Mkutano Mkuu
Kwa Nini Njia ya Agano
Mkutano mkuu wa Aprili 2021


Kwa Nini Njia ya Agano

Tofauti ya njia ya agano ni umuhimu wa kipekee na wa milele.

Katika huduma yake yote, Rais Russell M. Nelson amejifunza na kufundisha juu ya maagano ya Mungu na watoto Wake. Yeye mwenyewe ni mfano unaong’aa wa yule anayetembea kwenye njia ya agano. Katika ujumbe wake wa kwanza kama Rais wa Kanisa, Rais Nelson alisema:

“Dhamira yako ya kumfuata Mwokozi kwa kufanya maagano pamoja Naye na kisha kuyashika maagano haya kutafungua mlango kwa kila baraka ya kiroho na fursa zilizopo kwa wanaume, wanawake na watoto kila mahali.”

“… Ibada za hekaluni na maagano unayofanya huko ni muhimu katika kuimarisha maisha yako, ndoa yako na familia yako na uwezo wako wa kupinga mashambulizi ya adui. Kuabudu kwako hekaluni na huduma yako huko kwa niaba ya mababu zako kutakubariki na ongezeko la ufunuo binafsi na amani na kutaimarisha kujitolea kwako kubaki kwenye njia ya agano.”1

Njia ya agano ni nini? Ni njia moja inayoongoza kwenye ufalme wa selestia wa Mungu. Tunaianza njia kwenye lango la ubatizo na kisha “kusonga mbele tukiwa na imani imara katika Kristo, tukiwa na mng’aro mkamilifu wa tumaini, na upendo kwa Mungu na wanadamu wote [amri mbili kuu]… hadi mwisho.”2 Katika mwelekeo wa njia ya agano (ambayo, inapita mipaka ya maisha ya duniani), tunapokea ibada na maagano yote yanayohusu wokovu na kuinuliwa.

Ahadi yetu kuu ya agano ni kufanya mapenzi ya Mungu “na kutii amri zake katika vitu vyote atakavyotuamuru.”3 Kufuata kanuni na amri za injili ya Yesu Kristo siku kwa siku ndiyo njia ya furaha na ya kuridhisha zaidi maishani. Kwa sababu moja, mtu huepuka shida nyingi na majuto. Ngoja nitumie analojia ya michezo. Katika tenisi, kuna kitu kinachoitwa makosa yasiyolazimishwa. Haya ni mambo kama vile kupiga mpira wa kuchezea kwenye wavu au kukosea mara mbili wakati wa kupiga mpira. Makosa yasiyolazimishwa huzingatiwa kama matokeo ya makosa ya mchezaji badala ya kusababishwa na ustadi wa mpinzani.

Mara nyingi shida zetu au changamoto zetu ni za kujitakia, matokeo ya uchaguzi mbaya, au, tunaweza kusema, matokeo ya “makosa yasiyolazimishwa.” Wakati tunafuata kwa bidii njia ya agano, kiuhalisia tunaepuka “makosa mengi yasiyolazimishwa.” Tunaepuka aina anuwai za uraibu. Hatuanguki kwenye shimo la mwenendo wa kukosa uaminifu. Tunavuka shimo la uasherati na ukafiri. Tunawapita pembeni watu na vitu ambavyo, hata ikiwa ni maarufu, vinaweza kuhatarisha ustawi wetu wa kimwili na kiroho. Tunaepuka chaguzi ambazo zinawadhuru au kuwadhalilisha wengine na badala yake tunajenga mazoea ya nidhamu binafsi na huduma.4

Inasemekana kuwa Mzee J. Golden Kimball alisema, “Pengine sikuweza [daima] kutembea njia iliyonyooka na nyembamba, lakini [najaribu] kuivuka mara nyingi kadiri [ninavyoweza].”5 Katika wakati muhimu zaidi, nina hakika Kaka Kimball angekubali kwamba kubaki, sio tu kuvuka, njia ya agano ni tumaini letu kubwa kwa ajili ya kuepuka masaibu yenye huzuni yanayoweza kuepukwa kwa upande mmoja na kufanikiwa kushughulikia masaibu ambayo hayaepukiki kwa upande mwingine.

