“Septemba 28–Oktoba 11. 3 Nefi 17–19: ‘Tazama, Shangwe Yangu Imetimia,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)
“Septemba 28–Oktoba 11. 3 Nefi 17–19,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2020
Septemba 28–Oktoba 11
3 Nefi 17–19
“Tazama, Shangwe Yangu Imetimia”
Wakati sura za awali katika 3 Nefi zililenga hasa juu ya maneno ya Mwokozi, sura za 17–19 zinaelezea huduma na mafundisho Yake miongoni mwa watu. Unaposoma sura hizi, Roho Mtakatifu anakufundisha nini kuhusu Mwokozi?
Andika Misukumo Yako
Yesu Kristo alikuwa amehudumu kwa siku mzima katika nchi ya Neema, akifundisha injili Yake, akiwapa watu nafasi ya kuona na kugusa alama kwenye mwili Wake uliofufuka, na kushuhudia kwamba alikuwa Mwokozi aliyeahidiwa. Sasa ilikuwa ni wakati wa Yeye kuondoka. Alihitaji kurudi kwa Baba Yake, na alijua kwamba watu walihitaji muda kutafakari alichokuwa amefundisha. Kwa hivyo akiahidi kurudi tena siku iliyofuata, Aliruhusu umati kwenda majumbani kwao. Lakini hakuna aliyeondoka. Hawakusema kile walichokuwa wakihisi, lakini Yesu aliweza kukihisi: walitumaini ange “kaa nao kwa muda mrefu zaidi” (3 Nefi 17:5). Alikuwa na mambo mengine muhimu ya kufanya, lakini nafasi ya kuonyesha huruma kwa kawaida haiji kwa wakati unaofaa, kwa hivyo Yesu alikaa na watu kwa muda kidogo zaidi. Kilichofuata pengine ilikuwa ni mfano wa huduma ya upendo zaidi uliorekodiwa katika maandiko. Wale waliokuwepo waliweza tu kusema kwamba ilikuwa haielezeki (ona 3 Nefi 17:16–17). Yesu Mwenyewe alitoa muhtasari wa mbubujiko huu wa kiroho wa papo kwa papo kwa maneno haya rahisi: “Tazama, Shangwe Yangu Imetimia” (3 Nefi 17:20).
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kibinafsi
Mwokozi ni mfano wangu mkamilifu wa kuhudumia.
Tunajua ya kwamba kulikuwa na takriban watu 2,500 (ona 3 Nefi 17:25) ambao walishuhudia ziara ya kwanza ya Kristo, kama ilivyorekodiwa katika 3 Nefi 11–18. Bado Mwokozi alipata njia ya kuwahudumia Wanefi mmoja mmoja. Je, unajifunza nini kuhusu huduma kutokana na mfano wa Mwokozi katika sura hii? Je, ni mahitaji gani aliyo hudumu kwayo? Tafakari jinsi mfano Wake unavyoweza kukusaidia kuwahudumia wengine.
3 Nefi 17:13–22; 18:15–25; 19:6–9, 15–36
Mwokozi alitufundisha jinsi ya kusali.
Fikiria vile ambavyo ingekua kumsikia Mwokozi akisali kwa ajili yako. Je, angeweza kusema nini kwa niaba yako? Mafundisho Yake na sala katika sura hizi vinaweza kukupa wazo. Unaposoma, unajifunza nini kutokana na mfano wa Kristo ambao unaweza kufanya sala zako ziwe zenye maana zaidi? Ni baraka gani zitokanazo na sala umeziona katika maisha yako?
Ninaweza kushibishwa kiroho ninaposhiriki sakramenti.
Unaposoma 3 Nefi 18:1–12, tafakari jinsi kushiriki sakramenti kunavyoweza kukusaidia “kushiba” kiroho (3 Nefi 18:3–5, 9; ona pia 3 Nefi 20:1–9). Kwa mfano, ungeweza kutengeneza orodha ya maswali ya kuchochea tafakari binafsi wakati unaposhiriki sakramenti, kama vile, “Nina hisi vipi kuhusu Mwokozi na dhabihu Yake kwa ajili Yangu?” “Ni jinsi gani dhabihu Yake inaathiri maisha yangu ya kila siku?” au “Ni nini ninachofanya vyema kama mfuasi, na nini ninaweza kuboresha ?”
