“Septemba 21–27. 3 Nefi 12–16: ‘Mimi Ndiye Sheria, na Nuru,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)
“Septemba 21–27. 3 Nefi 12–16,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2020
Septemba 21–27
3 Nefi 12–16
“Mimi Ndiye Sheria, na Nuru”
Kuna kanuni nyingi katika 3 Nefi 12–16. Baadhi zimesisitizwa katika mwongozo huu, lakini waweza kupata zingine. Acha Baba wa Mbinguni kupitia Roho Wake, akufundishe kile unachohitaji hivi sasa.
Andika Misukumo Yako
Kama wanafunzi wa Yesu ambao walikusanyika katika mlima kule Galilaya, watu ambao walikusanyika hekaluni pale Neema walikuwa wameishi chini ya sheria ya Musa. Walikuwa wameifuata kwa sababu ilielekeza nafsi zao kwa Kristo (ona Yakobo 4:5), na sasa Kristo alisimama mbele yao, akitangaza sheria ya juu zaidi. Lakini hata wale miongoni mwetu ambao hawajawahi kuishi sheria ya Musa tunaweza kutambua kwamba kiwango ambacho Yesu aliwawekea wanafunzi Wake ni sheria ya juu zaidi. “Ningependa kwamba mngekuwa wakamilifu,” Alitangaza (3 Nefi 12:48). Kama hili linakufanya uhisi umepungukiwa, kumbuka kwamba Yesu alisema, “Heri wale walio masikini rohoni, ambao wanakuja kwangu, kwani ufalme wa mbinguni ni wao” (3 Nefi 12:3). Sheria hii ya juu ni mwaliko—njia nyingine ya kusema “Njooni kwangu na muokolewe” (3 Nefi 12:20). Kama sheria ya Musa, sheria hii inatuelekeza kwa Kristo—Yeye Pekee anayeweza kutuokoa na kutukamilisha. “Tazama,” Alisema, “Mimi Ndiye Sheria, na Nuru.” Nitazameni mimi, na mvumilie hadi mwisho, na mtaishi”(3 Nefi 15:9).
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kibinafsi
Mafundisho ya Mwokozi yananionyesha jinsi ya kuwa mfuasi wa kweli.
Kuna kweli nyingi, maneno ya ushauri, na maonyo katika 3 Nefi 12–14. Hii ni njia moja ya kujifunza na kutumia kile Mwokozi alichofundisha katika sura hizi: Chagua kundi la mistari, na ona kama unaweza kutengeneza muhtasari wa kile ambacho mistari hiyo inafundisha katika kauli moja inayoanza na “Wanafunzi wa kweli wa Yesu Kristo …” Kwa mfano, muhtasari wa 3 Nefi 14:1–5 waweza kuwa “Wanafunzi wa kweli wa Yesu Kristo hawahukumu .” Unaweza kutaka kuchagua mstari kutoka kwenye sura hizi ambao ni muhimu sana kwako na ukariri au unakili na uuweke mahali ambapo unaweza kuuona mara kwa mara. Tafakari jinsi unavyoweza kutumia kile unachojifunza kwa juhudi zako binafsi ili kuwa mwanafunzi bora wa Yesu Kristo.
Ona Pia Mathayo 5–7; Luka 6:20–49.
3 Nefi 12:1–2; 15:23–24; 16:1–6
Heri wao ambao wataamini bila kuona.
Ikilinganishwa na idadi mzima ya watoto wa Mungu, ni wachache ambao wamemuona Mwokozi na kusikia sauti Yake, kama watu wa Neema walivyofanya. Wengi wetu ni zaidi kama watu walioelezwa katika 3 Nefi 12:2; 15:23; na 16:4–6. Je, ni ahadi gani zimetolewa kwa watu kama hao katika mistari hii? Ni kwa jinsi gani ahadi hizi zimetimizwa katika maisha yako?
Ona pia Yohana 20:26–29; 2 Nefi 26:12–13; Alma 32:16–18.
3 Nefi 12:21–30; 13:1–8, 16–18; 14:21–23
Vitendo vya haki havitoshi; moyo wangu pia ni lazima uwe msafi.