Wengine wanaweza kusema, “Ninaweza kufanya chaguzi nzuri nikiwa na, au bila ubatizo; sihitaji maagano kuwa mtu mwenye heshima na aliyefanikiwa.” Hakika, kuna wengi ambao, wakati wao wenyewe hawako kwenye njia ya agano, hutenda kwa njia inayoonyesha chaguzi na michango ya wale walio kwenye njia. Unaweza kusema wanapata baraka za kutembea kwenye njia “inayofanana na ile ya agano”. Ni nini, basi, tofauti ya njia ya agano?

Kwa kweli, tofauti hiyo ni ya kipekee na yenye umuhimu wa milele. Inajumuisha asili ya utii wetu, tabia ya kujitolea kwa Mungu kwetu sisi, msaada wa kiungu tunaopokea, baraka zilizofungwa kwenye kukusanyika kama watu wa agano, na muhimu zaidi, urithi wetu wa milele.

Utiifu wa Dhati

Kwanza ni hali ya utii wetu kwa Mungu. Zaidi ya kuwa tu na nia njema, tunajitolea kwa dhati kabisa kuishi kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu. Katika hili, tunafuata mfano wa Yesu Kristo, ambaye, kwa kubatizwa, “anawaonyesha watoto wa watu kwamba, kulingana na mwili anajinyenyekeza mbele ya Baba, na kumshuhudia Baba kwamba yeye atakuwa mwaminifu kwake katika kutii amri zake.”6

Tukiwa na maagano, tunakusudia zaidi ya kuzuia tu makosa au kuwa na busara katika maamuzi yetu. Tunahisi kuwajibika kwa Mungu kwa chaguzi zetu na maisha yetu. Kujichukulia juu yetu jina la Kristo. Tunafokasi kwa Kristo—katika kuwa hodari katika ushuhuda wa Yesu na katika kukuza tabia ya Kristo.

Tukiwa na maagano, utii wa kanuni za injili hujikita katika nafsi zetu. Ninawajua wanandoa ambao, wakati wa ndoa yao, mke hakuwa akishiriki kikamilifu Kanisani na mume hakuwahi kuwa muumini wa Kanisa. Nitawarejelea kama Mary na John, si majina yao halisi. Watoto walipoanza kuzaliwa, Mary alihisi sana hitaji la kuwalea, kama maandiko yanavyosema, “katika malezi na maonyo ya Bwana.”7 John alikuwa akiunga mkono. Mary alitoa dhabihu muhimu kuwa nyumbani kufundisha injili kwa mpangilio endelevu. Alihakikisha kuwa familia inahusika kikamilifu kwenye ibada na shughuli Kanisani. Mary na John wakawa wazazi wa mfano, na watoto wao (wavulana wenye nguvu) walikua katika imani na kujitolea kwenye kanuni na viwango vya injili.

Wazazi wa John, babu na bibi wa wavulana, walifurahishwa na maisha mazuri na mafanikio ya wajukuu zao, lakini kwa sababu ya kupingana na Kanisa, walitaka kuelezea mafanikio haya kwa ustadi wa malezi ya John na Mary. John, ingawa hakuwa muumini wa Kanisa, hakuruhusu tathmini hiyo iende bila kupingwa. Alisisitiza kwamba walikuwa wakishuhudia matunda ya mafundisho ya injili—yale ambayo wanawe walikuwa wakipata kanisani na vile vile yaliyokuwa yakitokea nyumbani.

John mwenyewe alikuwa akishawishiwa na Roho, kwa upendo na mfano wa mkewe, na kwa ushawishi wa wanawe. Kwa wakati uliofaa, alibatizwa, kwa furaha kubwa ya washiriki wa kata na marafiki.

