“Kiambatisho: Kuwaandaa Watoto Wako kwa ajili ya Maisha Yote kwenye Njia ya Agano ya Mungu,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya 2023 (2022)
“Kiambatisho,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Agano Jipya 2023
Kiambatisho
Kuwaandaa Watoto Wako kwa ajili ya Maisha Yote kwenye Njia ya Agano ya Mungu
Kwa sababu Yeye anakupenda, anakuamini na anajua uwezo wako, Baba wa Mbinguni amekupatia wewe fursa ya kuwasaidia watoto wako kuingia na kuendelea kusonga kwenye njia Yake ya agano, njia ya kwenda kwenye uzima wa milele (ona Mafundisho na Maagano 68:25–28). Hii inajumuisha kuwasaidia wao kujitayarisha kufanya na kuyashika maagano matakatifu, kama vile agano la ubatizo na maagano yanayofanyika hekeluni. Kupitia maagano haya, watoto wako watakuwa wamejifungamanisha wao wenyewe kwa Mwokozi, Yesu Kristo.
Kuna njia nyingi za kuwaandaa watoto wako kwa ajili ya safari hii ya kwenye njia ya agano na Baba wa Mbinguni atakusaidia kugundua njia iliyo bora zaidi ya kuwasaidia. Unapotafuta mwongozo wa kiungu, weka akilini kwamba siyo kujifunza kote kunafanyika wakati wa masomo yaliyopangwa. Ukweli ni kwamba, sehemu ya kitu kinachofanya kujifunza nyumbani kuwa na nguvu zaidi ni fursa ya kujifunza kwa mfano na kupitia nyakati ndogo na za kawaida kabisa—aina ile ambayo hujitokeza katika njia ya asili katika mtiririko wa maisha ya kila siku. Kama vile tu kufuata njia ya agano ni njia endelevu, mchakato wa maisha yote, ndivyo ilivyo kujifunza kuhusu njia ya agano. (Ona “Nyumba na Familia,” Kufundisha katika Njia ya Mwokozi [2022], 30–31.)
Hapo chini kuna baadhi ya mawazo ambayo yaweza kuongoza zaidi kwenye mwongozo wa kiungu. Unaweza kupata mawazo ya ziada kwa ajili ya kuwafundisha watoto wa umri wa Msingi katika “Kuwaandaa Watoto kwa ajili ya Maisha Yote kwenye Njia ya Agano ya Mungu” katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi.
Ubatizo na Kuthibitishwa
Nefi alifundisha kwamba “lango ambalo [sisi] tutaingilia kwenye” njia ya agano “ni toba na ubatizo kwa maji” (2 Nefi 31:17). Jitihada zako za kuwasaidia watoto wako kujitayarisha kwa ajili ya ubatizo na kuthibitishwa kunaweza kuweka miguu yao thabiti kwenye njia hiyo. Jitihada hizi zinaanza na kufundisha kuhusu imani katika Yesu Kristo na toba. Pia zinajumuisha kufundisha kuhusu jinsi gani tunafanya upya maagano yetu ya ubatizo kwa kula sakramenti kila wiki.
Hapa kuna baadhi ya nyenzo ambazo zinaweza kukusaidia: 2 Nefi 31; Mada za Injili, “Ubatizo,” topics.ChurchofJesusChrist.org.
-
Wakati wowote unapokuwa na tukio ambalo linaimarisha imani yako katika Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo, lishiriki kwa watoto wako. Msaidie kuelewa kwamba imani ni kitu ambacho kinaweza kukua imara na imara kwa maisha yote. Ni yapi baadhi ya mambo ambayo mtoto wako anaweza kufanya ili kuikuza imani iwe imara katika Yesu Kristo kabla hajabatizwa?
