Njoo, Unifuate
Agosti 5–11. Warumi 1–6: ‘Uweza wa Mungu uuletao Wokovu’


“Agosti 5–11. Warumi 1–6: ‘Uweza wa Mungu uuletao Wokovu’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya 2019 (2019)

“Agosti 5–11. Warumi 1–6,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2019

Picha
Paulo akiandika waraka

Agosti 5–11

Warumi 1–6

“Uweza wa Mungu uuletao Wokovu”

Kuandika misukumo itakusaidia kukumbuka kile ambacho Roho anakufundisha. Fikiria pia kuandika jinsi unavyojisikia kuhusu misukumo hii.

Andika Misukumo Yako

Wakati Paulo alipoandika Waraka wake kwa waumini wa Kanisa la Rumi, ambao walikuwa ni makundi mbalimbali ya Wayahudi na Wayunani, Kanisa la Yesu Kristo lilikuwa limekua zaidi ya kundi dogo la waaminio kutoka Galilaya. Karibia miaka 20 baada ya Ufufuko wa Mwokozi, kulikuwa na mikusanyiko ya Wakristo karibu kila mahali ambako Mitume wangeweza kusafiri bila shaka yoyote—ikijumuisha Rumi, mji mkuu wa ufalme mkubwa. Lakini wakati hadhira ya karibu ya Paulo ilikuwa Watakatifu Warumi, ujumbe wake ni kwa watu wote, na inajumuisha sisi sote leo: “Injili ya Kristo … ni uweza wa Mungu uuletao wokovu kwa kila aaminiye” (Warumi 1:16, msisitizo umeongezwa).

Picha
ikoni ya kujifunza binafsi

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Binafsi

Warumi–Filemoni

Nyaraka ni nini na zimepangiliwa kwa namna gani?

Nyaraka ni barua zilizoandikwa na viongozi wa Kanisa kwa Watakatifu katika maeneo tofauti ya ulimwengu. Mtume Paulo aliandika nyingi za nyaraka hizi katika Agano Jipya—akianzia na Warumi na kumaliza na Filemoni. Nyaraka zake zimepangwa kwa urefu. Japokuwa Warumi ni waraka wa kwanza katika Agano Jipya, ulikuwa hasa umeandikwa karibia na mwisho wa safari za Paulo za kimisionari. Kwa maelezo zaidi kuhusu nyaraka, ona Kamusi ya Biblia, “Nyaraka za Paulo.”

Warumi 1–6

Ninapoonyesha imani kwa Mwokozi kwa kutii amri Zake, ninahesabiwa haki kupitia neema Yake.

Maana zifuatazo zinaweza kukusaidia kuelewa vizuri zaidi Waraka kwa Warumi:

Sheria:Paulo alipoandika juu ya “sheria,” alikuwa akimaanisha sheria ya Musa. Hali kadhalika, neno “matendo” katika maandishi ya Paulo mara nyingi lilihusu taratibu na matambiko ya sheria ya Musa. Paulo alitofautisha sheria hii na “sheria ya imani” (ona Warumi 3:27–31), au mafundisho ya Yesu Kristo, ambaye ndiye chanzo halisi cha wokovu wetu.

Kutahiri, kutokutahiri:Hapo kale, kutahiri kulikuwa ni ishara au alama ya agano Mungu alilofanya na Ibrahimu. Paulo alitumia neno “kutahiri” kutaja Wayahudi (watu wa agano) na “kutokutahiri” kutaja Wayunani (wale ambao siyo wa agano la Ibrahimu). Kutahiri siyo lazima tena kama ishara ya agano la Mungu kwa watu Wake (ona Matendo ya Mitume 15:23–29).

Kujihesabia haki, kuhesabu haki, kuhesabiwa haki:Maneno haya yanahusu ondoleo, au kusamehewa, dhambi. Tunapohesabiwa haki, tunasamehewa, tunatajwa wasio na hatia, na kuondolewa kwenye adhabu ya milele kwa dhambi zetu. Kama Paulo alivyoelezea, hii inawezekana kupitia Yesu Kristo (ona Mwongozo wa Maandiko, “Kuhesabia haki, Kuhesabu haki,” scriptures.lds.org; ona pia D. Todd Christofferson, “Kuhesabia haki na Kutakasa,” Ensign, Juni 2001, 18–25). Katika Warumi, maneno kama adilifu na enye maadili yanaweza kuonekana kama maneno yenye maana sawa na maneno haki na kuhesabia haki.

Neema:Neema ni “msaada mtakatifu … au nguvu, zinazotolewa kupitia huruma na upendo wa Yesu Kristo.” Kupitia neema, watu wote watafufuliwa na kupokea mwili usiokufa. Kwa kuongezea, “Neema ni nguvu ya kuwezesha ambayo inaruhusu wanaume na wanawake kujipatia uzima wa milele na kuinuliwa baada ya kutumia jitihada zao bora.” Hatupati neema kupitia jitihada zetu; bali, ni neema ambayo hutupatia “nguvu na msaada ili kufanya matendo mema ambayo [sisi] pengine tusingeweza kudumisha” Kamusi ya Biblia, “Neema”; ona pia Dieter F. Uchtdorf, “Zawadi ya Neema,” Ensign au Liahona, Mei 2015, 107; 2 Nefi 25:23).

