Huduma ya Umisionari Imebariki Maisha Yangu Milele
Ni sala yangu kwamba ninyi wavulana na wasichana na wazazi wenu mtaona na kujua jinsi huduma ya umisionari itabariki maisha yenu milele.
Asante, Rais Nelson, kwa kushiriki tena ushauri huo kuhusu huduma ya umisionari.
Akina kaka na akina dada, miaka kadhaa iliyopita wakati nikizungumza katika mkutano mkuu, uoni wa jicho langu la kushoto ghafla ulitatizwa na shida kwenye retina, ambapo hatimaye hali ilikuwa mbaya sana na imeniacha bila uoni katika jicho hilo.
Kama nilivyokabiliana na changamoto hii, nina shukrani daima kwa aina nyingine ya uoni, ikijumuisha ule wa utambuzi. Kama nilivyotazama nyuma katika maisha yangu, nimeweza kuona baadhi ya uzoefu ambao ulileta utofauti mkubwa. Mojawapo ya uzoefu huo ni jinsi huduma yangu ya kimisionari kama mvulana huko Uingereza ilivyobariki maisha yangu na kujenga hatima yangu ya kiroho.
Nimetafakati juu ya jinsi changamoto za uchumi zilizohusiana na Mdororo Mkuu wa Kiuchumi katika miaka ya 1930 zilizvyopelekea hali mbaya kwa wazazi wangu na familia yetu. Baba yangu alijihusisha sana na kuokoa biashara yake ya magari na kusaidia familia katika kipindi hiki kigumu kiasi kwamba kwa muda wazazi wangu hawakuhudhuria kanisani.
Ingawa hatukuhudhuria ibada kanisani kama familia, hiyo haikunizuia mimi kuhuduria mara chache na rafiki zangu.
Katika siku hizo, kwenda misheni kulikuwa akilini mwangu, lakini hakikuwa kitu nilichokizungumza na wazazi wangu.
Wakati nikihudhuria chuo, mimi pamoja na marafiki kadhaa tuliamua kwenda misheni. Nilikutana na askofu wangu, nikajaza fomu ya mombi ya kwenda misheni wakati wazazi wangu wakiwa hawapo. Waliporudi, niliwashangaza na habari kwamba nimeitwa kutumikia huko Uingereza. Nina shukuru kwa msaada wao wa dhati juu ya uamuzi huu na kwa marafiki wazuri ambao walinisaidia kuchagua kutumikia.
Huduma yangu ya umisionari iliniandaa kuja kuwa mume na baba bora na kufanikiwa katika biashara. Pia iliniandaa kwa ajili ya huduma ya maisha yote kwa Bwana na katika Kanisa Lake.
Katika mkutano mkuu wa Aprili 1985, nilipangiwa kuzungumza katika kikao cha ukuhani. Nilielekeza maneno yangu kwa wavulana. Nilizungumza kuhusu kujiandaa kutumikia kama mmisionari. Nilisema, “Kati ya mafunzo yote niliyopokea katika majukumu yangu Kanisani, hakuna yaliyokuwa ya muhimu zaidi kwangu kuliko mafunzo niliyopokea kama mmisionari wa miaka kumi na minane nikitumikia misheni.”1
Bwana anakujua. Unapotumikia misheni yako, utapata uzoefu ambao utakusaidia wewe kumjua Yeye vyema. Utakuwa kiroho katika kumtumikia Yeye. Katika jina Lake, utatumwa kwenye majukumu ya kuwatumikia wengine. Yeye atakupa uzoefu pamoja na ushawishi toka kwa Roho Mtakatifu. Bwana atakuindhinisha kufundisha katika jina Lake. Unaweza kumonyesha Yeye kwamba Anaweza kukuamini na kukutegemea.
Miezi mitano tu iliyopita, Mzee Jeffrey R. Holland na Mzee Quentin L. Cook, ambao pia walitumikia kama wamisionari katika Visiwa vya Uingereza, waliungana nami katika kukutana na waumini na wamisionari katika nchi hiyo nzuri. Nikiwa huko, nilitafakari juu ya uzoefu wangu kama mmisionari kijana. Ninashuhudia kwamba katika misheni yangu ndipo nilipojua kwamba Baba yangu wa Mbinguni na Mwokozi wangu, Yesu Kristo, Wananijua na kunipenda.
Nilibarikiwa kuwa na marais wa misheni wawili wa kupendeza, Selvoy J. Boyer na Stainer Richards, pamoja na wenzi wao waliojitolea, Glady Boyer na Jane Richards. Nikitazama nyuma, ninaweza hata kuona wazi zaidi kwamba waliniamini na kunipenda. Walinifunza injili. Walitarajia mengi kutoka kwangu. Walinipatia majukumu mengi yenye changamoto na ya kioungozi ili kunisaidia kukua na kujiandaa kwa ajili ya huduma ya maisha yote.
