Njoo, Unifuate
Desemba 31–Januari 6 Tunawajibika kwa Kujifunza Kwetu Wenyewe


Desemba 31–Januari 6. Tunawajibika kwa Kujifunza Kwetu Wenyewe,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya 2019 (2019)

Desemba 31–Januari 6. Tunawajibika kwa Kujifunza Kwetu Wenyewe,” Njoo Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2019

Picha
familia ikitazama picha katika albamu

Desemba 31–Januari 6

Tunawajibika kwa Kujifunza Kwetu Wenyewe

Madhumuni ya Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia ni kuwasaidia kuja kwa Kristo na kuwa waongofu zaidi katika injili Yake. Nyenzo hii inaweza kuwasaidia kuelewa maandiko na kupata ndani yake nguvu ya kiroho mnayohitaji wewe na familia yako. Kisha, katika madarasa yenu Kanisani, mtakuwa mmejiandaa kushiriki umaizi na kuwahimiza Watakatifu wenzenu katika juhudi zao za kumfuata Kristo.

Andika Misukumo Yako

Mnatafuta nini? Yesu aliwauliza wanafunzi Wake (Yohana 1:38). Unaweza kujiuliza swali kama hilo—kwani kile unachopata katika Agano Jipya mwaka huu kwa kiasi kikubwa kitategemea kile unachotafuta. “Tafuteni, nanyi mtaona” ni ahadi ya Mwokozi (Mathayo 7:7). Kwa hivyo uliza maswali yanayokuja akilini mwako wakati unapojifunza, na kisha tafuta majibu kwa bidii. Katika Agano Jipya utasoma kuhusu uzoefu wenye nguvu wa kiroho wa wafuasi wa Yesu Kristo. Kama mfuasi mwaminifu wa Mwokozi, unaweza kuwa na uzoefu wako wenye nguvu wa kiroho unapokubali mwaliko wa Mwokozi, unaopatikana kote kwenye chuo hiki kitakatifu, “Njoo, unifuate” (Luka 18:22).

Picha
Ikoni ya kujifunza binafsi

Mawazo ya Kujifunza Maandiko Binafsi

Kwa kweli kujifunza kutoka kwa Mwokozi, lazima mimi nikubali mwaliko Wake, “Njoo, unifuate.”

Mwaliko wa Mwokozi, “Njoo, Unifuate,” ni kwa wote—iwe sisi ni wapya kwenye njia ya ufuasi au tumeitembea maisha yetu yote. Huu ulikuwa ni mwaliko Wake kwa kijana mdogo tajiri ambaye alikuwa akijitahidi kushika amri (ona Mathayo 19:16–22). Alichojifunza—na ambacho wote tunapaswa kujifunza—ni kwamba kuwa mfuasi humaanisha kutoa nafsi zetu zote kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Tunaendelea katika ufuasi wetu tunapoainisha kile tunachokosa, kubadilika, na kutafuta kwa ukamilifu zaidi kuwafuata.

Kujifunza kutoka kwa Mwokozi huanza tunapojitahidi kuelewa kile Alichofundisha. Kwa mfano, jinsi gani uelewa wako kuhusu msamaha unaongezeka unapotafiti yafuatayo?

Mafundisho ya Mwokozi (ona Mathayo 6:14– 15; 18:21–35)

Mfano kutoka katika maisha Yake (ona Luka 23:33–34)

Hata hivyo, kujifunza hakukamiliki mpaka tunapomfuata Mwokozi kwa kuishi kile alichofundisha. Je, unawezaje kuwa mwenye kusamehe zaidi?

Kama unataka kujifunza zaidi, jaribu kitendo hiki kwa kanuni nyingine ya injili, kama vile upendo au unyenyekevu.

Ninawajibika kwa kujifunza kwangu mwenyewe.

Mzee David A. Bednar alifundisha: “Kama wanafunzi, wewe na mimi tuwe wenye kushughulika na kuwa watendaji wa neno na si tu wasikiaji ambao tunatendewa tu. Je, wewe na mimi ni mawakala wanaotenda na kutafuta kujifunza kwa imani, au tunasubiri kufundishwa na kutendewa? … Mwanafunzi anayetumia haki yake ya kujiamulia kwa kutenda kulingana na kanuni sahihi hufungua moyo wake kwa Roho Mtakatifu na hualika mafundisho Yake, nguvu yake ya kushuhudia, na ushahidi wenye kuthibitisha. Kujifunza kwa imani kunahitaji kujikaza kiroho, kiakili, na kimwili na sio tu upokeaji baridi’ (“Tafuta Kujifunza kwa Imani,” Ensign, Sept. 2007, 64).

Inamaanisha nini kuwajibika kwa kujifunza kwako mwenyewe? Angalia uwezekano wa majibu katika maelezo ya Mzee Bednar na katika maandiko yafuatayo: Yohana 7:17; 1 Wathesalonike 5:21; Yakobo 1:5–6, 22; 2:17; 1 Nefi 10:17–19; 2 Nefi 4:15; Alma 32:27; na Mafundisho na Maagano 18:18; 58:26–28; 88:118. Je, unajisikia kuongozwa kufanya nini zaidi katika kujishughulisha na kujifunza injili?

