Mkutano Mkuu
Mungu Miongoni Mwetu
Mkutano mkuu wa Aprili 2021


15:44

Mungu Miongoni Mwetu

Mungu yu miongoni mwetu—na binafsi alijihusisha na maisha yetu na kikamilifu anawaongoza watoto Wake.

Kote katika miaka yote, Mungu amezungumza kupitia watumishi Wake, manabii.1 Asubuhi hii tumepata fursa ya kumsikiliza nabii wa Mungu akizungumza na ulimwengu wote. Tunakupenda, Rais Nelson, na ninamhimiza kila mtu popote alipo ajifunze na kufuata maneno yako.

Kabla ya kutimiza miaka yangu 12 ya kuzaliwa, familia yetu alilazimika kutoroka nyumbani kwetu mara mbili na kuanza upya katikati ya vurugu, hofu, na taharuki za vita na mgawanyiko wa kisiasa. Ulikuwa wakati wa wasiwasi kwangu, lakini lazima ilikuwa inatisha sana kwa wazazi wangu wapendwa.

Mama na baba yangu walishiriki kiasi kidogo kuhusu mzigo huu nasi watoto wanne. Walistahimili uchovu na kuteseka kwa uwezo wao wote. Hofu lazima ilikuwa ikiwatesa, ikichukua masaa yao mengi na kufifisha tumaini lao.

Wakati huu wa kuogofya baada ya Vita vya II vya Dunia uliacha athari yake duniani. Uliacha athari yake juu yangu.

Hapo nyuma wakati huo, katika saa zangu za upweke, mara nyingi nilijiuliza, “Kuna tumaini lolote lililobaki ulimwenguni?”

Malaika Miongoni Mwetu

Nilipokuwa nikitafakari swali hii, niliwaza kuhusu wamisionari wetu vijana Wamarekani ambao walitumikia miongoni mwetu miaka hiyo. Walikuwa wameacha usalama wa nyumbani kwao umbali wa nusu ulimwengu na kusafiri hadi Ujerumani—nchi ya maadui zao wa karibu—ili kutoa tumaini tukufu kwa watu wetu. Hawakuja kulaumu, kutoa mhadhara, au kudhalilisha. Wao walitoa maisha yao ya ujana kwa hiari bila kufikiria malipo ya ulimwengu, wakitaka tu kuwasaidia wengine kupata furaha na amani wao waliyokuwa wameipata.

Kwangu mimi, wavulana na wasichana hawa walikuwa wakamilifu. Nina hakika walikuwa na mapungufu yao, lakini si kwangu. Mimi daima nitawafikiria kama walikuwa wakuu kushinda uhai—malaika wa nuru na utukufu, watumishi wa huruma, wema, na ukweli.

Wakati ulimwengu ulikuwa unazama katika ubeuzi, uchungu, chuki, na hofu, mfano na mafundisho ya vijana hawa wadogo yalinijaza kwa tumaini. Ujumbe wa injili waliotoa ulivuka mipaka ya kisiasa, historia, kinyongo, manung’uniko, na njama za kibinafsi. Ulitoa majibu tukufu kwa maswali muhimu tuliyokuwa nayo kipindi cha nyakati hizi ngumu.

Ujumbe ulikuwa kwamba Mungu yu hai na anajali kutuhusu, hata katika nyakati hizi za machafuko, mkanganyiko, na vurugu. Kwamba kwa kweli Yeye alitokea katika wakati wetu kurejesha ukweli na nuru—injili Yake na Kanisa Lake. Kwamba Yeye huzungumza na manabii tena; kwamba Mungu yu miongoni mwetu—na kibinafsi alijihusisha na maisha yetu na kikamilifu anawaongoza watoto Wake.

Inashangaza kile tunachoweza kujifunza tunapotazama kwa makini zaidi mpango wa wokovu na kuinuliwa wa Baba yetu wa Mbinguni, mpango wa furaha, kwa ajili ya watoto Wake. Tunapohisi kutokuwa muhimu, kutelekezwa, na kusahauliwa, tunajifunza kwamba tunaweza kuhakikishiwa kuwa Mungu hajatusahau—ni kweli, kwamba Yeye hutoa kwa watoto Wake wote kitu kisichofikirika: kuwa “warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo.”2

Hii inamaanisha nini?

Kwamba tutaishi milele, tutapokea utimilifu wa shangwe,3 na kuwa na uwezo wa “kurithi enzi, falme, himaya na nguvu.”4

Inanyenyekeza kujua kwamba kudra hii kuu na ya kiungu inawezakana—si kwa sababu ya vile tulivyo bali kwa sababu ya vile Mungu alivyo.

Tukijua hili, tunawezaje daima kunung’unika, au kubakia na machungu? Je, tunawezaje daima kutizama chini wakati Mfalme wa wafalme anatualika tupae kwenda katika kudra isiyofikirika ya furaha ya kiungu?5

Wokovu Miongoni Mwetu

Kwa sababu ya upendo mkamilifu wa Mungu kwa ajili yetu na dhabihu ya milele ya Yesu Kristo, dhambi zetu—zote kubwa na ndogo—zinaweza kufutwa na zisikumbukwe tena.6 Tunaweza kusimama mbele Zake wasafi, wenye kustahili, na waliotakaswa.

