huwajali wale wanaoonyesha imani yao Kwake.

Kanuni ya pili ya injili ni toba. Toba ni kugeuka kutoka katika dhambi na kumgeukia Mungu kwa ajili ya msamaha. Ni badiliko la akili na moyo. Kama Rais Nelson anavyofundisha, ni “kutenda na kuwa vizuri kidogo kila siku” (“Tunaweza Kufanya Vizuri Zaidi na Kuwa Wazuri zaidi,” Liahona, Mei 2019, 67).

Toba ni zaidi kama sabuni. Kama mhandisi wa kemikali, nilifanya kazi katika kiwanda cha sabuni huko Ufilipino. Nilijifunza jinsi ya kutengeneza sabuni na mchakato wa jinsi inavyofanya kazi. Unapochanganya mafuta pamoja na alkali na kuongeza viua bakteria, hutengeneza kitu chenye nguvu ambacho kinaweza kuondoa bakteria na virusi. Kama sabuni, toba ni kileta usafi. Inatupatia fursa ya kuondoa uchafu wetu na mabaki ya kale, hivyo kustahili kuwa pamoja na Mungu, kwani “hakuna kitu kichafu kinachoweza kurithi ufalme wa [Mungu]” (Alma 11:37).

Kupitia toba tunapokea nguvu ya kusafishwa, ya utakaso ya Yesu Kristo. Hii ni sehemu muhimu ya mchakato wa uongofu. Hili ndilo lililotokea kwa waAnti-Nefi-Lehi katika Kitabu cha Mormoni. Walikuwa Walamani ambao walikuwa wameongolewa kikamilifu kwamba “hawakuanguka tena” (ona Alma 23:6–8). Walizika silaha zao za vita na hawakuzichukua tena. Walikuwa radhi kufa kuliko kuvunja agano hilo. Na walithibitisha hilo. Tunajua kwamba dhabihu yao ilileta miujiza; maelfu waliopigana dhidi yao walitupa chini silaha zao na waliongolewa. Miaka kadhaa baadaye wana wao, ambao tunawajua kama vijana askari majasiri, walilindwa katika vita dhidi ya maadui wabaya sana!

Picha
Baba wa Mzee Revillo

Familia yangu na Watakatifu Wafilipino wengi walipitia mchakato sawa na huo wa uongofu. Tulipoikubali injili ya Yesu Kristo na kujiunga na Kanisa, tulibadili njia zetu na tamaduni zetu kuendana na injili. Ilibidi tuachane na desturi mbaya. Nililiona hili kwa baba yangu alipojifunza injili na kutubu. Alikuwa ni mvuta sigara mkubwa, lakini alitupa sigara zake mbali na kamwe hakushika tena. Kwa sababu ya uamuzi wake wa kubadilika, vizazi vinne kutokea kwake vimebarikiwa.

Picha
Vizazi vya familia ya Revillo

Toba hutuongoza kufanya na kutunza maagano kwa kupitia ibada takatifu. Ibada ya kwanza ya wokovu na kuinuliwa ni ubatizo kwa kuzamishwa kwa ajili ya ondoleo la dhambi. Ubatizo huturuhusu kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu na kuingia katika agano na Bwana. Tunaweza kufanya upya agano hili la ubatizo kila wiki tunaposhiriki sakramenti. Hili pia ni muujiza!

Akina kaka na dada, ninawaalikeni kuuleta muujiza huu ndani ya maisha yenu. Njooni kwa Yesu Kristo na chagueni kuonyesha imani yenu Kwake, mtubu na mfanye na kutunza maagano yanayopatikana katika ibada za wokovu na kuinuliwa. Hili litakuruhusu kuunganishwa na Kristo na kupokea nguvu na baraka za uungu (ona Mafundisho na Maagano 84:20)).

Ninashuhudia uhalisia wa Yesu Kristo na kwamba Anaishi na anampenda kila mmoja wetu. Ninajua kwamba injili yake inaweza kutuletea tumaini, amani na shangwe, sio tu kwa sasa, lakini pia itawabariki na wengine wengi katika vizazi vijavyo. Hiyo ndio sababu ya tabasamu nzuri na za kusisimua za Watakatifu wa Ufilipino. Ni muujiza wa injili na mafundisho ya Kristo. Ninashuhudia hili katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.

Chapisha