Mkutano Mkuu
Maskini Hawa
Mkutano mkuu wa Aprili 2021


9:33

Maskini Hawa

Katika kila kata na tawi tunamhitaji kila mmoja—wale ambao wanaweza kuwa imara na wale ambao huenda wanahangaika. Wote ni wa muhimu.

Kama mvulana, ninakumbuka nikiendesha gari pamoja na baba yangu na kuwaona watu kando ya barabara walio kwenye hali ngumu au waliohitaji msaada. Baba yangu kila mara alikuwa akisema “Pobrecito,” ambayo ilimaanisha “maskini hawa.”

Mara kadhaa, nilitazama kwa shauku wakati baba yangu alipokuwa anawasaidia wengi wa watu hawa, hasa wakati tulipokuwa tunasafiri kwenda Mexico kuwaona mababu zangu. Kwa kawaida, angemuona mtu mwenye uhitaji na kisha kwa faragha angetoa msaada uliohitajika. Baadaye niligundua kwamba alikuwa anawasaidia kujiunga na shule, kuwanunulia chakula, au kukidhi mahitaji yao kwa njia moja au nyingine. Alikuwa anamhudumia “maskini” ambaye alikutana nae. Kwa kweli, katika kukua kwangu siwezi kukumbuka wakati wowote ambapo sisi hatukuwa na mtu akiishi pamoja nasi ambaye alihitaji mahali pa kuishi walipokuwa wanafikia kwenye kujitegemea. Kutazama uzoefu huu kulijenga ndani yangu roho ya huruma kwa wanadamu wenzangu na wale wenye uhitaji.

Katika Hubiri Injili Yangu inasema: “Wewe umezungukwa na watu. Unawapita mtaani, unawatembelea nyumbani kwao, na unasafiri miongoni mwao. Wote ni watoto wa Mungu, akina kaka na dada zako. … Wengi wa watu hawa wanatafuta madhumuni ya maisha. Wanafikiria kuhusu kesho yao na familia zao” (Hubiri Injili yangu: Mwongozo wa Huduma ya Ummisionari [2018], 1).

Kwa miaka yote wakati nikitumikia katika Kanisa, nimejaribu kuwatafuta wale wanaohitaji msaada katika maisha yao, wa kimwili na kiroho. Ningesikia kila mara sauti ya baba yangu ikisema “Pobrecito,” maskini hawa.

Katika Biblia tunapata mfano wa kuvutia wa utunzaji wa maskini:

“Basi Petro na Yohana walikuwa wakikwea pamoja kwenda hekaluni, saa ya kusali, saa tisa.

“Na mtu mmoja aliyekuwa kiwete toka tumboni mwa mamaye alichukuliwa na watu, ambaye walimweka kila siku katika mlango wa hekalu uitwao Mzuri, ili aombe sadaka kwa watu waingiao ndani ya hekalu.

“Mtu huyu akiwaona Petro na Yohana wakiingia hekaluni aliomba apewe sadaka.

“ Na Petro, akimkazia macho pamoja na Yohana, akasema, Tutazame sisi.

“Akawaangalia, akitaraji kupata kitu kwao.

“Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende.

“Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu” (Matendo ya Mitume 3:1–7; msisitizo umeongezwa).

Katika kusoma tukio hili, nilishangazwa sana na matumizi ya neno akimkazia. Neno akimkazia linamaanisha kuelekeza macho au mawazo, au kutazama kwa dhamira (ona “fasten,” Dictionary.com). Petro alipokuwa akimtazama mtu huyu, alimwona kwa njia tofauti kuliko wengine. Alitazama zaidi ya ulemavu wake na udhaifu wake na angeweza kutambua kwamba imani yake ilikuwa ya kutosha kuponywa na kuingia hekaluni ili kupokea baraka alizokuwa anahitaji.

Nilitambua kwamba alimshika kwa mkono wa kuume na akamwinua. Akimsaidia mtu huyu kwa njia hii, Bwana kimiujiza alimponya, na “nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu” (Matendo ya Mitume 3:7). Upendo wake kwa mtu huyu na shauku ya kumsaidia vilisababisha ongezeko la nguvu na uwezo kwa mtu ambaye alikuwa mdhaifu.