Moyo wangu unafurika kwa shukrani kwa ajili ya Baba yangu wa Mbinguni. Ninafahamu kwamba Yeye hawezi kuwaacha watoto Wake wayumbeyumbe maishani bila tumaini la kudra angavu na ya milele. Yeye ametoa maelekezo ambayo hufunua njia ya kurudi Kwake. Na kitovu cha haya yote ni Mwanawe Mpendwa, Yesu Kristo,7 na dhabihu Yake kwa ajili yetu.

Upatanisho wa Mwokozi usio na mwisho hubadilisha kabisa jinsi tunavyoweza kuona uvunjaji wetu wa sheria na mapungufu yetu. Badala ya kuyazingatia na kuhisi kutoweza kukombolewa au kukosa tumaini, tunaweza kujifunza kutoka kwayo na kuhisi kuwa na tumaini.8 Zawadi ya utakasaji ya toba huturuhusu kuziacha dhambi zetu nyuma na kuibuka kama kiumbe kipya.9

Kwa sababu ya Yesu Kristo, makosa yetu hayapaswi kututambulisha. Yanaweza kutusafisha.

Kama vile mwanamuziki anayefanya mazoezi ya sauti, tunaweza kuona makosa yetu, mapungufu, na dhambi kama fursa kubwa za kujitambua, upendo wa kina na wa dhati kwa wengine, na kusafishwa kupitia toba.

Kama tutatubu, makosa hayatufanyi tusistahili. Ni sehemu ya maendeleo yetu.

Sisi wote tu watoto wachanga ukilinganisha na viumbe wa utukufu na ukuu ambao tumesanifiwa kuwa. Hakuna binadamu anayekua kutoka kutambaa hadi kutembea hata kukimbia pasipo kujikwaa kila mara, nundu, na michubuko. Hivyo ndivyo tunavyojifunza.

Kama tunafanya mazoezi kwa bidii, daima tukijitahidi kutii amri za Mungu, na kuweka juhudi zetu kwenye kutubu, kuvumilia, na kutumia kile ambacho tumejifunza, mstari juu ya mstari, tutakusanya nuru katika nafsi zetu.10 Na ingawa hatuwezi kuelewa kabisa uwezekano wetu kamili sasa, “Sisi tunajua kwamba wakati [Mwokozi] atakapoonekana,” tutaona uso Wake ndani yetu, na “tutamwona hata vile alivyo.”11

Ni ahadi tukufu jinsi gani!

Ndiyo, ulimwengu uko katika machafuko. Na ndiyo, tuna madhaifu. Lakini hatupaswi kuinamisha vichwa vyetu kwa kukata tamaa, kwa sababu tunaweza kumtumaini Mungu, tunaweza kumtumaini Mwanawe, Yesu Kristo, na tunaweza kuikubali zawadi ya Roho kutuongoza kwenye njia hii ielekeayo kwenye maisha yaliyojaa shangwe na furaha ya kiungu.12

Yesu miongoni Mwetu

Kila mara nimejiuliza, Kile ambacho Yesu angefundisha na kufanya kama Yeye angekuwa miongoni mwetu leo?

Baada ya Ufufuo, Yesu Kristo alitimiza ahadi Yake ya kutembelea “kondoo wengine.”13

Kitabu cha Mormoni: Ushuhuda Mwingine wa Yesu Kristo huzungumza juu ya kutokea kwake kwa watu wa bara la Amerika. Tuna kumbukumbu hii ya thamani kama ushahidi halisi wa kazi ya Mwokozi.

Watu wa Kitabu cha Mormoni waliishi upande mwingine wa dunia—historia yao, tamaduni, na mazingira ya kisiasa yalikuwa tofauti sana na ya watu Yesu aliowafundisha wakati wa huduma Yake duniani. Na bado Yeye aliwafunza mambo mengi sawa na yale aliyofunza katika Nchi Takatifu.

Kwa nini angefanya hivyo?

Mwokozi daima hufunza kweli za milele. Zinatumika kwa watu wa kila kizazi na katika mazingira yoyote.

Ujumbe wake ulikuwa na ni ujumbe wa tumaini na wa kustahili kuwa—ushuhuda kwamba Mungu Baba yetu wa Mbinguni hajawatelekeza watoto Wake.

Kwamba Mungu yu Miongoni Mwetu!

Miaka mia mbili iliyopita, Mwokozi alirudi tena duniani. Pamoja na Mungu Baba, Yeye alimtokea Joseph Smith wa umri wa miaka 14 na kuanzisha Urejesho wa injili na Kanisa la Yesu Kristo. Kutoka siku ile na kuendelea, mbingu zilifunguka, na wajumbe wa mbinguni waliteremka kutoka kumbi za utukufu wa milele. Nuru na elimu vilimiminwa kutoka kiti cha enzi cha selestia.

Bwana Yesu Kristo alizungumza kwa mara nyingine tena na ulimwengu.

Alisema nini?

