Mkutano Mkuu
Kujiandaa kwa ajili ya Ujio wa Pili wa Kristo
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2021


Kujiandaa kwa ajili ya Ujio wa Pili wa Kristo

Kuliko ilivyowahi kuwa hapo awali, tunatakiwa kukabiliana na uhalisia kwamba tunakaribia Ujio wa Pili wa Yesu Kristo.

Kama ilivyoandikwa kwenye Kitabu cha Mormoni, miaka sita kabla ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo, Samweli, Mlamani mwenye haki alitabiri kwa watu wa Nefi ambao kwa wakati huo walikuwa watu wakengeufu sana,1 juu ya ishara ambazo zingeambatana na kuzaliwa kwa Mwokozi. Kwa masikitiko, Wanefi wengi walizikataa ishara hizo kwa sababu ilikuwa “haina maana kwamba kiumbe kama Kristo [angeweza] kuja.”2

Kwa majuto, kulingana na kumbukumbu ya maandiko, Wayahudi wengi, katika hali kama hiyo, wasingeweza kukubali mtu aitwaye Yesu, kutoka jimbo lililoonekana dogo la Galilaya, alikuwa ni Masiya aliyesubiriwa kwa muda mrefu.3 Yesu, ambaye hakika alikuja kutimiza unabii mwingi uliotolewa na manabii wa Kiebrania, alikataliwa na hata kusulibiwa kwa sababu, kama nabii wa Kitabu cha Mormoni Yakobo alivyofundisha, Wayahudi “wakatafuta vitu ambavyo hawakuweza kufahamu.” Hatimaye, Yakobo anashuhudia kwamba “Mungu ameuondoa udhahiri wake kutoka kwao, na kuwapatia wao vitu vingi ambavyo hawawezi kufahamu, kwa sababu walivitamani. Na kwa sababu walivitamani Mungu alivitenda, ili wajikwaze.”4

Cha kustaajabisha, hakuna mafundisho, hakuna muujiza, na hakuna mwonekano hata wa malaika wa mbinguni, kama ilivyotokea kwa Lamani na Lamueli,5 kuonekana kuwa na nguvu za ushawishi kuwashawishi baadhi ya watu kubadilisha mwelekeo wao, mtazamo, au imani kwamba kitu fulani ni cha kweli. Hilo hutokea hasa wakati mafundisho au miujiza havikubaliani na matakwa ya mtu binafsi aliyokuwa nayo, matamanio, au mawazo.

Tafadhali kwa muda mchache hebu tofautisha maandiko mawili yafuatayo, la kwanza kutoka kwa Mtume Paulo akiongelea kuhusu siku za mwisho, akieleza njia za mwanadamu, na la pili kutoka kwa nabii Alma akionyesha jinsi Mungu anavyofanya kazi Zake kati ya wanadamu. Kwanza kutoka kwa Paulo:

“Hii inafahamika pia, kwamba katika nyakati za mwisho nyakati za hatari zitakuja.

“Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye tamaa, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi,

“Wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema,

“Wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu; …

“Wakijifunza siku zote, ila wasiweze kabisa kuufikia ujuzi wa kweli.”6

Na sasa kutoka kwa Alma, akionyesha kanuni ya msingi ya injili ya Yesu Kristo: “Sasa labda unadhani kwamba huu ni upuuzi ndani yangu; lakini tazama nakwambia, kwamba kupitia kwa vitu vilivyo vidogo na rahisi vitu vikubwa hutendeka; na njia ndogo mara nyingi hufadhaisha wenye hekima.”7

Tunaishi katika ulimwengu wa kisasa uliojawa na wingi wa maarifa na uhodari mwingi. Hata hivyo, mambo haya mara nyingi hugeuza msingi usio imara ambapo yamejengwa. Hatimaye, mambo haya hayaongozi kwenye ukweli halisi na kumwelekea Mungu na uwezo wa kupokea ufunuo, kupata maarifa ya kiroho, na kukuza imani katika Yesu Kristo inayoongoza katika wokovu.8

Kwa dhati tunakumbushwa maneno ya Bwana wetu kwa Tomaso na Mitume wengine katika ile jioni ya dhabihu Yake ya upatanisho: “Yesu alimwambia, mimi ni njia, ukweli, na uzima: hakuna mtu ajaye kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.”9

Kwa wale wenye macho ya kuona, masikio ya kusikia na mioyo ya kuhisi, kuliko ilivyowahi kuwa, tunatakiwa kukabiliana na uhalisia kwamba tunakaribia sana Ujio wa Pili wa Yesu Kristo. Kweli, magumu makubwa bado yanawasubiri wale walio duniani katika ujio Wake, lakini kuhusu hili, waaminifu hawana haja ya kuogopa.