-
Mtoto wako anapofanya uchaguzi usio sahihi, ongea kwa furaha kuhusu zawadi ya toba. Na wakati wewe unapofanya uchaguzi usio sahihi, shiriki furaha ambayo inakuja unapotubu. Shuhudia kwamba kwa sababu Yesu Kristo aliteseka na kufa kwa ajili ya dhambi zetu, alitupatia uwezo wa sisi kubadilika. Wakati mtoto wako anapoomba msamaha, msamehe bila sharti na kwa furaha.
-
Mwambie mtoto wako kuhusu ubatizo wako. Onyesha picha na shiriki kumbukumbu zako. Ongelea kuhusu jinsi ulivyohisi, jinsi maagano ya ubatizo wako yalivyokusaidia wewe kuja kumjua vyema zaidi Yesu Kristo na jinsi yanavyoendelea kubariki maisha yako. Mhimize mtoto wako kuuliza maswali.
-
Panapokuwa na ubatizo katika familia yako au kata yako, nenda na mtoto wako ili aone. Zungumzeni pamoja kuhusu kile ambacho wewe na mtoto wako mlikiona na mlivyohisi. Kama inawezekana, ongea na mtu anayebatizwa na kumwuliza maswali kama yafuatayo: “Je, umefanyaje uamuzi huu? Je, ulijiandaaje?”
-
Wakati wowote unapogundua mtoto wako anafanya kitu alichoahidi kukifanya, mpe pongezi za dhati. Onyesha kwamba kutimiza ahadi kunatusaidia sisi kujiandaa kushika maagano tunayofanya wakati tunapobatizwa. Tunamwahidi nini Mungu wakati tunapobatizwa? Yeye anatuahidi nini sisi? (ona Mosia 18:8–10, 13).
-
Wakati wewe na mtoto wako mnapopata tukio takatifu mkiwa pamoja (kama vile kanisani, wakati mkisoma maandiko au wakati mkimhudumia mtu), mwambie kuhusu hisia au msukumo huo wa kiroho ulionao. Mwalike mtoto wako ashiriki jinsi anavyohisi. Tambua njia tofauti za Roho anavyoweza kuongea kwa watu, ikijumuisha njia ambazo Yeye anaongea na wewe binafsi. Msaidie mtoto wako kuzitambua nyakati ambapo yeye anaweza kuhisi ushawishi wa Roho Mtakatifu.
-
Angalieni pamoja video chache katika mkusanyiko wa video zilizomo katika Maktaba ya Injili yenye kichwa cha habari “Hear Him!” Zungumzeni pamoja kuhusu njia tofauti ambazo watumishi wa Bwana wanaisikia sauti Yake. Mwalike mtoto wako kuchora picha au kutengeneza video kuhusu jinsi yeye anavyoisikia sauti ya Mwokozi.
-
Zungumzeni kuhusu jinsi kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kumekubariki wewe. Ni kwa jinsi gani umekuwa karibu zaidi na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo ulipowahudumia wengine na wengine walipokuhudumia wewe? Msaidie mtoto wako kufikiria njia za kuwahudumia na kuwaimarisha wengine kama muumini wa Kanisa.
-
Fanyeni sakramenti kuwa tukio takatifu na lenye furaha katika familia yenu. Msaidie mtoto wako kupanga njia za kufokasi juu ya Yesu Kristo wakati wa sakramenti. Je, ni kwa namna gani tutaonyesha kwamba sakramenti ni takatifu kwetu sisi?
-
Gazeti la Rafiki mara kwa mara linajumuisha makala, hadithi na shughuli ili kuwasaidia watoto kujiandaa kwa ajili ya ubatizo na kuthibitishwa. Acha mtoto wako achague baadhi ili asome na kufurahia pamoja na wewe. (Ona pia mkusanyiko wa “Preparing for Baptism” katika sehemu ya watoto ya Maktaba ya Injili.)
Kufundisha Watoto Wako kuhusu Ukuhani
Ukuhani ni mamlaka na nguvu za Mungu ambayo kwa njia hiyo Yeye hubariki watoto Wake. Ukuhani wa Mungu uko duniani leo katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Waumini wote wa Kanisa ambao wanashika maagano yao wanabarikiwa kwa nguvu ya ukuhani wa Mungu katika nyumba zao ili kujiimarisha wao wenyewe na familia zao (ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, 3.5, ChurchofJesusChrist.org). Nguvu hii itawasaidia waumini katika kufanya kazi ya Mungu ya wokovu na kuinuliwa katika maisha yao binafsi na familia (ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 2.2).
