Ikumbuke Njia yako ya Kurudi Nyumbani
Tunao mfano mkamilifu wa kufuata wa Yesu Kristo, na safari ya kuelekea nyumba yetu ya milele inawezekana tu kwa sababu ya mafundisho Yake, maisha Yake na dhabihu Yake ya upatanisho.
Mnamo 1946, mtafiti kijana Arthur Hasler alikuwa akipanda mlima kwenye mkondo wa mto karibu na mji wake aliokulia wakati alipopata uzoefu ambao uliongoza kwenye ugunduzi muhimu kuhusu jinsi samaki wanavyopata njia yao ya kurudi kwenye makazi yao walipozaliwa.
Kupanda juu mlimani, tena pasipo kuona maporomoko yake pendwa ya utotoni, Hasler ghafla alirejeshwa kwenye kumbukumbu yake iliyopotea. Alisema, “Wakati upepo mtulivu, wenye manukato ya maua ya mosses na columbine, ulipovuma kuzunguka mteremko wenye mawe, maelezo ya maporomoko haya na mandhari yake kwenye mlima ghafla vilinijia mawazoni.”1
Harufu hizi zilirejesha kumbukumbu zake za utotoni na kumkumbusha nyumbani.
Ikiwa harufu zinaweza kurejesha kumbukumbu kama hizo kwake, alikubali kwamba pengine harufu zinaweza kuwa kama kikumbushi kwa samaki ambao, baada ya miaka ya kuwa nje ya makazi yao, hurudi kwenye mkondo hasa wa uzao wao ili kutaga mayai.
Kufuatia tukio hili, Hasler, pamoja na watafiti wengine, waliendelea kuonesha kwamba samaki hukumbuka harufu hasa ambayo itawasaidia kuogelea maelfu ya maili kutafuta njia yao ya kurudi nyumbani kutoka baharini.
Maelezo haya yalinifanya niwaze kwamba moja ya mambo muhimu zaidi tunayoweza kufanya katika maisha haya ni kutambua na kukumbuka njia ya kurudi kwa Baba yetu wa Mbinguni na kwa uaminifu na furaha kuvumilia katika safari yote.
Nilitafakari juu ya vikumbushi vinne ambavyo, vikitumiwa kwa uendelevu katika maisha yetu, vinaweza kurejesha hisia za nyumbani kwetu mbinguni.
Kwanza, Tunaweza Kukumbuka Kwamba Sisi Ni Watoto wa Mungu
Tuna urithi wa kiungu. Kujua kwamba sisi ni watoto wa Mungu na kwamba Yeye anataka sisi turudi kwenye uwepo Wake ni moja ya hatua za kwanza kwenye safari yetu ya kurudi nyumbani kwetu mbinguni.
Jikumbushe mwenyewe juu ya urithi huu. Tenga muda kila mara kuboresha mfumo wa kinga yako ya kiroho kwa kukumbuka baraka ulizopokea kutoka kwa Bwana. Tumaini kwenye miongozo uliyokwisha kupewa kutoka Kwake, badala ya kuugeukia ulimwengu moja kwa moja kwa kupima ustahili wako binafsi na kutafuta njia yako.
Hivi karibuni nilimtembelea mpendwa wangu baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali. Aliniambia kwa hisia kwamba wakati akiwa amelala kwenye kitanda cha hospitali, yote aliyotamani ilikuwa ni mtu kumwimbia “Mie Mwana wa Mungu.” Wazo lile pekee, alisema, lilimpa amani aliyohitaji katika saa ile ya mateso.
Kujua wewe ni nani hubadili kile unachohisi na kile unachofanya.
Kuelewa wewe ni nani hasa kunakuandaa vyema kutambua na kukumbuka njia yako ya kurudi nyumbani kwako mbinguni na kutamani kuwa pale.
Pili, Tunaweza Kukumbuka Msingi Ambao Unatulinda Sisi
Nguvu huja kwetu wakati tunapobaki waadilifu, wakweli na waaminifu kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo, hata wakati wengine kwa nguvu wakipuuzia amri na kanuni za wokovu2.
Katika Kitabu cha Mormoni, Helamani aliwafundisha wana wake kukumbuka kwamba wanapaswa kujenga misingi yao juu ya Yesu Kristo ili wawe na nguvu za kuhimili majaribu ya ibilisi. Pepo zenye nguvu na vimbunga vya shetani vinatupiga, lakini havitakuwa na nguvu za kutuvuta chini ikiwa tumeweka tumaini letu mahali penye usalama—kwa Mkombozi wetu.3
Ninajua kutokana na uzoefu binafsi kwamba tunapochagua kuisikia sauti Yake na kumfuata, tutapokea usaidizi Wake. Tutapata mtazamo mpana wa hali zetu na uelewa mkubwa wa lengo la maisha. Tutahisi misukumo ya kiroho ambayo itatuongoza nyumbani kwetu mbinguni.
