“Septemba 4–10. 1 Wakorintho 14–16: ‘Mungu Si Mungu wa Machafuko, bali wa Amani’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya (2023)
“Septemba 4–10. 1 Wakorintho 14–16,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2023
Septemba 4–10
1 Wakorintho 14–16
“Mungu si Mungu wa Machafuko, bali wa Amani”
Andika misukumo yako wakati unaposoma 1 Wakorintho 14–16. Omba kuhusu kile ambacho Roho amekufundisha, na mwombe Baba wa Mbinguni akujulishe kama kuna zaidi ambacho Yeye angetaka ujifunze.
Andika Misukumo Yako
Kwa sababu Kanisa na mafundisho yake vilikuwa kwa kiasi fulani vipya katika Korintho, inaeleweka kwamba Watakatifu wa Korintho walikumbana na machafuko. Hapo mwanzo Paulo alikuwa amewafundisha ukweli muhimu wa injili: “Kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu … na kwamba alizikwa, na kwamba alifufuka tena siku ya tatu” (1 Wakorintho 15:3–4). Lakini punde baadhi ya waumini walianza kufundisha kwamba “hakuna ufufuko wa wafu” (1 Wakorintho 15:12). Paulo aliwasihi “kuzishika” kweli walizokuwa wamefundishwa (1 Wakorintho 15:2). Tunapokumbana na mawazo yanayopingana kuhusu kweli za injili, ni vizuri kukumbuka kwamba “Mungu si Mungu wa Machafuko, bali wa Amani” (1 Wakorintho 14:33). Kuwasikiliza watumishi wa Bwana walioteuliwa na kushikilia kweli hizi rahisi walizofundisha kwa kurudia rudia kunaweza kutusaidia kupata amani na “kusimama imara katika imani” (1 Wakorintho 16:13).
Mawazo kwa Ajili ya Kujifunza Binafsi Maandiko
Ninaweza kutafuta kipawa cha unabii.
Je, kipawa cha unabii ni nini? Je, ni uwezo wa kutabiri yajayo? Ni kwa ajili ya manabii peke yao? Au, mtu yeyote anaweza kupokea kipawa hiki?
Tafakari maswali haya unaposoma 1 Wakorintho 14:3, 31, 39–40. Ungeweza pia kusoma Ufunuo 19:10 na “Unabii, Kutoa unabii” katika Mwongozo wa Maandiko (scriptures.ChurchofJesusChrist.org). Kulingana na kile unachojifunza, ni kwa jinsi gani ungeweza kuelezea kipawa cha unabii? Je, Paulo yawezekana alimaanisha nini wakati alipowaalika Wakorintho “kutamani unabii”? (1 Wakorintho 14:39). Je, ni kwa jinsi gani wewe unaweza kukubali mwaliko huu?
Ona pia Yoeli 2:28–29; Alma 17:3; Mafundisho na Maagano 11:23–28.
Je! Ni kwa jinsi gani kauli hii kuhusu wanawake katika mistari hii inatumika leo?
Katika siku za Paulo, kulikuwa na matarajio tofauti kuhusu jinsi ambavyo wanawake wangeshiriki katika jamii, ikijumuisha katika mikutano ya kanisa. Vyovyote mafundisho katika 1 Wakorintho 14:34–35 yalivyomaanisha katika siku za Paulo, hayapaswi kueleweka kwamba wanawake hawawezi kuzungumza au kuongoza katika Kanisa leo (ona Tafsiri ya Joseph Smith, 1 Wakorintho 14:34 [katika 1 Wakorintho 14:34, tanbihi b]). Rais Russell M. Nelson alisema kwa wanawake wa Kanisa leo: “Sisi … tunahitaji nguvu yenu, uongofu wenu, kusadiki kwenu, uwezo wenu wa kuongoza, busara yenu, na sauti zenu. “Ufalme wa Mungu si kamili na hauwezi kukamilika bila wanawake wanaofanya maagano matakatifu, na kuyashika, wanawake wanaoweza kusema kwa uwezo na mamlaka ya Mungu! (Russell M. Nelson, “Ombi kwa Dada Zangu,” Liahona, Nov. 2015, 96).
Yesu Kristo alishinda mauti.