Maneno haya kutoka kwa Rais Henry B. Eyring yanaweza kukusaidia kutafakari njia moja ambayo Sakramenti inaweza kukusaidia kushiba Kiroho: “Unapochunguza maisha yako wakati wa ibada ya sakramenti, ninatumai ya kwamba mawazo yako hayatalenga tu kwenye vitu ambavyo hukufanya vyema lakini pia kwenye vitu ambavyo umeweza kufanya vyema—nyakati ambazo umeweza kuhisi ya kwamba Baba wa Mbinguni na Mwokozi walikuwa wamefurahishwa nawe. Waweza hata kuchukua muda wakati wa sakramenti kumuuliza Mungu akusaidie uone mambo haya. … Wakati nimefanya hivi, Roho amenithibitishia ya kwamba wakati bado niko mbali na ukamilifu, hali yangu ya leo ni bora kuliko ilivyokuwa jana. Na hii inanipa ujasiri kwamba, kwa sababu ya Mwokozi, ninaweza hata kuwa bora zaidi kesho” (“Na Daima Kumkumbuka,” Ensign, Feb. 2018, 5).
Wafuasi wa Yesu Kristo hutafuta kipawa cha Roho Mtakatifu.
Fikiria kuhusu sala uliyosema hivi karibuni. Sala zako zinakufundisha nini kuhusu tamaa zako za dhati? Baada ya kushinda siku mzima katika uwepo wa Mwokozi, umati “waliomba wapate kile ambacho walitaka zaidi—kipawa cha Roho Mtakatifu (3 Nefi 19:9). Unaposoma vifungu hivi, tafakari tamaa yako mwenyewe kwa ajili ya ushirika wa Roho Mtakatifu. Unajifunza nini kuhusu kutafuta ushirika wa Roho Mtakatifu?
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Familia Nyumbani
Unaposoma maandiko na familia yako, Roho anaweza kukusaidia kujua kanuni zipi zisisitizwe na kujadiliwa ili kukidhi mahitaji ya familia yako. Haya ni baadhi ya mawazo.
3 Nefi 17
Mnaposoma sura hii kama familia, fikiria kupumzika mara kwa mara ili kuialika familia yako kufikiria kana kwamba wanapitia matukio haya kwa wakati huo. Kwa mfano, unaweza kuuliza maswali kama “Ni mateso gani ungeyaleta kwa Mwokozi kuponywa? “Ungemtaka Yeye aombe nini kwa niaba yako?” au Ni wapendwa gani ungemtaka awabariki?” Kusoma sura hii kunaweza pia kukutia msukumo kusali kwa ajili ya wanafamilia, yako mmoja mmoja, kama Yesu alivyofanya.
3 Nefi 18:1–12
Inamaanisha nini “kushiba” kwa kushiriki sakramenti, na ni kwa jinsi gani tunapata uzoefu huu? Tunajifunza nini kutoka mistari 5–7 kuhusu sababu ya Yesu kutupatia ibada ya sakramenti?
3 Nefi 18:17–21
Je, tunajifunza nini kutoka kwenye aya hizi kuhusu malengo ya sala? Je, ni jinsi gani tunaweza kuboresha nguvu za kiroho za sala zetu, kama watu binafsi na kama familia?
3 Nefi 18:25; 19:1–3
Familia yetu imepata uzoefu gani kupitia kwa injili ambao tungependa kila mtu karibu nasi angeweze pia kuupata? Ni jinsi gani tunaweza kuiga mfano wa watu katika mistari hii na “kufanya kazi sana” (3 Nefi 19:3) kuwaleta wengine kwa Kristo, ili wao pia waweze “kuhisi na kuona ” (3 Nefi 18:25) kile ambacho tumepata katika injili?
Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kufundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.