Tunapokea ibada kwa mamlaka ya ukuhani. Wakati wanaume na wanawake wanapohudumu katika miito ya Kanisa, wanafanya hivyo kwa mamlaka ya ukuhani, chini ya maelekezo ya wale walio na funguo za ukuhani. Watoto wote wa Baba wa Mbinguni—wana na mabinti Zake—watabarikiwa wanapokuja kuuelewa vyema ukuhani.
Ili kujifunza zaidi kuhusu ukuhani, ona Russell M. Nelson, “Hazina za Kiroho,” Liahona, Nov. 2019, 76–79; Russell M. Nelson, “Thamani ya Nguvu ya Ukuhani,” Liahona, Mei 2016, 66–69; “Kanuni za Ukuhani,” mlango wa 3 katika Kitabu cha Maelezo ya Jumla.
-
Zifanye ibada za ukuhani kuwa sehemu endelevu ya maisha ya familia yako. Kwa mfano, msaidie mtoto wako kujiandaa kiroho kwa ajili ya sakramenti kila wiki. Mhimize mtoto wako kutafuta baraka za ukuhani wakati anapokuwa mgonjwa au anapohitaji faraja au mwongozo. Ifanye kuwa tabia kuonyesha njia ambazo Bwana anaibariki familia yako kupitia nguvu za ukuhani.
-
Mnaposoma maandiko kwa pamoja, angalia fursa za kujadili jinsi Mungu anavyobariki watu kupitia nguvu Yake. Shiriki uzoefu wako mwenyewe wa wakati ambapo Mungu alikubariki wewe kupitia ukuhani Wake. Kwa mifano ya baraka tunazopokea kutoka kwa Mungu kupitia ukuhani, ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 3.2, 3.5.
-
Jifunzeni safu ya mamlaka ya ukuhani ya mtu aliye katika familia yenu. (Wale wanaoshikilia Ukuhani wa Melkizedeki wanaweza kupokea safu zao za mamlaka ya ukuhani kwa kutuma barua pepe kwenda kwa LineofAuthority@ChurchofJesusChrist.org; ona pia “Request a Priesthood Line of Authority” katika Kituo cha Msaada ChurchofJesusChrist.org.) Zungumzeni kuhusu kwa nini ni muhimu kujua kwamba mamlaka ya ukuhani yanatoka kwa Yesu Kristo Mwenyewe? Je, ni kwa nini Yeye anashiriki ukuhani huo pamoja nasi?
-
Mfundishe mtoto wako kwamba baada ya ubatizo, yeye anaweza kupokea nguvu za ukuhani kwa kushika agano la ubatizo. Rejeleeni kwa pamoja ujumbe wa Rais Russell M. Nelson “Hazina za Kiroho” (Liahona, Nov. 2019, 76–79). Mwambie mtoto wako jinsi ambavyo ibada za ukuhani zimeleta nguvu ya Mungu katika maisha yako? Kwa ajili ya orodha ya baadhi ya njia ambazo kwazo tunabarikiwa na nguvu za ukuhani, ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 3.5.
-
Jadilianeni swali hili “Je, mtumishi wa Bwana yukoje?” Someni pamoja Mafundisho na Maagano 121:36–42, na tafuteni majibu. Wakati wowote unapogundua mtoto wako (au mtu mwingine yeyote) akitumia mojawapo ya kanuni au sifa zilizoko katika mistari hii, itaje.