Pia nimetafakari juu ya kuitwa na Rais Spencer W. Kimball ili kusimamia Misheni ya Canada Toronto pamoja na mke wangu mpendwa, Barbara, na watoto wetu wakiwa pamoja nasi. Rais Kimball alituita kutumikia mnamo Aprili 1974, punde baada yeye kutoa ujumbe wake wa kimisionari wenye msukumo wenye kichwa cha habari “Wakati Ulimwengu Utakapoongoka.”2 Katika ujumbe huu Rais Kimball alielezea ono lake la jinsi injili ambavyo ingepelekwa duniani kote. Aliomba wamisionari wengi zaidi kutoka kote ulimwenguni. Alitukumbusha juu ya matarajio ya Bwana “Na kwamba kila mtu … apaze sauti ya kuonya kwa wakazi wa dunia.”3 Mafundisho ya Rais Kimball kuhusu matarajio juu ya wavulana kutumikia misheni yalikuwa mada ya mazungumzo nyumbani kote duniani. Matarajio hayo bado hayajabadilika. Ninashukuru kwamba Rais Russell M. Nelson pia amesisitiza matarajio ya Bwana asubuhi hii.
Imekuwa karibu miaka 10 tangu Rais Thomas S. Monson alipotangaza kupunguzwa kwa umri wa umisionari kwa wavulana na wasichana.4 Katika mtazamo wangu, sababu ya msingi ya badiliko hili ilikuwa ni kuwapa vijana wetu wengi fursa ibadilishayo maisha kwa kutumikia kama mmisionari.
Kama Mtume wa Bwana Yesu Kristo, sasa ninatoa wito kwenu ninyi wavulana—na wasichana wale ambao mna hamu ya kutumikia misheni—kuanza sasa hivi kuzungumza na wazazi wenu kuhusu kutumikia misheni. Pia ninawaalika kuzungumza na rafiki zenu kuhusu kutumikia misheni, na ikiwa mmoja wa rafiki zenu hana uhakika kuhusu kutumikia, wahimizeni kuzungumza na askofu wao.
Jiwekeeni nadhiri wenyewe na kwa Baba wa Mbinguni kwamba mtatumikia misheni na kwamba kutoka wakati huu na kuendelea mtajitahidi kuiweka mioyo yenu, mikono yenu, na mawazo yenu safi na stahiki. Ninawaalika mpate ushuhuda thabiti wa injili ya urejesho ya Yesu Kristo.
Akina baba na akina mama wa vijana hawa wazuri, mna jukumu la muhimu katika mchakato huu wa maandalizi. Kuanzia leo zungumzeni na watoto wenu kuhusu huduma ya umisionari. Tunajua kwamba familia ni ushawishi mkuu zaidi katika kuwasaidia wavulana wetu na wasichana wetu kujiandaa.
Kama wewe bado ungali katika rika la huduma ya umisionari lakini bado hujatumikia kwa sababu ya janga la ulimwenguni kote au kwa sababu zingine, ninakualika utumikie sasa. Zungumza na askofu wako, na jiandae kumtumikia Bwana.
Ninawahimiza ninyi maaskofu muwasaidie wavulana na wasichana wote ambao wanakaribia umri wa umisionari kujiandaa kutumikia, na pia ninawahimiza ninyi maaskofu kutambua wale ambo umri wao unafaa lakini bado hawajatumikia. Ninamwalika kila mvulana kuwa mmisionari, vile vile kila msichana ambaye ana hamu ya kutumikia.
Kwa wamisionari wanaotumikia hivi sasa, tunawashukuru. Misheni yenu imekuwa katika wakati wa janga la ulimwenguni kote. Kama matokeo, uzoefu wa misheni yenu umekuwa tofauti na uzoefu wa misheni yangu au uzoefu wa wamisionari wowote waliotumikia kabla ya 2020. Ninajua haijawa rahisi. Lakini hata wakati wa nyakati hizi ngumu, Bwana amekuwa na kazi ya kufanya kwa ajili yenu, na ninyi mmeifanya vyema. Kwa mfano, ninyi mmetumia tekinolojia katika njia mpya kuwapata wale walio tayari kujifunza kuhusu Urejesho wa injili ya Yesu Kristo. Mnapotumikia kwa bidii na kulingana na uwezo wenu, ninajua kwamba Bwana anapendezwa na juhudi zenu. Ninajua kwamba huduma yenu itabariki maisha yenu.
Wakati mnapopumzishwa toka misheni yenu, kumbukeni hamjapumzishwa kushiriki kikamilifu Kanisani. Jengeni juu ya tabia nzuri mlizojifunza katika misheni yenu, endeleeni kuimarisha ushuhuda wenu, fanyeni kazi kwa bidii, salini, na muwe watiifu kwa Bwana. Yaheshimuni maagano mliyofanya. Endeleeni kuwabariki na kuwatumikia wengine.
Ni sala yangu kwamba ninyi wavulana na wasichana na wazazi wenu mtaona na kujua jinsi huduma ya umisionari itabariki maisha yenu milele. Na mjue katika akili zenu na mhisi katika mioyo yenu uwezo wa mwaliko Bwana aliotoa kwa wamisionari wa kupendeza wana wa Mosia. Yeye alisema, “Nendeni … na muimarishe neno langu; walakini mtakuwa wenye subira kwa uvumilivu na mateso, kwamba muwatolee mfano mwema … ndani yangu, na nitawafanya muwe chombo katika mikono yangu cha kuokoa nafsi nyingi.”5
Na Bwana awabariki vijana wa Kanisa wawe na hamu ya kujiandaa na kumtumikia Yeye ni sala yangu kwa unyenyekevu, ambayo naomba asubuhi hii katika jina takatifu la Bwana Yesu Kristo, amina.