Agano Jipya 2023
Agosti 28–Septemba 3. 1 Wakorintho 8–13: “Ninyi ni Mwili wa Kristo”


“Agosti 28–Septemba 3. 1 Wakorintho 8–13: “Ninyi ni Mwili wa Kristo’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya (2023)

“Agosti 28–Septemba 3. 1 Wakorintho 8–13,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2023

Picha
mkutano wa sakramenti

Agosti 28–Septemba 3

1 Wakorintho 8–13

“Ninyi ni Mwili wa Kristo”

Unaposoma 1 Wakorintho 8–13 kwa sala, Roho Mtakatifu anaweza kuzungumza nawe katika njia za utulivu (ona 1 Wafalme 19:11–12). Kuandika misukumo hii kutakusaidia kukumbuka hisia na mawazo uliyopata wakati wa kujifunza kwako.

Andika Misukumo Yako

Wakati wa Paulo, Korintho ilikuwa kitovu tajiri cha biashara ikiwa na wakazi kutoka maeneo yote ya Ufalme wa Rumi. Chenye tamaduni nyingi na madhehebu tofauti katika mji, waumini wa Kanisa katika Korintho walipata taabu kudumisha umoja, hivyo Paulo alitafuta kuwasaidia kupata umoja katika imani yao katika Kristo. Umoja huu ulipaswa kuwa zaidi ya kuishi pamoja kwa amani; Paulo hakuwa akiwaomba tu kuvumilia tofauti za kila mmoja. Bali, alifundisha kwamba unapojiunga na Kanisa la Yesu Kristo “unabatizwa kuwa mwili mmoja,” na kila kiungo cha mwili kinahitajika (1 Wakorintho 12:13). Muumini mmoja anapopotea, ni kama kupoteza kiungo, na mwili huwa dhaifu kama matokeo yake. Muumini mmoja anapoteseka, wote tunapaswa kuhisi mateso na kufanya sehemu yetu ili kuyapunguza. Katika aina hii ya umoja, tofauti siyo tu zinatambuliwa bali huifadhiwa kwa upendo mkubwa, kwa sababu bila waumini wenye karama na uwezo tofauti, mwili ungekuwa na uwezo mdogo. Hivyo kama unahisi kwamba daima umekuwa nyumbani ndani ya Kanisa au umejikuta unajiuliza kama kweli unastahili kuwa hapo, ujumbe wa Paulo kwako ni kwamba umoja siyo usawa. Unawahitaji Watakatifu wenzako, na Watakatifu wenzako wanakuhitaji.

Picha
ikoni ya kujifunza binafsi

Mawazo kwa Ajili ya Kujifunza Binafsi Maandiko

1 Wakorintho 10:1–13

Mungu hutoa njia ya kuponyoka majaribu.

Matukio ya Kiroho, hata yale ya kimiujiza, hayatupi msamaha wa majaribu ambayo ni “kawaida ya mwanadamu” (1 Wakorintho 10:13). Hiyo yaweza kuwa sababu moja ambayo Paulo aliandika kuhusu jinsi Waisraeli katika siku ya Musa walivyohangaika na majaribu, japokuwa walishuhudia miujiza mikuu (ona Kutoka 13:21; 14:13–31). Unaposoma 1 Wakorintho 10:1–13, ni maonyo gani katika uzoefu wa Waisraeli yanaonekana kutumika kwako? Je, ni aina gani ya “kuponyoka” kutoka kwenye majaribu ambayo Baba wa Mbinguni ametoa kwa ajili yako? (ona pia Alma 13:27–30; 3 Nefi 18:18–19).

1 Wakorintho 10:16–17; 11:16–30

Sakramenti hutuunganisha kama waumini wa Kanisa la Kristo.

Japokuwa sakramenti hujumuisha ahadi binafsi kati yako na Bwana, pia ni tukio ambalo unashiriki pamoja na wengine. Sisi daima tunapokea sakramenti pamoja, kama mwili wa Watakatifu. Soma kile ambacho Paulo alifundisha kuhusu sakramenti, na fikiria kuhusu jinsi gani ibada hii takatifu inaweza kuwasaidia “wengi” kuwa “wamoja” katika Kristo (1 Wakorintho 10:17). Ni jinsi gani kupokea sakramenti kunakusaidia kuhisi kuwa karibu na Kristo na waaminio wengine? Ni kwa namna gani mistari hii inashawishi hisia zako kuhusu sakramenti na njia ya kujiandaa kwa ajili ya kuipokea?

1 Wakorintho 11:11

Katika mpango wa Mungu, wanaume na wanawake wanahitajiana.

Katika 1 Wakorintho 11:4–15, Paulo alirejelea desturi za kitamaduni ambazo hatuzifuati leo. Hata hivyo, Paulo pia alifundisha ukweli muhimu ambao unatumika milele, unaopatikana katika mstari wa 11. Unafikiri mstari huo unamaanisha nini, na kwa nini ni muhimu? Mzee David A. Bednar alifundisha, “Mwanamume na mwanamke wamedhamiriwa kujifunza kutoka kwa kila mmoja, kuimarishana, kubarikiana, na kukamilishana” (“Tunaamini katika Kuwa Wasafi Kimwili,” Liahona, Mei 2013, 42). Ni kwa jinsi gani ukweli huu unapaswa kushawishi ndoa? Ni kwa jinsi gani ukweli huu unapaswa kuathiri jinsi tunavyotumikia katika Kanisa?