Wakati maisha hayajawa bila changamoto kwao na kwa watoto wao, Mary na John wanathibitisha kwa moyo wote kwamba hakika ni agano la injili ambalo ndilo msingi wa baraka zao. Wameona maneno ya Bwana kwa Yeremia yakitimizwa katika maisha ya watoto wao na pia yao wenyewe: “Nitaweka sheria yangu katika sehemu zao za ndani, na kuiandika katika mioyo yao; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.”8

Kuunganishwa kwa Mungu

Kipengele cha pili cha kipekee cha njia ya agano ni uhusiano wetu na Uungu. Maagano ambayo Mungu hutoa kwa watoto Wake hufanya zaidi tu ya kutuongoza. Yanatuunganisha Kwake na tukiwa tumeunganishwa Kwake, tunaweza kushinda mambo yote.9

Niliwahi kusoma makala ya mwandishi wa habari aliyekuwa na taarifa hasi ambaye alielezea kwamba jinsi tunavyofanya ubatizo wa wafu ni kuzamisha safu za filamu ndogo ndogo ndani ya maji. Halafu wale wote ambao majina yao yanaonekana kwenye filamu ndogo ndogo wanazingatiwa kuwa wamebatizwa. Njia hiyo itakuwa yenye ufanisi mkubwa, lakini inapuuza thamani isiyo na kikomo ya kila nafsi na umuhimu wa juu wa agano binafsi na Mungu.

“[Yesu] alisema … : Ingieni kwa mlango mwembamba; kwani mlango umesonga na njia ni nyembamba, iendayo uzimani, na kuna wachache ambao huipata.”10 Kwa mfano, mlango huu ni mwembamba sana kwamba unaruhusu mtu mmoja tu kuingia kwa wakati. Kila mmoja anaweka msimamo binafsi kwa Mungu na kama malipo anapokea kutoka Kwake agano binafsi, kwa jina, ambalo anaweza kutegemea kikamilifu sasa na milele. Tukiwa na ibada na maagano, “nguvu ya ucha mungu hujidhihirisha” katika maisha yetu.11

Msaada wa Kiungu

Hii inatuongoza kuzingatia baraka maalum ya tatu ya njia ya agano. Mungu hutoa zawadi isiyoweza kuelezeka kuwasaidia wafanya maagano kuwa watunza-maagano: zawadi ya Roho Mtakatifu. Zawadi hii ni wenza wa daima, ulinzi, na mwongozo wa Roho Mtakatifu.12 Pia anajulikana kama Mfariji, Roho Mtakatifu “hujaza tumaini na upendo kamili.”13 Yeye “anajua mambo yote, na anashuhudia juu ya Baba na Mwana,”14 ambao ushahidi wao tunaweka msimamo wa kuwa.15

Kwenye njia ya agano pia tunapata baraka muhimu za msamaha na utakaso kutokana na dhambi. Huu ni msaada ambao unaweza kuja tu kupitia neema ya kiungu, inayosimamiwa na Roho Mtakatifu. “Sasa hii ndiyo amri,” asema Bwana, “Tubuni nyinyi nyote katika sehemu zote za dunia, na mje kwangu na mbatizwe katika jina langu kwamba muweze kutakaswa kwa kupokea Roho Mtakatifu, ili msimame mbele yangu bila mawaa katika siku ya mwisho.”16

Kukusanyika pamoja na Watu wa Agano

Nne, wale wanaofuata njia ya agano hupata pia baraka za pekee katika mikusanyiko anuwai iliyochaguliwa ya kiungu. Unabii wa mkusanyiko halisi wa makabila ya Israeli yaliyotawanyika kwa muda mrefu katika nchi za urithi wao hupatikana kote katika maandiko.17 Utimilifu wa unabii na ahadi hizo sasa unaendelea kwa kukusanywa kwa watu wa agano katika Kanisa, ufalme wa Mungu duniani. Raisi Nelson anaeleza, “Tunapozungumza kuhusu kukusanya, kiurahisi tunasema kanuni hii ya kweli: kila mmoja wa watoto wa Baba yetu wa Mbinguni … anastahili kusikia ujumbe wa injili ya urejesho ya Yesu Kristo.”18

Bwana anawaamuru waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho Bwana anawaamuru waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho “inukeni na mng’are, ili nuru yenu ipate kuwa bendera kwa ajili ya mataifa; … ili kukusanyika pamoja juu ya nchi ya Sayuni, na juu ya vigingi vyake, kupata kuwa ngome, na makimbilio wakati wa tufani, na ghadhabu wakati itakapomwagwa pasipo kuchanganywa juu ya dunia yote.”19

