Bariki katika Jina Lake
Kusudi la kupokea kwetu ukuhani ni kuturuhusu sisi kuwabariki watu kwa niaba ya Bwana, tukifanya hivyo katika jina Lake.
Ndugu zangu wapendwa, watumishi katika ukuhani wa Mungu, ni heshima kwangu kuzungumza nanyi usiku wa leo. Ninawahesimu sana na kuwashukuru. Ninapozungumza nanyi na kusikia imani yenu kuu, ni imani yangu kwamba daima kuna ongezeko la nguvu za ukuhani katika ulimwengu, pamoja na akidi imara na wenye ukuhani wengi walio waaminifu.
Katika dakika chache za kuwa nanyi jioni hii, nitazungumza kwa wale miongoni mwenu ambao mnataka kuwa na hata matokeo ya kufaa zaidi katika huduma yenu binafsi ya ukuhani. Mnajua amri ambayo mnayo ya kukuza wito wenu wa kuhudumu.1 Lakini unaweza kujiuliza wito huu unaweza kumaanisha nini kwako.
Nitaanza na mashemasi wapya kwa sababu wao ndiyo wana uwezekano mkubwa wa kuhisi kutokuwa na uhakika kuhusu kile inachomaanisha kukuza huduma yao ya ukuhani. Wazee waliotawazwa hivi karibuni wanaweza pia kutaka kusikiliza. Askofu katika wiki zake za kwanza za huduma anaweza kuvutiwa kusikiliza pia.
Ni muhimu kwangu kutazama nyuma siku zangu kama shemasi. Natamani kwamba mtu angekuwa ameniambia kwa kipindi hicho kile ambacho nitapendekeza sasa. Ingesaidia katika majukumu yote ya ukuhani ambayo nimepatiwa tangu wakati huo—hata yale ambayo ninapokea sasa.
Nilitawazwa kuwa shemasi katika tawi dogo sana kiasi kwamba nilikuwa shemasi pekee na kaka yangu Ted akiwa mwalimu pekee. Sisi tulikuwa familia pekee katika tawi. Tawi lote lilikutana katika nyumba yetu. Kiongozi wa ukuhani kwangu mimi na kaka yangu alikuwa mwongofu mpya ambaye alikuwa punde tu yeye mwenyewe amepokea ukuhani. Niliamini wajibu wangu pekee wa ukuhani ulikuwa tu kupitisha sakramenti sebuleni kwetu.
Wakati familia yetu ilihamia Utah, nilijikuta katika kata kubwa yenye mashemasi wengi. Katika mkutano wangu wa kwanza hapo, niliwaangalia mashemasi—ilionekana kwangu kama jeshi—wakitembea kwa makini walipokuwa wanapitisha sakramenti kama timu iliyofundishwa vyema.
Niliogopa kiasi kwamba Jumapili iliyofuata nilienda mapema katika jengo la kata ili niwe pekee yangu wakati hakuna yeyote ambaye angeniona. Nakumbuka kwamba ilikuwa ni kata ya Yalecrest huko Jijini Salt LaKe, na kata ilikuwa na sanamu kwenye uwa wake. Nilienda nyuma ya sanamu na kuomba kwa dhati msaada wa kutokushindwa ninapoichukuwa nafasi yangu ya kupitisha sakramenti. Ombi hilo lilijibiwa.
Lakini najua sasa kwamba kuna njia bora ya kuomba na kufikiria tunapojaribu kukua katika huduma yetu ya ukuhani. Nimekuja kuelewa kwa nini watu wanapatiwa ukuhani. Kusudi la sisi kupokea ukuhani ni kuturuhusu kuwabariki watu kwa niaba ya Bwana, tukifanya hivyo katika jina Lake.2
Ilipita miaka mingi baada ya kuwa shemasi nilipopata kujifunza maana ya hili kwa vitendo. Kwa mfano, kama kuhani mkuu, nilipewa jukumu la kutembelea mkutano wa sakramenti katika kituo cha kulelea wazee. Niliombwa kupitisha sakramenti. Badala ya kufikiria kuhusu mchakato au umakini wa njia niliyopitisha sakramenti, nilitazama sura za kila kikongwe. Niliona wengi wao wakilia. Mwanamke mmoja alishika mkono wa shati langu, akainua uso wake na kusema kwa sauti, “Ee, Asante, asante.”