Dhamira moja unayoweza kugundua katika sura hizi ni mwaliko wa Mwokozi kuishi sheria ya juu—kuwa wenye haki siyo tu katika vitendo vyetu lakini pia katika mioyo yetu. Tafuta dhamira hii wakati Mwokozi anapozungumzia mabishano (3 Nefi 12:21–26), uovu (3 Nefi 12:27–30), sala (3 Nefi 13:5–8), na mfungo (3 Nefi 13:16–18). Ni mifano gani mingine unayoweza kupata? Unaweza kufanya nini ili kusafisha tamaa za moyo wako badala ya kufokasi tu kwenye matendo vya nje?
Kama nitatafuta “vitu vizuri” kutoka kwa Baba wa Mbinguni, nitavipokea.
Rais Russell M. Nelson alisema: “Je, Mungu kweli anataka kuongea na wewe? Ndiyo! … Ee, kuna mengi zaidi ambayo Baba yako wa Mbinguni anataka uyajue” (“Ufunuo kwa ajili ya Kanisa, Ufunuo kwa ajili ya Maisha Yetu,” Ensign au Liahona, Mei 2018, 95). Unaposoma mwaliko wa Bwana katika 3 Nefi 14:7–11 kuuliza, kutafuta, na kubisha, tafakari “vitu vizuri” ambavyo anaweza kutaka kuviomba. Maandiko ya ziada yafuatayo yanaweza kukusaidia kuelewa jinsi ya kuuliza, kutafuta, na kubisha. Yanaweza pia kusaidia kuelezea ni kwa nini baadhi ya sala hazijibiwi kwa namna unavyotarajia: Isaya 55:8–9; Helamani 10:5; Moroni 7:26–27, 33, 37; na Mafundisho na Maagano 9:7–9.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Familia Nyumbani
Unaposoma maandiko na familia yako, Roho anaweza kukusaidia kujua kanuni zipi zisisitizwe na kujadiliwa ili kukidhi mahitaji ya familia yako. Haya ni baadhi ya mawazo.
3 Nefi 12:48
Ni jinsi gani ujumbe wa Mzee Jeffrey R. Holland “Hatimaye—Muwe Wakamilifu” (Ensign au Liahona, Nov. 2017, 40–42) unatusaidia kuelewa maneno ya Mwokozi katika mstari huu? Pia unaweza kupata msaada katika Moroni 10:32–33.
3 Nefi 12:9, 38–42; 14:3–5, 12
Ni kwa jinsi gani mstari huu unatumika katika uhusiano miongoni mwa wanafamilia? Pengine familia yako inaweza kuweka malengo pamoja ya kuishi kulingana na kanuni hizi kwa uaminifu zaidi.
3 Nefi 13:19–21
Mistari hii ingeweza kushawishi majadiliano kuhusu nini familia yako inathamini. Je, kuna hazina hapa duniani ambazo zinakuzuia kuweka hazina mbinguni? Unaweza kuimarisha hoja hii kwa kuiongoza familia katika kutafuta hazina ya vitu nyumbani kwako ambavyo vinakumbusha wanafamilia kuhusu hazina yenye thamani ya milele.
3 Nefi 14:7–11
Watoto wadogo wanaweza kufurahia mchezo, uliotiwa msukumo na 3 Nefi 14:8–9, ambapo wanaomba kitu na kupokea kitu tofauti kabisa. Mwokozi alitaka tujue nini kuhusu Baba wa Mbinguni wakati aliposhiriki mfano huu?
3 Nefi 14:15–20
Ni “matunda mema” yapi yanatusaidia kujua kwamba Joseph Smith, au Rais wa Kanisa sasa wa hivi, ni nabii wa kweli?
3 Nefi 14:24–27
Fikiria kuhusu njia unazoweza kusaidia familia yako kupata taswira ya fumbo lililo katika mistari hii. Pengine wanafamilia wanaweza kuchora picha, kufanya vitendo, au kujenga vitu kwenye msingi imara na msingi wa mchanga.
Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kufundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.