Mioyo Imeunganishwa Pamoja
Unapojitanua kwa ukarimu, kujali na huruma, ninaahidi kwamba utainyosha mikono iliyolegea na utaiponya mioyo.
Utangulizi
Je! si ya kufurahisha jinsi ugunduzi muhimu wa kisayansi wakati mwingine unavyohamasishwa na matukio rahisi kama vile tufaha linaloanguka kutoka kwenye mti?
Leo, acha nishiriki ugunduzi ambao ulitokea kwa sababu ya kikundi cha sampuli cha sungura.
Katika miaka ya 1970, watafiti walianzisha jaribio la kuchunguza athari za lishe kwenye afya ya moyo. Kwa kipindi cha miezi kadhaa, walilisha kundi la sungura walio chini ya uangalizi chakula chenye mafuta mengi na kufuatilia shinikizo lao la damu, mapigo ya moyo na cholesterol.
Kama inavyotarajiwa, sungura wengi walionyesha ongezeko la mafuta ndani ya mishipa yao. Walakini haya hayakuwa yote! Watafiti walikuwa wamegundua kitu ambacho kilikuwa na maana zaidi. Ingawa sungura wote walikuwa na idadi kubwa ya mafuta, kundi moja kwa kushangaza lilikuwa na chini ya asilimia 60 kuliko mengine. Ilionekana kana kwamba walikuwa wakitazama makundi mawili tofauti vya sungura.
Kwa wanasayansi, matokeo kama haya yanaweza kusababisha kukosa usingizi. Jinsi gani hii iliwezekana? Sungura wote walikuwa ni uzao mmoja kutoka New Zealand, kutoka kwenye jeni iliyofanana. Wote walikuwa wamepokea kiasi sawa cha chakula kila mmoja.
Hii ingeweza kumaanisha nini?
Je! Matokeo haya yalibatilisha utafiti? Je! Kulikuwa na makosa katika muundo wa jaribio?
Wanasayansi walihangaika kuelewa matokeo haya yasiyotarajiwa!
Mwishowe, walielekeza umakini wao kwa wafanyakazi wa utafiti. Je! iliwezekana kwamba watafiti walikuwa wamefanya kitu kuathiri matokeo? Walipofuatilia hii, waligundua kwamba kila sungura aliye na mafuta machache alikuwa chini ya uangalizi wa mtafiti mmoja. Aliwalisha sungura wake chakula sawa na kila mtu mwingine. Lakini, kama mwanasayansi mmoja alivyoripoti, “alikuwa mtu mwenye ukarimu usio wa kawaida na mwenye kujali.” Alipowalisha sungura, “alizungumza nao, aliwabembeleza na kuwashikashika. … ‘Hakuweza kuacha kufanya hivyo. Hivyo ndivyo alivyokuwa.’”1
Alifanya zaidi ya kuwapa tu sungura chakula. Aliwapa upendo!
Kwa mtazamo wa kwanza, ilionekana kuwa haiwezekani kuwa hii inaweza kuwa sababu ya tofauti kubwa, lakini timu ya utafiti haikuweza kuona uwezekano mwingine wowote.
Kwa hivyo, walirudia jaribio—wakati huu wakidhibiti kwa umakini kila tofauti. Wakati walipochambua matokeo ya mwisho, kitu kile kile kilitokea! Sungura chini ya uangalizi wa mtafiti mwenye upendo walikuwa na matokeo mazuri zaidi ya kiafya.
Wanasayansi walichapisha matokeo ya utafiti huu katika jarida maarufu la Sayansi.2
Miaka kadhaa baadaye matokeo ya jaribio hili bado yanaonekana kuwa na ushawishi ndani ya jamii ya matabibu. Katika miaka ya hivi karibuni, Dkt. Kelli Harding alichapisha kitabu kilichoitwa The Rabbit Effect ambacho kinabeba jina la utafiti. Hitimisho lake: “Chukua sungura mwenye mtindo mbaya wa maisha. Zungumza naye. Mshikilie. Mwonyeshe upendo. … Uhusiano ulileta tofauti. … Mwishowe,” anahitimisha, “kile kinachoathiri afya yetu kwa njia zenye maana zaidi kinahusiana zaidi na jinsi tunavyotendeana, jinsi tunavyoishi, na jinsi tunavyofikiria juu ya maana ya kuwa mwanadamu.”3
Katika ulimwengu wa kidunia, madaraja yanayounganisha sayansi na kweli za injili wakati mwingine huonekana kuwa machache na ya mbali. Walakini kama Wakristo, wafuasi wa Yesu Kristo, Watakatifu wa Siku za Mwisho, matokeo ya utafiti huu wa kisayansi yanaweza kuonekana kuwa ya kukubalika zaidi kuliko ya kushangaza. Kwangu mimi, hii inaweka tofali jingine katika msingi wa ukarimu kama kanuni ya msingi ya injili—kanuni ambayo inaweza kuponya mioyo kihisia, kiroho na kama ilivyoonyeshwa hapa, hata kimwili.