-
Wakati wewe au mtoto wako anapotumia funguo kufungua mlango au kuwasha gari, chukua muda huo kulinganisha funguo hizo na funguo zinazoshikiliwa na viongozi wa ukuhani. (Kwa ajili ya maana ya funguo za ukuhani, ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 3.4.1). Je, funguo za ukuhani “zinafungua” au “kuwasha” nini kwa ajili yetu sisi? Ona pia Gary E. Stevenson, “Je, Ziko Wapi Funguo na Mamlaka ya Ukuhani?,” Liahona, Mei 2016, 29–32; “Where Are the Keys?” (video), ChurchofJesusChrist.org.
-
Unapokuwa unatengwa kwa ajili ya wito, mwalike mtoto wako awepo, kama inawezekana. Acha mtoto wako akuone ukitekeleza wito wako. Unaweza hata kutafuta njia sahihi ambazo yeye anaweza kukusaidia. Elezea jinsi unavyoihisi nguvu ya Bwana katika wito wako.
Kwenda hekaluni—Kubatizwa na kuthibitishwa kwa ajili ya Wafu
Mahekalu ni sehemu ya mpango wa Baba wa Mbinguni kwa ajili ya watoto Wake. Ndani ya mahekalu, tunafanya maagano matakatifu na Baba wa Mbinguni tunaposhiriki katika ibada takatifu, ambazo zote zinatuelekeza kwa Yesu Kristo. Baba wa Mbinguni ametoa njia kwa watoto Wake wote kufanya maagano na kushiriki katika ibada, ikiwajumuisha wale ambao hawakupokea ibada na maagano hayo katika maisha haya. Mwanzoni mwa mwaka ambao yeye anatimiza miaka 12, mtoto wako anakuwa mkubwa vya kutosha kubatizwa na kuthibitishwa hekaluni kwa ajili ya mababu waliofariki.
Ili kujifunza zaidi kuhusu ubatizo na uthibitisho kwa ajili ya wafu, ona “About Proxy Baptism and Confirmation,” temples.ChurchofJesusChrist.org.
-
Hudhurieni hekaluni mara nyingi kadiri hali yenu inavyoruhusu. Zungumza na mtoto wako kuhusu kwa nini unakwenda na jinsi gani hekalu linakusaidia wewe kuhisi uko karibu zaidi na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo.
-
Rejeleeni na kujadili maswali ya kibali cha kuingia hekaluni kwa pamoja. Ongea na mtoto wako kuhusu kile kinachotokea katika mahojiano ya kibali cha hekaluni. Shiriki ni kwa nini kuwa na kibali cha hekaluni ni muhimu kwako.
-
Someni pamoja Malaki 4:6. Zungumza kuhusu jinsi ambavyo mioyo yenu ingeweza kuwageukia mababu zenu. Jifunze zaidi kuhusu mababu zenu kwa kupekua historia ya familia yenu kwa pamoja. FamilySearch.org. Watafuteni mababu ambao wanahitaji kubatizwa na kuthibitishwa. Mshauri wa kazi ya hekaluni na historia ya familia wa kata yako anaweza kukusaidia.
-
Rejeleeni kwa pamoja baadhi ya nyenzo katika mkusanyiko wenye kichwa cha habari “Hekalu” katika sehemu ya watoto ya Maktaba ya Injili. (Ona pia “Preparing Your Child for Temple Baptisms and Confirmations” kwenye ChurchofJesusChrist.org.)
Kupokea Baraka ya Patriaki
Baraka ya patriaki inaweza kuwa chanzo cha mwongozo, faraja na uvuvio. Baraka hiyo ina ushauri binafsi kutoka kwa Baba wa Mbinguni kuja kwetu sisi na inatusaidia kuelewa utambulisho wetu na madhumuni yetu ya milele. Msaidie mtoto wako kujiandaa kupokea baraka ya patriaki kwa kumfundisha juu ya umuhimu na asili takatifu ya baraka ya patriaki.
Ili kujifunza zaidi, ona Mada za Injili, “Baraka za Patriaki,” topics.ChurchofJesusChrist.org.
