Kufundisha katika Njia ya Mwokozi
Jukumu linabaki moja kwa moja juu ya kila mmoja wetu kufuata mfano wa Bwana na kufundisha kama Yeye.
Walimu wa Kipekee
Miezi michache iliyopita, mwenzangu tuliyesoma naye kutoka mji wangu wa Overton, Nevada, alipendekeza tuandae zawadi ya Krismasi kwa ajili ya mwalimu wetu mpendwa wa chekechea, ambaye karibuni alikuwa amesherehekea miaka yake 98 ya kuzaliwa. Alitufundisha kuwa wakarimu, umuhimu wa kulala vizuri, furaha ya maziwa na biskuti za graham pamoja na kupendana. Asante, Dada Davis, kwa kuwa mwalimu mzuri hivyo.
Nilikuwa na mwalimu mwingine wa kipekee wakati nikihudhuria Chuo cha Ricks miaka mingi iliyopita. Nilikuwa nikijiandaa kuhudumu misheni na nilidhani ingekuwa ya kupendeza kuhudhuria darasa la maandalizi ya umisionari. Kile nilichopitia kilibadili maisha yangu.
Toka siku ya kwanza ya darasa, nilitambua nilikuwa kwenye uwepo wa mwalimu mkuu. Mwalimu alikuwa Kaka F. Melvin Hammond. Nilijua Kaka Hammond alimpenda Bwana na alinipenda mimi. Ningeweza kuona hilo kwenye uso wake na kusikia hilo katika sauti yake. Alipofundisha, Roho aliangaza akili yangu. Alifundisha mafundisho, lakini pia alinialika nijifunze mwenyewe. Mwaliko huo ulinisaidia kuona wazi jukumu langu la kujifunza mafundisho ya Bwana mimi mwenyewe. Uzoefu huo ulinibadili milele. Asante, Kaka Hammond, kwa kufundisha katika njia ya Mwokozi.
Akina kaka na akina dada, kila mmoja anastahili kuwa na aina hii ya uzoefu wa kujifunza kote nyumbani na kanisani.
Utangulizi wa Njoo, Unifuate unatoa ono la nini mafundisho kama ya Kristo yanaweza kufanikisha. “Dhumuni la kujifunza na kufundisha injili,” inasema, “ni kuongeza uongofu wetu kwa Yesu Kristo na kutusaidia sisi kuwa zaidi kama Yeye. … Aina ya kujifunza injili inayoimarisha imani yetu na kuongoza kwenye muujiza wa uongofu haitokei yote kwa wakati mmoja. Inakwenda zaidi ya darasani mpaka kwenye moyo wa mtu binafsi na nyumbani.”1
Maandiko yanaonyesha kwamba huduma ya Mwokozi katika Amerika ya kale ilikuwa na mafanikio na ilienea kiasi kwamba “watu wote walimgeukia Bwana, nchini kote, wote Wanefi na Walamani, na hakukuweko na mabishano na ugomvi miongoni mwao, na kila mtu alimtendea mwingine haki.”2
Ni jinsi gani mafundisho yetu yanaweza kuwa na matokeo sawa kwa wale tunaowapenda? Ni jinsi gani tunaweza zaidi kufundisha kama Mwokozi na kuwasaidia wengine kuwa waongofu zaidi? Niruhusuni niwape mapendekezo machache.
Mwige Mwokozi
Kwanza na muhimu zaidi, jichukulie juu yako kujifunza yote uwezayo kuhusu Mwalimu Mkuu Mwenyewe. Ni jinsi gani alionyesha upendo kwa wengine? Walihisi vipi wakati Alipofundisha? Je, Alifundisha nini? Matarajio Yake yalikuwa nini kwa wale Aliowafundisha? Baada ya kuchunguza maswali kama haya, tathmini na rekebisha njia yako ya ufundishaji ili iwe zaidi kama Yake.
Kanisa linatoa nyenzo nyingi za kufundishia katika Gospel Library app na kwenye ChurchofJesusChrist.org. Mojawapo ya nyenzo hizo inaitwa Kufundisha katika Njia ya Mwokozi. Ninawaalika msome na mjifunze kila neno lake. Kanuni zake zitakusaidia katika juhudi zako za kuwa zaidi kama Kristo katika kufundisha kwako.
