Mkutano Mkuu
“Tazama! Mimi ni Mungu wa Miujiza”
Mkutano mkuu wa Aprili 2021


“Tazama! Mimi ni Mungu wa Miujiza”

Miujiza, ishara, na maajabu ni mengi miongoni mwa wafuasi wa Yesu Kristo leo, katika maisha yako na yangu.

Wapendwa akina kaka na dada zangu, ni fursa iliyoje kusimama mbele yenu leo. Nikiungana na wa wale ambao tayari wamehutibia mkutano huu, ninashuhudia kwenu kwamba Yesu Kristo yu hai. Anaongoza Kanisa Lake; Anazungumza na nabii Wake, Rais Russell M. Nelson na Anawapenda watoto wote wa Baba wa Mbinguni.

Katika Jumapili hii ya Pasaka tunaadhimisha Ufufuko wa Yesu Kristo, Mwokozi na Mkombozi wetu,1 Mungu Mwenye Nguvu, Mfalme wa Amani.2 Upatanisho Wake, uliokamilika kwa Ufufuko Wake baada ya siku tatu katika kaburi la kuazima, unasimama kama muujiza mkubwa katika historia ya mwanadamu. “Kwani tazama,” Yeye alisema, “Mimi ni Mungu; na Mimi ni Mungu wa miujiza.”3

“Je, miujiza imekoma kwa sababu Kristo amepaa mbinguni, na ameketi mkono wa kulia wa Mungu?”4 nabii Mormoni anauliza katika Kitabu cha Mormoni. Anajibu, “La; wala malaika hawajakoma kuwahudumia watoto wa watu.”5

Kufuatia kusulubiwa, malaika wa Bwana alimtokea Mariamu pamoja na wanawake wengine wachache ambao walikuwa wameenda kaburini kupaka mafuta mwili wa Yesu. Malaika alisema:

“Kwa nini mnatafuta aliye hai katika wafu?6

“Hayupo hapa: amefufuka.”7

Nabii wa Kitabu cha Mormoni Abinadi alitangaza juu ya muujiza huo:

“Na kama Kristo hangefufuka kutoka kwa wafu, … hakungekuwa na ufufuo.

“Lakini kuna ufufuo, kwa hivyo kaburi halina ushindi, na uchungu wa kifo umemezwa katika Kristo.”8

Matendo ya miujiza ya Yesu Kristo yalisababisha wanafunzi wa mwanzo kujiuliza: “Ni nani huyu basi hata anaamuru upepo na maji, navyo vyamtii.”9

Mitume wa mwanzo walipomfuata Yesu Kristo na kumsikia akifundisha injili, walishuhudia miujiza mingi. Waliwaona “Vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa na viziwi wasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wakapata kuhubiriwa injili.”10

Miujiza, ishara, na maajabu ni mengi miongoni mwa wafuasi wa Yesu Kristo leo, katika maisha yako na yangu. Miujiza ni matendo ya kiungu, madhihirisho na maonyesho ya nguvu ya Mungu isiyo na kikomo na uthibitisho kwamba Yeye “ni yule yule jana, leo, na hata milele.”11 Yesu Kristo, aliyeziumba bahari, anaweza kuzituliza; Yeye ambaye amewapa vipofu kuona anaweza kuinua macho yetu kuelekea mbinguni; Yeye aliyewatakasa wenye ukoma anaweza kutibu udhaifu wetu; Yeye aliyemponya yule mtu aliyepooza anaweza kutuita tuamke kwa “Njoo, unifuate.”12

Wengi wenu mmeshuhudia miujiza, zaidi ya jinsi mnavyotambua. Inaweza kuonekana kuwa midogo ikilinganishwa na Yesu kufufua wafu. Lakini ukubwa hautofautishi muujiza, ila kwamba tu ulitoka kwa Mungu. Baadhi wanapendekeza kwamba miujiza ni bahati mbaya tu au bahati nzuri. Lakini nabii Nefi aliwahukumu wale ambao “wanadharau uwezo na miujiza ya Mungu, na kujihubiria wao wenyewe hekima yao na elimu yao, ili wafaidike.”13

Miujiza hufanywa kwa nguvu ya kiungu na Yeye aliye “Mwenye nguvu ya kuokoa.”14 Miujiza ni muendelezo wa mpango wa milele wa Mungu; miujiza ni mtitiriko wa maisha kutoka mbinguni kwenda duniani.

Wakati wa majira ya majani kupukutika mwaka uliopita mimi na Dada Rasband tulikuwa njiani kwenda Goshen, Utah, kwa hafla ya matangazo ya ulimwengu mzima ya uso kwa uso yaliyotangazwa kwa watu zaidi ya 600,000 katika lugha 16 tofauti.15 Programu ile ilikuwa ni kufokasi juu ya matukio ya Urejesho wa injili ya Yesu Kristo, kwa maswali yaliyowasilishwa na vijana wakubwa kutoka ulimwenguni kote. Mimi na Dada Rasband binafsi tulikuwa tumepitia maswali hayo; yalitupa nafasi ya kushuhudia juu ya Joseph Smith kama nabii wa Mungu, nguvu ya ufunuo katika maisha yetu, Urejesho unaoendelea wa injili ya Yesu Kristo, na kweli na amri ambazo tunazithamini. Wengi wanaosikiliza leo walikuwa sehemu ya tukio hilo la kimuujiza.