Mioyo Imeunganishwa Pamoja
Alipoulizwa, “Mwalimu, ni amri ipi iliyo kuu?” Mwokozi alijibu “kumpenda Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote,” ikifuatiwa na, “Mpende jirani yako kama nafsi yako.”4 Jibu la Mwokozi linaimarisha wajibu wetu wa kimbingu. Nabii wa kale aliamuru “kwamba pasiwe na ubishi kati yetu, lakini kwamba [tutazame] kwa jicho moja … , mioyo [yetu] ikiwa imeunganishwa pamoja kwa umoja na kwa kupendana sisi kwa sisi.”5 Tunafundishwa zaidi kuwa “nguvu au uwezo … unapaswa kudumishwa … kwa upole na unyenyekevu, … kwa upendo, … usio unafiki.”6
Ninaamini kanuni hii ina matumizi kwa Watakatifu wote wa Siku za Mwisho: watu wazima, vijana, na watoto.
Kwa kuzingatia hilo, acha nizungumze moja kwa moja na ninyi ambao ni watoto wa umri wa Msingi.
Tayari mnaelewa umuhimu wa kuwa wakarimu. Kibwagizo cha moja ya nyimbo zenu za Msingi, “I’m Trying to Be Like Jesus,” kinafundisha:
Pendaneni kama Yesu anavyowapenda.
Jaribu kuonyesha ukarimu katika yote unayofanya.
Kuwa mpole na mwenye upendo kwa matendo na kwa mawazo,
Kwani haya ndiyo mambo Yesu aliyofundisha.7
Hata kwa kufanya hivyo, wakati mwingine unaweza kupata wakati mgumu. Hapa kuna hadithi ambayo inaweza kukusaidia kuhusu mvulana wa Msingi anayeitwa Minchan Kim kutoka Korea Kusini. Familia yake ilijiunga na Kanisa karibu miaka sita iliyopita.
“Siku moja shuleni, wenzangu kadhaa walikuwa wakimdhihaki mwanafunzi mwingine kwa kumwita majina mabaya. Ilionekana kama ya kufurahisha, kwa hivyo kwa wiki chache nilijiunga nao.
“Wiki kadhaa baadaye, mvulana yule aliniambia kuwa ingawa alijifanya hajali, aliumizwa na maneno yetu, na alilia kila usiku. nilikaribia kulia aliponiambia. Nilijuta sana na nilitaka kumsaidia. Siku iliyofuata nilimwendea na kuweka mkono wangu begani mwake na kuomba msamaha, nikisema, ‘Samahani sana kwamba nilikufanyia dhihaka.’ Aliitikia kwa kichwa kwa maneno yangu, na macho yake yakajaa machozi.
“Lakini watoto wengine waliendelea kumdhihaki. Kisha nilikumbuka kile nilichojifunza katika darasa la Msingi: chagua mema. Hivyo niliwaomba wana darasa wenzangu waache. Wengi wao waliamua kutobadilika na walinikasirikia. Lakini mmoja wa wavulana wengine alisema samahani, na sisi watatu tukawa marafiki wazuri.
“Ingawa watu wachache bado walikuwa wakimdhihaki, alijisikia vizuri kwa sababu alikuwa na sisi.
“Nilichagua mema kwa kumsaidia rafiki mwenye uhitaji.”8
Je! Huu sio mfano mzuri kwako kujaribu kuwa kama Yesu?