Fungulia Nguvu za Familia
Pendekezo langu linalofuata linaweza kuelezewa kwa uzoefu niliokuwa nao miezi michache iliyopita wakati nilipopita kumtembelea rafiki mpendwa. Niliweza kumsikia mkewe kwa nyuma akizungumza na mtu, hivyo kwa haraka niliaga ili aweze kurejea kwa familia yake.
Saa moja au zaidi baadaye nilipokea ujumbe huu wa arafa kutoka kwa mkewe mpendwa: “Kaka Newman, asante kwa kuja. Tulipaswa kukukaribisha ndani, lakini ninataka kushiriki nawe kile tulichokuwa tunafanya. Tangu mwanzo wa janga la ulimwengu tumekuwa tukijadili Njoo, Unifuate pamoja na watoto wetu wakubwa kila Jumapili kupitia Zoom. Imekuwa kiuhalisia ikileta miujiza. Ninadhani ni mara ya kwanza kwa binti yetu kusoma Kitabu cha Mormoni yeye mwenyewe. Leo ilikuwa somo la mwisho kwenye Kitabu cha Mormoni na tulikuwa mwishoni wakati ulipokuja. … Ninafikiri utavutiwa kusikia jinsi Njoo Unifuate, Zoom na janga la ulimwengu vilivyotoa fursa kwa muda muafaka kubadili moyo. … Inanifanya nijiulize ni miujiza midogo midogo mingapi imekuwa ikitendeka kipindi hiki cha zuio la kukusanyika.”
Hii inasikika kwangu kama utimizwaji wa ahadi Rais Russell M. Nelson aliyoitoa mnamo Oktoba 2018. Alisema kwamba ujifunzaji wa injili unaolenga nyumbani, unaosaidiwa na Kanisa “una uwezo wa kufungulia nguvu za familia, pale kila familia inapofuatilia kwa makini na uangalifu ili kubadilisha nyumba zao kuwa kimbilio la imani. Ninaahidi kwamba unapofanya bidii kupanga upya nyumba yako kuwa kituo cha kujifunza injili, baada ya muda Siku zako za Sabato zitakuwa takatifu sana. Watoto wako watafurahia kujifunza na kuishi mafundisho ya Mwokozi. … Mabadiliko katika familia yako yatakuwa ya ajabu na ya kudumu.”3 Ni ahadi tukufu jinsi gani!
Ili uwe hakika wenye kubadili maisha, uongofu kwa Yesu Kristo lazima uhusishe nafsi yetu yote na upenye kila kipengele cha maisha yetu. Hii ndiyo sababu unapaswa kufokasi kwenye kiini cha maisha yetu—familia zetu na nyumba zetu.
Kumbuka Kwamba Uongofu Ni Suala Binafsi
Pendekezo langu la mwisho ni kukumbuka kwamba uongofu lazima utoke ndani. Kama ilivyoelezwa katika mfano wa wanawali kumi, hatuwezi kumpa mtu mwingine mafuta ya uongofu wetu, kadiri ambavyo tungetamani kufanya hivyo. Kama Mzee David A. Bednar alivyofundisha: “Mafuta haya ya thamani yanapatikana tone moja baada ya jingine … kwa uvumilivu na bila kukoma. Hakuna njia ya mkato; hakuna maandalizi ya mwisho ya ghafla yanaweza kufanywa.”4
Njoo, Unifuate imejikita kwenye ukweli huo. Ninailinganisha na malaika aliyemsaidia Nefi kujifunza kuhusu Yesu Kristo kwa kusema “Tazama!”5 Kama vile malaika huyo, Njoo, Unifuate inatualika kutazama katika maandiko na maneno ya manabii wa siku za leo ili kumpata Mwokozi na Kumsikia Yeye. Kama vile Nefi, tutafunzwa na Roho sisi binafsi wakati tukisoma na kutafakari maneno ya Mungu. Njoo, Unifuate ni ubao imara unaomsaidia kila mmoja wetu kuzama kwa kina kwenye maji ya uzima ya mafundisho ya Kristo.
