”Uongofu Ndiyo Lengo Letu,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)
“Uongofu Ndiyo Lengo Letu,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2020
Uongofu Ndiyo Lengo Letu
Dhumuni la kujifunza na kufundisha injili ni kuongeza uongofu wetu na kutusaidia sisi kuwa zaidi kama Yesu Kristo. Kwa sababu hii, tunapojifunza injili, hatutafuti tu taarifa mpya; tunataka kuwa “kiumbe kipya” (2 Wakoritho 5:17). Hii inamaanisha kumtegemea Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo ili watusaidie kubadili mioyo yetu, mitazamo yetu, matendo yetu, na asili yetu hasa.
Lakini aina ya kujifunza injili inayoimarisha imani yetu na kutuongoza kwenye badiliko la kimiujiza la uongofu haitokei yote kwa wakati mmoja. Inakwenda zaidi ya darasani mpaka kwenye moyo na nyumba ya mtu binafsi. Inahitaji uthabiti, juhudi za kila siku kuelewa na kuishi injili. Uongofu wa kweli unahitaji ushawishi wa Roho Mtakatifu.
Roho Mtakatifu hutuongoza kwenye ukweli na anatoa ushahidi juu ya ukweli huo (ona Yohana 16:13). Yeye huangaza akili zetu, huchochea uelewa wetu, na hugusa mioyo yetu kwa ufunuo kutoka kwa Mungu, ni chanzo cha ukweli wote. Roho Mtakatifu husafisha mioyo yetu. Yeye huchochea ndani yetu tamaa ya kuishi katika kweli, na hutunong’onezea njia za kufanya hili. Hakika, “Roho Mtakatifu … atatufundisha [sisi] mambo yote” (Yohana 14:26).
Kwa sababu hizi, katika juhudi zetu za kuishi, kujifunza, na kufundisha injili, lazima kwanza na zaidi ya yote tutafute wenza wa Roho. Lengo hili linapaswa kutawala chaguzi zetu na kuongoza mawazo na matendo yetu. Tunapaswa kutafuta chochote kinachokaribisha ushawishi wa Roho na kukataa chochote kinachofukuza ushawishi huo—kwani tunajua kwamba kama tunaweza kuwa wenye kustahili uwepo wa Roho Mtakatifu, tunaweza pia kustahili kuishi katika uwepo wa Baba wa Mbinguni na Mwanawe, Yesu Kristo.