Sasa nina nukuu kutoka Mada za Injili ya Kanisa chini ya kichwa cha habari “Ujio wa Pili wa Yesu Kristo”:

“Wakati Mwokozi atakapokuja tena, Atakuja katika nguvu na utukufu kurejesha dunia kama ufalme Wake. Ujio Wake wa Pili utaashiria mwanzo wa milenia.

“Ujio wa Pili utakuwa wa kuogofya, muda wa kuomboleza kwa waovu, lakini itakuwa siku ya amani kwa wenye haki. Bwana alitangaza:

“‘Kwani wale walio na hekima na kupokea ukweli, na kumchukua Roho Mtakatifu kuwa kiongozi wao, na hawajadanganyika—amini ninawaambia, hawatakatiliwa chini na kutupwa katika moto, bali watastahimili siku ile.

“‘Na dunia itatolewa kwao kwa urithi; nao wataongezeka na kuwa na nguvu, na watoto wao watakua pasipo dhambi hadi kwenye wokovu.

“‘Kwa kuwa Bwana atakuwa katikati yao, na utukufu wake utakuwa juu yao, naye atakuwa mfalme wao na mtoa sheria wao’ (Mafundisho na Maagano 45:57–59).”10

Katika maandalizi yetu ya Ujio wa Pili wa Yesu Kristo, ninatoa maelezo muhimu ya faraja kwa waaminio kutoka kwa Amosi nabii wa Agano la Kale: “Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.”11

Katika roho hii, nabii wa Bwana wa sasa kwa ulimwengu, Rais Russell M. Nelson, ametupa ushauri wa sasa wenye msukumo: “Injili ya Yesu Kristo ni injili ya toba. Kwa sababu ya Upatanisho wa Mwokozi, injili Yake inatoa mwaliko wa kuendelea kubadilika, kukua, na kuwa wasafi zaidi. Ni injili ya matumaini, ya uponyaji, na ya kuleta ukuaji. Kwa hiyo, injili ni ujumbe wa furaha! Roho zetu hufurahi kwa kila hatua ndogo tunayopiga kusonga mbele.”12

Ninashuhudia pasipo shaka na kuthibitisha uhalisia wa Mungu na miujiza yake katika maisha ya kila siku kwa watu wengi, wote wa hali za maisha ya chini na juu. Hakika, uzoefu mwingi mtakatifu unazungumzwa kwa nadra, kwa sehemu ni kwa sababu ya asili yake ya kiungu na uwezekano wa kukejeliwa na wale wasioujua vizuri.

Kuhusu hili, nabii wa mwisho wa Kitabu cha Mormoni, Moroni, anatukumbusha:

“Na tena ninawazungumzia nyinyi ambao hukataa unabii wa Mungu, na kusema kwamba haifanyiki tena, kwamba hakuna ufunuo, wala unabii, wala vipawa, wala uponyaji, wala kuzungumza kwenye lugha za kigeni, na kutafsiri lugha;

“Tazama nawaambia, yule anayekana vitu hivi hajui injili ya Kristo; ndio, hajasoma maandiko; na ikiwa ameyasoma, hayaelewi.

“Kwani si tunasoma kwamba Mungu ni yule yule jana, na leo, na hata milele, na kwake hakuna kubadilika wala kivuli cha kugeukageuka?”13

Ninamalizia mazungumzo yangu na tamko lenye msukumo kutoka kwa Nabii Joseph Smith, alilolitoa karibia na mwishoni mwa huduma yake pale alipotazamia Ujio wa Pili wa Yesu Kristo: “Je, Hatupaswi kuendelea na lengo hilo kubwa? Twende mbele na siyo nyuma. Ujasiri, ndugu [na, niongeze, akina dada]; na mbele, mbele kwenye ushindi! Acheni mioyo yenu ifurahi, na kuwa yenye furaha zaidi.”14 Katika hili naongeza ushahidi wangu katika jina la Yesu Kristo, amina.

Chapisha