Nahitaji kujua ukweli mwenyewe.

Pengine unawajua watu ambao hawajawahi kuonekana kupoteza imani yao, bila kujali kinachotokea katika maisha yao. Wanaweza kukukumbusha kuhusu wanawali watano wenye busara katika fumbo la Mwokozi (ona Mathayo 25:1–13). Ambacho unaweza usikione ni jitihada zao za bidii katika kuimarisha shuhuda zao juu ya ukweli. Wote lazima tutafute kwa bidii kuimarisha shuhuda zetu kwa sababu, kama wanawali wapumbavu walivyojifunza, hatuwezi kuazima uongofu kutoka kwa mtu mwingine.

Je, tunapataje na kulea shuhuda zetu wenyewe? Andika mawazo yako unapotafakari maandiko yafuatayo: Luka 11:9–13; Yohana 5:39; Yohana 7:14–17; Matendo 17:10–12; 1 Wakorintho 2:9–11; na Alma 5:45–46. (Ona pia “Ushuhuda,” Mada za Injili, topics.lds.org.)

Picha
msichana kando ya njia

Kila mmoja wetu lazima apate ushuhuda wake mwenyewe.

Je, ninapaswa kufanya nini ikiwa nina maswali?

Unapotafuta ufahamu wa kiroho, maswali yatakujia akilini. Kanuni zifuatazo zinaweza kukusaidia kushughulikia maswali katika njia zinazojenga imani na ushuhuda:

  1. Tafuta uelewa kupitia vyanzo vitakatifu vilivyoteuliwa. Mungu ni chanzo cha kweli yote, na Anafunua ukweli kupitia Roho Mtakatifu, maandiko, na manabii na mitume Wake.

  2. Tenda kwa Imani. Kama majibu hayaji mara moja, amini kwamba Bwana atakufunulia majibu kwa wakati sahihi. Kwa wakati huu, endelea kuishi kwenye ukweli ambao tayari unaujua.

  3. Kuwa na mtazamo wa milele. Jaribu kuona mambo kama Bwana anavyoyaona, si kama ulimwengu unavyoyaona. Yatazame maswali yako katika muktadha wa mpango wa wokovu wa Baba yetu wa Mbinguni.

Picha
Ikoni ya kujifunza kwa familia.

Mawazo ya Kujifunza Maandiko Kwa Familia na Jioni ya Familia Nyumbani.

Unaposoma maandiko na familia yako, Roho anaweza kukusaidia kujua kanuni zipi zisisitizwe na kujadiliwa ili kukidhi mahitaji ya familia yako. Haya ni baadhi ya mapendekezo:

Mathayo 13:1-23

Njia moja kuu ya kusaidia familia yako kujiandaa kujifunza kutoka katika Agano Jipya mwaka huu ni kurejea fumbo la mpanzi. Familia yako inaweza kufurahia kuangalia aina tofauti za udongo karibu na nyumbani kwenu kupata taswira ya aina ya udongo iliyoelezewa katika fumbo. Je, tunaweza kufanya nini ili kuendeleza “udongo mzuri” nyumbani kwetu? (Mathayo 13:8).

Wagalatia 5:22–23; Wafilipi 4:8

“Tunawashauri wazazi na watoto kuvipa kipaumbele sala ya familia, jioni ya familia nyumbani, kujifunza injili na maelekezo yake, na burudani nzuri za kifamilia. Licha ya shughuli au mahitaji mengine kuwa yenye kustahili na sahihi nyumbani katu zisiruhusiwe kuchukua nafasi ya kazi takatifu zilizopangwa kitakatifu ambazo ni wazazi na familia tu wanaoweza kuzitekeleza.” (“Barua kutoka Urais wa Kwanza,” Liahona, Dec. 1999, 1).

Mwanzo wa mwaka ni wakati mzuri kufanya baraza la familia kuhusu kufanya nyumba yenu iwe zaidi kitovu cha injili. Je, ni mawazo gani huja akilini unaposoma baraka na ushauri katika Wagalatia 5:22–23 na Wafilipi 4:8? Pengine ungeweza kutengeneza mabango ya kuweka kuzunguka nyumba ilikuwa kujikumbusha malengo yenu.

Kwa mawazo zaidi juu ya kufundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii ndani ya Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.

Kuboresha Kujifunza Binafsi

Tafuta mafundisho. Mafundisho ya injili ni ukweli usiobadilika milele. Rais Boyd K. Packer alitangaza kwamba “injili ya kweli, iliyoeleweka, hubadili mitazamo na tabia” (“Watoto Wadogo,” Ensign, Nov. 1986, 17). Pale wewe na familia yako mnapojifunza maandiko, tafuta kweli ambazo zitawasaidia kuishi zaidi kama Mwokozi.

Picha
Yesu Kristo

Nuru ya Ulimwengu, na Brent Borup

Picha
Kristo akitoka kaburini

Amefufuka, na Del Parson

Chapisha