“JanuarI 7–13. Mathayo 1; Luka 1: ‘Na Iwe Kwangu kama Ulivyosema’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya 2019 (2019)
“JanuarI 7–13. Mathayo 1; Luka 1,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya 2019
Januari 7–13
Mathayo 1; Luka 1
“Na Iwe Kwangu kama Ulivyosema”
Unaposoma na kutafakari Mathayo 1 na Luka 1, andika misukumo ya kiroho unayopokea. Je, ni mafundisho gani ya injili unayopata hapa? Je, ni ujumbe gani utakuwa wa thamani kubwa kwako na kwa familia yako? Mawazo ya kujifunza katika muhtasari huu yanaweza kukusaidia kugundua utambuzi wa ziada.
Andika Misukumo Yako
Kutokana na mtazamo wa maisha ya kidunia, ilikuwa haiwezekani. Bikira kupata mimba. Wala mwanamke tasa ambaye alipita umri wa miaka ya kuzaa mtoto. Lakini Mungu alikuwa na mpango wa kuzaliwa kwa Mwanawe na Yohana Mbatizaji, hivyo wote wawili Mariamu na Elisabeti, kinyume na uwezekano wote wa kidunia, wakawa akina mama. Inaweza kusaidia kukumbuka uzoefu wao wa kimuujiza pale tunapokabiliwa na jambo linaloonekana kutowezekana. Je, sisi tunaweza kushinda udhaifu wetu? Je, tunaweza kugusa moyo wa mwanafamilia asiye na mwitikio? Gabrieli kwa urahisi angeweza kuwa anaongea nasi wakati alipomkumbusha Mariamu,”Kwa Mungu hakuna lisilowezekana” (Luka 1:37). Na jibu la Mariamu linaweza kuwa letu wakati Mungu anafunua mapenzi Yake: “Na Iwe kwangu kama ulivyosema” (Luka 1:38).
Mawazo ya Kujifunza Maandiko Binafsi
Je, Mathayo na Luka walikuwa kina nani?
Mathayo alikuwa mtoza ushuru wa Kiyahudi, ambaye Yesu alimwita kama mmoja wa Mitume Wake (ona Mathayo 10:3; ona pia Kamusi ya Biblia, “Watoza ushuru”). Mathayo aliandika injili yake hasa kwa Wayahudi wenzake; kwa hivyo, alichagua kusisitiza unabii wa Agano la Kale kuhusu Masiya ambao ulitimizwa kupitia maisha na huduma ya Yesu.
Luka alikuwa myunani (si-Myahudi) tabibu aliyesafiri pamoja na Mtume Paulo. Aliandika injili yake baada ya kifo cha Mwokozi hasa kwa hadhira isiyokuwa ya Wayahudi. Alishuhudia juu ya Yesu Kristo kama Mwokozi wa wote Wayunani na Wayahudi. Aliandika maelezo ya matukio yaliyoonekana kwa macho katika maisha ya Mwokozi, na alijumuisha hadithi zaidi zilizohusu wanawake ikilinganishwa na injili zingine.
Ona pia Kamusi ya Biblia, “Injili,” “Mathayo,” “Luka.”
Je, kwa nini Mwokozi alihitajika kuzaliwa na mama mwenye mwili unaokufa na Baba mwenye mwili usiokufa?
Rais Russell M. Nelson alielezea kwamba Upatanisho wa Yesu Kristo “ulihitaji dhabihu ya kipekee kwa kiumbe asiyekufa ambaye hayuko chini ya mauti. Tena Yeye alilazimika kufa na kuchukua tena Mwili wake. Mwokozi alikuwa ni mtu pekee ambaye angeweza kutimiza hili. Kutoka kwa mama yake alirithi uwezo wa kufa. Kutoka kwa Baba Yake alipata uwezo juu ya kifo” (“Uthabiti katikati ya Mabadiliko,” Ensign, Nov. 1993, 34).
Baraka za Mungu huja kwa wakati Wake Yeye.
Kwa sababu zozote zile, muda wa Mungu ilimaanisha kwamba baraka ambayo Elisabeti na Zakaria walitamani, ya kupata mtoto, ilikuja baadaye sana kuliko walivyotegemea. Kama ukijikuta unapaswa kusubiri baraka, au kama inaonekana kwamba Mungu hasikii maombi yako, hadithi ya Elisabeti na Zakaria yaweza kuwa ukumbusho kwamba Mungu hajakusahau. Anao mpango kwa ajili yako, na daima hutimiza ahadi zake kwa Watakatifu Wake watiifu. Kama Mzee Jeffrey R. Holland alivyoahidi, “Baadhi ya baraka huja mapema, baadhi huchelewa, na baadhi haziji mpaka mbinguni; lakini kwa wale wanaokumbatia injili ya Yesu Kristo, zinakuja” (“Kuhani Mkuu wa Vitu Vizuri Vijavyo,” Ensign, Nov. 1999, 38). Je, ni kwa jinsi gani Zakaria na Elisabeti walibaki waaminifu? (ona Luka 1:5–25, 57–80). Je, uko katika hali ya kusubiria baraka? Je, unahisi Bwana anatarajia ufanye nini wakati ukisubiri?
