Napenda Kuona Hekalu
Ni ndani ya hekalu ambapo tunaweza kupokea hakikisho la muunganiko wa upendo wa familia ambao utandelea baada ya kifo na kudumu milele.
Kaka na dada zangu wapendwa, nashukuru kuwa nanyi katika kikao hiki cha kwanza cha Mkutano Mkuu. Wanenaji, muziki, na maombi yameleta Roho—pamoja na hisia ya nuru na tumaini.
Hisia hiyo imeleta katika kumbukumbu yangu siku ya kwanza nilipoingia katika Hekalu la Salt Lake. Nilikuwa mvulana mdogo. Wazazi wangu walikuwa ndio wenzi wangu wa pekee siku hiyo. Ndani, walisimama kwa dakika ili kumsalimu mfanyakazi wa hekaluni. Mimi nilitembea mbele yao, peke yangu kwa dakika.
Nilisalimiwa na mwanamke mdogo mwenye mvi aliyevaa vazi jeupe la kupendeza la hekaluni. Alinitazama, akatabasamu, na kisha kusema kwa sauti laini, “Karibu hekaluni Kaka Eyring.” Kwa dakika nilifikiri alikuwa malaika kwa sababu alijua jina langu. Sikuwa nimetambua kwamba kadi ndogo yenye jina langu ilikuwa imewekwa kwenye mkunjo wa koti langu.
Nilipiga hatua na kumpita na nikasimama. Nilitazama juu kwenye dari ndefu nyeupe ambayo ilifanya chumba kuwa na nuru kiasi kwamba ilionekana kama ilikuwa wazi kuelekea mawinguni. Na katika wasaa ule, wazo likanijia akilini mwangu kwa maneno haya dhahiri: “Nimewahi kuwa mahali hapa angavu kabla.” Lakini kisha ghafla yakaja akilini mwangu, sio kwa sauti yangu, maneno haya: “Hapana, hujawahi kamwe kuwa mahali hapa kabla. Unakumbuka wakati kabla ya kuzaliwa kwako. Ulikuwa mahali patakatifu kama hapa.”
Nje ya mahekalu yetu, tunaweka maneno, “Utakatifu kwa Bwana.” Mimi binafsi ninajua kwamba maneno hayo ni ya kweli. Hekalu ni mahali patakatifu ambapo ufunuo huja kwetu kwa urahisi ikiwa mioyo yetu imefunguliwa na tu wastahiki wa ufunuo huo.
Baadaye siku hiyo ya kwanza mimi tena nilihisi Roho hiyo hiyo. Sherehe ya hekaluni hujumuisha baadhi ya maneno ambayo yalileta hisia za mwako ndani ya moyo wangu, zikithibitisha kwamba kile kilichokuwa kikifanyika kilikuwa cha kweli. Kitu nilichohisi kilikuwa cha binafsi kwangu kuhusiana na siku zangu za usoni, na kilikuja kuwa kweli miaka 40 baadae kupitia wito wa kuhudumu kutoka kwa Bwana.
Nilipata hisia hizo hizo wakati nilipofunga ndoa katika Hekalu la Logan Utah. Rais Spencer W. Kimball alifanya uunganisho. Kwa maneno machache aliyosema, alitoa ushauri huu, “Hal na Kathy, muishi ili kwamba wakati wito utakapokuja, mnaweza kuondoka kwa urahisi.”
Aliposema maneno hayo machache, niliona wazi akilini mwangu, katika rangi kamili, kilima chenye mteremko mkali na barabara ikielekea juu. Ua mweupe ulielekea upande wa kushoto wa barabara na kupotelea kwenye safu za miti huko juu ya kilima. Nyumba nyeupe ilionekana kidogo tu miongoni mwa miti.
Mwaka mmoja baadaye, nilitambua kilima kile wakati baba mkwe wangu alipokuwa akiendesha gari kuelekea juu kwenye ile barabara. Ilikuwa kwa ukamilifu kile nilichoona wakati Rais Kimball alipotoa ushauri wake hekaluni.
Tulipofika juu ya kilima, baba mkwe wangu alisimama karibu na ile nyumba nyeupe. Alituambia kwamba yeye na mke wake watanunua ile ardhi na majengo na kwamba alitaka mimi na binti yake tuishi upande wa nyumba ya wageni. Wao wangeishi katika nyumba kubwa, umbali mchache tu kutoka tulipo. Kwa hiyo, katika kipindi cha miaka 10 tuliyoishi katika hayo mazingira mazuri ya familia, mimi na mke wangu tungesema karibu kila siku, “Inatupasa tufurahie haya, kwa sababu hatutaishi hapa kwa muda mrefu.”