Tatu, Tunaweza Kukumbuka Kuwa Wenye Kuomba
Tunaishi kwenye wakati ambapo kwa mguso mmoja tu au sauti ya amri, tunaweza kuanza kutafuta majibu kwenye karibia kila mada katika wingi wa data zilizotunzwa na kupangiliwa kwenye mtandao mpana na mkubwa wa kompyuta.
Kwa upande mwingine, tunao urahisi wa mwaliko wa kuanza kutafuta majibu kutoka mbinguni. “Omba daima, na Mimi nitakumwagia Roho wangu juu yako.” Kisha Bwana anaahidi, “Na baraka kubwa itakuwa juu yako—ndiyo, hata zaidi kuliko kama ungelipata hazina za dunia na uozo uliomo ndani yake.”4
Mungu ana uelewa mkamilifu wa kila mmoja wetu na yu tayari kusikiliza maombi yetu. Tunapokumbuka kuomba, tunapata upendo Wake wa kuidhinisha, na kadiri tunavyoomba kwa Baba yetu wa Mbinguni katika jina la Kristo, ndivyo zaidi tunavyomleta Mwokozi katika maisha yetu na tutatambua vizuri zaidi njia Aliyoionesha ya nyumbani kwetu mbinguni.
Nne, Tunaweza Kukumbuka Kuwahudumia Wengine
Tunapojitahidi kumfuata Yesu Kristo kwa kuhudumu na kuonesha ukarimu kwa wengine, tunaufanya ulimwengu kuwa mahali pazuri zaidi.
Matendo yetu yanaweza kwa umuhimu mkubwa kubariki maisha ya wale wanaotuzunguka na maisha yetu wenyewe vile vile. Huduma ya upendo huongeza maana kwenye maisha ya wote mtoaji na mpokeaji.
Usipuuzie uwezekano ulionao wa kuwashawishi wengine kwa wema, vyote kwa huduma ya matendo yako na kwa huduma ya mfano wako.
Huduma ya upendo kwa wengine hutuongoza kwenye njia ya nyumbani kwetu mbinguni—njia ya kuwa kama Mwokozi wetu.
Mnamo 1975, kama matokeo ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, Arnaldo na Eugenia Teles Grilo pamoja na watoto wao walitakiwa kuacha nyumba yao na kila kitu walichokuwa wamejenga kupitia miongo mingi ya juhudi. Wakiwa wamerejea katika nchi yao ya asili ya Ureno, Kaka na Dada Teles Grilo walikabiliwa na changamoto ya kuanza upya tena. Lakini miaka kadhaa baadaye, baada ya kujiunga na Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, walisema, “Tulipoteza kila kitu tulichokuwa nacho, lakini ilikuwa jambo zuri kwa sababu ilitupa msukumo wa kuzingatia umuhimu wa baraka za milele.”5
Walipoteza nyumba yao ya duniani, lakini walipata njia ya kurudi nyumbani kwao mbinguni.
Chochote ambacho lazima uache ili kuifuata njia ya nyumbani mbinguni siku moja kitaonekana kama si dhabihu kabisa.
Tunao mfano mkamilifu wa kufuata wa Yesu Kristo, na safari ya kuelekea nyumba yetu ya milele inawezekana tu kwa sababu ya mafundisho Yake, maisha Yake na dhabihu Yake ya upatanisho—ikiwa ni pamoja na kifo Chake na Ufufuko Wake.
Ninawaalika mpate uzoefu wa shangwe ya kukumbuka kwamba sisi ni watoto wa Mungu na kwamba Yeye aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanaye6 ili atuoneshe njia. Ninawaalika mkumbuke kuwa waaminifu, muelekeze maisha yenu kwa Mwokozi na kujenga msingi wenu juu Yake. Kumbukeni kuwa wenye kuomba katika safari yenu na kuwahudumia wengine njiani.
Wapendwa akina kaka na akina dada, Jumapili hii ya Pasaka, ninatoa ushuhuda kwamba Yesu Kristo ni Mkombozi na Mwokozi wa ulimwengu. Yeye ndiye yule atakayetukaribisha kwenye meza ya maisha yenye shangwe na kutuongoza katika safari yetu. Na tumkumbuke na tumfuate Yeye nyumbani. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.