Je, ni ujumbe gani mwingine Bwana anaweza kuwa nao kwa ajili yako katika hadithi hii?
Walio waaminifu kwa hiari hujiweka chini ya mapenzi ya Mungu.
Kama Mariamu, wakati mwingine tunakuta kwamba mipango ya Mungu kwa ajili ya maisha yetu ni tofauti na kile tulichopanga. Je, unajifunza nini kutoka kwa Mariamu kuhusu kukubali mapenzi ya Mungu? Katika majedwali yafuatayo, andika maelezo kutoka kwa malaika na kwa Mariamu (ona Luka 1:26–38), sambamba na ujumbe unaopata katika maelezo yao:
Maneno ya malaika kwa Mariamu |
Ujumbe kwa ajili yangu |
---|---|
Maneno ya malaika kwa Mariamu “Bwana yu pamoja nawe” (mstari 28). | Ujumbe kwa ajili yangu Bwana anajua hali na masumbuko yangu. |
Maneno ya malaika kwa Mariamu | Ujumbe kwa ajili yangu |
Maneno ya malaika kwa Mariamu | Ujumbe kwa ajili yangu |
Majibu ya Mariamu |
Ujumbe kwa ajili yangu |
---|---|
Majibu ya Mariamu “Litakuwaje neno hili?” (mstari 34). | Ujumbe kwa ajili yangu Ni SAWA kuuliza maswali ninapokosa kuelewa. |
Majibu ya Mariamu | Ujumbe kwa ajili yangu |
Majibu ya Mariamu | Ujumbe kwa ajili yangu |
Unaposoma kuhusu mfano wa uadilifu wa Yusufu katika Mathayo1:18–25, unajifunza nini kuhusu kukubali mapenzi ya Mungu? Ungejifunza nini kutokana na uzoefu wa Zakaria na Elisabeti? (ona Luka 1).
Ona pia Mosia 3:19; Luka 22:42; Helamani 10:4–5; Kamusi ya Biblia, “Gabrieli.”
Mariamu hushuhudia kuhusu huduma ya Yesu Kristo.
Maneno ya Mariamu katika Luka 1:46–55 yalitabiri vipengele vya huduma ya Mwokozi. Je, unajifunza nini kuhusu Yesu Kristo kutokana na maneno ya Mariamu? Je, ni umaizi gani wa ziada unapata kuhusu baraka ambazo Mwokozi hutoa kwa kulinganisha mistari hii na maneno ya Hana katika 1 Samueli 2:1–10 na mahubiri ya Mlimani ya Yesu katika Mathayo 5:4–12? Je, Roho anakufundisha nini unapotafakari umaizi huu?
Mawazo ya Kujifunza Maandiko Kwa Familia na Jioni ya Familia Nyumbani.
Unaposoma maandiko na familia yako, Roho anaweza kukusaidia kujua kanuni zipi zisisitizwe na kujadiliwa ili kukidhi mahitaji ya familia yako. Haya ni baadhi ya mapendekezo:
Wakati familia yako ikisoma historia ya nasaba ya Yesu, unaweza kuelezea kwamba maelezo yanatoa asili ya nasaba Yake ya kifalme kuanzia Yusufu kurudi nyuma mpaka kwa Mfalme Daudi. Nasaba hii ilikuwa muhimu kwa sababu ilikuwa imetabiriwa kwamba Masiya angekuja kupitia nasaba ya Daudi (ona Yeremia 23:5–6). Hii yaweza kuwa nafasi nzuri ya kujadili historia yako mwenyewe ya familia na kusimulia baadhi ya hadithi kuhusu mababu zako. Je, ni kwa namna gani kujua kuhusu historia ya familia yako huibariki familia yako?
Je, ni kwa nini watu katika mistari hii wamekuwa wenye woga? Je, ni kitu gani hutusababisha kusikia woga? Je, ni kwa namna gani Mungu amekuwa akituambia “usiogope”?
Ili kuwasaidia wanafamilia yako kujenga imani kwamba “kwa Mungu hakuna lisilowezekana,” mngeweza kupekua Luka 1 pamoja na kutafuta mambo ambayo Mungu aliyafanya ambayo yangeweza kufikiriwa kama yasiyowezekana. Je, ni hadithi gani zingine wangeweza kushiriki—kutoka kwenye maandiko au maisha yao wenyewe—ambapo Mungu alifanya mambo yaliyoonekana kutowezekana? Kutafuta kutoka kwenye Kitabu cha Sanaa ya Injili kunaweza kuwasaidia kufikiria mawazo.
Kwa mawazo zaidi juu ya kufundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii ndani ya Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.