Mkutano Mkuu
COVID-19 na Mahekalu
Mkutano mkuu wa Aprili 2021


COVID-19 na Mahekalu

Tunzeni maagano na baraka zenu za hekaluni ziwe mbele akilini mwenu na mioyoni mwenu. Bakieni wakweli kwenye maagano ambayo mmeyafanya.

Kaka na dada zangu wapendwa, kwa kweli tumekuwa na karamu ya kiroho. Nina shukrani jinsi gani kwa ajili ya maombi, jumbe, na muziki wa mkutano wote. Asante kwa kila mmoja wenu kwa kujiunga nasi, popote mlipo.

Mapema mwaka jana, kwa sababu ya janga la COVID-19 na hamu yetu ya kuwa raia wema ulimwenguni, tulifanya maamuzi magumu ya kufunga mahekalu yote kwa muda. Katika kipindi cha miezi iliyofuatia, tumehisi kupata mwongozo wa kufungua mahekalu polepole kupitia hatua za tahadhari sana. Mahekalu sasa yanafunguliwa katika awamu nne, yakifuata kikamilifu taratibu za serikali na itifaki za usalama.

Kwa mahekalu katika awamu ya 1, wenzi wanaostahili ambao walikuwa wamepokea endaumenti zao wenyewe hapo awali wanaweza kuunganishwa kama mume na mke.

Kwa mahekalu katika awamu ya 2, ibada zote kwa ajili ya walio hai zinafanywa, ikijumuisha endaumenti ya mtu binafsi, kuunganishwa kwa mume na mke na kuunganishwa watoto kwa wazazi. Hivi karibuni tumefanyia marekebisho vigezo vya awamu ya 2 na sasa vinaruhusu vijana wetu, waumini wapya, pamoja na wengine walio na kibali cha matumizi yenye ukomo kushiriki katika ubatizo kwa niaba, kwa ajili ya mababu zao.

Kwa mahekalu katika awamu ya 3, wale walio na miadi iliyopangwa wanaweza kushiriki siyo tu katika ibada kwa ajili ya walio hai bali pia ibada zote kwa niaba, kwa ajili ya mababu zao waliokufa.

Awamu ya 4 ni kurejea kwenye shughuli za kawaida, za hekalu kikamilifu.

Tunawashukuru kwa uvumilivu wenu na huduma ya kujitolea wakati huu wa kipindi cha mabadiliko na chenye changamoto. Ninaomba kwamba hamu yenu ya kuabudu na kuhudumu katika hekalu itawaka kwa uangavu zaidi sasa kushinda wakati wowote ule.

Yawezekana mnajiuliza ni lini mtaweza kwenda tena hekaluni. Jibu: Hekalu lenu litafunguliwa wakati taratibu za serikali yenu zitakaporuhusu. Wakati janga la COVID-19 katika eneo lenu litakapokuwa katika viwango salama, hekalu lenu litafunguliwa tena. Fanyeni yote mnayoweza kusaidia kushusha idadi ya COVID chini katika eneo lenu ili kwamba fursa zenu za hekalu ziweze kuongezeka.

Kwa sasa, shikeni maagano yenu ya hekaluni na baraka ziwe mbele akilini mwenu na mioyoni mwenu. Bakieni wakweli kwenye maagano ambayo mmeyafanya.

Tunajenga sasa kwa ajili ya baadaye! Mahekalu arobaini na moja kwa sasa yapo kwenye ujenzi au ukarabati. Mwaka uliopita, licha ya janga la ulimwengu, ardhi zilichimbwa kwa ajili ya mahekalu mapya 21!

Tunataka kuleta nyumba ya Bwana hata karibu zaidi na waumini wetu, kwamba waweze kuwa na fursa takatifu ya kuhudhuria hekaluni mara nyingi kadiri hali zao zitakavyoruhusu.

Ninapotangaza mipango yetu ya kujenga mahekalu mengine 20 zaidi, ninawatafakari na kuwasifu waanzilishi—waliopita na wa siku za leo—ambao maisha yao yaliyowekwa wakfu yalisaidia kutengeneza historia hii leo. Hekalu jipya litajengwa katika kila moja ya maeneo yafuatayo: Oslo, Norway; Brussels, Belgium; Vienna, Austria; Kumasi, Ghana; Beira, Mozambique; Cape Town, South Africa; Singapore, Republic of Singapore; Belo Horizonte, Brazil; Cali, Colombia; Querétaro, Mexico; Torreón, Mexico; Helena, Montana; Casper, Wyoming; Grand Junction, Colorado; Farmington, New Mexico; Burley, Idaho; Eugene, Oregon; Elko, Nevada; Yorba Linda, California; na Smithfield, Utah.

Mahekalu ni sehemu muhimu ya Urejesho wa injili ya Yesu Kristo katika utimilifu wake. Ibada za hekaluni zinajaza maisha yetu kwa nguvu na uwezo usiopatikana kwa njia nyingine yoyote. Tunamshukuru Mungu kwa ajili ya baraka hizo.

Tunapohitimisha mkutano huu, tunaelezea tena upendo wetu kwa ajili yenu. Tunaomba kwamba Mungu awamiminie baraka Zake na kumtunza kila mmoja wenu. Kwa pamoja, tunajishughulisha katika huduma Yake takatifu. Kwa ujasiri, acha sote tusonge mbele katika kazi tukufu ya Bwana! Juu ya hili ninaomba katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.

Chapisha