Mtakuwa Huru
Yesu Kristo ni nuru ambayo tunapaswa kuishikilia hata katika nyakati za giza za maisha yetu.
Wapendwa kaka na dada zangu, ninayo furaha kuwahutubia kutoka Afrika. Ni baraka kuwa na teknolojia siku hizi na kuitumia katika njia iliyo sahihi kabisa kuwafikia nyote popote mlipo.
Mnamo Septemba 2019, Dada Mutombo na Mimi, wakati tukihudumu kama viongozi wa Misheni ya Maryland Baltimore, tulipata bahati ya kutembelea baadhi ya sehemu za kihistoria za Kanisa huko Palmyra, New York, wakati tukihudhuria semina za uongozi wa misheni. Tulimalizia matembezi yetu katika Kijisitu Kitakatifu. Nia yetu katika kutembelea Kijisitu Kitakatifu haikuwa kupata udhihirisho maalumu au ono, bali tulihisi uwepo wa Mungu katika sehemu hii takatifu. Mioyo yetu ilijawa na furaha kwa ajili ya Nabii Joseph Smith.
Wakati tukirudi Dada Mutombo aligundua kwamba nilikuwa na tabasamu kubwa wakati naendesha gari, kwa hiyo aliuliza, “Nini sababu ya msisimko wako?”
Nilijibu, “Mpendwa wangu Nathalie, ukweli utasimama daima dhidi ya uongo, na giza halitaendelea duniani kwa sababu ya injili ya urejesho ya Yesu Kristo.”
Mungu Baba na Yesu Kristo walimtembelea kijana Joseph Smith kuleta katika mwanga kile kilichokuwa kimefichwa, ili tuweze kupata “ufahamu wa mambo kama yalivyo, … kama yalivyokuwa, na kama [yatakavyo kuwa]” (Mafundisho na Maagano 93:24).
Baada ya takribani miaka miambili, wengi bado wanautafuta ukweli unaohitajika kuwa huru dhidi ya baadhi ya tamaduni na uongo ambao adui husambaza ulimwenguni kote. Wengi “wanafumbwa macho na hila za ujanja wa mwanadamu” (Mafundisho na Maagano 123:12). Katika barua yake kwa Waefeso, Paulo alifundisha: “Amka, wewe usinziaye, Ufufuke katika wafu, Na Kristo atakuangaza” (Waefeso 5:14). Mwokozi aliahidi kwamba Atakuwa mwanga kwa wale wote wasikiao maneno Yake (ona 2 Nefi 10:14).
Miaka thelathini na tano iliyopita, wazazi wangu pia walikuwa wamepofushwa na kwa kukata tamaa wakitafuta kujua ukweli na walikuwa na dukuduku juu ya wapi pa kuupata. Wazazi wangu wote walizaliwa kijijini, ambako tamaduni zilikuwa zimekita mizizi katika maisha ya watu binafsi na familia. Wote walitoka kijijini walipokuwa bado vijana na kuja mjini, wakitafuta maisha bora.
Walioana na kuanza familia katika njia isiyo ya kifahari. Tulikuwa takribani watu nane katika nyumba ndogo—wazazi wangu, dada zangu wawili na mimi, na binamu aliyekuwa akiishi na sisi. Nilijiuliza ikiwa tulikuwa kweli familia, kwani hatukuruhusiwa kukaa meza moja wakati wa kupata chakula cha jioni na wazazi wetu. Baba yetu alipokuwa akirudi kutoka kazini, mara tu alipoingia ndani ya nyumba, tulitakiwa kutoka na kwenda nje. Usiku ulikuwa mfupi kwetu, kwani hatukuweza kulala kwa sababu ya kukosa amani na upendo wa kweli katika ndoa ya wazazi wetu. Nyumba yetu si tu ilikuwa ndogo kwa ukubwa, bali pia ilikuwa sehemu ya giza. Kabla ya kukutana na Wamisionari, tulihudhuria katika makanisa mbali mbali kila Jumapili. Ilikuwa wazi kwamba wazazi wetu walikuwa wanatafuta kitu ambacho dunia isingeweza kuwapa.
Hii ilienedelea mpaka tulipokutana na Mzee na Dada Hutchings, wamisionari wa kwanza wana ndoa walioitwa kutumikia katika Zaire (ijulikanayo kwa sasa kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo au Congo-Kinshasa). Tulipoanza kukutana na hawa Wamisionari wa kupendeza, ambao walikuwa kama malaika walio kuja kutoka kwa Mungu, niligundua kwamba kuna kitu kilianza kubadilika katika familia yetu. Baada ya ubatizo wetu, kiukweli tulianza kuwa na mwendelezo wa mfumo mpya wa maisha kwa sababu ya injili ya urejesho. Maneno ya Kristo yalianza kupanua mioyo yetu. Yalianza kuangazia uelewa wetu na yalikuwa matamu kwetu, kulingana na ukweli tulioupokea yalikuwa ya hekima na tuliweza kuona mwanga, na mwanga huu uliendelea kuwa angavu na angavu kila siku.
Uelewa huu wa kwa nini ya injili ulikuwa unatusaidia sisi kuwa zaidi kama Mwokozi. Ukubwa wa nyumba yetu haukubadilika; hata hali zetu za kijamii. Ila nilishuhudia mabadiliko ya moyo kwa wazazi wangu kadiri tulivyosali kila siku, asubuhi na jioni. Tulijifunza Kitabu cha Mormoni; tulifanya jioni ya familia; hakika tukawa familia. Kila Jumapili tuliamka saa 12 za asubuhi kujiandaa kwenda kanisani, na tuliweza kusafiri kwa saa kadhaa kuhudhuria mikutano ya Kanisa kila juma bila kunung’unika. Ilikuwa ni uzoefu kushuhudia. Sisi, ambao awali tulitembea katika giza, tulifukuza giza kutoka miongoni mwetu (ona Mafundisho na Maagano 50:25) na kuona “mwanga mkuu” (2 Nefi 19:2).