Hapo awali matangazo hayo yalikuwa yafanyike kutokea katika Kijisitu Kitakatifu huko New York, mahali ambapo, kama Joseph Smith alivyoshuhudia “nikawaona Viumbe wawili, ambao mngʼaro na utukufu wao wapita maelezo yote, wakiwa wamesimama juu yangu angani. Mmoja wao akaniambia, akiniita mimi kwa jina na kusema, huku akimwonyesha yule mwingine—Huyu ni Mwanangu Mpendwa. Msikilize Yeye!16 Hilo, akina kaka na akina dada, lilikuwa muujiza.

Picha
Yerusalemu imewekwa Goshen, Utah

Janga la ulimwengu lilitulazimisha kuhamishia matangazo hayo Goshen, Utah, mahali ambapo Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho limeunda upya, kwa ajili ya utengenezaji wa sinema, sehemu ya Yerusalemu ya zamani. Mimi na Dada Rasband tulikuwa ndani ya maili chache kutoka Goshen jioni hiyo ya Jumapili wakati tulipoona moshi mzito ukitoka upande ule wa mwisho wa safari yetu. Moto wa mwituni ulikuwa ukiwaka katika eneo hilo, na tulikuwa na hofu kuwa matangazo yangeweza kuwa hatarini. Hakika, dakika ishirini kabla ya saa 12:00, muda wetu wa matangazo, umeme katika eneo lote ulikuwa umekatika. Hakuna umeme! Hakuna matangazo. Kulikuwa na jenereta moja ambalo baadhi walidhani lingeweza kutupatia umeme, lakini hakukuwa na hakikisho kwamba linaweza kuendesha vifaa vya kisasa vilivyokuwepo.

Picha
Moshi kutoka kwenye moto

Sisi sote tuliokuwa kwenye programu hiyo, ikiwa ni pamoja na wasimulizi, wanamuziki, na mafundi—hata vijana wakubwa 20 wa ndugu wa familia zetu— tuliwekeza kikamilifu katika kile kilichopaswa kufanyika. Niliondoka mbali na machozi na kukanganyikiwa kwao na nikamsihi Bwana kwa ajili ya muujiza. “Baba wa Mbinguni,” niliomba, “mara chache sana nimekuomba muujiza, lakini ninaomba mmoja sasa. Mkutano huu lazima ufanyike kwa ajili ya vijana wetu wakubwa kote ulimwenguni. Tunahitaji umeme ili tuendelee ikiwa ni mapenzi yako. ”

Dakika saba baada ya saa kumi na mbili, kama vile umeme ulivyokatika kwa haraka, ndivyo ulivyorudi tena. Kila kitu kilianza kufanya kazi, kuanzia muziki na vipaza sauti hadi video na vifaa vyote vya kurusha matangazo. Tulikuwa nje ya muda na tulianza kwa kuharakisha. Tulikuwa tumepata muujiza.

Picha
Onyesho la muziki wakati wa tukio la Uso kwa Uso.

Wakati mimi na Dada Rasband tulipokuwa ndani ya gari tukirudi nyumbani jioni ile, Rais na Dada Nelson walituandikia ujumbe huu wa maandishi: “Ron, tunataka mjue kwamba mara tu tuliposikia umeme umekatika, tuliomba kwa ajili ya muujiza.”

Katika maandiko ya siku za mwisho imeandikwa: “Kwani Mimi, Bwana, nimeunyosha mkono wangu ili kuzitakasa nguvu za mbinguni; hamwezi kuona hili sasa, bado kipindi kifupi nanyi mtaona, na kujua kuwa Mimi ndiye, na kwamba nitakuja na kutawala pamoja na watu wangu.”17

Hivyo ndivyo ilivyotokea. Bwana alikuwa ameweka mkono Wake na umeme ukawaka.

Miujiza hufanywa kupitia nguvu ya imani, kama Rais Nelson alivyotufundisha kwa nguvu katika kikao kilichopita. Nabii Moroni aliwasihi watu, “Kwani kama hakuna imani miongoni mwa watoto wa watu Mungu hawezi kufanya miujiza miongoni mwao; kwa hivyo, hakujionyesha mpaka baada ya imani yao.”

Aliendelea:

“Tazama, ilikuwa imani ya Alma na Amuleki ambayo ilisababisha gereza kuanguka chini.

“Tazama, ilikuwa imani ya Nefi na Lehi ambayo ilileta mabadiliko juu ya Walamani, kwamba walibatizwa kwa moto na kwa Roho Mtakatifu.

