Njoo, Unifuate
Oktoba 12–18. 3 Nefi 20–26: “Nyinyi Ni Watoto wa Agano”


“Oktoba 12–18. 3 Nefi 20–26: ‘Nyinyi ni Watoto wa Agano,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)

“Oktoba 12–18. 3 Nefi 20–26,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2020

Kristo anawatokea Wanefi

Kielelezo cha Kristo akiwatokea Wanefi na Andrew Bosley

Oktoba 12–18

3 Nefi 20–26

“Nyinyi Ni Watoto wa Agano”

Akizungumza juu ya maandiko, Yesu mara nyingi alitumia neno tafuta (ona 3 Nefi 20:11; 23:1, 5). Unaposoma 3 Nefi 20–26, nini utakachotafuta?

Andika Misukumo Yako

Wakati unaposikia watu wakitumia istilahi kama nyumba ya Israeli, je unahisi kana kwamba wanazungumza kuhusu wewe? Wanefi na Walamani walikuwa wa ukoo halisi wa Israeli—historia yao hata inaanzia Yerusalemu—lakini kwa baadhi yao, Yerusalemu lazima ilionekana kama “nchi iliyo mbali, nchi ambayo hatuijui” (Helamani 16:20). Ndio, walikuwa “tawi la mti wa Israeli,” lakini pia walikuwa “wamepotoka kutoka kwenye kiwiliwili chake” (Alma 26:36; ona pia 1 Nefi 15:12). Lakini wakati Mwokozi alipowatokea, Aliwataka wajue kwamba hawakuwa wamepotea Kwake. “Nyinyi ni wa nyumba ya Israeli,” Alisema, “na ni wa agano” (3 Nefi 20:25). Unaweza kusema kitu sawa na hicho kwako leo hii, kwa yeyote ambaye anabatizwa na kufanya maagano na Yeye pia ni wa nyumba ya Israeli, “wa agano,” bila ya kujali uzao wako au mahali unapoishi. Hii ina maana kwamba, wakati Yesu anapozungumza kuhusu nyumba ya Israeli, Anazungumza kuhusu wewe . Maelekezo ya kubariki “jamaa yote ya dunia” ni kwa ajili yako (3 Nefi 20:27). Mwaliko wa “amka tena, na jivike nguvu yako” ni kwa ajili yako (3 Nefi 20:36). Na ahadi Yake ya thamani, “Wema wangu hautaondoka kutoka kwako, wala agano langu la amani kuondolewa,” ni kwa ajili yako (3 Nefi 22:10).

ikoni ya kujifunza kibinafsi

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kibinafsi

3 Nefi 20–22

Katika siku za mwisho, Mungu atafanya kazi kubwa na ya ajabu.

Mwokozi aliupa umati ahadi za ajabu na akatabiri kuhusu siku zijazo za watu Wake wa agano—na hii inakujumuisha wewe. Rais Russell M. Nelson alisema: “Sisi ni miongoni mwa watu wa agano wa Bwana. Yetu ni heshima ya kushiriki kibinafsi katika utimilifu wa ahadi hizi. Ni wakati wa kusisimua kuwa hai!” (“Kukusanywa kwa Israeli waliotawanyika,” Ensign au Liahona, Nov. 2006, 79).

Tafuta unabii kuhusu siku za mwisho katika maneno ya Mwokozi katika 3 Nefi 20–22. Ni upi kati ya unabii huu ni wa kusisimua zaidi kwako? Ni kitu gani unaweza kufanya kusaidia kutimiza unabii uliopo katika sura hizi?

Kumbuka kwamba 3 Nefi 21:1–7 inaonyesha kujitokeza kwa Kitabu cha Mormoni (“vitu hivi ” katika mistari 2 na 3) ni ishara kwamba ahadi za Mungu tayari zimeanza kutimizwa. Ni zipi ahadi hizo, na ni jinsi gani Kitabu cha Mormoni kinasaidia kuzitimiza?

Ona pia Russell M. Nelson, “Tumaini la Israeli” (ibada duniani kote kwa ajili ya vijana, Juni 3, 2018), broadcasts.ChurchofJesusChrist.org.

3 Nefi 20:10–12; 23; 26:1–12

Mwokozi ananitaka nitafute maneno ya manabii.

Maneno na vitendo vya Yesu kote katika sura hizi vinaonyesha jinsi anavyohisi juu ya maandiko. Unajifunza nini kuhusu maandiko ndani ya 3 Nefi 20:10–12; 23; na 26:1–12? Ni kipi unachopata katika mistari hiii ambacho kinakutia msukumo “kupekua vitu hivi kwa bidii”? (3 Nefi 23:1).

