Mkutano Mkuu
Mwokozi Wetu Binafsi
Mkutano mkuu wa Aprili 2021


Mwokozi Wetu Binafsi

Kwa sababu ya dhabihu Yake ya upatanisho, Mwokozi ana nguvu ya kusafisha, kuponya, na kutuimarisha mmoja mmoja.

Ninashukuru kuwa nanyi asubuhi hii ya kupendeza ya Pasaka. Wakati ninapofikiria kuhusu Pasaka, napenda kurudia katika akili yangu maneno yaliyosemwa na malaika kwa wale waliokuwa kwenye Kaburi la Bustanini: “Kwa nini mnamtafuta aliye hai katika wafu? Hayupo hapa, amefufuka.”1 Ninashuhudia kwamba Yesu wa Nazareti alifufuka na yu hai.

Mnafikiri Nini juu ya Kristo?

Miaka thelathini na minne iliyopita, mimi na mmisionari mwenza tulikutana na kumfundisha msomi aliyekuwa mwandishi mchangiaji katika gazeti la eneo lile huko Jiji la Davao, Ufilipino. Tulifurahia kumfundisha kwa sababu alikuwa na maswali mengi na alikuwa mwenye kuheshimu sana imani zetu. Swali la kukumbukwa zaidi alilotuuliza lilikuwa “mnafikiri nini juu ya Kristo?”2 Sisi kwa msisimko tulishiriki hisia zetu na kutoa ushuhuda wa Yesu Kristo. Baadaye alichapisha makala juu ya mada ileile ambayo ilikuwa na maneno na virai vya kupendeza kuhusu Mwokozi. Nakumbuka kuvutiwa lakini pengine si kuinuliwa. Ilikuwa na taarifa nzuri lakini haikuwa na maana na ilikosa nguvu za kiroho.

Kupata Kumjua Zaidi

“Mnafikiri nini juu ya Kristo?” Ninatambua kwamba jinsi ninavyomjua Mwokozi kwa undani kwa kipekee kunashawishi uwezo wangu wa kumsikia Yeye vile vile jinsi ninavyomfuata. Miaka michache iliyopita, Mzee David A. Bednar aliuliza maswali yafuatayo kama sehemu ya mazungumzo yake: “Je tunajua tu kuhusu Mwokozi, au tunatafuta kumjua Yeye zaidi? Je, tunatafutaje kumjua Bwana?”3

Nilipojifunza na kutafakari, nilifikia kwenye utambuzi makini kwamba kile ninachokijua kuhusu Mwokozi kilizidi kwa kiasi kikubwa jinsi ninavyomjua hasa. Kisha niliazimia kuweka juhudu zaidi kwenye kumjua Yeye. Nina shukrani sana kwa maandiko na shuhuda za wafuasi wanaume na wanawake wa Kanisa letu. Safari yangu mwenyewe kwa miaka michache iliyopita imenipeleka kwenye mada nyingi za kujifunza na ugunduzi. Ninaomba kwamba Roho Mtakatifu atafikisha kwako leo ujumbe mkubwa zaidi kuliko maneno yasiyotosha ambayo nimeyaandika.

Kwanza, tunahitaji kutambua kwamba kumjua Mwokozi ni lengo muhimu mno la maisha yetu. Linapaswa kuchukua kipaumbele juu ya kitu kingini chochote.

“Na uzima wa milele ndio huu, kwamba wakujue wewe Mungu wa pekee wa kweli na Yesu Kristo uliyemtuma.”4

“Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima: mtu haji kwa Baba,ila kwa njia ya mimi.”5

“Mimi ndimi nuru ya ulimwengu: yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.”6

Pili, tunapozidi kumjua Mwokozi, mafungu ya maandiko na maneno ya manabii yanakuwa ya ndani na yenye maana kwetu kiasi kwamba yanakuwa maneno yetu wenyewe. Hii sio kuhusu kunakili maneno, hisia, na uzoefu wa wengine kadiri ilivyo kujua kwa ajili yetu wenyewe, katika njia yetu wenyewe ya kipekee, kwa kufanyia majaribio juu ya neno7 na kupokea ushahidi kutoka kwa Roho Mtakatifu. Kama nabii Alma alivyotangaza:

“Hamfikirii kwamba mimi mwenyewe najua vitu hivi? Tazama, nawashuhudia kwamba mimi najua kuwa vitu hivi ambavyo nimezungumza ni vya kweli. Na mnadhani kwamba ninajuaje ukweli wake?

“Tazama, ninawaambia kwamba yamesababishwa kujulikana kwangu na Roho Mtakatifu wa Mungu. Tazama, nimefunga na kusali siku nyingi ili nivijue vitu hivi mimi mwenyewe. Na sasa ninavijua mwenyewe kuwa ni vya kweli; kwani Bwana Mungu amevidhihirisha kwangu kwa Roho wake Mtakatifu; na hii ni roho ya ufunuo ambayo iko ndani yangu.”8

Tatu, Uelewa zaidi kwamba Upatanisho wa Yesu Kristo unahusika kwetu binafsi na kwa mtu mmoja mmoja utatusaidia kumjua Yeye. Mara nyingi ni rahisi zaidi kwa sisi kufikiri na kuzungumzia juu ya Upatanisho wa Kristo kwa maneno ya kawaida kuliko kutambua umuhimu wake binafsi katika maisha yetu. Upatanisho wa Yesu Kristo ni usio na kikomo na wa milele na yote yaliyozunguka katika upana na kina chake si kingine bali matokeo ya wote mtu binafsi na mmoja mmoja. Kwa sababu ya dhabihu Yake ya upatanisho, Mwokozi ana nguvu ya kusafisha, kuponya, na kutuimarisha mmoja mmoja.

