Mkutano Mkuu
Nuru Huambatana na Nuru
Mkutano mkuu wa Aprili 2021


Nuru Huambatana na Nuru

Tunapoongeza imani yetu katika Kristo, tunapokea nuru katika kipimo kinachoongezeka hadi inalifukuza giza lote.

Wapendwa kaka na dada zangu, ninashangilia pamoja nanyi katika Jumapili hii iliyobarikiwa ya Pasaka katika kutafakari nuru tukufu iliyopambazuka duniani kwa Ufufuko wa Bwana na Mwokozi wetu, Yesu Kristo.

Wakati wa huduma Yake duniani, Yesu alitamka: “Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.”1 Roho ya Kristo “iko ndani ya vitu vyote, [na] hutoa uhai kwa vitu vyote.”2 Huishinda giza ambalo vinginevyo lingetuzunguka sisi.

Miaka kadhaa iliyopita, katika kutafuta matukio yasiyo ya kawaida, wanangu wawili na mimi tuliambatana na kikundi cha wavulana kwenda huko Moaning Cavern, paliitwa hivyo kwa sababu ya sauti ambayo wakati mmoja ilitoa mwangwi kinywani mwake. Hili ni pango lenye kina cha futi 180, llilonyooka kwenda chini, pango moja kubwa huko California.

Picha
Moaning Cavern

Kuna njia mbili tu za kwenda chini: ngazi salama za mzunguko au kushuka kwa kamba kwenye sakafu ya pango; mimi pamoja na vijana wangu tulichagua kushuka kwa kamba. Mwanangu mkubwa alitangulia kwanza wakati mimi na mwangu mdogo kabisa kwa makusudi tulikuwa wa mwisho ili tushuke pamoja.

Baada ya waongozaji wetu kutuelekeza na kutufunga kwenye kamba imara, tulirudi nyuma hadi tulipokuwa tumesimama kwenye kingo nyembamba na tukakusanya ujasiri wetu, kwani hapa palikuwa mahali pa mwisho pa kugeukia, na mahali pa mwisho kuweza kuona mwanga wowote wa jua kutoka kwenye kinywa cha pango hilo.

Hatua yetu iliyofuata kurudi nyuma ilitutupa ndani ya pango kuu refu mfano wa kanisa kuu na pana kiasi kwamba lingeweza kumeza Sanamu nzima ya Liberty Huko tulisokotwa katika kubiringika taratibu wakati macho yetu yakijirekebisha kuona kwenye kiza. Tulipoendelea kushuka, mng’aro wa mwanga wa umeme uliangaza ukuta wa kushangaza wa chokaa.

Pasipo kutoa tahadhari, mwangaza ghafla ukatoweka kabisa. Tukining’inia juu ya kilindi, tulikuwa tumemezwa katika giza zito sana kiasi kwamba hatukuweza kuona mikono yetu juu ya kamba iliyokuwa mbele yetu. Sauti mara moja ikaita, ”Baba, upo?”

“Niko hapa, Mwanangu, niko hapa,” nilijibu.

Upotevu usiotegemewa wa mwangaza ulipangwa kuonyesha kwamba pasipo umeme, giza la lile pango lilikuwa halipenyeki. Giza lilishinda; sisi “tulilihisi” giza. Mwangaza uliporudi, giza mara moja likashindwa, kama vile tu giza lazima daima lishindwe hata kwa mwangaza ulio dhaifu kabisa. Mimi na wanangu tumeachwa na kumbukumbu ya giza ambalo hatujawahi kulijua, na shukrani kubwa kwa ajili ya mwangaza ambao kamwe hatuwezi kuusahau na hakikisho kwamba katu hatuko gizani pekee yetu kabisa

Kushuka kwetu pangoni kwa namna fulani kunafanana na safari yetu duniani. Tuliondoka kutoka kwenye nuru tukufu ya mbinguni na kushuka kuvuka pazia la usahaulifu hadi ulimwengu uliotiwa giza. Baba yetu wa Mbinguni hakutuacha gizani bali alituahidi mwangaza kwa ajili ya safari yetu kupitia Mwanawe Mpendwa, Yesu Kristo.

Tunajua kwamba mwangaza wa jua ni wa lazima kwa wenye uhai wote duniani. Vivyo hivyo mwangaza utokao kwa Mwokozi ni wa muhimu kwa maisha yetu ya kiroho. Katika upendo wake mkamilifu, Mungu hutoa Nuru ya Kristo kwa kila mtu “ajaye ulimwenguni”3 ili wapate “kujua mema na mabaya”4 na washawishike “kutenda mema daima.”5 Nuru hiyo, inajifunua yenyewe kupitia kile daima tukiitacho dhamiri yetu, ikituashiria sisi daima kutenda na kuwa bora, na bora zaidi.