Warumi 2:17–29

Matendo yangu ya nje lazima yaakisi kuongezeka kwa uongofu wa ndani.

Mafundisho ya Paulo huonyesha kwamba baadhi ya Wakristo wa Kiyahudi katika Rumi bado waliamini kwamba utiifu kwa ibada na matambiko ya sheria ya Musa ulileta wokovu. Hii inaweza kuonekana kama tatizo ambalo halihusiki tena kwani hatuishi kwa sheria ya Musa. Lakini unaposoma maandiko ya Paulo, hasa Warumi 2:17–29, fikiria kuhusu jitihada zako mwenyewe za kuishi injili. Je, matendo yako ya nje, kama vile kupokea sakramenti au kuhudhuria hekaluni, hukuongoza kwenye uongofu na kuimarisha imani yako katika Kristo? (ona Alma 25:15–16). Ni kwa jinsi gani unaweza kuhakikisha kwamba matendo yako ya nje yanakupeleka kwenye badiliko la moyo?

Ona pia Dallin H. Oaks, “Changamoto ya Kuwa,” Ensign, Nov. 2000, 32–34.

Warumi 3:10–315

Kupitia Yesu Kristo, ninaweza kusamehewa dhambi zangu.

Baadhi ya watu wanaweza kujisikia kuvunjika moyo na tangazo la Paulo la kijasiri kwamba “hakuna mwenye haki, hata mmoja” (Warumi 3:10). Lakini pia kuna ujumbe wa matumaini katika Warumi. Utafute katika sura 3 na 5, na fikiria ni kwa nini kukumbuka kwamba “wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu” (Warumi 3:23) ni hatua muhimu kuelekea kwenye kujifunza “kufurahi katika tumaini” kupitia Yesu Kristo (Warumi 5:2).

Warumi 6

Injili ya Yesu Kristo hunialika “kuenenda katika upya wa uzima.”

Paulo alifundisha kwamba injili inapaswa kubadilisha jinsi tunavyoishi. Ni kauli zipi katika Warumi 6 ungetumia kumsaidia mtu kuelewa ni jinsi gani injili imekusaidia “kuenenda katika upya wa uzima”? (mstari 4). Ni uzoefu gani binafsi ungeweza kusimulia?

Picha
ikoni ya kujifunza kifamilia.

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Familia Nyumbani.

Unaposoma maandiko na familia yako, Roho anaweza kukusaidia kujua kanuni zipi zisisitizwe na kujadiliwa ili kukidhi mahitaji ya familia yako. Hapa kuna baadhi ya mapendekezo:

Warumi 1:16–17

Ni kwa jinsi gani tunaweza kuonyesha kwamba “hatuionei haya injili ya Yesu Kristo”?

Warumi 3:23–28

Baadhi ya watu wanaweza kusema kwamba kwa sababu tunahesabiwa haki tu kwa neema ya [Mungu]” (Tafsiri ya Joseph Smith, Warumi 3:24 [in Warumi 3:24, rejeo a]), hakuna kinachohitajika kwetu ili kupokea neema. Hata kama kamwe hatuwezi kufanya vya kutosha ili “kupokea” neema ya Mungu, Mungu hututaka kufanya mambo fulani ili kuipokea hiyo neema. Je, tunaweza kufanya nini ili kupokea neema?

Warumi 5:3–5.

Ni taabu zipi ambazo tumezipitia? Ni kwa jinsi gani taabu hizi zilitusaidia kuendeleza uvumilivu, uzoefu, na tumaini?

Warumi 6:3–6.

Ni nini Paulo alisema katika mistari hii kuhusu ishara ya ubatizo? Pengine familia yako inaweza kupanga kuhudhuria ubatizo unaokuja. Au mmoja katika familia yako anaweza kuonyesha picha au kumbukumbu kutoka kwenye ubatizo wake. Ni kwa jinsi gani kufanya na kushika maagano yetu ya ubatizo hutusaidia “kuenenda katika upya wa uzima”?

Picha
Mwanaume akimbatiza mwenzake ziwani

Ubatizo huashiria kuanza maisha mapya kama mfuasi wa Kristo.

Kwa mawazo zaidi juu ya kufundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii ndani ya Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.

Kuboresha Kujifunza Binafsi

Uliza Maswali Unapojifunza. Unapojifunza maandiko, maswali yanaweza kuja akilini. Tafakari maswali haya na tafuta majibu. Kwa mfano, katika Warumi 1–6 unaweza kutafuta majibu kwa swali “Neema ni nini?”

Chapisha