Ufufuko wa Yesu Kristo ni muhimu sana kwenye Ukristo, mtu anaweza kusema kwamba bila ufufuko hakuna Ukristo—kwa kutumia maneno ya Paulo, “kuhubiri kwetu ni bure, na imani yenu ni bure” (1 Wakorintho 15:14). Bado baadhi ya Watakatifu wa Korintho walikuwa wakifundisha kwamba hakutakuwepo na “ufufuko wa wafu” (1 Wakorintho 15:12). Unaposoma jibu la Paulo katika 1Wakorintho15, chukua muda kidogo kutafakari ni jinsi gani maisha yako yangekuwa tofauti kama usingeamini katika Ufufuko (ona 2 Nefi 9:6–19; Alma 40:19–23; Mafundisho na Maagano 93:33–34). Je, kirai “Kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni bure” kinamaanisha nini kwako? (mstari wa 17).
Kuna umuhimu pia wa kutambua kwamba Paulo alirejelea ubatizo wa wafu kama ushuhuda wa uhalisia wa ufufuko (ona 1 Wakorintho 15:29. Ni kwa jinsi gani kazi ya hekalu na historia ya familia vimeimarisha imani yako katika fundisho la ufufuko?
Ona pia Mafundisho na Maagano 138:11–37.
Miili iliyofufuka ni tofauti na miili yenye kufa.
Je, umewahi kujiuliza mwili uliofufuka unafananaje? Kulingana na 1 Wakorintho 15:35, baadhi ya Wakorintho walijiuliza jambo kama hilo. Soma jibu la Paulo katika mstari wa 36–54, na andika maneno na virai ambavyo huelezea tofauti kati ya miili yenye kufa na miili iliyofufuka. Unapofanya hivyo, ungeweza kulinganisha mstari wa 40– 42 na Mafundisho na Maagano 76:50–112. Ni nini ufunuo huu kwa Nabii Joseph Smith unaongeza kwenye uelewa wako? (Ona pia Tafsiri ya Joseph Smith, 1 Wakorintho 15:40 [katika 1 Wakorintho 15:40, tanbihi a]). Kwa nini kweli hizi ni muhimu kwako?
Ona pia Luka 24:39; Alma 11:43–45; Mafundisho na Maagano 88:14–33.
Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko kama Familia na Jioni ya Nyumbani
-
1 Wakorintho 15:29.Tunajifunza kutoka mstari wa 29 kwamba Watakatifu wa kale walishiriki katika ubatizo wa wafu, kama vile tunavyofanya leo. Ni kwa jinsi gani tunaweza kuwaelezea wengine kwa nini tunabatizwa kwa niaba ya mababu zetu? (ona “What Are Baptisms for the Dead?,” [video], ChurchofJesusChrist.org). Tunaendeleaje kama familia kufanya ibada za hekaluni kwa ajili ya mababu zetu waliofariki ambao wanazihitaji? Unaweza kupata taarifa zaidi za mada hii katika makala ya Mada za Injili “Ubatizo wa Wafu” (topics.ChurchofJesusChrist.org) na katika FamilySearch.org.
-
1 Wakorintho 15:35–54.Ni vitu au picha gani ungeweza kuonyesha ili kuisaidia familia yako kuelewa baadhi ya maneno ambayo Paulo aliyatumia kuelezea jinsi miili yenye kufa ilivyo tofauti na miili iliyofufuka? Kwa mfano, kuonyesha kwa mfano tofauti kati ya kuharibika na kutokuharibika, (ona mstari 52–54) unaweza kuonyesha metali iliyopata kutu na metali ambayo haipati kutu. Au unaweza kutofautisha kitu dhaifu na kitu chenye nguvu (ona mstari 43).
-
1 Wakorintho 15:55–57.Majadiliano kuhusu mistari hii yanaweza kuwa ya maana hasa kama familia yako inamjua mtu ambaye amefariki. Wanafamilia wanaweza kutoa shuhuda juu ya jinsi Yesu Kristo anavyoondoa “uchungu wa mauti” (mstari wa 56).
-
1 Wakorintho 16:13.Ili kuwasaidia washiriki wa familia yako kujihusisha na mstari huu, unaweza kuchora duara ardhini na kumuelekeza mwanafamilia “kusimama imara” ndani yake akiwa amefumba macho yake. Kisha wengine wangejaribu kumsukuma au kumvuta ili atoke kwenye duara hilo. Je, kuna tofauti gani iliyopo wakati mwanafamila huyo ndani ya duara anapokuwa hajafumba macho na anapoweza “kutazama”? Tunaweza kufanya nini ili “kusimama imara” wakati tunapojaribiwa kufanya chaguzi mbaya? (Ona pia “Stay in the Boat and Hold On!,” [video], ChurchofJesusChrist.org).
Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.
Wimbo uliopendekezwa: “Amefufuka!,” Nyimbo za Kanisa, na. 199.