Jukumu la mzazi linafanana katika njia nyingi. Watoto hurithi mambo mengi kutoka kwa wazazi wao, lakini ushuhuda si moja ya mambo hayo. Hatuwezi kuwapa watoto wetu ushuhuda zaidi kama ambavyo hatuwezi kuilazimisha mbegu ikue. Lakini tunaweza kuweka mazingira ya kustawi, yenye udongo mzuri, yasiyo na miiba ambayo “italisonga neno.” Tunaweza kujitahidi kujenga hali zenye tija ili kwamba watoto wetu—na wengine tunaowapenda—waweze kupata nafasi kwa ajili ya mbegu, “[kusikia] neno, na [kulielewa] neno”6 na kugundua wao wenyewe “kwamba mbegu ni nzuri.”7
Miaka kadhaa iliyopita, mimi na mwanangu Jack tulipata nafasi ya kucheza gofu huko St. Andrews Scotland, ambapo mchezo wa gofu ulianzia. Ilikuwa ya kupendeza! Katika kurejea kwangu nilijaribu kuwaelezea wengine ukubwa wa tukio. Lakini sikuweza. Picha, video na maelezo yangu mazuri havikuwa vya kutosha kabisa. Hatimaye nilitambua kwamba njia pekee ya mtu kujua uzuri wa St. Andrews ni kupata uzoefu wake—kuona njia pana za nyasi fupi, kuvuta hewa, kuhisi upepo kwenye nyuso zao, na kupiga mpira nje mara kadhaa kwenye mchanga na misitu minene, vitu ambavyo tulifanya.
Ndivyo ilivyo kwa neno la Mungu. Tunaweza kulifundisha, tunaweza kulihubiri, tunaweza kulifafanua. Tunaweza kuongea juu ya hilo, tunaweza tukalielezea, tunaweza hata kutoa ushuhuda juu ya hili. Lakini isipokuwa pale tu mtu ahisi neno takatifu la Mungu likitonatona juu ya nafsi yake kama vile umande utokao mbinguni kupitia nguvu ya Roho,8 itakuwa kama vile kutazama kadi au picha za mtu za matembezi. Unapaswa kwenda pale wewe mwenyewe. Uongofu ni safari binafsi—safari ya kukusanyika.
Kila mtu anayefundisha nyumbani na kanisani anaweza kuwapa wengine fursa ya kuwa na uzoefu wao binafsi wa kiroho. Kupitia uzoefu huu, “watajua ukweli wa vitu vyote” wao wenyewe.9 Rais Nelson alifundisha, “Ikiwa unayo maswali ya dhati kuhusu injili au Kanisa, kadiri unavyochagua kuacha Mungu ashinde, utaongozwa kupata na kuelewa ukweli mkamilifu, wa milele ambao utayaongoza maisha yako na kukusaidia kubaki imara kwenye njia ya agano.”10
Kwa kasi Boresha Ufundishaji
Ninawaalika viongozi na walimu katika kila kikundi cha Kanisa kushauriana pamoja na wazazi na vijana ili kwa kasi kuboresha ufundishaji katika kila nyanja—katika vigingi, katika kata na majumbani. Hili litafikiwa kwa kufundisha mafundisho na kualika majadiliano yaliyojawa na Roho kuhusu kweli ambazo Roho Mtakatifu ametufundisha katika nyakati tulivu za kujifunza kwetu binafsi.
Rafiki zangu wapendwa katika Kristo, jukumu linabaki moja kwa moja juu ya kila mmoja wetu kufuata mfano wa Bwana na kufundisha kama Yeye. Njia yake ni njia ya kweli! Tunapomfuata Yeye “wakati atakapoonekana tutakuwa kama yeye, kwani sisi tutamwona vile alivyo; ili tuwe na tumaini hili; ili tutakaswe hata vile alivyo mtakatifu.”11 Katika jina lake Yeye ambaye amefufuka, Mwalimu Mkuu Mwenyewe, Yesu Kristo, amina.