Bwana alikuwa amebariki huduma yangu iliyotolewa katika jina Lake. Siku hiyo nilikuwa nimeomba kwa ajili ya muujiza kama huo kuja badala ya jinsi nitakavyofanya vyema sehemu yangu. Niliomba kwamba watu wangehisi upendo wa Bwana kupitia huduma yangu ya upendo. Nimejifunza huu ndio ufunguo wa kuwahudumia na kuwabariki wengine katika jina Lake.
Nimesikia tukio la hivi karibuni ambalo limenikumbusha upendo kama huo. Wakati mikutano yote ya Kanisa ilisitishwa kwa sababu ya kuenea kwa COVID-19, kaka mtumishi alikubali kazi kutoka kwa rais wa akidi ya wazee kubariki na kuhudumia sakramenti kwa dada aliyekuwa anamtumikia. Wakati alipompigia simu ili aombe kumletea sakramenti, alikubali shingo upande, akiona vibaya kumtoa nyumbani katika nyakati hatari na pia kuamini kwamba mambo yangerudi upesi ktika hali yake ya kawaida.
Wakati alipowasili katika nyumba yake Jumapili ile, dada alikuwa na ombi moja. Je, wangeweza kwenda nyumba jirani na pia kuwa na sakramenti na jirani yake wa miaka 87? Kwa idhini ya askofu, alikubali.
Kwa wiki nyingi, nyingi sana, na kwa uangalifu wa kukaa mbali kwa makini sana na vigezo vingine vya usalama, hili kundi dogo la Watakatifu lilikutana kila Jumapili kwa ajili ya mkutano mfupi wa sakramenti. Kwa vipande vichache tu vya mkate na vikombe vya maji—lakini machozi mengi yalidondoka kwa ajili ya uzuri wa upendo wa Mungu.
Baada ya muda, kaka mtumishi, familia yake, na yule dada aliyekuwa akimtumikia waliweza kurudi kanisani. Lakini kwa yule mjane wa miaka 87, ambaye ni jirani, kwa sababu ya tahadhari kubwa, ilibidi abakie nyumbani. Kaka yule mtumishi—kumbuka kuwa kazi yake ilikuwa kwa yule jirani yake na hata siyo kwa huyu dada mkongwe—bado mpaka leo kimya kimya huja nyumbani kwa yule mama kila Jumapili, akiwa na maandiko na kipande kidogo cha mkate mkononi, ili kuhudumia sakramenti ya Chakula cha Bwana.
Huduma yake ya ukuhani, kama yangu katika kituo cha kulelea wazee, hutolewa kwa upendo. Ukweli ni kwamba, kaka mtumishi hivi karibuni alimuuliza askofu wake kama kuna wengine katika kata ambao angeweza kuwaangalia. Hamu yake ya kukuza huduma yake ya ukuhani imeongezeka alipokuwa anatumikia katika jina la Bwana na katika njia inayojulikana Naye pekee. Sijui kama huyu kaka mtumishi alikuwa ameomba, kama nilivyofanya, kwa ajili ya wale aliowatumikia ili kujua mapenzi ya Bwana, lakini kwa sababu huduma yake imekuwa katika jina la Bwana, matokeo yamekuwa ni yale yale.
Matokeo kama hayo ya kushangaza huja wakati ninapoomba kabla ya kutoa baraka ya ukuhani kwa mtu aliye mgonjwa au aliye katika wakati wa shida. Ilitokea siku moja hospitalini wakati madaktari wasio na subira waliponiomba—na zaidi kuniomba—wakiniagiza mimi—kuharakisha na kuwaachia nafasi ya wao kufanya kazi yao, badala ya kunipa fursa ya kutoa baraka ya ukuhani. NIlibakia kwanza, na kutoa baraka. Na huyo msichana niliyembariki siku hiyo, ambaye madaktari walidhani angekufa, aliishi. Nina shukrani wakati huu kwamba katika siku hiyo, sikuruhusu hisia zangu mwenyewe kunizuia lakini nilihisi kwamba Bwana alitaka msichana huyo kupokea baraka. Na nilijua ni baraka gani: nilimbariki aponywe. Na aliponywa.