3 Nefi 2224

Mungu ni mwenye rehema kwa wale wanaorudi Kwake.

Katika 3 Nefi 22 na 24, Mwokozi ananukuu maneno kutoka Isaya na Malaki ambayo yamejaa picha ang’avu na milinganisho—mawe ya msingi yenye rangi za kupendeza, makaa ya mawe katika moto, fedha iliyosafishwa, madirisha ya mbinguni. Inaweza kupendeza kutengeneza orodha yake. Je, kila kimoja kinakufundisha nini kuhusu uhusiano kati ya Mungu na watu Wake. Kwa mfano, 3 Nefi 22:4–8 inafananisha Mungu na mume na watu Wake kama mke. Kusoma kuhusu picha hizi kunaweza kukuchochea kufikiria kuhusu uhusiano wako na Bwana. Ni jinsi gani ahadi katika sura hizi zimetimizwa katika maisha yako? (ona hasa 3 Nefi 22:7–8, 10–17; 24:10–12, 17–18).

3 Nefi 25:5–6

Moyo wangu unapaswa kuwageukia mababu zangu.

Kurejea kwa Eliya kulikuwa kumesubiriwa kwa hamu kubwa na Wayahudi kote ulimwenguni kwa kipindi cha karne nyingi. Watakatifu wa Siku za Mwisho wanajua ya kwamba Eliya amekwisharudi, alipomtokea Joseph Smith Katika Hekalu la Kirtland katika mwaka wa 1836 (ona MM 110:13–16). Kazi ya kuigeuza mioyo iwaelekee kina baba—kazi ya historia ya hekalu na familia—inaendelea vyema. Ni uzoefu gani umepata ambao umekusaidia kugeuza moyo wako kuelekea kwa mababu zako?

ikoni ya kujifunza kifamilia

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Familia Nyumbani

Unaposoma maandiko na familia yako, Roho anaweza kukusaidia kujua kanuni zipi zisisitizwe na kujadiliwa ili kukidhi mahitaji ya familia yako. Haya ni baadhi ya mawazo.

3 Nefi 22:2

Baada ya kusoma mstari huu, pengine unaweza kujitengenezea hema nyumbani na uzungumzie vile ambavyo Kanisa ni kama hema nyikani. Inaweza kumaanisha nini “kuongeza urefu wa kamba [zake]” na “kuvikaza vigingi [vyake]”? Ni jinsi gani tunawaalika wengine kutafuta “kimbilio” ndani ya Kanisa? (ona the video “Karibu” kwenye ComeUntoChrist.org).

1:17

3 Nefi 23:6–13

Kama Mwokozi angechunguza maandishi ambayo familia yetu imeyaweka, ni maswali gani Anaweza kuuliza? Kuna matukio yoyote muhimu au uzoefu wa kiroho ambao tunapaswa kuuandika? Sasa waweza kuwa wakati mzuri wa kutengeneza au kuongeza kwenye kumbukumbu ya familia na kushauriana pamoja kuhusu kipi cha kujumuisha. Wanafamilia wadogo wanaweza furahia kupamba maandishi yenu kwa picha au michoro. Kwa nini ni muhimu kuandika kumbukumbu za kiroho za familia zetu?

3 Nefi 24:7–18

Ni kwa jinsi gani tumepata uzoefu wa baraka za kulipa zaka zilizoahidiwa katika mistari hii? Ujumbe wa Mzee David A. Bednar “Madirisha ya Mbinguni” (Ensign au Liahona, Nov. 2013, 17–20) unaweza kuwasaidia wanafamilia kutambua baraka hizi.

3 Nefi 25:5–6

Ni jinsi gani unaweza kuwasaidia wanafamilia yako kugeuza mioyo yao kuelekea kwa baba zao? Pengine unaweza kuwapangia wanafamilia wajifunze kuhusu mmoja wa mababu zenu na kushiriki na wanafamilia wengine kile ambacho walijifunza (ona FamilySearch.org). Au mnaweza kushirikiana kumtafuta babu ambaye anahitaji ibada za hekaluni na kupanga safari ya kwenda hekaluni kufanya ibada hizo.

Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kufundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Ishi ushuhuda wako. “Unafundisha kile ulicho,” Mzee Neal A. Maxwell alifundisha. “Sifa zako zitakumbukwa zaidi … kuliko kweli fulani katika somo fulani” (“Siku Chache Tu” [hotuba kwa walimu wa Mfumo wa Elimu wa Kanisa, Sept. 10, 1982], 2). Kama unataka kufundisha kanuni fulani, fanya juhudi kuishi kanuni hiyo.

Yesu Akisoma kumbukumbu za Wanefi pamoja na Nefi

Leta Hapa kumbukumbu, na Gary L. Kapp