-
Shiriki na mtoto wako uzoefu wako wa kupokea baraka ya patriaki. Ungeweza kushiriki mambo kama vile jinsi wewe ulivyojiandaa kuipokea, imekusaidiaje wewe kuja karibu zaidi na Mungu na jinsi unavyoitumia baraka hiyo katika maisha yako. Pia ungeweza kumwalika mtoto wako kuzungumza na washiriki wengine wa familia ambao wamekwisha kupokea baraka zao za patriaki.
-
Pangeni muda wa kurejelea kwa pamoja baadhi ya nyenzo katika Mada za Injili, “Baraka za Patriaki.” Ili kujifunza kuhusu mchakato wa kupokea baraka ya patriaki, ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 18.17.
-
Kama unao mababu waliopokea baraka za patriaki, ingeweza kuwa ya kuvutia kuzisoma baadhi pamoja na mtoto wako. Ili kuomba baraka za mababu ambao wamekwishafariki, ingia kwenye ChurchofJesusChrist.org, bofya ikoni ya akaunti kwenye kona ya juu kulia ya skirini, na chagua “Patriarchal Blessing.”
-
Baada ya mtoto wako kuwa amepokea baraka ya patriaki, waalike wanafamilia waliokuwepo kuandika hisia zao na kushiriki hisia hizo na mtoto wako.
Kwenda Hekaluni—Endaumenti
Mungu anataka kuwapa, au kuwabariki, watoto Wake wote kwa “uwezo utokao juu” (Mafundisho na Maagano 95:8). Tunaenda hekaluni ili kupokea endaumenti yetu sisi wenyewe mara moja tu, lakini maagano tunayofanya na Mungu na nguvu za kiroho anazotupatia kama sehemu ya endaumenti hiyo inaweza kutubariki sisi kila siku ya maisha yetu.
Ili kujifunza zaidi kuhusu endaumenti ya hekaluni, ona “Kuhusu Endaumenti ya Hekaluni,”. temples.ChurchofJesusChrist.org; Russell M. Nelson, “Jiandae kwa Baraka za Hekaluni,” Ensign, Okt. 2010, 41–51.
-
Onesha picha ya hekalu ndani ya nyumba yenu. Mwambie mtoto wako kuhusu hisia ulizopata ulipokuwa hekaluni. Ongelea mara kwa mara kuhusu mapenzi yako kwa Bwana na nyumba Yake na maagano ambayo umefanya humo.
-
Chunguzeni kwa pamoja temples.ChurchofJesusChrist.org. Someni kwa pamoja makala kama vile “Kuhusu Endaumenti za Hekaluni” na “Jitayarishe kwa ajili ya Nyumba ya Bwana.” Acha mtoto wako aulize maswali yoyote aliyonayo kuhusu hekalu. Kwa mwongozo kuhusu kile unachoweza kuongea nje ya hekalu, ona ujumbe wa Mzee David A. Bednar “Kujiandaa Kupata Kila Kitu Kinachohitajika” (Liahona, Mei 2019, 101–4; ona hususani sehemu yenye kichwa cha habari “Mafunzo na Maandalizi ya Hekaluni Yanayolenga Nyumbani na Kusaidiwa na Kanisa”).
-
Wewe na mtoto wako mnaposhiriki katika au kuwa mashahidi wa ibada nyingine (kama vile sakramenti au baraka ya uponyaji), tengeni muda wa kujadiliana ishara zilizohusika katika ibada hiyo. Je, alama hizo zinawakilisha nini? Je, ni kwa jinsi gani zinashuhudia juu ya Yesu Kristo? Hii inaweza kumsaidia mtoto wako kujitayarisha kutafakari maana ya kiishara ya ibada za hekaluni, ambazo pia zinashuhudia juu ya Yesu Kristo.
-
Msaidie mtoto wako kutambua jinsi yeye anavyoshika agano la ubatizo lililoelezewa katika Mosia 18:8–10, 13. Pia msaidie mtoto wako kutambua jinsi Bwana anavyombariki yeye. Jenga kujiamini kwa mtoto wako katika uwezo wake wa kushika maagano.