Ona pia Jean B. Bingham, “Kuungana katika Kufanikisha Kazi ya Mungu,” Liahona, Mei 2020, 60–63.

1 Wakorintho 12–13

Karama za kiroho hutolewa ili kuwanufaisha watoto wote wa Baba wa Mbinguni.

Orodha ya karama za kiroho katika 1 Wakorintho 12–13 siyo kamilifu. Lakini ni mahala pazuri pa kuanzia unapogundua na kutafakari karama za kiroho Baba wa Mbinguni alizokupatia. Makala “Karama za Kiroho” katika Mada za Injili (topics.ChurchofJesusChrist.org) inaweza kukusaidia kuelewa karama hizi vizuri zaidi. Unaposoma orodha ya Paulo, ungeweza kuongeza baadhi ya ulizotambua kwa wengine, wewe mwenyewe, au kwa watu wengine katika maandiko. Kama una baraka ya patriaki, inaweza pia kutaja baadhi ya karama zako za kiroho. Je, ni kwa jinsi gani karama hizi zinakusaidia kuwabariki wengine? Fikiria jinsi unavyoweza kutafuta “sana karama zilizo kuu” (1 Wakorintho 12:31).

Ona pia 1 Wakorintho 14; Moroni 10:8–21, 30; Mafundisho na Maagano 46:8–26; Makala ya Imani 1:7.

Picha
ikoni ya kujifunza kama familia

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko kama Familia na Jioni ya Nyumbani

1 Wakorintho 9:24–27.Kwa kuwa Paulo alilinganisha kuishi injili na mashindano ya mbio, unaweza kuwa na mbio za familia kuelezea kwa mfano hoja yake. Toa zawadi kwa kila mtu anayemaliza mbio, na jadili ni kwa jinsi gani wote wenye bidii katika kumfuata Yesu Kristo katika maisha haya hupokea taji “isiyoharibika” (1 Wakorintho 9:25; ona pia 2 Timotheo 4:7–8). Je, mkimbiaji hufanya nini ili kujiandaa kwa ajili ya mbio? Sisi tunaweza kufanya nini ili kujiandaa kurudi kwa Baba wa Mbinguni?

Picha
wakimbiaji uwanjani

Paulo alifananisha kuishi injili na mashindano ya mbio.

1 Wakorintho 12:1–11.Baada ya kusoma mistari hii kwa pamoja, fikiria kumpa kila mtu kipande cha karatasi kikiwa na jina la mwanafamilia mwingine juu yake. Waombe kila mmoja aorodheshe karama za kiroho wanazogundua mtu yule anazo. Kisha mnaweza kupitisha karatasi katika duara mpaka kila mmoja amepata nafasi ya kuandika kuhusu karama za kila mwanafamilia.

1 Wakorintho 12:3.Kwa nini Roho Mtakatifu ni muhimu katika kupata ushuhuda wa Yesu Kristo? Je, tunaweza kufanya nini katika kumualika Roho Mtakatifu kuimarisha shuhuda zetu juu yake Yeye?

1 Wakorintho 12:12–27.Analojia ya Paulo ya mwili inaweza kuwa ni njia ya kukumbukwa katika kujadili umoja wa familia. Kwa mfano, wanafamilia wanaweza kujaribu kuchora mwili uliotengenezwa na macho tu au masikio (ona mstari wa 17). Je, mistari hii hupendekeza nini kuhusu jinsi tunavyopaswa kutendeana kila mmoja kama wanafamilia?

1 Wakorintho 13:4–8.Ufafanuzi wa Paulo juu ya hisani unaweza kuwa kaulimbiu yenye mwongozo kwa familia yako. Unaweza kumpangia kila mwanafamilia kujifunza kirai katika mstari 4–8 na kufundisha wanafamilia wengine kile inachomaanisha kwa kutumia maelezo, mifano, na uzoefu binafsi. Je, ni kwa jinsi gani Mwokozi ni mfano wa sifa hizi? Mnaweza pia kutengeneza mabango pamoja kwa kila mojawapo ya virai na kuyaweka kuzunguka nyumba yenu. Kuwa mbunifu!

Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.

Wimbo uliopendekezwa: “Love Is Spoken Here,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 190–91.

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Onyesha andiko. Chagua mstari unaouona una maana, na ubandike mahali ambapo wanafamilia watauona kila mara. Waalike wanafamilia wengine kufanya zamu ya kuchagua andiko la kubandika.

Picha
mkutano wa sakramenti

“Mkate tunaomega, si ushirika wa mwili wa Kristo? Kwa kuwa sisi tulio wengi tu mkate mmoja, na mwili mmoja” (1 Wakorintho 10:16–17).

Chapisha