Sasa, kwa vijana wa kiume na wa kike, mnapoendelea kukua, kuwadhihaki wengine kunaweza kuwa ni hatari sana. Wasiwasi, unyogovu, na mbaya zaidi mara nyingi ni matokeo ya uonevu. “Wakati uonevu sio dhana mpya, mitandao ya kijamii na teknolojia vimeleta uonevu kwa kiwango kipya. Umekua tishio la mara kwa mara, tishio endelevu—uonevu wa mtandaoni.”9
Kwa wazi, adui anatumia hii kukiumiza kizazi chenu. Hakuna mahali pa hili katika mtandao wako, vitongoji, shule, akidi au madarasa. Tafadhali fanya yote uwezayo kufanya maeneo haya kuwa ya ukarimu na salama. Ikiwa unaangalia tu au kushiriki katika yoyote ya haya, sijui ushauri bora kuliko ule uliotolewa hapo awali na Mzee Dieter F. Uchtdorf:
“Inapokuja kwenye kuchukia, kusengenya, kudharau, kudhihaki, kuwa na kinyongo au kutaka kudhuru, tafadhali fanya yafuatayo:
“Acha!”10
Umesikia hilo? Acha! Unapojitanua kwa ukarimu, kujali, na huruma, hata kidijitali, ninaahidi kwamba utainyosha mikono iliyolegea na utaiponya mioyo.
Baada ya kuzungumza na watoto wa Msingi na vijana, sasa ninaelekeza ujumbe wangu kwa watu wazima wa Kanisa. Tunalo jukumu la msingi kuweka viwango na kuwa mfano wa kuigwa wa ukarimu, ujumuishaji, na ustaarabu—kufundisha tabia kama ya Kristo kwa kizazi kinachoinukia katika kile tunachosema na jinsi tunavyotenda. Ni muhimu hususani tunapogundua mabadiliko ya kijamii kuelekea mgawanyiko katika siasa, tabaka la kijamii na karibu kila tofauti nyingine iliyoundwa na wanadamu.
Rais M. Russell Ballard pia amefundisha kwamba Watakatifu wa Siku za Mwisho sio tu lazima wawe wakarimu kwa kila mmoja wao bali pia kwa kila mtu karibu nasi. Alisema: “Mara kwa mara nasikia waumini wakiwakosea wale wa imani zingine kwa kuwapuuza na kuwatenga. Hii inaweza kutokea hasa katika jamii ambazo waumini wetu ndio wengi. Nimesikia juu ya wazazi wenye mawazo finyu ambao huwaambia watoto kwamba hawawezi kucheza na mtoto fulani katika kitongoji kwa sababu tu familia yake sio ya Kanisa letu. Tabia ya aina hii haiendani na mafundisho ya Bwana Yesu Kristo. Siwezi kuelewa ni kwa nini muumini yeyote wa Kanisa letu anaruhusu mambo ya aina hii kutokea. … Sijawahi kusikia waumini wa Kanisa hili wakihimizwa kuwa kitu chochote isipokuwa wenye upendo, ukarimu, uvumilivu, na wakarimu kwa marafiki zetu na majirani wa imani zingine.”11
Bwana anatutarajia tufundishe kuwa ujumuisho ni njia chanya kuelekea umoja na kwamba utengano unasababisha mgawanyiko.
Kama wafuasi wa Yesu Kristo, tunasikitishwa tunaposikia jinsi watoto wa Mungu wanavyotendewa vibaya kulingana na utaifa wao. Tumevunjika moyo kusikia juu ya mashambulio ya hivi karibuni kwa watu ambao ni Weusi, Waasia, Walatino, au wa kikundi kingine chochote. Chuki, mgogoro wa utaifa au vurugu havipaswi kuwa na nafasi yoyote katika vitongoji vyetu, jamii au ndani ya Kanisa.
Hebu kila mmoja wetu, bila kujali umri wetu, tujitahidi kuwa bora.
Wapendeni Adui Zenu
Unapojitahidi kukua katika upendo, heshima na ukarimu, bila shaka utaumizwa au kuathiriwa vibaya na uchaguzi mbaya wa wengine. Tunafanya nini basi? Tunafuata ushauri wa Bwana “wapendeni adui zenu … na waombeeni wale wanaowachukia ninyi.”12
Tunafanya kila tuwezalo kushinda jaribu ambalo limewekwa katika njia yetu. Tunajitahidi kuvumilia hadi mwisho, wakati wote tukiomba kwamba mkono wa Bwana ubadilishe hali zetu. Tunatoa shukrani kwa wale anaowaweka katika njia yetu kutusaidia.
