“Januari 6–12. 1 Nefi 1–7: ‘Nitaenda na Kutenda,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)
“Januari 6–12. 1 Nefi 1–7,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2020
Januari 6–12
1 Nefi 1–7
“Nitaenda na Kutenda”
Nefi aliandika “vitu vya Mungu” (1 Nefi 6:3). Unaposoma maandishi ya Nefi, tilia maanani vitu vya Mungu utakavyovipata, hasa misukumo kutoka kwa Roho.
Andika Misukumo Yako
Kitabu cha Mormoni kinaanza na historia ya familia ya kweli iliyokuwa ikipitia mapambano ya kweli. Ilitokea mnamo 600 K.K, lakini kuna mambo kuhusu historia hii ambayo yanaweza kuonekana yanajulikana kwa familia siku hizi. Familia hii ilikuwa ikiishi katika dunia yenye uovu uliokithiri, Lakini Bwana aliwaahidi ya kwamba kama wangemfuata, angewaongoza hadi mahali palipo salama. Katika safari walikuwa na nyakati nzuri na nyakati mbaya; walipata uzoefu wa baraka nyingi na miujiza, lakini pia walikuwa na mashindano na ugomvi. Ni nadra katika maandiko kupata historia ndefu kama hii kuhusu familia ambayo inajaribu kuishi injili: baba ambaye anapambana kuchochea imani katika familia yake, wana wakiamua ikiwa watamwamini, mama ambaye ana wasiwasi kwa ajili ya usalama wa watoto wake, na ndugu walio na wivu na ugomvi—na wakati mwingine wakisameheana. Kwa ujumla, kuna nguvu ya kweli katika kufuata mifano ya imani ambayo hii familia—licha ya udhaifu wao—walidhihirisha.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kibinafsi
Maandiko ni ya thamani kubwa.
Sura sita za kwanza za Kitabu cha Mormoni zina marejeleo mengi ya vitabu vitakatifu, maandishi matakatifu, na neno la Bwana. Unaposoma 1 Nefi 1–6, unajifunza nini kuhusu kwa nini neno la Mungu lina “thamani kubwa”? (1 Nephi 5:21). Je, vifungu hivi vinakufundisha nini kuhusu maandiko? Unapata nini ambacho kinakutia msukumo kupekua maandiko kwa kujitolea zaidi?
Ona pia “Scriptures Legacy” (video, ChurchofJesusChrist.org).
Kitabu cha Mormoni kinashuhudia juu ya Yesu Kristo.
Kweli katika lengo lililo kwenye ukurasa wake wa jina—kuwashawishi wote kwamba Yesu ndiye Kristo—Kitabu cha Mormoni kinaanza na ono la Lehi la ajabu kumhusu Mwokozi. Je, unajifunza nini kuhusu Yesu Kristo kutokana na kile Lehi alichoona? Ni nini baadhi ya kazi za Mwokozi zilizo “kuu na za ajabu” maishani mwako? (1 Nefi 1:14).
Wakati ninapomtafuta na kumwamini Bwana, Anaweza kulainisha moyo wangu.
Ingawaje Lamani, Lemueli, na Nefi walikua kwa pamoja katika familia moja na kuwa na uzoefu sawa, kuna tofauti kubwa kati ya jinsi walivyoitikia muongozo mtakatifu ambao baba yao alipokea katika sura hii. Unaposoma 1 Nefi 2, tafuta kama unaweza kugundua kwa nini moyo wa Nefi ulikuwa umelainishwa na mioyo ya ndugu zake haikuwa hivyo. Ungeweza pia kufikiria kuhusu muitikio wako mwenyewe kwenye maongozi kutoka kwa Bwana, iwe kupitia Roho Mtakatifu au nabii Wake. Ni wakati gani wewe umehisi Bwana akilainisha moyo wako ili uweze kwa urahisi kukubali mwongozo na ushauri Wake?
Mungu atatayarisha njia ili niweze kutenda mapenzi Yake.
