Agano Jipya 2023
Agosti 7–13. Warumi 1–6: “Nguvu za Mungu katika Ukombozi”


“Agosti 7–13. Warumi 1–6: ‘Nguvu za Mungu katika Ukombozi’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya 2023 (2022)

“Agosti 7–13. Warumi 1–6,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2023

Picha
Paulo akiandika waraka

Agosti 7–13

Warumi 1–6

“Nguvu za Mungu katika Ukombozi”

Kuandika misukumo itakusaidia kukumbuka kile ambacho Roho anakufundisha. Fikiria pia kuandika jinsi unavyohisi kuhusu misukumo hii.

Andika Misukumo Yako

Wakati Paulo alipoandika waraka wake kwa waumini wa Kanisa la Rumi, ambao walikuwa ni makundi mbalimbali ya Wayahudi na Wayunani, Kanisa la Yesu Kristo lilikuwa limekua zaidi ya kundi dogo la waaminio kutoka Galilaya. Karibia miaka 20 baada ya Ufufuko wa Mwokozi, kulikuwa na mikusanyiko ya Wakristo karibu kila mahali ambapo Mitume wangeweza kusafiri bila shaka yoyote—ikijumuisha Rumi, mji mkuu wa ufalme wenye nguvu. Bado, ukilinganisha na ukubwa wa ufalme wa Rumi, Kanisa lilikuwa dogo na kila wakati likiteswa. Katika hali kama hizo, baadhi “waliionea haya injili ya Kristo”—lakini, bila shaka, si Paulo. Alijua na kushuhudia kwamba nguvu ya kweli, “nguvu ya Mungu katika Ukombozi,” inapatikana katika injili ya Yesu Kristo (Warumi 1:16).

Picha
ikoni ya kujifunza binafsi

Mawazo kwa Ajili ya Kujifunza Binafsi Maandiko

Nyaraka ni nini, na zimepangwa kwa namna gani?

Nyaraka ni barua zilizoandikwa na viongozi wa Kanisa kwa Watakatifu katika maeneo tofauti ya ulimwengu. Mtume Paulo aliandika nyingi za nyaraka hizi katika Agano Jipya—akianzia na Warumi na kumaliza na Waebrania. Nyaraka zake zimepangwa kwa kuzingatia urefu, isipokuwa Waebrania (ona Kamusi ya Biblia, “Nyaraka za Paulo”). Japokuwa Warumi ni waraka wa kwanza katika Agano Jipya, ulikuwa hasa umeandikwa karibia na mwisho wa safari za Paulo za kimisionari.

Warumi 1–6

“Wenye haki wataishi kwa Imani.”

Ufafanuzi ufuatao unaweza kukusaidia kuelewa vizuri zaidi Waraka kwa Warumi:

Sheria.Paulo alipoandika juu ya “sheria,” alikuwa akimaanisha sheria ya Musa. Neno “matendo” katika maandishi ya Paulo mara nyingi lilirejea matendo ya nje yaliyohusishwa na sheria ya Musa. Fikiria jinsi sheria ya Musa na matendo yaliyohitajika chini ya sheria hiyo ni tofauti na “sheria ya imani” iliyoelezewa katika Warumi 3:23–31.

Kutahiri, kutokutahiri:Hapo kale, kutahiri kulikuwa ni ishara au alama ya agano Mungu alilofanya na Ibrahimu. Paulo alitumia neno “kutahiri” akimaanisha Wayahudi (watu wa agano) na “kutokutahiri” akimaanisha Wayunani. Tafakari kile ambacho Warumi 2:25–29 hufundisha kuhusu kile inachomaanisha hasa kuwa watu wa Mungu wa agano. Kumbuka kwamba kutahiri siyo lazima tena kama ishara ya agano la Mungu kwa watu Wake (ona Matendo ya Mitume 15:23–29).

Kujihesabia haki, kuhesabu haki, kuhesabiwa haki:Maneno haya yanahusu ondoleo, au kusamehewa, dhambi. Tunapohesabiwa haki, tunasamehewa, tunatajwa wasio na hatia, na kuondolewa kwenye adhabu ya milele kwa ajili ya dhambi zetu. Unapoona maneno haya, tazama kile Paulo alichofundisha kuhusu kile kinachofanya kujihesabia haki kuwezekane (ona pia Mwongozo wa Maandiko, “Kujihesabia haki, Kuhesabu haki,” scriptures.ChurchofJesusChrist.org; D. Todd Christofferson, “Kujihesabia Haki na Kutakaswa,” Ensign, Juni 2001, 18–25). Katika Warumi, maneno kama “adilifu” na “enye maadili” yanaweza kuonekana kama maneno yenye maana sawa na maneno “haki” na “kuhesabia haki.”