Simu ilikuja kutoka kwa Kamishina wa Elimu wa Kanisa, Neal A. Maxwell. Onyo lililotolewa na Rais Kimball la kuweza “kuondoka kwa urahisi” lilikuwa uhalisia. Ilikuwa wito wa kuacha kile kilichokuwa kinaonekana kama fursa nzuri ya familia kwenda kutumikia katika jukumu katika sehemu ambayo sikujua chochote kuihusu. Familia yetu ilikuwa tayari kuacha muda na sehemu ile iliyobarikiwa kwa sababu nabii, ndani ya hekalu takatifu, mahali pa ufunuo, aliona tukio la siku za usoni ambalo kwalo sisi tulikuwa tumeandaliwa.
Mimi najua kwamba mahekalu ya Bwana ni mahali patakatifu. Kusudi langu leo katika kuzungumza juu ya mahelalu ni kuongeza hamu yenu na yangu ya kuwa wastahiki na tayari kwa ajili ya ongezeko la fursa za uzoefu wa hekaluni ambazo zinakuja kwetu.
Kwangu mimi, hamasa kuu ya kuwa mstahiki wa uzoefu wa hekaluni ni kile ambacho Bwana amesema juu ya nyumba Zake takatifu:
“Na alimradi watu wangu wakinijengea nyumba katika jina la Bwana, na ikiwa hawataruhusu kitu chochote kichafu kuingia ndani yake, ili isichafuliwe, utukufu wangu utatulia juu yake;
“Ndiyo, na uwepo wangu utakuwa ndani yake, kwa kuwa nitakuja ndani yake, na wote walio safi moyoni ambao watakuja ndani yake watamwona Mungu.
“Lakini kama itachafuliwa sitakuja ndani yake, na utukufu wangu hautakuwa humo; kwa kuwa sitakuja ndani ya mahekalu yasiyo matakatifu.”1
Rais Russell M. Nelson ameweka wazi kwetu kwamba tunaweza “kumwona” Mwokozi ndani ya hekalu katika hali ambayo Yeye hatakuwa tena asiyejulikana kwetu. Rais Nelson alisema hivi: “Sisi tunamwelewa Yeye. Tunaelewa kazi Yake na utukufu Wake. Na tunaanza kuhisi athari yake isiyo na mwisho ya maisha Yake yasiyo na kifani.”2
Kama wewe au mimi tutaenda hekaluni tukiwa si wasafi vya kutosha, hatutaweza kuona, kwa nguvu za Roho Mtakatifu, mafundisho ya kiroho kuhusu Mwokozi ambayo tunaweza kuyapokea ndani ya hekalu.
Tunapokuwa wastahiki kupokea mafundisho hayo, kutakuwa na ongezeko kupitia uzoefu wetu wa hekaluni tumaini, furaha, na msimamo wa kutegemea mema kote maishani mwetu. Tumaini hilo, furaha, na msimamo wa kutegemea mema hupatikana tu kwa kukubali ibada zinazofanywa ndani ya mahekalu matakatifu. Ni ndani ya hekalu ambapo tunaweza kupokea hakikisho la muunganiko wa upendo wa familia ambao utandelea baada ya kifo na kudumu milele.
Miaka kadhaa iliyopita, nikiwa ninahudumu kama askofu, kijana mmoja mtanashati alikataa mwaliko wangu wa kuwa mstahiki kuishi na Mungu katika familia milele. Kwa njia ya kichokozi aliniambia juu ya nyakati nzuri alizofurahia pamoja na rafiki zake. Nilimruhusu azungumze. Kisha aliniambia kuhusu wakati wa moja ya karamu zake, katikati ya makelele, ambapo ghafla aligundua kwamba alihisi upweke. Nilimwuliza ni nini kilikuwa kimetokea. Alisema kwamba alikuwa amekumbuka wakati mmoja akiwa mvulana mdogo, akiwa ameketi kwenye miguu ya mama yake, mama akiwa amemkumbatia. Kwa wasaa ule wakati akisimulia hadithi hiyo, alitokwa na machozi. Nilimwambia kile nilichojua ni kweli: “Njia pekee ya wewe kuwa na hisia ya kumbatio hilo la familia milele ni kuwa mstahiki wewe mwenyewe na kuwasaidia wengine kupokea ibada za kuunganisha za hekaluni.”
Hatujui maelezo ya muunganiko wa familia katika ulimwengu wa roho au kile kinachoweza kutokea baada ya sisi kufufuka. Lakini tunajua kwamba nabii Eliya alikuja kama ilivyoahidiwa kuigeza mioyo ya baba iwaelekee watoto na ya watoto iwaelekee baba zao.3 Na tunajua kwamba furaha yetu ya milele hutegemea juu ya jithada zetu za kutoa furaha hiyo hiyo ya kudumu kwa wengi wa ukoo wetu kadiri tunavyoweza.