Wakati Bwana alipowaamuru Lehi na familia yake waziendee bamba za shaba kutoka kwa Labani, hakutoa maelezo bayana kuhusu jinsi amri hii ilipaswa kutimizwa. Hii mara nyingi huwa kweli kwenye amri zingine au ufunuo binafsi tunaopokea kutoka kwa Mungu, na hii inaweza kupelekea sisi kuhisi ya kwamba Amehitaji “kitu kigumu” (1 Nefi 3:5). Ni nini kinakutia msukumo kuhusu jibu la Nefi kwa amri ya Bwana, linalopatikana katika 1 Nefi 3:7, 15–16? Kuna chochote ambacho unahisi kutiwa msukumo “kwenda na kutenda”?
Unapojifunza 1 Nefi 1–7, tafuta jinsi ambavyo Mungu aliwatayarishia njia Lehi na familia yake. Jinsi gani amefanya hivi kwako?
Ona pia Mithali 3:5–6; 1 Nefi 17:3; “Utiifu,” Mada za Injili, topics.ChurchofJesusChrist.org; Mkusanyiko wa video za Kitabu cha Mormoni ChurchofJesusChrist.org au the Gospel Library app.
Kukumbuka kazi za Mungu kunaweza kunipa imani ya kutii amri Zake.
Wakati Lamani na Lemueli walipohisi kutaka kunung’unika, kawaida walikuwa na Nefi na Lehi karibu kuwatia moyo na kuwaonya. Unapohisi kunung’unika, kusoma maneno ya Nefi na Lehi kunaweza kuleta ushauri na mtazamo wenye thamani. Ni jinsi gani Nefi na Lehi walijaribu kuwasaidia wanafamilia wao kujenga imani katika Mungu? (ona 1 Nefi 4:1–3; 5:1–8; 7:6–21). Unajifunza nini kutokana na mifano yao ambacho kinaweza kukusaidia wakati unapojaribiwa kunung’unika au kukaidi?
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Familia Nyumbani
Unaposoma maandiko na familia yako, Roho anaweza kukusaidia kujua kanuni zipi zisisitizwe na kujadiliwa ili kukidhi mahitaji ya familia yako. Haya ni baadhi ya mawazo.
1 Nefi 1–7
Kote katika 1 Nefi 1–7, ungeweza kuwatia moyo wanafamilia kutambua mahusiano kati ya wanafamilia wa Lehi na Saria. Nini tunaweza kujifunza kutoka kwenye mahusiano haya ambacho kinaweza kusaidia familia yetu?
1 Nefi 2:20
Kanuni iliyopo katika 1 Nefi 2:20 imerudiwa mara nyingi kote katika Kitabu cha Mormoni. Ni kwa jinsi gani wanafamilia wako wanaweza kuitumia maishani mwao wakati mnapojifunza pamoja kitabu cha Mormoni mwaka huu? Pengine mnaweza kutengeneza bango kwa pamoja lililo na ahadi ya Bwana katika mstari huu na mliweke nyumbani kwenu. Linaweza kuwa ukumbusho kwa ajili ya kujadiliana mara kwa mara jinsi ambavyo mmeona Bwana akiifanikisha familia yenu wakati mlipotii amri Zake. Zingatia kuandika matukio haya kwenye bango.
1 Nefi 2:11–13; 3:5–7
Pengine familia yako ingeweza kufaidika kutokana na kuangalia tofauti kati ya majibu ya Lamani na Lemueli kwa amri za Bwana na majibu ya Nefi. Tunaweza tukajifunza nini kutoka 1 Nefi 2:11–13; 3:5–7 kuhusu kunung’unika? Ni baraka gani huja wakati tunaonyesha imani?
1 Nefi 3:19–20; 5:10–22; 6
Mistari hii yaweza kuipa familia yako msukumo wa kuweka kumbukumbu ya matukio muhimu na uzoefu kutoka kwenye maisha yenu. Pengine mngeweza kuanzisha shajara ya familia, inayofanana na kumbukumbu ambazo Nefi na Lehi waliandika kuhusu uzoefu wao wa kifamilia. Nini unaweza kujumuisha katika kumbukumbu ya familia yako?
1 Nefi 7:19–21
Ni nini kinatuvutia kuhusu mfano wa Nefi katika mistari hii? Ni jinsi gani familia yetu inabarikiwa wakati “tunaposameheana kweli”?
Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.