Imetokea mara nyingi sana nilipokuwa nikimpa mtu aliyeonekana yu karibu kufa, na wanafamilia wamekizunguka kitanda, wakitumaini baraka za uponyaji. Hata ikiwa nina muda kidogo, mara zote huwa ninaomba kujua ni baraka gani Bwana aliyohifadhi ambayo ninaweza kutoa katika jina Lake. Na ninaomba ili kujua jinsi Yeye anavyotaka kumbariki mtu huyo na siyo kile au watu waliosimama karibu wanataka. Uzoefu wangu ni kwamba hata kama baraka siyo ile wengine wanatamani kwa ajili yao wenyewe au wapendwa wao, Roho hugusa mioyo yao ili kupata kuikubali na faraja badala ya kukata tamaa.
Mwongozo huo huo huja kwa mapatriaki wanapofunga na kuomba kwa ajili ya kuongozwa kutoa baraka Bwana aliyonayo kwa ajili ya mtu. Tena, nimesikia baraka zikitolewa ambazo zilinishangaza na kumshanga mtu aliyekuwa anapokea baraka hiyo. Ni wazi, baraka ilitoka kwa Bwana—yote maonyo yaliyo ndani yake pamoja na ahadi zinazotolewa katika jina la Lake. Hatimaye maombi na mfungo wa patriaki vilijibiwa na Bwana.
Kama askofu, nilijifunza nilipokuwa nikifanya usaili wa ustahiki kwa kumuomba Bwana aniwezeshe kujua kile Yeye alichokuwa anataka kwa ajili mtu yule, nikizuia mwongozo wowote Yeye anaotoa usiingiwe na ukungu kwa sababu ya hukumu yangu mwenyewe. Hiyo ni vigumu kama Bwana, kwa upendo, anataka kumbariki mtu kwa kumrudi. Inahitaji juhudi kubwa kubaini kile Bwana anakitaka na kile wewe unakitaka na huyo mtu mwingine anataka.
Ninaamini kwamba tunaweza kukuza huduma yetu ya ukuhani katika maisha yetu yote na labda hata zaidi ya hapo. Itategemea bidii yetu katika kujaribu kujua mapenzi ya Bwana na juhudi zetu za kusikia sauti Yake ili kwamba tuweze kujua vyema zaidi kile Yeye anataka kwa ajili ya mtu yule tunayemtumikia kwa ajili Yake. Ukuaji huo utakuja katika hatua ndogo ndogo. Unaweza kuja pole pole, lakini utakuja. Bwana anaahidi hivi kwetu sisi:
“Kwani yeyote aliye mwaminifu katika kupata kuhani hizi mbili ambazo nimezinena, na kutukuza wito wake, hutakaswa na Roho kwa kufanywa upya miili yao.
“Wanakuwa wana wa Musa na Haruni na uzao wa Ibrahimu, na kanisa na ufalme, na wateule wa Mungu.
“Na pia wale wote waupokeao ukuhani huu wananipokea Mimi, asema Bwana.”3
Ni ushuhuda wangu kwamba funguo za ukuhani zilirejeshwa kwa Nabii Joseph Smith. Watumishi wa Bwana walitokea kutoka mbinguni ili kurejesha ukuhani kwa ajili ya matukio makubwa ambayo yamefunguliwa na ambayo yako mbele yetu. Israeli itakusanywa. Watu wa Bwana wataandaliwa kwa ajili ya Ujio Wake wa Pili ulio mtukufu. Urejesho huu utaendelea. Bwana atafunua mengi ya mapenzi Yake kwa nabii Wake na kwa watumishi Wake.
Mnaweza kuhisi kutofaa ukilinganisha na jambo kubwa ambalo Bwana atalifanya. Kama unahisi hivyo, ninakualika uulize kwa maombi jinsi Bwana anavyokuona wewe. Yeye anakujua wewe binafsi, Yeye ndiye aliyekutunuku ukuhani, na kuinuka kwako na kukuza ukuhani ni jambo muhimu Kwake kwa sababu Yeye anakupenda na Anakuamini kuwa utawabariki watu Anaowapenda katika jina Lake.
Ninakubarikini sasa ili muweze kuhisi upendo Wake na tumaini Lake, katika jina la Bwana Yesu Kristo, amina.