Nimeguswa na mfano huu kutoka kwenye historia yetu ya mwanzo ya Kanisa. Wakati wa msimu wa baridi wa 1838, Joseph Smith na viongozi wengine wa Kanisa walizuiliwa katika Jela ya Liberty wakati Watakatifu wa Siku za Mwisho walipofukuzwa kwa nguvu kutoka kwenye nyumba zao katika jimbo la Missouri. Watakatifu walikuwa maskini, wasio na marafiki, na walioteswa sana kwa baridi na ukosefu wa rasilimali. Wakazi wa Quincy, Illinois, waliona shida yao ya kukata tamaa na wakawafikia kwa huruma na urafiki.
Wandle Mace, mkazi wa Quincy, baadaye alikumbuka wakati alipowaona Watakatifu kando ya Mto Mississippi katika mahema ya muda: “Wengine walikuwa na shuka zilizotandazwa, kutengeneza makazi madogo kutokana na upepo, … watoto walikuwa wakitetemeka kuzunguka moto ambao upepo uliupuliza kwa hivyo haukuwasaidia sana. Watakatifu maskini walikuwa wakiteseka sana.”13
Wakiona shida ya Watakatifu, wakaazi wa Quincy walijumuika pamoja kutoa misaada, wengine walisaidia hata kuwasafirisha marafiki zao wapya kuvuka mto. Mace aliendelea, “[Wao] walichangia kwa hiari; wafanyabiashara wakigombea kati yao ni nani anayeweza kusaidia kwa ukarimu zaidi … kwa … nyama ya nguruwe, … sukari, … viatu na nguo, kila kitu masikini hawa waliofukuzwa walichohitaji zaidi.”14 Muda si mrefu, wakimbizi walizidi idadi ya wakaazi wa Quincy, ambao walifungua nyumba zao na kushiriki rasilimali zao chache kwa dhabihu binafsi.15
Watakatifu wengi walinusurika wakati wa baridi kali kwa sababu tu ya huruma na ukarimu wa wakaazi wa Quincy. Malaika hawa wa kidunia walifungua mioyo na nyumba zao, wakileta lishe ya kuokoa maisha, joto na—pengine muhimu zaidi—mkono wa urafiki kwa Watakatifu wanaoteseka. Ingawa kukaa kwao Quincy kulikuwa kwa muda mfupi, Watakatifu hawakusahau kamwe deni lao la shukrani kwa majirani zao wapendwa na Quincy ilijulikana kama “mji wa kimbilio.”16
Wakati shida na mateso vinapoletwa kwetu kwa matendo ya kukosoa, hasi au ya roho mbaya, tunaweza kuchagua kumtumaini Kristo. Tumaini hili linatokana na mwaliko Wake na ahadi ya “changamkeni, kwa kuwa nitawaongoza”17 na kwamba Yeye ataweka wakfu mateso yenu kwa faida yenu.18
Mchungaji Mwema
Acha tumalizie pale tulipoanzia: mlezi mwenye huruma, anajitanua kwa ukarimu kwa roho ya kulea na matokeo yasiyotarajiwa—kuponya mioyo ya wanyama ambao amepewa jukumu la kuwachunga. Kwa nini? Kwa sababu yeye ndivyo alivyo!
Tunapoangalia kupitia lenzi zetu za injili, tunatambua kwamba sisi pia tuko chini ya uangalizi wa mlezi mwenye huruma, ambaye hujiongeza kwa ukarimu na roho ya kulea. Mchungaji Mwema anamjua kila mmoja wetu kwa jina na ana mapendeleo binafsi kwetu.19 Bwana Yesu Kristo mwenyewe alisema: “Mimi ndimi mchungaji mwema, na nawajua kondoo wangu. … Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo.”20
Katika wikiendi hii takatifu ya Pasaka, napata amani ya kudumu kwa kujua kwamba “Bwana ndiye mchungaji wangu”21 na kwamba kila mmoja wetu anajulikana Kwake na chini ya uangalizi wake mkarimu. Tunapokabiliana na upepo na dhoruba za maisha, magonjwa na majeraha, Bwana—Mchungaji wetu, Mlezi wetu—ataturutubisha kwa upendo na ukarimu. Ataponya mioyo yetu na kuzirejesha nafsi zetu.
Juu ya hili ninashuhudia—na juu ya Yesu Kristo kama Mwokozi wetu na Mkombozi wetu—katika jina la Yesu Kristo, amina.