Wakati nikitumikia kama Sabini wa Eneo, nilitenga usiku wa kila Jumanne kufanya matembezi ya uhudumiaji pamoja na marais wa vigingi katika majukumu yangu. Niliwaalika kupanga na wale waliokuwa na mahitaji ya ibada ya injili ya Yesu Kristo au wale waliokuwa hawashiki maagano waliyokuwa wameyafanya. Kupitia uhudumiaji wetu wa kila mara na wenye kusudi, Bwana alikuza juhudi zetu na tuliweza kuwapata watu na familia ambazo zilikuwa na uhitaji. Hawa walikuwa ndio “maskini” ambao waliishi katika vigingi tofauti ambapo tulitumikia.

Wakati mmoja, niliandamana na Rais Bill Whitworth, rais wa Kigingi cha Sandy Utah Canyon View, kufanya matembezi ya uhudumiaji. Alikuwa anasali ni nani tunapaswa kumtembelea, akijaribu kuwa na uzoefu sawa na wa Nefi, ambapo “akiongozwa na Roho, bila kujua kimbele vitu ambavyo angefanya” (1 Nefi 4:6). Alionyesha kwamba tunapohudumu, tunapaswa kuongozwa na ufunuo kwa wale ambao wana mahitaji zaidi, na sio kupitia orodha au kufanya matembezi kwa watu binafsi kwa kufuata mpangilio. Tunapaswa kuongzwa na nguvu za mwongozo.

Ninakumbuka kutembelea nyumba ya wenzi vijana, Jeff na Heather, na mvulana wao mdogo, Kai. Jeff alilelewa kama muumini hai wa Kanisa. Alikuwa mwana riadha mwenye talanta na alikuwa na kazi ya kutegemewa. Alianza kutoka kwenye Kanisa katika miaka ya ujana wake. Baadaye, alipata ajali ya gari, ambayo iligeuza mkondo wa maisha yake. Tulipoingia nyumbani kwao na kufahamiana nao, Jeff alituuliza kwa nini tulikuja kuiona familia yao. Tulijibu kwamba kulikuwa na karibia waumini 3,000 ambao waliishi katika mipaka ya kigingi. Kisha nilimuuliza, “Jeff, kati ya nyumba zote ambazo tungetembelea usiku wa leo, tuambie kwa nini Bwana ametutuma sisi hapa.”

Kwa hilo, Jeff akapatwa na hisia na kuanza kushiriki nasi baadhi ya wasiwasi wake na baadhi ya mambo waliyokuwa wanapambana nayo kama familia. Tulianza kushiriki kanuni tofauti tofauti za injili ya Yesu Kristo. Tuliwaalika wao wafanye mambo machache mahususi ambayo yangeonekana kama changamoto mwanzoni bali kadiri muda unavyosonga yangewaletea furaha kuu na shangwe. Kisha Rais Whitworth alimpatia Jeff baraka ya ukuhani ili kumsaidia kushinda changamoto zake. Jeff na Heather walikubali kufanya kile tulichowaalika wafanye.

Takribani mwaka mmoja baadaye, ilikuwa ni fursa yangu kumwona Jeff akimbatiza mke wake, Heather, kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Sasa wanajiandaa kuingia hekaluni kuunganishwa kama familia kwa muda na milele yote. Matembezi yetu yaligeuza mkondo wa maisha yao yote ya kimwili na kiroho.

Bwana ametamka:

“Kwa hiyo, uwe mwaminifu; simama katika ofisi ambayo nimekuteua; wasaidie wadhaifu, inyooshe mikono iliyolegea, na yaimarishe magoti yaliyo dhaifu” (Mafundisho na Maagano 81:5).

“Na katika kufanya mambo haya utakuwa umefanya mema makuu kwa wanadamu wenzako, na utakuwa umeukuza utukufu wake aliye Bwana wako” (Mafundisho na Maagano 81:4).

Akina kaka na dada, Mtume Paulo alifundisha kipengele muhimu katika uhudumiaji wetu. Alifundisha kwamba sisi ni “mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake” (1 Wakorintho 12:27) na kwamba kila kiungo cha mwili kinahitajika ili kuhakikisha kwamba mwili wote unajengwa. Kisha alifundisha ukweli wenye nguvu ambao ulipenya kwa kina ndani ya moyo wangu nilipokuwa nausoma. Alisema, “Bali zaidi sana vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa vinyonge zaidi, vyahitajiwa zaidi: na vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa havina heshima, viungo vile twavipa heshima zaidi” (1 Wakorintho 12:22–23; msisitizo umeongezwa).