Tunapoongeza imani yetu katika Kristo, tunapokea nuru katika kipimo kinachoongezeka hadi inalifukuza giza lote linalowezekana kukusanyika kutuzunguka sisi. “Kile kilicho cha Mungu ni nuru; na yule ambaye huipokea nuru, na kukaa ndani ya Mungu, hupokea nuru zaidi; na nuru hiyo huzidi kungʼara hata mchana mkamilifu.”6

Nuru ya Kristo inatuandaa sisi kupokea ushawishi wa Roho Mtakatifu, ambayo ni “nguvu ya Mungu ya ushawishi … juu ya ukweli wa Injili.”7 Mshirika wa tatu wa Uungu, Roho Mtakatifu ni “mtu wa kiroho.”8 Chanzo kikuu cha nuru ambayo Baba wa Mbinguni anatoa kwako wewe katika maisha haya huja kutoka kwa kupitia Roho Mtakatifu, ambaye ushawishi wake “utaiangaza akili yako [na] kuijaza nafsi yako kwa shangwe.”9

Katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, kupitia mamlaka ya ukuhani yaliyorejeshwa, wewe unabatizwa kwa kuzamishwa kwa ajili ya ondoleo la dhambi. Kisha, mikono inawekwa juu ya kichwa chako na hiki “kipawa cha ajabu, kisichosemeka”10 cha Roho Mtakatifu kinatolewa kwako.

Baada ya hapo, matamanio na matendo yako yanapokuwa katika njia ya agano, Roho Mtakatifu, kama nuru iliyo ndani yako, atafunua na kushuhudia juu ya ukweli,11 kuonya juu ya hatari, kufariji12 na kukusafisha,13 na kutoa amani14 katika nafsi yako.

Kwa sababu “nuru huambatana na nuru,”15 wenza wa kudumu wa Roho Mtakatifu utakuongoza katika kuchagua kile kitakacho kuweka wewe katika nuru; kinyume chake, chaguzi zilizofanywa pasipo kuwa na ushawishi wa Roho Mtakatifu zitaelekea kukuongoza kwenye vivuli na gizani. Kama Mzee Robert D. Hales alivyofundisha: “Wakati nuru inapokuwepo, giza linatiishwa na lazima liondoke. … Wakati nuru ya kiroho ya Roho Mtakatifu inapokuwepo, giza la Shetani hutoweka.”16

Naomba nipendekeze kwamba, pengine, huu ni wakati wa kujiuliza mwenyewe: Je, ninayo hiyo nuru katika maisha yangu? Kama hapana, ni lini mara ya mwisho nilikuwa nayo?

Kama vile tu mwanga wa jua unavyoiangaza dunia kila siku ili kufanya upya na kusaidia uhai, nawe unaweza kila siku kuangaza nuru iliyo ndani yako unapochagua kumfuata Yeye—Yesu Kristo.

Tone la mwangaza wa jua linaongezwa kila wakati unapomtafuta Mungu katika sala; kujifunza maandiko ili “kumsikiliza Yeye”;17 kufanyia kazi mwongozo na ufunuo kutoka kwa manabii wetu walio hai; na kutii na kushika amri ili “tutembee katika ibada zote za Bwana.”18

Utaualika mwangaza wa jua wa kiroho nafsini mwako na amani katika maisha yako kila wakati unapotubu. Unapopokea sakramenti kila wiki ili kujichukulia juu yako jina la Mwokozi, ili daima umkumbuke Yeye na kushika amri Zake, nuru yake itaangaza ndani yako.

Kuna mwangaza wa jua nafsi mwako kila wakati unaposhiriki injili na kutoa ushuhuda wako. Kila wakati mnapotumikiana kama Mwokozi alivyofanya, mtahisi mwako wake katika mioyo yenu. Nuru ya Baba wa Mbinguni daima hukaa ndani ya hekalu Lake takatifu na juu ya wale wote wanaojipeleka wenyewe katika nyumba ya Bwana. Nuru yake iliyo ndani yako inaongezeka kwa matendo yako ya ukarimu, uvumilivu, msamaha, hisani na inajionyesha yenyewe katika uso wako wa furaha. Kwa upande mwingine, tunatembea vivulini tunapokuwa na haraka sana ya kukasirika au wagumu sana kusamehe. “Unapoiweka sura yako kuelekea kwenye mwangaza wa jua, vivuli haviwezi kuvumilia bali kurudi nyuma.”19

Unapoishi ili kuwa mwenye kustahili wenzi wa Roho Mtakatifu, hakika wewe “unaongeza uweza wako wa kiroho wa kupokea ufunuo.”20

Maisha huleta changamoto na kukatishwa tamaa, na sisi sote lazima tukabiliane na siku za giza na dhoruba. Kupitia hayo yote, kama “tutaacha Mungu ashinde katika maisha yetu,”21 nuru ya Roho Mtakatifu itatufunulia kwamba kuna kusudi na maana katika majaribu yetu, na kwamba majaribu haya hatimaye yatatubadilisha na kuwa bora zaidi, watu waliokamilika zaidi wenye imani imara na matumaini angavu katika Kristo, tukijua kwamba Mungu alikuwa pamoja nasi katika siku zetu za giza. Kama Rais Nelson alivyoshauri, “Giza linaloongezeka ambalo linaambatana na ongezeko la taabu linaifanya nuru ya Yesu Kristo iangaze zaidi na zaidi.”22

Majira ya maisha yetu yanaweza kutupeleka sehemu tusiyotegemea na tusiyoipenda. Kama dhambi ndiyo imekufikisha huko, kunja pazia la giza na anza sasa kwa unyenyekevu kumwendea Baba yako wa Mbinguni kwa moyo uliovunjika na roho iliyopondeka na utubu. Yeye atasikia sala yako ya dhati. Kwa ujasiri leo, “ukijongea karibu [Naye] na [Yeye] atajongea karibu na wewe.”23 Haujapita kamwe uwezo wa kuponya wa Upatanisho wa Yesu Kristo.