-
Zungumza kwa uwazi na mara kwa mara kuhusu jinsi maagano yako ya hekaluni yanavyoongoza chaguzi zako na kukusaidia kukua na kuwa karibu zaidi na Yesu Kristo. Ungeweza kutumia Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 27.2, ili kurejelea maagano tunayofanya hekaluni.
Kuhudumu Misheni
Mzee David A. Bednar alifundisha: “Kitu kimoja kilicho muhimu sana unachoweza kufanya ili kujiandaa kwa ajili ya wito wa kuhudumu ni kuwa mmisionari mapema kabla wewe hujaenda misheni. … Kitu muhimu hapa sio kwenda misheni; badala yake cha muhimu hapa ni wewe kuwa mmisionari na kuhudumu katika maisha yetu yote kwa moyo wetu, nguvu, akili na uwezo wetu wote. … Unajiandaa kwa ajili ya kazi ya umisionari kwa maisha yote” (“Becoming a Missionary,” Liahona, Nov. 2005, 45–46). Uzoefu mtoto wako alionao wa kuwa mmisionari utambariki yeye milele, siyo tu kwa kipindi cha muda fulani ambao atahudumu kama mmisionari.
Ili kujifunza zaidi, ona Russell M. Nelson, “Kuhubiri Injili ya Amani,” Liahona, Mei 2022, 6–7; M. Russell Ballard, “Huduma ya Kimisionari Imebariki Maisha Yangu Milele,” Liahona, Mei 2022, 8–10; Matayarisho ya Umishonari: Kuzoea Maisha ya Umishonari, ChurchofJesusChrist.org.
-
Onyesha mfano jinsi ya kushiriki injili katika njia za kawaida. Daima uwe macho kuona fursa za kushiriki na wengine hisia zako kuhusu Baba wa Mbinguni na Mwokozi na baraka unazopokea kama muumini wa Kanisa Lake. Waalike wengine kuungana na familia yako katika shughuli za Kanisa na za kifamilia.
-
Tafuta fursa za familia yako kukutana na wamisionari. Waalike kuwafundisha marafiki zako au wape nafasi ya kuwafundisha watu nyumbani mwako. Waulize wamisionari kuhusu uzoefu wanaoupata na jinsi gani huduma ya umisionari inavyowasaidia wao kusogea karibu zaidi na Yesu Kristo. Pia waulize walifanya nini (au wanachotamani kuwa wangefanya) ili kujiandaa kuwa wamisionari.
-
Kama wewe ulihudumu misheni, ongea kwa uwazi na mara kwa mara kuhusu uzoefu wako. Au waalike marafiki au wanafamilia ambao wamehudumu misheni kuzungumzia kuhusu uzoefu wao. Ungeweza pia kuongea kuhusu njia ambazo umeshiriki injili na wengine maisha yako yote. Msaidie mtoto wako kufikiria njia anazoweza kushiriki injili.
-
Mpe mtoto wako fursa ya kufundisha familia yako kanuni za injili. Mtoto wako pia anaweza kufanya mazoezi ya kushiriki imani yake na wengine. Kwa mfano, mngeweza kujadiliana maswali kama “Je ni jinsi gani tungeweza kutambulisha Kitabu cha Mormoni kwa mtu ambaye hajapata kukisikia?” Au “Jinsi gani tungeweza kuelezea uhitaji wetu wa Mwokozi kwa mtu asiye Mkristo?”
-
Msaidie mtoto kuhisi faraja anapozungumza na watu. Je, ni zipi baadhi ya njia nzuri za kuanzisha mazungumzo? Mhimize mtoto wako kujifunza jinsi ya kusikiliza kile wengine wanachosema, kuelewa kile kilicho katika mioyo yao na kushiriki ukweli wa injili ambao ungeweza kubariki maisha yao.
-
Tafuta fursa kwa ajili ya mtoto wako kujifunza kuhusu tamaduni na imani zingine. Msaidie kutambua na kuheshimu kanuni nzuri na za kweli katika imani za wengine.