Basi, katika kila kata na tawi tunamhitaji kila mmoja—wale walio na nguvu na wale ambao huenda wanahangaika. Wote ni wa lazima katika kujenga “mwili mkamilifu wa Kristo.” Mara nyingi najiuliza ni kina nani tunawakosa katika mikusanyiko yetu tofauti tofauti ambao wengetuimarisha na kutufanya wakamilifu.

Mzee D. Todd Christofferson alifundisha “Katika Kanisa hatujifunzi tu mafundisho matakatifu; tunapata uzoefu wa matumizi yake. Kama mwili wa Kristo, waumini wa Kanisa wanahudumiana wao kwa wao katika uhalisi wa maisha ya kila siku. Sisi sote hatujakamilika. … Katika mwili wa Kristo, hatuna budi kutenda zaidi ya mawazo na maneno ya kuinua na kuwa na ‘uzoefu wetu binafsi’ tunapojifunza ‘kuishi pamoja kwa upendo’ [Mafundisho na Maagano 42:45]” (“Kwa Nini Kanisa,” Liahona, Nov. 2015, 108–9).

Ndoto ya Brigham Young

Mnamo mwaka 1849, Brigham Young alipata ndoto ambapo alimwona Nabii Joseph Smith akionekana kulisha kundi kubwa la kondoo na mbuzi. Baadhi ya wanyama hawa walikuwa wakubwa na wazuri; wengine walikuwa wadogo na wachafu. Brigham Young alikumbuka akimtazama Nabii Joseph Smith machoni na kusema, “Joseph, wewe una zizi lililo na kiza … ambalo sijawahi kuliona katika maisha yangu; wewe utafanya nini nao?” Nabii, ambaye alionekana kutokuwa na wasiwasi na hili zizi korofi, kwa urahisi alijibu, “[Brigham] wote ni wazuri katika nafasi zao.”

Wakati Rais Young alipoamka, alielewa kwamba wakati Kanisa litakusanya namna tofauti ya “kondoo na mbuzi,” ni jukumu lake kuwaleta wote ndani na kumruhusu kila mmoja wao kufikia uwezo wake mkamilifu wanapochukua nafasi zao katika Kanisa. (Imetoholewa kutoka kwa Ronald W. Walker, “Brigham Young: Student of the Prophet,” Ensign, Feb. 1998, 56–57.)

Akina kaka na dada, chanzo cha hotuba yangu kilikuja nilipokuwa nikifikiria kwa kina kuhusu yule ambaye kwa sasa hajihusishi na Kanisa la Yesu Kristo. Kwa muda huu ningependa kuzungumza na kila mmoja wao. Mzee Neal A. Maxwell amefundisha kwamba “watu kama hao mara nyingi hukaa karibu sana—lakini hawashiriki kikamilifu katika—Kanisa. Hawatakuja ndani ya ukumbi wa kanisa, wala hawataondoka kwenye baraza lake. Hawa ndio wale ambao wanahitaji na wanahitajika na Kanisa, lakini ambao, kwa sehemu, ‘wanaishi bila Mungu katika ulimwengu’ [Mosia 27:31]” (“Kwa Nini Si Sasa?Ensign, Nov. 1974, 12).

Ninatoa mwaliko wa Rais wetu mpendwa Russell M. Nelson kama alivyonena kwa mara ya kwanza kwa waumini wa Kanisa. Alisema: “Sasa, kwa kila muumini wa Kanisa ninasema: Baki katika njia ya agano. Dhamira yako ya kumfuata Mwokozi kwa kufanya maagano pamoja Naye na kisha kuyashika maagano hayo kutafungua mlango kwa kila baraka ya kiroho na fursa kwa wanaume, wanawake, na watoto kila mahali.”

Kisha alisihi: “Sasa, ikiwa umechepuka kutoka njiani, naomba nikualike kwa matumaini yote ya moyo wangu tafadhali rudi. Bila kujali wasiwasi wako, changamoto zako, kuna nafasi yako katika hili, Kanisa la Bwana. Wewe na vizazi ambavyo havijazaliwa mtabarikiwa kwa matendo yako kwa sasa kurejea katika njia ya agano” (“Tunaposonga Mbele Pamoja,” au Liahona, Apr. 2018, 7; msisitizo umeongezwa).

Ninashuhudia juu Yake, hata Yesu Kristo, Mtumishi Bwana na Mwokozi wetu sote. Nawaalika kila mmoja wetu kuwatafuta “pobrecitos,” “maskini hawa” miongoni mwetu ambao wana uhitaji. Hili ndilo tumaini na ombi langu katika jina la Yesu Kristo, amina.