Neema.Neema ni “msaada mtakatifu … au nguvu, zinazotolewa kupitia rehema na upendo wa Yesu Kristo.” Kupitia neema, watu wote watafufuliwa na kupokea mwili usiokufa. Kwa kuongezea, “neema ni nguvu ya kuwezesha ambayo inaruhusu wanaume na wanawake kujipatia uzima wa milele na kuinuliwa baada ya kutumia jitihada zao wenyewe zilizo bora.” Hatuwezi kupata neema kupitia juhudi zetu, bali, ni neema ambayo hutupa sisi “nguvu na msaada wa kutenda matendo mema ambayo [sisi] bila hivyo hatungeweza kudumisha” (Kamusi ya Biblia, “Neema”; ona pia 2 Nefi 25:23; Dieter F. Uchtdorf, “Kipawa cha Neema,” Liahona, Mei 2015, 107–10; Brad Wilcox, “Neema Yake Inatosha,” Liahona, Sept. 2013, 43–45). Unaposoma Warumi, andika kile unachojifunza kuhusu neema ya Mwokozi.

Warumi 2:17–29

Matendo yangu ya nje lazima yaakisi na kuongeza uongofu wangu.

Baadhi ya Wakristo wa Kiyahudi katika Rumi bado waliamini kwamba utiifu kwa ibada na matambiko ya sheria ya Musa vilileta wokovu. Hii inaweza kuonekana kama tatizo ambalo halihusiki tena kwani hatuishi kwa sheria ya Musa. Lakini unaposoma maandiko ya Paulo, hasa Warumi 2:17–29, fikiria kuhusu jitihada zako mwenyewe za kuishi injili. Je, utendaji wako wa nje, kama vile kupokea sakramenti au kuhudhuria hekaluni, huongeza uongofu wako na kuimarisha imani yako katika Kristo? (ona Alma 25:15–16). Kuna kitu fulani unapaswa kubadili ili kwamba matendo yako ya nje yakupeleke kwenye badiliko la moyo?

Ona pia Dallin H. Oaks, “Changamoto ya Kuwa,” Ensign, Nov. 2000, 32–34.

Warumi 3:10–315

Kupitia Yesu Kristo, ninaweza kusamehewa dhambi zangu.

Baadhi ya watu wanaweza kuhisi kuvunjika moyo kwa tangazo la Paulo la kijasiri kwamba “hakuna mwenye haki, hata mmoja” (Warumi 3:10). Lakini pia kuna ujumbe wa matumaini katika Warumi. Utafute katika sura ya 3 na 5, na fikiria ni kwa nini kukumbuka kwamba “wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu” (Warumi 3:23) ni hatua muhimu kuelekea kwenye kujifunza “kufurahi katika tumaini” kupitia Yesu Kristo (Warumi 5:2).

Warumi 6

Yesu Kristo hunialika “kuenenda katika upya wa uzima.”

Paulo alifundisha kwamba injili ya Yesu Kristo inapaswa kubadilisha jinsi tunavyoishi. Ni kauli zipi katika Warumi 6 zinazoelezea jinsi ya kumfuata Mwokozi zimekusaidia “kuenenda katika upya wa uzima”? (mstari wa 4).

Picha
ikoni ya kujifunza kama familia

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko kama Familia na Jioni ya Nyumbani

Warumi 1:16–17.Ni kwa jinsi gani tunaweza kuonyesha kwamba “hatuionei haya injili ya Yesu Kristo”?

Warumi 3:23–28.Mnaposoma mistari hii, mngeweza kujadili tofauti kati ya “kujipatia neema ya Mungu, ambako kamwe hatuwezi kufanya, na kuipokea, ambako lazima tufanye. Ni lini tulihisi hiyo neema ya Mungu? Ni kwa jinsi gani tunaweza kuipokea kwa ukamilifu zaidi?

Warumi 5:3–5.Ni taabu zipi ambazo sisi tumezipitia? Ni kwa jinsi gani taabu hizi zilitusaidia kuendeleza uvumilivu, uzoefu, na matumaini?

Warumi 6:3–6.Je, Paulo alisema nini katika mistari hii kuhusu ishara ya ubatizo? Pengine familia yako inaweza kupanga kuhudhuria ubatizo unaokuja. Au mmoja katika familia yako anaweza kuonyesha picha au kumbukumbu kutoka kwenye ubatizo wake. Ni kwa jinsi gani kufanya na kushika maagano yetu ya ubatizo hutusaidia “kuenenda katika upya wa uzima”?

Picha
mwanamume akimbatiza mwenzake ziwani

Ubatizo unaashiria kuanza maisha mapya kama mfuasi wa Kristo.

Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.

Wimbo uliopendekezwa: “When I Am Baptized,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 103.

Kuboresha Kujifunza Binafsi

Uliza Maswali Unapojifunza. Unapojifunza maandiko, maswali yanaweza kuja akilini. Tafakari maswali haya na tafuta majibu. Kwa mfano, katika Warumi 1–6 unaweza kutafuta majibu kwa swali “Neema ni nini?”

Picha
Kristo akimuinua msichana kutoka kwenye kijito

Usiogope, na Greg K. Olsen

Chapisha