Ninahisi hamu hiyo hiyo ya kufanikiwa katika kuwaalika wanafamilia walio hai kuwa na hamu ya kuwa wastahiki kupokea na kuheshimu ibada za kuunganisha za hekaluni. Hiyo ni sehemu ya kukusanya Israeli kulikoahidiwa katika siku za mwisho pande zote mbili za pazia.
Mojawapo ya fursa zetu kuu ni wakati wanafamilia wetu wanapokuwa wadogo. Wanazaliwa na Nuru ya Kristo kama zawadi. Inawasaidia kutambua kile kilicho chema na kile kilicho kibaya. Kwa sababu hiyo, hata kuona hekalu au picha ya hekalu kunaweza kupanda ndani ya mtoto hamu ya kuwa mwenye kustahili siku moja kuingia ndani yake.
Kisha siku inaweza kufika wakati, kama vijana, wanapokea kibali cha hekaluni ili kufanya ubatizo kwa niaba ndani ya hekalu. Katika uzoefu huo, hisia zao zinaweza kukua kwamba ibada za hekaluni daima zinaelekeza kwa Mwokozi na Upatanisho Wake. Wanapohisi wanatoa nafasi kwa mtu katika ulimwengu wa roho ya kusafishwa dhambi, hisia zao zitaongezeka za kumsaidia Mwokozi katika kazi Yake takatifu ya kumbariki mtoto wa Baba yetu wa Mbinguni.
Nimeona nguvu za uzoefu huo zikibadili maisha ya kijana. Miaka kadhaa iliyopita, nilienda na binti yangu hekaluni wakati wa jioni. Alikuwa wa mwisho kuhudumu kwa niaba katika mahali pa kubatizia. Binti yangu aliulizwa kama angebakia kwa muda zaidi ili kumalizia ibada kwa ajili ya watu wote ambao majina yao yalikuwa yameandaliwa. Alisema ndiyo.
Nilitazama wakati binti yangu akiingia katika kisima cha ubatizo. Ubatizo ulianza. Binti yangu mdogo alitiririkwa na maji usoni mwake kila mara alipoinuliwa kutoka kwenye maji. Aliulizwa tena na tena, “Unaweza kufanya zaidi?” Kila mara alisema ndiyo.
Kama baba aliyejali, nilianza kutumaini kwamba angeweza kuachiwa asifanye zaidi. Lakini bado nakumbuka uthabiti wake wakati alipoulizwa ikiwa angeweza kufanya zaidi na kusema kwa sauti ndogo imara, “Ndiyo.” Alibakia mpaka mtu wa mwisho kwenye orodha ya siku ile alipopokea baraka ya ubatizo katika jina la Yesu Kristo.
Nilipotoka hekaluni pamoja naye usiku ule, nilishangazwa na kile nilichokuwa nimekiona. Mtoto alikuwa ameinuliwa na kubadilishwa mbele ya macho yangu kwa kumtumikia Bwana katika nyumba Yake. Bado nakumbuka hisia ya nuru na amani tulipokuwa tunatembea kutoka hekaluni.
Miaka imepita. Yeye bado anasema ndiyo kwa swali kutoka kwa Bwana ikiwa ataweza kufanya zaidi kwa ajili Yake wakati inapokuwa vigumu. Hilo ndilo huduma ya hekaluni inachoweza kufanya kutubadili na kutuinua. Hiyo ndiyo sababu tumaini langu kwenu na familia yenu yote pendwa ni kwamba mtakua katika hamu na azimio la kuwa wastahiki kuingia katika nyumba ya Bwana kila mara kadiri hali zenu zitakavyoruhusu.
Yeye anataka kuwakaribisha huko. Ninaomba kwamba mtajaribu kujenga hamu katika mioyo ya watoto wa Baba wa Mbinguni kwenda huko, ambapo wanaweza kuhisi kuwa karibu na Yeye, na kwamba mtawaalika pia mababu zenu kustahili kuwa pamoja Naye na pamoja nanyi milele.
Maneno haya yanaweza kuwa yetu:
Napenda kuona hekalu.
Nitaenda huko siku moja
Kuhisi Roho Mtakatifu,
Kusikiliza na kuomba.
Kwani hekalu ni nyumba ya Mungu,
Mahali pa upendo na uzuri.
Nitajitayarisha Ningali kijana;
Huu ni wajibu wangu mtakatifu.4
Ninatoa ushuhuda wangu wa dhati kwamba sisi ni watoto wa Baba wa Mbinguni mwenye upendo. Yeye alimchagua Mwanawe Mpendwa, Yesu Kristo, kuwa Mwokozi na Mkombozi wetu. Njia pekee ya kurudi kuishi pamoja na Wao na pamoja na familia zetu ni kupitia ibada za hekalu takatifu. Ninashuhudia kwamba Rais Russell M. Nelson anashikilia na kutumia funguo zote za ukuhani ambazo hufanya uzima wa milele uwezekane kwa watoto wote wa Mungu. Ninashuhudia hivyo, katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.