“Tazama, ilikuwa imani ya Amoni na ndugu zake ambayo ilileta muujiza mkuu miongoni mwa Walamani. …

“Na wala kwa muda wowote hakujawa na yeyote ambaye amefanya miujiza mpaka awe na imani; kwa hivyo waliamini kwanza katika Mwana wa Mungu.”18

Ningeweza kuongeza kwenye mfululizo huo wa maandiko, “Ilikuwa imani ya wasanii vijana wakubwa, wataalamu wa matangazo, viongozi na waumini wa Kanisa, mtume na nabii wa Mungu ambao waliomba muujiza huu mkubwa sana kwamba umeme ulirejeshwa kwenye kijiji hiki kilichopangwa filamu kufanyika huko Goshen, Utah.”

Miujiza inaweza kuja kama jibu kwa maombi. Miujiza si mara zote huwa kile tunachoomba au kutarajia, lakini tunapomtumaini Bwana, Yeye atakuwa pale na Yeye atakuwa sahihi. Atafanya muujiza huo uendane na wakati tunapouhitaji.

Bwana hufanya miujiza ili kutukumbusha sisi juu ya uweza Wake, upendo Wake kwetu, ufiko Wake kutoka mbinguni hadi kwenye uzoefu wetu wa kidunia, na hamu Yake ya kufundisha yale ambayo ni ya thamani zaidi. “Yule aliye na imani kwangu ya kuponywa,” Aliwaambia Watakatifu mnamo 1831, na ahadi hiyo inaendelea hadi hivi leo, “na hakuteuliwa kufa, ataponywa.”19 Kuna sheria zilizowekwa mbinguni, na sisi daima tuko chini ya sheria hizo.

Kuna nyakati tunatarajia muujiza wa kumponya mpendwa wetu, kurudisha nyuma kitendo kisicho cha haki, au kulainisha moyo wenye chuki au nafsi iliyokata tamaa. Tukiangalia vitu kupitia macho ya kidunia, tunataka Bwana aingilie kati, kurekebisha kile kilichovunjika. Kupitia imani, muujiza utakuja, ingawa sio lazima kwenye ratiba yetu au kwa azimio tulilotamani. Je! Hiyo inamaanisha kwamba sisi sio waaminifu au hatustahili kuingilia Kwake kati? Hasha. Sisi ni wapendwa wa Bwana. Alitoa uhai wake kwa ajili yetu, na Upatanisho Wake unaendelea kutuachilia kutokana na mizigo na dhambi pale tunapotubu na kumkaribia.

Bwana Ametukumbusha, “wala njia zenu si njia Zangu.”20 Anatuambia, “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha”21—ondoeni wasiwasi, kukata tamaa, hofu, kutokuamini, wasiwasi kuhusu wapendwa wenu, kwa ndoto zilizopotea au kuvunjika. Amani katikati ya kukanganyikiwa au huzuni ni muujiza. Kumbuka maneno ya Bwana: “Sikusema amani akilini mwako kuhusiana na jambo hili? Ni ushahidi gani mkubwa zaidi unaoweza kupata kuliko kutoka kwa Mungu?”22 Muujiza ni kwamba Yesu Kristo, Yehova Mkuu, Mwana wa Aliye juu Zaidi, anajibu kwa amani.

Kama vile alivyoonekana kwa Mariamu kwenye bustani, akimwita kwa jina, Yeye anatuita sisi tutekeleze imani yetu. Mariamu alikuwa akitafuta kumtumikia na kumtunza. Ufufuko Wake haukuwa kile alichotarajia, lakini ilikuwa ni kulingana na mpango mkuu wa Furaha.

“Shuka msalabani,”23 umati wa wasioamini walimdhihaki Yeye pale Kalvari. Angeweza kufanya muujiza kama huo. Lakini alijua mwisho kuanzia mwanzo, na alikusudia kuwa mwaminifu kwenye mpango wa Baba Yake. Mfano huo haupaswi kupotea kwetu.

Kwetu sisi katika wakati wa majaribu, Amesema, “Tazama majeraha yaliyotobolewa ubavuni mwangu, na pia alama za misumari katika mikono na miguu yangu; kuweni waaminifu, zishikeni amri zangu, na mtaurithi ufalme wa mbinguni.”24 Huo, akina kaka na dada zangu, ndio muujiza ulioahidiwa kwetu sote.

Katika Jumapili hii ya Pasaka, tunapoadhimisha muujiza wa Ufufuko wa Bwana wetu, kama Mtume wa Yesu Kristo, kwa unyenyekevu ninaomba kwamba mtahisi nguvu ya Mkombozi katika maisha yenu, kwamba maombi yenu kwa Baba yetu wa Mbinguni yatajibiwa kwa upendo na kujitolea alikoonesha Yesu Kristo kote katika huduma yake. Ninaomba kwamba msimame imara na kwa uaminifu katika yote yanayokuja. Na ninawabariki kwamba miujiza itendeke kwenu kama tulivyoona sisi katika Goshen—ikiwa ni mapenzi ya Bwana. Tafuteni baraka hizi zitumwazo kutoka mbinguni katika maisha yenu pale “mnapomtafuta huyu Yesu ambaye manabii na mitume wameandika juu yake, kwamba neema ya Mungu Baba, na pia Bwana Yesu Kristo, na Roho Mtakatifu, ambaye anawashuhudia Wao, ipate kuwa nanyi na kuishi ndani yenu milele.”25 Katika Jina la Yesu Kristo, amina.

Chapisha