Kwenda Hekaluni—Kuunganishwa
Hekaluni, mume na mke wanaweza kuoana kwa milele yote. Hili linatokea katika ibada inayoitwa kuunganishwa. Hata kama ibada hii inaweza ikawa baada ya miaka mingi ijayo kwa mwanao au binti yako mambo madogo madogo, rahisi na endelevu mfanyayo kwa pamoja wakati wa miaka hiyo inaweza kumsaidia yeye kujiandaa kwa ajili ya baraka hii ya kupendeza.
Ili kujifunza zaidi, ona Mada za Injili, “Sealing,” topics.ChurchofJesusChrist.org.
-
Someni kwa pamoja “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu” kwenye ChurchofJesusChrist.org. Tangazo hili linafundisha nini kuhusu furaha katika maisha ya familia na kuhusu ndoa zenye mafanikio? Kwa pamoja na mtoto wako, chagueni moja ya kanuni zilizoorodheshwa katika tangazo ili mjifunze. Mnaweza kutafuta maandiko yanayohusiana na kanuni hiyo katika Mwongozo wa Maandiko. Mnaweza pia kuweka malengo ya kutumia kanuni hiyo kwa ukamilifu zaidi katika familia yenu. Mnapofanyia kazi malengo yenu, jadilianeni kwa pamoja matokeo ambayo kanuni hiyo yanayo katika maisha ya familia.
-
Pamoja na mtoto wako, someni ujumbe wa Rais Dieter F. Uchtdorf wa “Katika Kuwasifu Wale Wanaohudumu” (Liahona, Mei 2016, 77–80). Unapofika kwenye sehemu yenye kichwa cha habari “Jumuiya ya Vitu vya Kutumia Mara Moja na Kutupa,” unaweza kutafuta vitu ndani ya nyumba yako ambavyo vinatumika mara moja na kutupwa na vitu vingine ambavyo siyo vya kutupwa. Zungumza kuhusu vile ambavyo unavitendea vitu kwa utofauti unapotaka vidumu kwa muda mrefu. Je, hii inapendekeza nini kuhusu jinsi tunavyopaswa kuzichukulia ndoa na mahusiano ya familia? Tunajifunza nini kingine kutoka kwenye ujumbe wa Rais Uchtdorf kuhusu jinsi Mwokozi anavyoweza kutusaidia sisi kujenga ndoa na familia imara?
-
Kama umeoa au kuolewa, kuwa muwazi kwa mtoto wako kuhusu mambo unayohisi mnafanya vyema kama wanandoa, mambo mnayojifunza na njia ambazo mnajaribu kuboresha. Kama wewe na mwenza wako mmekwisha unganishwa hekaluni, mwonyeshe mtoto wako kwa mfano jinsi mnavyojitahidi kushika maagano baina yenu wananndoa pamoja na Bwana. Mwambie mtoto wako jinsi mnavyojitahidi kuwafanya Baba wa Mbinguni na Mwokozi kuwa kitovu cha uhusiano wenu na jinsi Wao wanavyowasaidia.
-
Wakati maamuzi ya familia yanapohitaji kufanyika, fanyeni baraza la familia na kujadiliana. Hakikisha kwamba maoni ya washiriki wote wa familia yamesikilizwa na kuthaminiwa. Tumia majadiliano haya kama fursa ya kuweka mfano wa mawasiliano yenye afya na ukarimu katika mahusiano ya familia, hata wakati ambapo siyo kila mmoja anaona mambo kwa njia sawa.
-
Kunapokuwa na kutokukubaliana au mfarakano katika familia, onyesha uvumilivu na huruma. Msaidie mtoto wako kuona jinsi kutatua mfarakano katika njia kama za Kristo inaweza kumsaidia yeye kujiandaa kwa ajili ya familia yenye furaha. Someni pamoja Mafundisho na Maagano 121:41–42, na zungumza kuhusu jinsi kanuni katika mistari hii zinavyoweza kutumika katika ndoa.