Kwa baraka zetu, mengi ya maneno Yake yameandikwa katika Mafundisho na Maagano—yanayopatikana kwa kila mmoja ulimwenguni ambaye anataka kuyasoma na kujifunza. Ni ya thamani jinsi gani maneno haya kwetu leo!

Na hatupaswi kushangaa kupata kwamba Mwokozi hufunza tena ujumbe muhimu wa injili Yake: “Nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa uwezo wako wote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote; na katika jina la Yesu Kristo utamtumikia yeye.”14 Yeye hutuongoza kumtafuta Mungu15 na kuishi mafundisho Yeye aliyofunua kwa watumishi Wake, manabii.16

Yeye hutufunza kupendana17 na kuwa “tujae hisani kwa wanadamu wote.”17

Yeye anatualika tuwe mikono Yake, tuenende katika kutenda kazi njema.19 “Tusipende kwa neno … bali kwa tendo na kweli.”20

Anatupatia changamoto ya kutii agizo Lake kuu: kupenda, kushiriki, na kuwaalika wote kwenye injili Yake na Kanisa Lake.21

Yeye hutuamuru tujenge mahekalu matakatifu na kuingia ndani na kutumikia humo.22

Anatufundisha tuwe wafuasi Wake—kwamba mioyo yetu haipaswi kupendelea nguvu binafsi, utajiri, sifa, au madaraka. Yeye hutufunza “tuyaweke kando mambo ya ulimwengu huu, na kuyatafuta mambo ya ulimwengu ulio bora.”23

Yeye anatuhimiza tutafute shangwe, kuelimika, amani, ukweli furaha,24 na ahadi ya kutokufa na uzima wa milele.25

Acha tuchukue hii hatua moja zaidi. Tuseme Yesu angekuja kwenye kata yako, tawi lako, au nyumbani kwako leo. Ingekuwaje?

Yeye angeweza kuona ndani ya moyo wako hasa. Muonekano wa nje ungepoteza umuhimu wake. Yeye angekujua vile ulivyo. Yeye angejua matamanio ya moyo wako.

Wapole na wanyenyekevu Yeye angewainua.

Wagonjwa Yeye angewaponya.

Wenye shaka Yeye angewatia imani na ujasiri wa kuamini.

Yeye angetufunza kufungua mioyo yetu kwa Mungu na kuwafikia wengine.

Yeye angetambua na kutukuza unyofu, unyenyekevu, ukamilifu, uaminifu, huruma, na hisani.

Kumtazama mara moja katika macho Yake na kamwe hatungekuwa vile tulivyo. Tungebadilika milele. Tukigeuzwa kwa utambuzi wa kina kwamba, hakika, Mungu yu miongoni mwetu.

Tunapaswa Kufanya Nini?26

Natazama nyuma kwa ukarimu yule mvulana niliyekuwa wakati wa miaka ya kukua kwangu. Kama ningeweza kurudi nyuma tena, ningemfariji na kumwambia akae katika njia sahihi na kuendelea kutafuta. Na ningemuomba amwalike Yesu Kristo katika maisha yake, kwani Mungu yu miongoni mwetu!

Kwenu ninyi, akina kaka na akina dada, marafiki zangu wapendwa, na kwa wale wote wanaotafuta majibu, ukweli, na furaha, ninawapa ushauri huo huo: endeleeni kutafuta kwa imani na subira.27

Ombeni, nanyi mtapewa. Bisheni nanyi mtafunguliwa.28 Mtumaini Bwana.29

Katika maisha yetu ya kila siku ni kazi yetu kubwa na fursa yenye baraka kukutana na Mungu.

Tunapoweka kando kiburi na kusogelea kiti Chake cha enzi kwa moyo uliovunjika na roho iliyopondeka,30 Yeye atasongea karibu nasi.31

Tunapotafuta kumfuata Yesu Kristo na kutembea njia ya ufuasi, mstari juu ya mstari, siku itafika ambapo tutafurahia ile zawadi isiyofikirika ya kupokea utimilifu wa furaha.

Marafiki zangu wapendwa, Baba yenu wa Mbinguni anawapenda kwa upendo mkamilifu. Yeye amethibitisha upendo Wake katika njia zisizo na mwisho, lakini juu ya yote kwa kumtoa Mwanawe wa Pekee kama dhabihu na kama zawadi kwa watoto Wake ili kufanya kurudi kwa wazazi wetu wa mbinguni kuwe halisi.

Ninatoa ushahidi kwamba Baba yetu wa Mbinguni yu hai, kwamba Yesu Kristo huongoza Kanisa Lake, kwamba Rais Russell M. Nelson ni nabii Wake.

Ninatoa kwenu upendo wangu na baraka katika msimu huu wa Pasaka ya furaha. Fungueni mioyo yenu kwa Mwokozi na Mkombozi wetu, bila kujali hali zenu, majaribu, mateso, au makosa; mnaweza kujua kwamba Yeye yu hai, kwamba Yeye anawapenda, na kwamba kwa sababu Yake, ninyi kamwe hamtakuwa wapweke.

Mungu yu Miongoni Mwetu.

Juu ya hili ninashuhudia na kutoa ushahidi wangu katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.