Ninatoka kwa wazazi wema na kwa mababu waaminifu ambao walijibu nuru ya Yesu Kristo na injili Yake, na ikabariki maisha yao na vizazi ambavyo vilifuata kwa uimara wa kiroho. Baba yangu mara kwa mara alizungumza kuhusu baba yake, Milo T Dyches, na kusimulia jinsi imani kwa Mungu ilivyokuwa nuru kwake mchana na usiku. Babu alikuwa mlinzi wa msitu na mara kwa mara aliendesha farasi peke yake milimani, akiaminisha maisha yake pasipo kuwa na swali kwenye maelekezo ya na utunzaji wa Mungu.

Siku moja ya majira ya miti kupukutisha majani, babu alikuwa peke yake kwenye milima mirefu. Majira ya baridi tayari yalikuwa yamekwisha onyesha uso wake wakati alipomwandaa mmoja kati ya farasi wake awapendao, Old Prince, na kupanda kwenda kwenye kiwanda cha kupasulia mbao ili kupima magogo kabla hayajapasuliwa kuwa mbao.

Jioni ilipofika, alimaliza kazi yake na akapanda juu ya farasi wake. Wakati huo, hali ya joto ilikuwa imeshuka, na dhoruba ya theluji ilikuwa ikifunika mlima. Pasipo mwanga au njia ya kumwongoza, alimgeuza Prince kuelekea uelekeo aliodhani ungewaongoza kurudi kwenye kambi ya walinzi wa msitu.

Picha
Milo Dyches akisafiri kwenye dhoruba

Baada ya kusafiri maili kadhaa gizani, Prince alipunguza mwendo, kisha akasimama. Babu alirudia rudia kumhimiza Prince kusonga mbele, lakini farasi alikataa. Theluji iliendelea kujaa kuwazunguka, ndipo babu alipotambua kwamba alihitaji msaada wa Mungu. Kama alivyokuwa amefanya katika maisha yake yote, kwa unyenyekeu “[aliomba] kwa imani, pasipo shaka yo yote.”24 Sauti ndogo, tulivu ikajibu, “Milo, mpe Prince kichwa chake.” Babu akatii, na alipolegeza mikono yake katika kushikilia hatamu, Prince alijigeuza na kwa kishindo aliongoza uelekeo mwingine. Baada ya masaa kadhaa baadae, Prince alisimama tena na kushusha chini kichwa chake. Babu aliona kwamba kwa usalama kabisa wamefika lango la kituo cha walinzi wa msitu.

Na kwa jua la asubuhi, Babu aliweza kufuatilia alama za miguu ya Prince kwenye theluji. Alivuta pumzi ndefu alipokuwa amepata mahali alipompa Prince kichwa chake: palikuwa ukingoni kabisa mwa mteremko wa ghafla wa mlima mrefu sana, mahali ambapo hatua moja tu mbele ingeweza kuwatosa wote farasi na babu kwenye mauti yao katika majabali ya mawe yaliyokuwa chini.

Kutokana na tukio hilo na mengine mengi, Babu alishauri, “mwenza bora na mkubwa ambaye unaweza kuwa naye ni Baba yako wa Mbinguni.” Wakati baba yangu angesimulia hadithi hii ya Babu, ninakumbuka kwamba yeye angenukuu kutoka katika maandiko:

“Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe.

Katika njia zako zote mkiri Yeye, naye ataongoza mapito yako.”25

Picha
Mwokozi akiwa ameshikilia taa

Ninashuhudia kwambaYesu Kristo ni nuru isiyo na mwisho ambayo “huangaza gizani.”26 Hakuna giza ambalo linaweza kuififisha, kuizima, kuishinda nguvu, au kuiangusha nuru hiyo. Baba yetu wa Mbinguni huitoa bure nuru hiyo kwako. Kamwe hauko pekee yako. Yeye anasikia na kujibu kila ombi. Yeye “amekuita wewe kutoka gizani kuja katika nuru yake ya kupendeza.”27 Unaposema, “Baba, Baba, upo? Yeye daima atajibu, “Niko hapa, mwanangu, niko hapa.”

Ninatoa ushahidi kuwa Yesu Kristo alikamilisha mpango wa Baba wa Mbinguni kama Mwokozi na Mkombozi wetu;28 Yeye ni nuru yetu, uzima wetu, na ni njia yetu. Nuru Yake kamwe haitafifia,29 utukufu Wake kamwe hautakoma, upendo Wake kwako ni wa milele—jana, leo, na milele. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.

Chapisha