Nakumbuka siku moja, nilipokuwa siko tayari kuamka mapema asubuhi kwa ajili ya sala ya familia, nilinung’unika kwa dada zangu, “Hivi hakuna kitu kingine hakika tunaweza kufanya katika nyumba hii, kusali, kusali, kusali tu.” Baba yangu alisikia maoni yangu. Nakumbuka alichokifanya, alivyonifundisha kwa upendo lakini kwa uthabiti, “Kwa muda utakao kuwa katika nyumba hii, utasali, na kusali, na kusali.”
Maneno ya baba yangu yalisikika kila siku masikioni mwangu. Unafikiri Dada Mutombo na Mimi tunafanya nini kwa watoto wetu? Tunasali, na kusali na kusali. Huo ndio urithi wetu.
Mtu aliyezaliwa kipofu na aliyeponywa na Yesu Kirsto, baada ya kuzongwa na majirani na Mfarisayo, alisema:
“Mtu yule aitwaye Yesu alifanya tope, akanipaka machoni akaniambia, Nenda katika bwawa la Siloamu, ukanawe: basi nikaenda na kunawa, nikapata kuona. …
“…Kitu kimoja [ambacho] nafahamu [ni] kwamba … nilkuwa kipofu, na sasa [naweza] ona” (Yohana 9:11, 25).
Nasi pia tulikuwa vipofu na sasa tunaweza kuona. Injili iliyorejeshwa imeathiri familia yetu tangu wakati huo. Kuelewa kwa nini ya injili kumebariki vizazi vitatu vya familia yangu na itaendelea kubariki vizazi vingi vijavyo.
Yesu Kristo ni nuru ing’aayo gizani. Yeye ambaye humfuata “hatatembea gizani, bali atapata nuru ya uzima” (Yohana 8:12).
Takribani mwaka kati ya 2016 na 2017, watu katika mkoa wa Kasai walikabiliana na mkasa mbaya. Zilikuwa ni nyakati za giza kwa watu sababu ya mgongano kati ya kundi la mashujaa wa kiasili na majeshi ya serikali. Ghasia zilisambaa kutoka miji ya jimbo la kati la Kasai mpaka jimbo kubwa la Kasai. Watu wengi walikimbia kutoka kwenye nyumba zao kwa ajili ya usalama na kujificha vichakani. Hawakuwa na chakula wala maji, au chochote kimsingi, na kati ya hao walikuwepo waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho katika eneo la Kananga. Baadhi ya Waumini wa Kanisa waliuwawa na wanamgambo.
Kaka Honoré Mulumba wa kata ya Nganza katika Kananga na familia yake alikuwa kati ya watu wachache waliobaki wamejificha katika nyumba zao, pasipo kujua pa kwenda kwa sababu mitaa yote ilikuwa imegeuzawa uwanja wa kulenga shabaha. Siku moja wanamgambo majirani waligundua uwepo wa Kaka Mulumba na familia yake, wakati jioni moja walipokwenda nje kujaribu kutafuta mboga katika bustani ya familia kwa ajili ya kujipatia chakula. Kundi la wanajeshi lilikuja katika nyumba yao na kuwatoa nje na kuwaambia wachague kufuata matendo yao ya uwanamgambo au watauwawa.
Kwa ujasiri Kaka Mulumba aliwambia, “mimi ni muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Familia yangu na mimi tumemkubali Yesu Kirsto na tuna imani katika Yeye. Tutabaki waaminifu katika maagano yetu na tutakubali kufa.”
Waliwaambia, “Kama mlivyomchagua Yesu Kristo, miili yenu italiwa na mbwa,” na waliahidi kurudi tena. Lakini kamwe hawakuwahi kurudi, na familia ilibaki pale kwa miezi miwili zaidi na hawakuwaona tena. Kaka Mulumba na familia yake walisimama katika mwanga wa imani yao. Walikumbuka maagano yao na walilindwa.
Yesu Kristo ni nuru ambayo tunapaswa kuishikilia hata katika nyakati za giza za maisha yetu (ona 3 Nefi 18:24). Unapochagua kumfuata Kristo, unachagua kubadilishwa. Mtu anayebadilika kwa ajili ya Kristo, ataongozwa na Kristo, na tutauliza, kama Paulo alivyofanya, “Bwana, utataka mimi nifanye nini?” (Matendo ya Mitume 9:6). “Tutafuata njia zake” (1 Petro 2:21). “Tutatembea, kama yeye alivyotembea” (1 Yohana 2:6). (Ona Ezra Taft Benson, “Born of God,” Tambuli, Oktoba, 1989, 2, 6.)
Ninashuhudia juu ya Yake kwamba alikufa, alizikwa, na kufufuka tena siku ya tatu na kupaa mbinguni ili mimi na wewe tupate baraka za kutokufa na kuinuliwa. Yeye ni “nuru, … uhai, na ukweli” (Etheri 4:12). Yeye ni dawa na tiba ya mvurugano wa dunia. Yeye ni kipimo cha ubora wa kuinuliwa, hata Yesu Kristo. Katika jina la Yesu Kristo, amina.