Pia kuna mkusanyiko wa kila wiki wa watu wa agano kwenye nyumba ya sala katika siku ya Bwana, ili tuweze “kujilinda na dunia pasipo mawaa.”20 Ni mkusanyiko wa kushiriki mkate na maji ya sakramenti kwa ukumbusho wa Upatanisho wa Yesu Kristo na wakati wa “kufunga na kuomba, na kuzungumza mmoja na mwingine kuhusu ustawi wa nafsi [zetu].”21 Kama kijana, nilikuwa muumini pekee wa Kanisa katika darasa langu la shule ya upili. Nilifurahia ushirika wa marafiki wengi wazuri shuleni, lakini niligundua kuwa nilitegemea sana mkutano huu wa Sabato kila wiki ili kuniburudisha na kunifanya upya kiroho, na hata kimwili. Jinsi gani tumehisi kupotea kwa mkusanyiko huu wa kawaida wa agano wakati wa janga la sasa la ulimwengu, na jinsi gani kwa shauku tunatazamia wakati ambapo tunaweza kukusanyika tena kama hapo awali.

Watu wa agano pia hukusanyika kwenye hekalu, nyumba ya Bwana, kupata ibada, baraka, na ufunuo unaopatikana kipekee huko. Nabii Joseph Smith alifundisha: “Nini ilikuwa nia ya kukusanyika … kwa watu wa Mungu katika kipindi chochote cha ulimwengu? … Lengo kuu lilikuwa kumjengea Bwana nyumba ambayo kwayo angeweza kufunua kwa watu wake ibada za nyumba Yake na utukufu wa ufalme Wake, na kuwafundisha watu njia ya wokovu; kwani kuna baadhi ya ibada na kanuni ambazo, wakati zinapofundishwa na kutekelezwa, lazima zifanyike mahali au katika nyumba iliyojengwa kwa kusudi hilo.”22

Kurithi Ahadi za Agano

Mwisho, ni katika tu kufuata njia ya agano kwamba tunarithi baraka za Ibrahimu, Isaka, na Yakobo, baraka za juu za wokovu na kuinuliwa ambazo ni Mungu tu anayeweza kutoa.23

Marejeo ya Kimaandiko kwa watu wa agano mara nyingi humaanisha uzao halisi wa Ibrahimu au “nyumba ya Israeli.” Lakini watu wa agano pia ni pamoja na wote wanaopokea injili ya Yesu Kristo.24 Paulo alieleza:

“Maana kadiri wengi wenu mlivyobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. …

“Na ikiwa ninyi ni wa Kristo, basi ninyi ni uzao wa Ibrahimu, na warithi kulingana na ahadi.”25

Wale ambao ni waaminifu kwenye maagano yao “watatokea katika ufufuo wa wenye haki.”26 Wao “hukamilishwa kupitia Yesu mpatanishi wa agano jipya. … Hawa ndio wale ambao miili yao ni ya selestia, ambao utukufu wao ni ule wa jua, hata utukufu wa Mungu, mkuu kuliko wote.”27 “Kwa hiyo, vitu vyote ni mali yao, iwe uzima au mauti, au vile vilivyopo, au vile vitakavyo kuwepo, vyote ni vyao nao ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu.”28

Acha tufuate wito wa nabii wa kubaki kwenye njia ya agano. Nefi alituona sisi na wakati wetu na akaandika, “Mimi, Nefi, niliona nguvu za mwana kondoo wa Mungu, kwamba ziliwashukia watakatifu wa kanisa la mwanakondoo, na kwa watu wa agano wa Bwana, ambao walitawanyika kote usoni mwa dunia; na walikuwa wamejikinga kwa utakatifu na kwa nguvu za Mungu katika utukufu mkuu.”29

Pamoja na Nefi, “nafsi yangu hufurahia” katika maagano ya Bwana.”30 Katika Jumapili hii ya Pasaka, ninatoa ushuhuda wa Yesu Kristo, ambaye Ufufuo wake ni tumaini letu na hakikisho lisilopingika la yote yaliyoahidiwa kwenye njia na mwisho wa njia ya agano. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.

Chapisha