Hamu pekee ya Mwokozi, kusudi lake pekee, toka mwanzo kabisa, lilikuwa kufanya mapenzi ya Baba. Mapenzi ya baba yalikuwa kwa yeye kusaidia katika “[kuleta] kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu”9 kwa kuwa “mwombezi wetu kwa Baba.”10 Hivyo,“ ingawa alikuwa Mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata; naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii.”11

“Na atakwenda, na kuteseka maumivu na masumbuko na majaribio ya kila aina. …

“Na atajichukulia kifo, ili afungue kamba za kifo … na atajichukulia unyonge wao, ili moyo wake ujae rehema, … ili ajue kulingana na mwili jinsi ya kuwasaidia watu wake kulingana na unyonge wao.

“… Mwana wa Mungu anateseka katika mwili ili achukue dhambi za watu wake, kwamba aondoe uvunjaji wao wa sheria kulingana na nguvu za ukombozi wake.”12

Ningependa kushiriki uzoefu wa kawaida ambao unaeleza kwa mifano mapambamo ambayo wakati mwingine tunapaitia ili kukumbatia asili binafsi ya Upatanisho wa Bwana.

Miaka kadhaa iliyopita, kwa mwaliko wa kiongozi wangu msimamizi, Nilisoma Kitabu cha Mormoni ukurasa hadi ukurasa na niliwekea alama mistari ambayo ilirejelea Upatanisho wa Bwana. Kiongozi wangu pia alinialika kutayarisha muhtasari wa ukurasa mmoja wa kile nilichojifunza. Nilijisemea mwenyewe, “Ukurasa mmoja? Hakika, hiyo ni rahisi.” Kwa mshangao wangu, hata hivyo, Niliona kazi kuwa ngumu kweli kweli na nilishindwa.

Nilielewa tangu wakati ule kwamba Nilishindwa kwa sababu nilikosa lengo na nilikuwa na matazamio yasiyo sahihi. Kwanza, nilitegemea muhtasari kuwa wa kuvutia kwa kila mtu. Muhtasari ulikuwa kwa ajili yangu na sio kwa ajili ya mwingine yeyote. Ulikusudiwa kuteka hisia zangu na mihemko kuhusu Mwokozi na kile Alichofanya kwa ajilli yangu ili kwamba kila wakati ninapousoma, utaleta uzoefu wa kiroho wa kupendeza, wenye kugusa na uzoefu binafsi.

Pili, Nilitegemea muhtasari kuwa mkubwa na uliochanganuliwa na wenye maneno na virai vikubwa. Ulikuwa kamwe si kuhusu maneno makubwa. Ulikusudiwa kuwa tangazo la wazi na la kawaida la kusadikisha. “Kwani nafsi yangu inafurahia unyoofu; kwani kwa namna hii ndivyo Bwana Mungu anavyotenda kazi miongoni mwa wanadamu. Kwani Bwana Mungu hutoa nuru kwa ufahamu.”13

Tatu, nilitegemea uwe mkamilifu, muhtasari wa kufunga mihutasari yote—muhtasari wa mwisho ambao mtu hawezi na hapaswi kuongeza juu yake— badala ya kazi inayoendelea ambayo ninaweza kuongeza neno hapa au kirai pale kadiri uelewa wangu wa Upatanisho wa Yesu Kristo unavyoongezeka.

Ushuhuda na Mwaliko

Kama mvulana, nilijifunza sana kutokana na mazungumzo yangu na askofu wangu. Wakati wa miaka hiyo ya utoto, Nilijifunza kupenda maneno haya kutoka kwenye wimbo wa Kanisa nilioupenda:

Nashangaa sana ninavyopendwa na Yesu,

Nashangazwa na neema ambazo ananipa.

Natetemeka kujua kwamba kwa ajili yangu alisulubuwa,

Kwamba kwa ajili yangu, mwenye dhambi, aliteseka, alitokwa damu na kufa.

Ee, ni ya kupendeza kwamba alinijali

Vya kutosha kufa kwa ajili yangu!

Ee, ni ya kupendeza, ya kupendeza kwangu!14

Nabii Moroni alitualika: “Na sasa, nimekupendekeza kumtafuta huyu Yesu ambaye manabii na mitume wameandika kumhusu.”15

Rais Russell M. Nelson aliahidi kwamba “Ikiwa [sisi] tutaendelea kujifunza yote tunayoweza kuhusu Yesu Kristo, … uwezo [wetu] wa kuepuka dhambi utaongezeka. Hamu [yetu] ya kutii amri itaongezeka.”16

Kwenye Jumapili hii ya Pasaka, kama vile Mwokozi alivyotoka kwenye kaburi Lake, sisi na tuamke kutoka kwenye usingizi wetu wa kiroho na kuinuka juu ya mawingu ya mashaka, mafumbato ya woga, sumu ya kiburi na ukimya wa kuridhika. Yesu Kristo na Baba wa Mbinguni wako hai. Ninashuhudia juu ya upendo Wao mkamilifu kwetu. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.

Chapisha